HATIMAYE ile sinema maarufu ijulikanayo kama Bunch of Thieves (BoT) imekwisha! Sinema hii maarufu yenye kila ukatili, ujambazi, upofu, ufisi, ufisadi, utaahira, uhujumu na kila aina ya jinai ilitungwa na Benny (Hyena) M. Kappy.
Katika sinema hii Jackal (Mbwamwitu) Kwetty anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kusaka ufalme katika nchi ya Thugsland.
Watu wa Thugsland hupenda sana kuitana majina ya wanyama. Hivyo msishangae kuona majina ya wafalme hawa wawili ambayo kimsingi yanawasilisha tabia na hulka zao.
Kwetty hana pesa wala sera zaidi ya sanaa na longo longo katika azma yake ya kukalia kiti cha enzi cha ufalme. Hana ajenda wala mpango wowote zaidi ya kukamia kukwapua kama hana akili nzuri. Anautaka ufalme kwa udi na uvumba ingawa hana lolote la kuwafanyia wananchi zaidi ya kuwaingiza kwenye matatizo.
Katika kampeni zake za kuusaka ufalme, anaahidi pepo itakayogeuka jehanamu huku akiwahonga waandishi wa habari, wanajeshi, polisi na wengine wenye nafasi anaowapa vyeo kama fadhila jambo ambalo baadaye linakuwa tatizo sugu na hatari kwake.
Katika kufanikisha hili, maskini Kappy anaamuru hazina ya nchi iibiwe ili kupata pesa ya kuendeshea mipango ya kuupata ufalme kwa Kwetty, ambaye baadaye atalipa fadhila kwa kumkingia kifua mfalme.
Kappy kutokana naye kuhomola kama hana akili nzuri hasa akiongozwa na bi mkubwa wake Anatamaa. Kwa kujua alivyomesi, anaamua kuingia mkataba wa siri ili kuepuka kunyea debe baada ya kukabidhi taji la ufalme. Mpango huu mchafu unaratibiwa na jizi maarufu liitwalo Devil Lally akisaidiwa na jizi jingine liitwalo Matus Yumby.
Majizi haya yanafanikisha ujambazi huu kwa ujuha na ukatili sana kiasi cha wananchi wa nchi ya Thugsland kuachwa midomo wazi hasa pale Kwetty anapomfikisha mbele ya makuhani wajulikanao kama maruhani, Yumby.
Kinachowakera ni ukweli kuwa Yumby hafikishwi mahakamani ili haki kutendeka bali kuwahadaa wananchi na kuichezea shere mahakama inayotumika kama kikaragosi cha kubariki ujambazi na jinai za watawala!
Wakati Yumby akifikishwa mbele ya makuhani, Lally anayeyuka kinamna na kuacha zigo lote kwa Yumby. Anatokomea ughaibuni na hajulikani alipo.
Mchezo huu mchafu unapewa jina la EPA yaani Enabling Profiligacy Action. Chini ya mpango huu, yanaundwa makampuni hewa na kwenda benki na kukwanyua njuluku zinazowekwa kwenye akaunti mbali mbali za Chama Cha Maulaji (CCM) siyo chama cha mapinduzi chonde chonde) ambacho baaadaye kinawahonga wananchi na kunyakua taji la ufalme.
Mchezo mzima unaishia mbele ya baraza la makuhani linalokaa kwenye mji wa Kisooty na kufanya kile ambacho kila mmoja alikitegemea kutokana na mazoea ya kulindana na kufugana kwenye bahari ya mapapa wa ufisadi.
Pesa inatembezwa na siku ya siku Yumby anayewakilisha watawala wezi anashinda kesi kwa kupewa adhabu ya kifungo cha siku mbili. Umma wa wananchi unamwaga machozi na vilio kutawala wakililia hazina yao iliyobunguliwa huku makuhani na wakuu wakichekelea kwa ushindi ambao ni dhahiri, utaiangamiza nchi ya Thugsland.
Pamoja na ushindi huu bado wananchi wanajua kilichofanyika na kama si woga walikuwa na kila sababu ya kuwatia adabu mafisadi hawa wanaotumia sheria kama karatasi za chooni.
Baada ya makuhani kupinda na kunyea sheria, wananchi wengi wanasikika wakilaani sheria chafu na makuhani wachafu walioamua kuitumia sheria kujinufaisha kwa kuwaletea nakama umma.
Wakati hitimisho la sinema hii yenye kusikitisha na kuamsha hasira likifikiwa, mambo mengi ya ajabu yanaonekana. Mfalme bado anajipiga kifua kuwa ameweza kuleta haki ilhali ameipora na kuitukana. Amevunja na kutumia sheria vibaya. Lakini bado anajipa matumaini kuwa anatawala kwa sheria na haki wakati ukweli ni kwamba anatawala kwa vurugu na ujambazi.
Kinachokera zaidi ni kusikia walamba viatu na wapiga filimbi wa mfalme wakimsifia upumbavu badala ya kumwambia ukweli kuwa haki haijatendeka.
Katika sinema hii kuna kibaraka mmoja aitwaye Bogus Lemar. Huyu bwana amekuwa changudoa wa mfalme hakuna. Ameuza kichwa chake na mwili wake kiasi cha kusifia kila uchafu wa mfalme kiasi cha wananchi kuongeza jina Bogus yaani hovyo kwenye jina lake.
Msomi mmoja aitwaye Wheelbarrow Weapon, ambaye ndiye aliyefichua uchafu wa wafalme hawa bazazi anasikika akisema, “tumeliwa”. Je, nani atamsikiliza iwapo matumbo yameteka vichwa kiasi cha makamasi kutumika badala ya ubongo? Hii ndiyo hali ya kusikitisha ya nchi ya Thugsland.
Pamoja na kelele na vilio vyote, mfalme ameziba masikio na kuendeleza uharibifu wake. Hakuna alichowahi kufanikiwa tangu anyakue taji zaidi ya kuliangamiza taifa.
Anatumia na kuponda atakavyo huku wananchi wakipondwa na umaskini na mateso makubwa. Yeye na ukoo wake wanafaidi ufalme ukiachia mbali walamba viatu na wadandizi kila aina wanaoimba utukufu wa mfalme katikati ya maangamizi.
Badala ya kuwa mfalme wa watu wote, mfalme amegeuka mfalme wa wezi na fisi wachache aliojizungushia bila kujali kinachoendelea nje ya genge hili hatari kwa mustakabali wa taifa!
Kuna kitu kimoja kimejidhihirisha vilivyo kwenye filamu hii. Ni ile hali ya mfalme kuwa kipofu kiasi cha kutumiwa na wachumia tumbo wenye hata uwezo mdogo wa kufikiri kiasi cha yeye kujijengea mazingira magumu siku taji likimtoka.
Na yote hii imesababishwa na mfalme kutawala kwa kuangalia nyuma badala ya mbele. Amejijengea sifa za ajabu na umaarufu wa kipuuzi kiasi cha kushindwa kusoma alama za nyakati! Anaalika vurugu asijue kwenye vurugu hizi muathirika wa kwanza anaweza kuwa yeye. Tumewaona wangapi tena wenye akili zao.
Hata hivyo inatia faraja kugundua usemi maarufu kuwa muonee huruma msomi aliyepotezwa na mjinga, sawa na mfalme aliyepotoshwa na walamba viatu vyake au hata mkewe na mashoga zake kama Samson aliyepotoshwa na Delilah.
Japo mfalme anajifanya kutosikia, ameishaonyesha wazi kutikisika kiasi cha kuishi kwa wasi wasi.
Hata akisikia mlipuko wa pancha anahaha akidhani wananchi wamekuja kumpa haki yake kwa kuwafanyia mambo mabaya. Ana furaha usoni. Moyoni keshaoza kwa huzuni, majuto na ghadhabu.
Kitambo kidogo kabla ya sinema kuisha, mfalme anasikika akipayuka kuliko hata Mpayukaji mwenyewe. Anaonyesha kukata tamaa na kutokuwa na matumaini ingawa anajipa matumaini kwa kuwapa matumaini hewa wananchi ambao nao wameishamshtukia na kumchoka.
Loh, ngoja nipige mguu mapema. Maana hawachagui pa kupiga. Tukutane wiki ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 2, 2010.
No comments:
Post a Comment