Thursday, 27 May 2010

Sera yangu sasa ni kitochi mpango mzima

KWA vile urais ni ulaji rahisi wa dezo, nina azima ya kuwa rais wenu siku moja inshallah.

Baada ya kugundua mambo si mambo huko tuendako hasa kuhusiana na ulaji wangu, nilikuna kichwa.

Baada ya kukuna nimeiibuka na kitu cha kupigiwa mfano ambacho kitaniseleleza madarakani kwenye kijiwe.

Nimeongea na wazee wa kimeku na kuibuka na kitu kipya kinachoitwa kitochi. Sisemi tumehalalisha rushwa japo ni hivyo. Soma taratibu mzee wa Kitochi asiinyake akanifanyia kitu mbaya. Sitaki kuitwa maelekezo kutoa maelezo.

Kwa vile nimekuwa nikitawala walevi wenye njaa kama ng’ombe wanaohitaji majani, nilibuni takrima. Kimsingi bila njaa hakuna takrima na bila takrima hakuna njaa.

Nikiwa nimeandamana na vigogo wote wa chama, tulikaa kwenye jukwaa la VIP au Very Infamous Persons.

Kwanza, nieleze. Chama changu kimebadilishwa jina. Kinaitwa CCT yaani Chama Cha Takrima na sera yetu kuu ni ukarimu ambao adui yangu Msomi Mkatatamaa anasema utageuka kuwa ufisadi na uchakaramu uchwara. Nimebuni sera hii baada ya wimbo wangu wa jogoo na kamba za mambo safi kwa wote kutofua dafu miaka yote nenda rudi niliyotawala kijiwe.

Walevi wamengojea mambo kuwa safi bila majibu. Sasa mambo si safi ni chafu hakuna mfano. Sasa yatakuwa safi japo kwa msimu.

Ni juzi tu wanywaji walitaka kugoma na kuandamana kupinga sera yangu ya kunywa na kula peke yangu mimi, mama watoto, vitegemezi na maswahiba zangu.

Kwa vile hii ni lala salama yangu, lazima niwafunge kamba walevi kwa kuwapa vitochi vitakapoanza kuwachoma hapo baadaye walie na ujuha na uroho wao.

Kwa vile najua walevi wanapenda vya dezo, hawatakwepa kuuvaa mkenge kichwa kichwa.

Sitanii. japo yule mtendwa wa kubangaiza kwenye ulaji aliopewa na mtangulizi wangu amejikomba na kusema kuwa niliposema kuwa sera yangu ni kitochi nilikuwa natania, sina utani wa namna hii. Nafanya kweli-kuwabamiza walevi mkenge kwa mara nyingine.

Msishangae kumsikia mgosi Makambale na wapambe zangu wengine wakiimba kitochi tochi ila tusimulikane. Hayo tuyaache kwanza.

Chini ya sera ya kitochi, lazima mtu apigwe kitochi hadi azimie aweze kuachia kula. Bila kuwalewesha walevi wakazimia kwa makamuzi hawawezi kuachia. Si unajua usawa na ukapa huu?

Jamaa zangu maadui zangu wameishaanza kuzoza kuwa napanga kucheza mchezo mchafu. Hakuna mchezo mchafu hapa. Kama hamna sera wala sura ukiachia mbali mafweza na maepa basi njooni kwangu kama Lyatongolwa niwape kitochi mtulize boli.

Jamaa zangu wa mitaa ya Kwa Mfugambwa, Tandale kwa Mtogole, Uwanja wa fisi, Sisi kwa Sisi, Kwa Binti Kahenga Mburahati na Kigogo Luhanga bila kuwasahau wa kule Mbagala kaeni mkao wa kula. Japo kitochi ni cha akina meku, hata sisi wakwerezi huwa tunacho. Kinaitwaje? Msiniulize. Kitochi ni kitochi tu.

Kule Ntwara kina njomba mjue nkojo itaua mtu. Maeno ya Nakapanya, Nanguruwe, Nanyumbu, Nanyamba, Naumbu na Namtumbuka kaeni chonjo kitochi chaja.

Akina Mugabo pale Buzebazeba, Heru juu, Ruchugi, Mganza, Nguruka, Kazuramimba na Nyumbigwa elewa gwagwa itanyonga mwana wa mtu.

Kule Moshi pale Soweto, Nronga, Kalali, Nkwarungo, Kishumundu kwa bi Tunituni, Mashati na Karanga kaeni mkao wa kula. Maeneo ya Vunjo, Rombo na Nkweshoo mtulie tu. Jamaa zangu akina Lyatongolwa na Senti Mbili watatembeza kitochi kama hawana akili nzuri.

Mwakaleli, Matema, Nzove, Tukuyu na maeneo ya Kasumulu msikonde. Mambo ya kutupiana mimawe yamepitwa na wakati. Mambo ni kwa kitochi ila tusimulikane wala kuchomana bali kupeana maulaji.

Pia kutakuwa na migebuka kwa sana ili kushushia kitochi baada ya kusota kwa miaka mingi bila kulowanisha makoo.

Nikishawatwanga walevi kitochi, watafuatia marafiki zangu ambao nao lazima niwalipe fadhila ya kitochi kwa kunipigia ndogo ndogo.

Hapa nitaanzisha nafasi nyingi za ulaji kwenye utawala wa kijiwe ili sote tusherehekee matokeo ya kitochi.

Wale wanaopinga kitochi wasahauni kama masahauni tulivomsahau kwenye umoja wa vija--- we koma!

Sasa niwaeleze uzuri wa sera ya kitochi. Sera ya kitochi inasifika sana kwa kuruhusu watu wote kula pamoja. Mnahomola sehemu sehemu halafu mnahongana kiasi cha kutokuwapo mtu wa kulalamika kuwa hakushiriki uhomozi ambao wajinga wasiojua mambo wanaita ufisadi.

Watu wakishashiba kitochi hawawezi kuwaza vibaya kama kugoma au kuandamana. Wataandamanaje wakati nao ni sehemu ya jinai yenyewe? Nani ataandamana au kulaumu wakati alikula yeye.

Hamkumbuki yule jamaa aliyewaambia walevi kuwa wasimsumbue na kutaka huduma kwani ukuu wake aliupata toka kwao kwa kuwapa kitochi. Maskini majuha wale hawakujua kuwa mtindo wa kisasa ni kula na kulipa!

Uzuri mwingine wa kitochi ni kwamba ukishahomola hulazimiki kutangaza utajiri wako. Ukitangaza unatangaza umaskini kama yule jamaa yangu aliyepindishwa na mizengwe.

Pia sera ya kitochi ni uruhusu mtu kuwa mbwi kiasi cha mambo kujiendea bila kusumbuka.

Chini ya sera ya kitochi maisha yanakuwa kama sherehe. Kila mtu anafurahi kivyake japo baadaye wengi huanza kulia tokana na hangover.

Hapa ndipo mawe yote hufunuliwa na hatimaye mhusika kujikuta ni sehemu ya jinai. Onyo. Wakati huu huwa mhusika ameishachelewa kiasi cha kuishia kulaumu kila mtu.

Ukiwa unapata kitochi unasahau adha za vitegemezi, michango ya skuli, ada na upuuzi mwingine. Kitochi kikishakuchoma na kukutocha unauona ukweli ukiwa umekutolea macho usijue la kufanya. Kwa wasio na subira huanza kuhama vyama mara CCT.

Mara CCWM yaani Chukua Cha Wengine Mapema, KHAFU yaani Kaangika Hatimaye Uanze fujo na kulia lia ili uitwe kwenye ulaji kwa njia ya kuunda ushirika wa fisi na mbuzi.

Mie huko siko! Sipo kabisa msijeanza kusema yakhe weye watuonea maya ati.

Uzuri mwingine wa sera ya kitochi ni kuruhusu ulevi kupindukia. Waweza kulewa na kutapika hata kupuupu na mtu asiulize. Unakula na kunywa mle mle na kupuupu na kutapika kama mainzi kama alivyowahi kusema balozi mmoja kuwa jamaa zetu fulani hula na kwenda kutapika kwenye miguu ya wishitiri wao ambao nao siku hizi wamestukia ulaji na ufisi ahadi wa jamaa zetu wa nonihino.

Pia unaweza ukalewa kitochi hata mamlaka ukatukana na kukashifu mradi ulevi tu. Juzi hamkusikia nilivyolewa nikawatukana na kuwatisha walaji? Mmesahau nilivyo wafokea na kuwakashifu kama sina akili nzuri? Huu ndiyo uzuri wa kitochi.

Kitochi hukufanya ufanye mambo kitoto. Watoto hupigana punde hupatana. Ndiyo maana utoto na ukichaa havina mpaka. Hamkuona juzi wazee wa kitochi walivyofanya mambo ya kitoto kiasi cha kuitwa watu wazima hovyo?

Pia sera ya kitochi inaruhusu kutunga sheria halafu unazivunja unapostuka au kulewa. Kawaida ya walevi ni kutunga sheria na kuzivunja hapo hapo. Leo unaweza kumuona baba mtu na heshima zake akiingia baa kukamata ulabu akiwa na nyodo na maringo.

Atafunga hata tai umdhanie fulani kumbe hovyo! Mpe dakika tano baada ya kukamua kitochi, mara ataanza kukonyeza wauza baa huku akimtazama kila mtu kwa dharau na hasira utafikiri ndiye aliyezaa juha hili!

Ataingia baa kwa sauti ya upole hasa anapomuita barmaid. Punde ataanza kumtangazia ndoa utadhani hana mke.

Baadaye atampa ofa kama hana akili nzuri. Mwisho wa yote atastukia pesa yote imeishaishia kwenye kitochi na nyama choma kiasi cha kushindwa hata kulipia bia ya mwisho.

Hapa ndipo kuitana majina ya ajabu ajabu huanza. Muuza baa aliyekuwa akiitwa sweet na angel mara hugeuka shetani, changu na nyang’au na majina mengine ambayo si rahisi kuyaandika.

Hapa ndipo kanuni na sheria zote huvunjwa. Hapa ndipo baba zima hukojoa pembeni mwa shimo hata ukutani huku likiyumba utadhani mlingoti wa gari!

Kitochi hufunga milango yote ya maarifa kiasi cha baba zima kugeuka bonge ya bwege. Badala ya kutembea kwa madaha kama lilivyokuja huanza kutambaa utadhani beibi wa miezi minne. Utalisikia jitu likiapia ng’ombe na kuku wakati nyumbani halina mfugo bali panya!

Hayo tuyaache. Tuyaache wale jamaa wanaojisifia kuleta maendeleo wakati wameleta maangamio wasijesema nawanga wao.

Wow! Time is up and what’s up. Acha nijitoe wasomi wasijenifuma naongea ung’eng’e mbuzi wakanitia aibu bure.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 26, 2010.

No comments: