Wednesday, 23 June 2010

Tusikwepe ukweli, huu ni urais wa kununua

WATANZANIA ni watu wa ajabu kidogo. Si kwamba wana macho nyuma au wana sura za ajabu ajabu kama Barney wa kwenye katuni za kitoto. Wala hawana uajabu wowote kimaumbile bali kiakili na kitabia.

Hakuna kitu kilichonishangaza kama jina lao kutumika kuendeleza wizi wa pesa za umma na hongo ukiachia mbali ufisadi wa kunuka.

Bado ni jina lao hili hili linalotumiwa na ombaomba wa masuti kwenda kwa wafadhili kupewa pesa ya kuja kufisidi! Nao kwa bahati mbaya wamekubali kujirahisisha na kujikomba kwa kundi la watesi wao kiasi cha kushangilia na kushabikia maafa yao.

Je, hawa wana tofauti na nondo mdudu ambaye huona mwanga na kuchachawa kiasi cha kuishia kuunguzwa na moto utoao mwanga huu?

Je, hawa wana tofauti na mbwa ambaye huwinda na kuishia kupewa kwato na mapupu huku nyama safi ikifaidiwa na amfugaye?

Ukiangalia Chama Cha Mapinduzi (CCM) “kinavyochangisha” pesa kwa ajili ya uchaguzi, utajua ninachomaanisha kwa kusema Watanzania ni watu wa ajabu.

Ni wa ajabu kutokana na kusahau kuwa ni CCM hii hii iliyotuhumiwa kuchota pesa toka Benki Kuu mwaka 2005 toka kwenye fuko la pesa ya malipo ya madeni ya nje (EPA). Wamesahau kuwa ni CCM hii hii iliyotuhumiwa kuiba pesa ya umma kwa kutumia kampuni lake la Deep Green Finance.

Wamesahau kuwa ni CCM hii hii iliyotuhumiwa kutumia kampuni la Meremeta kuiba pesa ya umma kwa ajili ya uchaguzi unaodaiwa kuwa ulimwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani kwa njia ya kuchafuana na rushwa!

Ni Watanzania hawa hawa wamesahau kuwa ni CCM hii hii iliyotuhumiwa kutumia wafanyabiashara wezi na mafisadi wakuu kuifadhili na kuiba pesa husika katika kashfa hizo tajwa!

Ajabu wamesahau kuwa katikati ya hujuma hizi kuna CCM na Kikwete ambao kwa pamoja hakuna aliyewahi kukanusha tuhuma tajwa hapo juu!

Wamesahau kuwa ni Kikwete huyu huyu ambaye amelipa fadhila kwa kuwanyamazia watuhumiwa wote wakiwamo chama chake hata yeye mwenyewe!

Ni mpumbavu ang’atwaye na nyoka kwenye shimo moja mara mbili. Ni maafa ya kutisha hili linapofanywa na nchi.

Tutafakari na kujiuliza. Je, Kikwete ni maskini wa kuhitaji kuchangiwa hata pesa ya kuchukulia fomu?

Je, wanaofanya hivyo licha ya kulea ufisadi na kuathirika na ufisadi wa kiakili hawajikombi, kujihujumu, kujidhalilisha na kugeuka tishio kwa mustakabali wa taifa?

Hakuna umaskini na ufisadi mbaya kama wa kiakili. Tujihoji na kujisuta. Kikwete amefanya nini cha mno kuwatajirisha Watanzania kiasi cha kumpenda hadi kumchangia ukiachia mbali kujikomba na mapenzi ya mshumaa?

Je, mke wa Kikwete chini ya Kampuni yake ya WAMA inayoingiza mamilioni kila uchao kwa mgongo wa ikulu wamekosa pesa ya kumchangia Kikwete kama kweli ni mchovu kiasi hiki?

Mchezo huu mchafu wa kujikomba ulianzia Bukoba ambapo umoja wa vijana wa CCM huko ulimchangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kuchukulia fomu hapo Juni mwaka jana.

Je, vijana wa namna hii wanaojikomba na kujigeuza vifaa vya kutumiwa wanaweza kulifaa taifa?

Je, hawa si aibu kwa taifa hata wazazi wao na kwao wenyewe? Je, hawa wana tofauti na nepi ambayo hukumba kila uchafu? Ajabu vijana hawa wanaojifanya kuwa na uchungu na Kikwete ni wale wale wanaoathiriwa na ukosefu wa ajira na mikopo kwa ajili ya elimu ya juu, ukiachia mbali matatizo mengine mengi!

Je, kweli waliochanga hii pesa ni vijana au wametumiwa na wafadhili wa Kikwete ambao hawataki kujulikana?

Tunaambiwa CCM imeishachangisha kiasi cha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kumwezesha Kikwete kushinda.

Je, huku ni kumwezesha kushinda au kununua urais? Je, urais wa kununua unatufaa na unaweza kutuvusha kwenye karne hii?

Mbona wapambe uchwara wa Kikwete wanasema: yu maarufu kuliko chama na ametenda mengi ukiachia mbali kuwa chaguo la Mungu? Ni chaguo gani la Mungu hata watu, linahitaji mabilioni kuweza ‘kushinda?’

Sisi ni watu wa ajabu kweli kweli. Tuna uwezo wa kuchangisha bilioni 50.

Hapo hapo tunakwenda kwa wafadhili kujidhalilisha kuomba za kugharimia uchaguzi!

Tuna jeuri na ubavu wa kuchangisha mabilioni kwa ajili ya mtu mmoja. Tunakosa za kuchapishia vitambulisho vya taifa, kununulia madawa mahospitalini ambapo wagonjwa wetu wanalala wanne kitanda kimoja! Huyu atokanaye na bilioni 50 si rais wetu bali wa wale waliomchangia (waliomnunua).

Hii ni biashara ikulu ambayo Baba wa Taifa alituasa kuiogopa kama ukoma. Huu licha ya kuwa wizi na ufisadi ni uhaini-kwani tunaifanyia uhuni katiba yetu inayosema rais wa Tanzania atapatikana kwa uchaguzi huru na wa haki.

Ajabu huyu tunayemchangia utamsikia akitoa somo la uwajibikaji, uzalendo na usafi! Huyu ni mbinafsi na mchoyo, taka usitake japo hataki kukubali hili. Heri tutangaze ufalme tunusuru nchi.

Hivi pesa hii ingetumika kununulia vifaa mashuleni tungeboresha elimu yetu kwa kiasi gani?

Kweli Watanzania ni watu wa ajabu. Ajabu ya maajabu hata Kikwete mwenyewe ameridhia mchezo huu mchafu wa rushwa na ufisadi!

Nani amesahau kuridhia kwake kwa kitochi (takrima) ambayo bila shaka ataitoa kutokana na hizo bilioni hamsini! Je, mtu wa namna hii licha ya kuvurunda anatufaa kweli?

Juzi nilisikia Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye mwanae anakabiliwa na kashfa ya kutumia madaraka yake kusaka ubunge akisema kuwa CCM ilishindwa Moshi Mjini kutokana na njaa ya wanachama wake. Anajigamba kuwa mwaka huu watairejesha Moshi Mjini kwa vile wana mabilioni ya kumwaga.

Kinachothibitisha uajabu wa Watanzania ni pale mtu atakapoiba au kununua kura wazi wazi halafu wakimtangaza wanasema ameshinda kwa kishindo wakati si kushinda bali kuiba kwa kishindo. Huu ni uchafu.

Watanzania wataendeleza rekodi yao ya kuwa watu wa ajabu watakapokubali kuchezewa mchezo mchafu tena kwenye uchaguzi mwakani.

Na hali ilivyo wameisha halalisha uchafu huu. Kwa kukubali chama kichangishe mabilioni, tena kutoka kwa vyanzo vyenye kutia mashaka, ni ushahidi wazi kuwa wameishakubali kuibiwa haki kwa mara ya pili na chama kile kile na mtu yule yule ambaye utawala wake umeweka rekodi ya kuwa na kashfa kuliko tawala zilizopita zikiwekwa pamoja.

Swali linalojitokeza kila mara ni je, Watanzania wanamchangia rais kwa utajiri gani walio nao na umaskini gani rais alionao?

Je, wanaomchangia kweli ni Watanzania au wezi wachache waliovumiliwa na Watanzania?

Hapa hatujaongelea utawala wa kifalme uliojengwa na Kikwete ambapo wake, watoto na marafiki za rais wanaifuja nchi kwa mgongo wake.

Tuache upumbavu na kujikomba kwa watesi wetu. Tusimame tuhoji mantiki na vyanzo vya pesa hii chafu. Tuhoji na kukumbushia maadili ambapo hata huyu mnayemchangia amegoma kutaja mali zake na bado mnaendelea kumwamini na kumuabudia kwa njaa zenu vichwani. Atawajibikaji kwenu atakaowahonga badala ya wale waliomuwezesha kuwanunua? Hapa ndipo jibu la swali la Baba wa Taifa kuwa wanakimbilia nini ikulu wakati hakuna biashara utalipata barabara.

Laiti angekuwa hai akalisikia mwenyewe! Angekufa kwa mshtuko kuona wanaotarajiwa wawe wasomi pale Dodoma kujikomba na kumchangia sh 1,200,000 mtu anayewabana mikopo. Kama usomi ni huu, heri kuitwa kihiyo.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 23, 2010.

No comments: