Japo mimi si mshauri wa rais Jakaya Kikwete, kama mwananchi, nataka nijipe fursa hii japo kwa mara moja. Juzi niliona picha nyingi kwenye mitandao zikimwonyesha rais akipokea misaada toka kwa balozi wa China yenye thamani ya shilingi 51,000,000 ambazo ni sawa na takribani dola 42,000 na ushei. Kwa cheo cha rais na ratiba yake finyu, kuhusika kwenye kupokea udoho kama huu ni kupoteza muda na kumdhalilisha.
Na hii si mara ya kwanza kwa rais kutumiwa vibaya. Aliwahi kuonekana akipokea misaada uchwara toka kwa wahindi fulani. Aliwahi kuonekana akiongea na Didier Drogba mwanasoka wa Ivory Coast anayecheza mpira wa kulipwa Ulaya. Pia aliwahi kuonekana akipewa jezi ya mchezaji Ronaldo wa Real Madrid ya Hispania. Ajabu aliipokea kwa shangwe bila roho kumsuta kuwa ukiona vyaelea vyaundwa. Yeye ametengeneza akina Ronaldo wangapi tangu aingie madarakani? Naye meya wa jiji alishabikia dharau hii kana kwamba hakuna vitu vingine vya maana vya kumpa! Kweli wazungu wanajua kutuchezea akili!
Kwa wanaojua hadhi ya rais, kupokea upuuzi kama baiskeli, pikipiki na viatu si sehemu yake. Rais anapaswa awapokee wageni wa hadhi yake. Kama ni kufuata itifaki, rais hapaswi hata kumpokea waziri mkuu vinginevyo awe ndiye mkuu wa nchi kama ilivyo kwa India, Kanada na nchi nyingine.
Juzi rais alionekana akipeana mikono na wachezaji wa timu ya Brazil jambo ambalo lilipaswa kufanywa na waziri wa michezo hata mwenyekiti wa TFF.
Baada ya hapo ratiba ya ziara yake mkoani Kilimanjaro alipokumbwa na aibu ya magari yake kujazwa mafuta machafu, alipangiwa kufunga tawi la Benki ya Biashara ya Kenya (KCB). Kwa wenye akili hili lilipaswa liwe suto kwa sera yake ya ubinafsishaji wa kiwendawazimu na kijambazi. Je Tanzania ina mradi gani wa maana Kenya zaidi ya kulilisha taifa hili kiasi cha kuweza kuuza hata Sudan ya Kusini. Hata katika biashara hii wafanyabiashara wa kitanzania hawanufaiki. Kwani wakenya hugoma kununua kutoka kwao na hivyo kulazimika kulanguliwa nao tayari kupata soko zuri Sudan. Kwanini Kenya waweze sisi tushindwe? Aibu.
Na hii imekuwa tabia inayoota sugu ambapo rais ameanza kutumiwa na hata wafanyabiashara wenye kutia mashaka kufanya shughuli ambazo si saizi yake.
Kama sikosei, udhalili huu umeanzia kule. Rais amekuwa akitumiwa vibaya. Anavunjiwa hadhi. Sijui kwanini washauri wake hawalioni kama hata yeye halioni?
Hebu piga picha rais anakwenda kupokea msaada wa shilling milioni hamsini tena hafla yake kufanyika ikulu. Je hafla hiyo imetumia shilingi ngapi? Maana siku zote wageni wanapomtembelea rais ikulu lazima awakirimu. Si ajabu ukakuta pesa iliyotumika ukichanganya na muda wa rais ni zaidi ya msaada uliotolewa. Ndiyo. Maana hesabu za watawala wetu zina utata. Wanatumia pesa nyingi kwenda nje kuomba pesa kidogo. Na hii ndiyo maana inafanya iwe rahisi kuwatuhumu kwenda kwenye shopping na kukagua miradi yao au hata kujilisha upepo.
Kuna hata kwa rais kugeuzwa bidhaa rahisi kwa wafanya biashara na watafutaji umaarufu wa shilingi mbili. Licha ya kupoteza heshima na muda wa umma, kuna hata hii tabia ya rais kutumiwa kwenye shughuli zisizoendana na hadhi na hata sheria. Rejea kwa mfano rais kufungua hoteli Arusha na baada ya muda mfupi ikabomolewa sehemu zake kutokana na kuvunja sheria. Rais na hoteli tena ya mtu binafsi wapi na wapi?
Marehemu baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere hakuwahi kuhudhuria harusi za wafanyabiashara au kufungua biashara zao. Alijua fika wafanyabishara wangetumia picha yake na wao hata kukwepa kodi na kuwatisha maafisa wa chini kama ambavyo iliwahi kudaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyabiashara wachafu nchini hasa wenye asili ya kigeni. Huu mchezo upo ingawa hatutaki kukubali. Nenda kwenye baadhi ya maduka ya wahindi. Utakuta wametundika picha zao na rais ukutani. Ili iweje? Wawatishe watu wa kodi hata kuvutia wafanyabiashara wanaotafuta dili.
Tusishangae siku moja rais kualikwa kwenda kwenye ngoma ya dogoli.
Kinachokera ni ukweli kuwa rais anapata muda wa kupokea misaada ambayo ingepokelewa hata na mnikulu au katibu kiongozi lakini anakosa muda wa kusoma miswaada anayosaini kama ilivyotokea kwenye mswaada wa uchaguzi ambao uliingizwa vifungu kinyume cha sheria bila ridhaa wala taarifa ya bunge.
Afadhali hata muda huu anaotumia kufanya vitu visivyoligana na hadhi yake angeutumia hata kujisomea na hatimaye kuandika hata kitabu kimoja. Maana baada ya marais wa kizazi cha uhuru waliofuata ni wavivu wa kusoma na kuandika vitabu ukiachia mbali kutojua mambo mengi wanayopaswa kuyajua. Urais umegeuzwa kuwa kama u-master of ceremony.
Hata ukiangalia hotuba zinazotolewa na marais wa kizazi hiki ukilinganisha na kilichopita utagundua kuwa ni nyepesi. Ikija kwenye kuwajibika ndiyo usiseme. Rais anamaliza muda wake bila kutangaza mali zake nasi tunaendelea kuaminishwa kuwa anafaa!
Nisingependa Kikwete ahitimishe utabiri wa mwalimu Nyerere kuwa ikulu imegeuka sehemu ya wafanyabiashara chafu. Ingawa balozi wa China anawakilisha taifa lake, siamini kama anaweza kumshauri rais wake apoteze muda wa umma kupokea vitu vidogo kama baiskeli na viatu vya shilingi milioni 51.
Japo tunaweza kuwalaumu washauri wa rais kwa kutomshauri vizuri, kuna upande wa pili. Kutokana na rais kupenda kuendelea kuwa mdarakani, anahitaji kila tukio linaloweza kumjenga awepo. Atapokea baiskeli ambazo zimetolewa na wachina. Lakini zikifikishwa kwa walengwa utasikia baiskeli za Kikwete. Wapambe wake watafanya hivyo naye akijua kuwa ni kinyume. Lakini kwa vile zinamuongezea mileage atanyamaza ilmradi wapiga kura wamepata taarifa na kushawishika. Hii nayo inaweza kuwa rushwa. Maana tangu uchaguzi ukaribie utasikia rais katoa saruji kwa shule fulani. Unashangaa rais anapopata hii pesa ya kutoa misaada hii. Mfano kwa karibuni ni kufichuka kwa taarifa kuwa kulikuwa na kasheshe wilayani Pangani mkoani Tanga kutokana na kutumiwa vibaya mifuko 500 ya saruji iliyotolewa na rais kwa ajili ya ujenzi wa bweni kwenye shule ya Bushiri.
Kuhusu hili mkuu wa mkoa Said Kalembo alikaririwa akisema: “Hivi rais akija hapa tutamuambia kitu gani kuhusiana na mifuko ya saruji aliyoipatia wilaya kwa jili ya ujenzi wa mabweni ya Sekondari ya Bushiri kwa kuwa hamna kilichofanyika? Hii ni aibu.”
Kutokana na rais kujiingiza kwenye biashara isiyomhusu hata watendaji wadogo mikoani na wilayani wanajua udhaifu wake kiasi cha kutotekeleza maagizo yake. Wanajua udhaifu wake kuwa anasahau. Anasema mengi na kukumbuka machache. Wanalijua hili fika. Wanajua kuwa anapata muda wa kutosha wa kusafiri na kukutana na akina Drogba lakini hana muda wa kushughulikia masuala muhimu na makubwa ya kitaifa kama kutoa dira ya taifa.
Hivi siku tukiletewa kibonzo kikimuonyesha rais na suti yake akisakata mchiriku au mpira tutaanza kulaumu anadhalilishwa?
1 comment:
Umenena ukweli mtupu rais wetu amekuwa kama changudoa kwa wafanyabiashara matapeli. Keep it up
Post a Comment