Thursday, 27 May 2010

Siri ya serikali kununua mashangingi

SERIKALI ya Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa serikali tajiri sana duniani kutegemea na inavyotumia na kufuja pesa.

Tukio lililoripotiwa hivi karibuni mkoani Kilimanjaro ambapo Katibu Tawala wa Mkoa, Hilda Gondwe, aliuziwa gari aina ya Toyota Land Cruiser VX lililonunuliwa miaka mitatu iliyopita kwa sh 155,000,000 linaweza kutufungua macho ni kwanini serikali inapenda sana kununua magari haya ya bei mbaya pamoja na uchumi mbovu unaotegemea wafadhili na kuombaomba.

Inashangaza serikali ya namna hii kufumbia macho hasara ya sh 149, 000,000 tena zikisababishwa na mtu mmoja mdogo tu!

Hapa ushahidi wa mazingira ni kwamba watendaji wa serikali wanapenda kununua magari haya kama mradi wao wa kuyapata chee baada ya kuyatumia kwa muda mfupi.

Je, huko nje kuna akina Gondwe wangapi waliofanikisha hujuma hii kwa mlipa kodi na kwa muda gani?

Kwa ufupi, hapa ndipo pesa ya umma inapoteketea. Wanajiuzia magari, majumba, samani na kujitwalia mikopo. Hapa ndipo siri ya viongozi wetu kujitwalia Kiwira ilipo.

Leo utashangaa kuona mtu kama Spika wa Bunge akiishi kwenye nyumba ya kupanga inayokamua dola 7,000,000 karibia milioni kumi na ushei kwa mwezi.

Je, nyumba ya spika ya serikali iko wapi? Imeshauzwa kwa waliomtangulia? Mie sijui.

Huu ni ufisadi uliopindukia ambao unapaswa kuchunguzwa na kukomeshwa mara moja.

Leo kwa mfano, serikali itajenga majumba ya bei mbaya hadi mabilioni kwa watendaji wake. Wakimaliza muda wao wanajiuzia hayo majumba kwa bei ya kichaa. Rejea kwa mfano TANESCO kutokuwa na nyumba na kukarabati nyingine kwa mabilioni.

Ukichunguza kwa mfano nyumba anayoishi Spika na kulipa pango la shilingi milioni kumi na ushei, utakuta mwenye nyumba hii ana ukaribu na wenye madaraka. Je, namna hii tunaweza kusonga mbele?

Ingawa tukio la Gondwe kwa uzembe na ufisadi wa Tanzania litapita kama tukio dogo, kimsingi hii ni kashfa iliyopaswa kutufumbua macho na kuhakikisha kila jiwe linafunuliwa kujua mashangingi yanayoondolewa kwenye matumizi yanakwenda wapi. Tungehakikisha tunayarejesha yote.

Kinachokera ni wizi huu kuitwa uuzaji kiasi cha aliyejitwalia shangingi hili kujitetea eti ameuziwa na hana uwezo wa kujiuzia!

Tunakwenda wapi? Waliotuahidi maisha bora na haki wako wapi? Hawaoni kufuru na hujuma hii? Wapo kwenye madaraka kwa faida gani kama tunaibiwa mchana?

Kinachotisha na kusikitisha ni ukweli kuwa mhusika kuuhujumu umma anakwenda kwa cheo cha afisa tawala.

Kweli huyu ni afisa tawala au afisa twawala? Je, katika muda aliotumikia ofisini ameishafanya madili mangapi kama haya? Je, huyu naye ametangaza mali zake ili tujue zimepatikana vipi?

Je, huko nje wako wangapi wanaojiuzia majumba, kujipa tenda kupitia makampuni yao feki, kupeleka watoto wao nje kwa scholarships za umma, kujipendelea kwenye kila wafanyalo? Je, serikali itamchukulia hatua gani mtu kama huyu ili liwe somo na fundisho kwa wengine wenye tabia kama hii?

Nimegundua kwanini kelele zetu za kutaka nyumba za umma zilizonyakuliwa na utawala uliopita zinapuuzwa?. Huwezi kujua. Huenda hao tunaowaambia wazirejeshe kwa kutumia madaraka yao nao ni sehemu ya kundi la walionufaika na ujambazi huu.

Tukio hili pia limefichua uchoyo, ubinafsi na israfu ya watawala wetu visivyo na mfano.

Kwa mfano chanzo kilichofichua ufisadi huu kinasema kuwa gari husika lilikuwa likitumiwa na mkuu wa mkoa wa zamani wa Kilimanjaro Mohamed Babu lakini mkuu wa mkoa aliyefuatia Monica Mbega alilikataa kiasi cha kuilazimisha serikali kununua jingine aina ya Toyota Landcruicer V8 VX kwa thamani ya sh milioni 190.

Hivi mkuu wa mkoa wa namna hii anaweza kuisongeza nchi mbele kimaendeleo? Je, hii ni aina ya viongozi tunaotaka kwa stahiki ya taifa maskini kama letu? Kwanini hatuwezi hata kuwaiga jirani zetu wa Kenya?

Gondwe alipoulizwa ni kwanini alijiuzia gari la umma alikuwa na haya ya kusema: “Nisema tu kwamba mimi sina mamlaka ya kujiuzia gari, nimefuata taratibu zote. Niliandika barua kwenda Utumishi kuomba kununua gari, Utumishi nao wakawaandikia Miundombinu na baada ya kumaliza mchakato wao Miundombinu wakanijibu.”

Je, hii ni kweli? Kama hakujiuzia ni nani amejiuzia iwapo yeye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli wa ofisi ya mkuu wa mkoa?

Ingekuwa vizuri aliyemuuzia awe mtu au kikao wajulikane. Maana hawa ndiyo wahujumu wa ofisi ya mkuu wa mkoa.

Tukubaliane. Namna hii nchi yetu imegeuka shamba la panya ambapo kila panya huguguna kilicho mbele yake. Mtendaji wa kijiji atataka anunuliwe pikipiki na baada ya miaka mitatu anajiuzia kwa bei ya kutupa.

Mtendaji mkuu wa wilaya, kadhalika, atajiuzia vilivyopo chini ya mamlaka yake, Waziri atajiuzia nyumba ya umma na rais anajitwalia Kiwira akitaka.

Mkuu wa mbuga za wanyama ataunda kampuni ya uwindaji huku mkuu wa barabara akiunda ya ujenzi na kujigawia miraba ya kuwinda huku wa barabara akijipa tenda ya ujenzi wa barabara ambayo ataijenga kwa kiwango cha chini akijilipa kwa bei ya juu.

Hii ni mifano kidogo ya kuonyesha ufisadi katika jamii yetu. Hali hizi nimeziongelea vizuri kwenye kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI, ambapo mbunge na mkuu wa mkoa wanashirikiana kutaka kujiuzia kijiji kwa kumtumia wakala wao mwekezaji Glutton Sucker.

Wanatumia ofisi za umma kuuibia umma kiasi cha wananchi kuathirika na kutangaza saa ya ukombozi ambapo serikali fisadi inayoangushwa kwa nguvu ya umma na kufanya uchunguzi wa utendaji wake na kuishia kuwafunga watawala walioangushwa na umma.

Japo kisa kizima ni cha kubuni, tuendako kitakuja kuwa kweli kama hatutachukua hatua kuondoa hali hii inayozidi kuhalalishwa kutokana na wakuu wetu kuibariki na kuikumbatia.

Kama tutakuwa wakweli tutagundua kuwa kwa cheo na kipato cha Gondwe, si rahisi mtu kuhimili kumilki shangingi baada ya kustaafu.

Hii maana yake ni kwamba kuna kipato kisicho na maelezo ambacho kinawawezesha watu kama hawa kuhimili gharama kubwa ya kutunza madude haya baada ya kustaafu.

Hapa ndipo utagundua mzizi wa umaskini wa walio wengi na ukwasi wa wezi wachache. Hapa ndipo ilipo siri ya mapenzi ya serikali kwa mashangingi pamoja na kelele nyingi za kupinga israfu na ufisadi huu. Tieni akilini.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 26, 2010.

3 comments:

Bennet said...

Huu kweli ni ufisadi mwingine wa hali ya juu, kama gari linahitaji kuuzwa nahisi lingeuzwa kwa mnada serekali isingekosa angalau milioni 50, hiyo gari kuuzwa kwa milioni moja ni aibu kwa sababu hata bajaji mbovu hupati kwa milioni moja

Mfalme Mrope said...

Staili hii ya uuzaji wa mali za serikali kwa watendaji wake kwa bei chee haikuanza jana wala juzi. Nimeshuhudia kwa macho yangu mwenyewe! Huu ni wizi wa mali ya umma lakini bahati mbaya wale tuliowaweka watulinde sisi wananchi na mali zetu sirikalini ndio hao hao wenye mchezo mchafu. Angalia barua ya kwa Che Nanihii hapa. Ni ubaradhuli tu ndio uendeleao si huko kwenye siri kali wala huku wachukuako vyao mapema. Kwa ufupi ni kwamba tunapiga hatua mbili mbele na kurudi nyuma hatua kumi.... HATUTOFIKA NG'O...

Anonymous said...

hi everyone. call me cheap and i think i am, but ive paid a lot of money on vhs & dvd movies. As well as im not spending a bunch of money on a brand new player at this time. ive learned the video creators are going to start phasing out dvd format take the place of HD DVD or bluray. and read that spiderman 3 will just come out in bluray. therefore i guess my issue is, can i convert a bluray film to dvd file format using a dvd burner, dvd software, and [url=http://www.topvideoconverter.com/blu-ray-to-dvd-converter/]convert blu ray to dvd software[/url]. sorry for the other post. thanks for any help.