Thursday, 10 June 2010

ICC adui yangu namba moja

HEBU piga picha. No. fikiria. Mtu umekwanyua vijisenti vya wanuka njaa na umaskini ili uvitumie kuwahonga upate ukuu ambao ni ulaji wa dezo kwako familia na marafiki zako halafu jitu linataka kutia kichumvi.

Hebu jaribu kufikiria. Unajipinda na kutengeneza dili kama HEPA, Richmonduli hata Kagoda halafu jitu lililoko huko Uropa linakuja na wazo kuwa ufungwe spidi gavana na kupelekwa The Hague ukanyee debe.

Je, namna hii ni wakuu wangapi katika bara hili la mwanga liitwalo la giza tutapona kama kweli hii itakuwa kweli na si geresha bwege? Msidhani natania. Kuna balaa linaundwa huko Uropa ili kuvuruga mavituz yetu.

Kwaza lazima niseme tena kwa kinywa kipana. Wazungu ni waoga, waongo na wanafiki. Kwanini wangoje Joji Kichaka amalize ngwe zake? Au ni kwa vile alikuwa akitawala taifa dume duniani? Kwani wanadhani tumesahau alivyoiba kura?

Mbona haya mazungu hayaendi kumshitaki malkia wa Uingrishi ambaye huwa anatanua tena bila ya kuandaa uchaguzi kiini macho hata angalau kwa kuiba hizo kura? Jamani eleweni. Huu ni ubaguzi wa rangi usio na mfano nasema.

Rafiki yangu Moi Kibaka juzi kanitonya.

Anasema tuwe macho na tukae chonjo lolote laweza kutokea hasa kwetu sie tulioweka tukachukua waa. Kibaka hafichi. Akiangalia yanayojiri kwenye kaya yake anasema wazi wakuu tutaumbuka. Anayebishia hili ajikumbushe Charles Taylor alifanywa nini?

Shujaa mzima yuko ananyea debe huku shujaa mwingie Omari Bashiri akitafutwa naye akanyee debe. Hawa jamaa hawana adabu. Nasikia kuwa Karumekenge na Madevu nao walionywa na EU na ICC kuwa kama watarudia upuuzi na madudu yao watanyea debe.

Hii ndiyo siri ya jamaa yangu kuuogopa ulaji kama ukoma huku Madevu akisilimishwa na kuongelea matambuano na amani wakati aliishaapa asingemtambua mtu wala malaika hadi yeye akalie kiti! Hamuoni alivyoingia ndoa ya mkeka kichwa kichwa akidhani ataukwaa ukuu ale dezo na kupunyua kama jamaa yake na shoga yake mpya Karumekenge?

Kuna jamaa moja limeniudhi nusu nijinyotoe roho. Si lilisema kuwa eti itungwe sheria ya kuwabana hata bibi wakubwa zetu kutokana na wao kutumia migongo yetu kufanya biashara ya kimachinga kama kuanzisha NGOs za uongo na ukweli ili mradi wachume.

Haya majuha kweli kweli. Si lipo jingine lililosema eti bi Nkubwa wangu ni muongo na mnafiki kutokana na kusema kuwa aliwahi kunyanyaswa alipokuwa akijifungua.

Lilisema eti hizi zilikuwa longo longo na kamba za kuwafungia walevi kuwa anawajali kiasi cha kuongopa. Linataka aeleze ni lini, wapi na nani alifanya kitendo hiki kwenye kaya ambapo wakubwa na miungu watu wasioweza kuguswa na vinyangarika waitwao manesi.

Sasa kama ni kamba au longo longo wewe inakuhusu nini. Si uache walevi waukwae mkenge wadhani bi nkubwa anawapenda wakati ukweli ni kwamba anawaponda kwa ulevi na ujuha wao.

Turejee kwa hili li ICC au International Criminals’ Court. yaani mahakama la wahalifu. Kuna jamaa lenye midevu kama Osama liitwalo Okampu Mreno. Hili jamaa linanikera na nalichukia kuliko hata huo ukoma.

Linasema kwa nyodo kuwa litatukomesha utadhani limewahi kukalia kiti cha enzi! Si lingejaribu kuutafuta ukuu lijue siri ya mchezo kuliko kupayuka hovyo.

Kwanza najua. Hili jamaa ni li-reno. Linatokea Ureno, taifa ambalo liliwatesa na kuwaua wanamapinduzi wengi. Wako wapi kina Eduardo Mondlane, Samora Machel, Louis Amircal Cabral, Augustino Neto na wengine wengi ambao waliuawa kwa njama za Wareno?

Mbona sijasikia hili likimshughulisha huyu Mreno uchwara? Anatufanya wote mabwege siyo? Hivi jamaa hili lilitaka tule polisi siyo?

Kwanza niseme wazi tena kwa kinywa kipana: Mreno hanitishi wala hatampata mtu. Lazima tupinge ukoloni huu mamboleo wa kutaka kuingilia madaraka yetu na kuvuruga amani na mshikamano. Sijui yanapata wapi mshipa wa kuhoji mamlaka yatokayo kwa Mungu.

Hivi hawa hawajui sisi ni chaguo la Mungu? Yaelekea hawa jamaa ni makafiri wasiosoma neno la Mungu lisemalo kuwa kila mamlaka hutoka kwa Mungu.

Mie nalishauli hili li-Mreno liseme shida yake ili likatiwe kitu kidogo kama akina Alex Stewart badala ya kuingilia ulaji wa watu. Kwanza pesa ya walevi inaliuma nini iwapo si yake?

Kisheria Mreno ni mhaini anayetaka kupindua serikali za wananchi tena wenye jamhuri zao.

Jamani tuache mchezo. Hali inatisha. Juzi nilimsikia rafiki yangu M7 akiwalaani wafadhili akitaka washughulike na ujenzi wa barabara badala ya kujisumbua kutaka kuingilia chafuzi zetu.

Kuna jamaa alimzodoa kuwa ameishiwa. Maana anataka wafadhili watoe mchicha wa kujengea barabara halafu wana siasia waukwibe na kutumia kuwahongea walevi.

Hawa jamaa si mabwege kama tunavyoweza kujidanganya kama jamaa yangu waliyempunguzia njuluku akajitia sizitaki mbichi hizi wakati hata pupi anayovaa na bi nkubwa wake imenunuliwa kwa njuluku za wafadhili hao hao anaojidai kuwatishia nyau.

M7 ameshtuka baada ya kaya yake kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa ICC wa kuharibu ulaji wetu.

Hata ukiona walioufungua ni wale wale wezi wa kula ambao nao kama M7 nadhani wamepewa onyo kuwa zao zinahesabika.

Je, walevi wanalipokeaje hili? Je, ni suto kwao kuwa wameshindwa kujikomboa hivyo Wazungu wameona wawakomboe ili waache kuwategemea kwa kuwabomu na kukopa kila uchao?

Mie mwenzenu niko nawaza la kufanya. Kama si wapambe wangu ningependa niachane na ukuu kabla sijalikoroga nikashindwa kulinywa.

Maana mambo yangu yanajulikana nilivyotembeza njuluku nilizoiba kijiweni kuwahonga walevi walionichagua wakidhani nitawakomboa wasijue nitawaangamiza.

Halafu kuna jambo jingine nasikia li-Mreno linataka kupendekeza. Linasema eti ambaye atachaguliwa kuwa mkuu asipotangaza mali zake au kumdhibiti bi nkubwa wake naye afikishwe The Hague.

Baada ya hili kujulikana nilisikia mimbea fulani ikisema eti hata walioghushi vyeti vya elimu na kuzaliwa nao wafikishwe The Hague.

Wengine wanataka hata Kagoda na Richmonduli nao wafikishwe The Hague kwa vile walitenda makosa ya ukatili dhidi ya mifuko ya binadamu.

Mie ningependekeza hata wale wanaochoma mibaka wakiabudia mibaka nao wafikishwe The Hague bila kusahau wauza unga maarufu wanaofadhili vyama na serikali.

Hata wale walioiba nyumba za walevi nao wangefikishwa huko ili wanyee debe kama Taylor au wafie huko kama Slobodan Milosevic.

Nasikia kuna mijitu inataka orodha ya waharifu wa kufikishwa The Hague iongezwe kiasi cha kuhusisha hata wezi kama mzee wa Vijsenti aliyeficha mabilioni ya madafu kule kwa Maza visiwani Jersey baada ya jamaa yake kumkingia kifua kutokana na kumsaidia kutengeneza Mahepe ya HEPA.

Kwa vile mie si mwoga na sina mpango wa kutengeneza HEPA tena, nilimpigia simu Mreno angoje kidogo nimalize kufanya vitu vyangu ndiyo awabane majuha wengine isipokuwa mimi.

Kuonyesha nisivyo mwoga na aibu niliunga mkono ukoloni huu nilipoitwa kutoa nasaha ingawa rohoni nilikuwa na unywanywa sina mfano.

Kwa vile mambo yanaanza kubadilika na kuharibika, nimewataarifu kina Mbwamwitu, Kanji Rosttamu na Ewassa kila mtu abebe furushi lake na tusilaumiane.

Ingawa walevi wameonekana kushabikia ujinga huu, kuna siku hawa wakoloni wanaoongozwa na Mreno kudai tutaje hata nyumba zetu ndogo na watoto wetu wa nje ya ndoa. Sijue nani atapona hapa?

Wakati natafakari huu upuuzi wa Mreno, roho inaniuma kuona nimeishachangisha vibilioni kidogo kwa ajili ya kitochi, vingi vikitoka kwa watu wachafu. Lakini nitaongea na wanasheria wangu wajenge hoja kuwa ukarimu au takrima si tendo baya linalopaswa kuchukuliwa kama kosa la jinai.

Lazima sheria hata kama ni za kimataifa zitambue kuwa ukarimu ni jadi yetu.

Pia nitashauri wahoji ni kwanini watu wanataka kutumia sheria kuvuruga mshikamano na amani tulivyorithi toka kwa mashujaa wetu?

Naona dege la Mreno linakaribia kutua airport ngoja nikitoe lisije likanikamata na kunisukumiza The Hague nikanyee debe.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 9, 2010.

No comments: