Rafiki yangu alinipigia simu kwa mshangao toka Arusha. Alikuwa akinifahamisha siasa chafu zinazoendelea mkoani Arusha na Manyara.
Tangu mgogoro huu anze baada ya waziri mkuu aliyetimuliwa Edward Lowassa kutolewa kafara kuiokoa serikali ya swahiba yake rais Jakaya Kikwete, kumekuwako na majeruhi wengi mmojawapo maarufu akiwa mbunge wa Simanjiro Christopher ole Sendeka aliyefunguliwa kesi mbili zilizobainika kuwa za kutunga.
Je kesi za Sendekeza zinahusianaje na Lowassa? Simpo. Ni kutokana na waliokuwa nyuma ya kesi hizi kuwa wapambe na maswahiba wa Lowassa ambao alianza kuwatumia kuonyesha makucha yake pindi alipoteuliwa kwa utata kuwa waziri mkuu katika serikali ya swahiba yake kabla ya kuvurunda na kutolewa kafara ili kuinusuru serikali ambayo kama si uoni mfupi wa watanzania ilikuwa itimuliwe kutokana na ufisadi wa wazi.
Siasa za kuhasimiana hazipo Arusha na Manyara tu. Ziko Tanzania nzima hasa baada ya Chama Cha Mapinduzi kumeguka kwenye makundi mengi makuu yakiwa yale ya wanaopinga ufisadi na wanaonufaika na ufisadi. Haya yalipewa jina la mitandao hasa kipindi kile cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005.
Japo mitandao ni sehemu ya makundi haya mawili, ilikuwa mingi kulingana na wana-CCM walioonyesha kuwa na kiu na nguvu ya kuwania urais baada ya kwisha muda wa rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye ugombea wake ulizua mitandao lakini ikauawa na ushawishi wa baba wa taifa marehemu Mwl. Julius Nyerere aliyemuunga mkono wazi wazi na kumwingiza madarakani.
Japo kuna mitandao mingi, leo tutaongelea kundi moja kubwa lenye ushawishi serikalini la Lowassa-Rostam-Kikwete. Ingawa wachambuzi hawalitaji wazi wazi kama lilivyo, kundi hili linawakilisha wale wanaonufaika na ufisadi kutokana na kuwa na watuhumiwa wengi wa ufisadi ambao serikali imeshindwa kuwashughulikia. Badala yake inashughulikia wale wanaotaka washughulikiwe.
Kundi la pili ni la Sitta-Mwakyembe. Hili kundi linapata jina lake kutokana na spika wa Bunge Samuel Sitta kuridhia bunge kuunda tume teule kuchunguza kashfa ya Richmond. Tume hii iliongozwa na mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe hivyo kuwa kinara wa kundi ambalo linasakamwa kwa kila gharama na kundi la kwanza kutokana na kuhofia kuweza kusababisha litimliwe madarakani.
Hatutaeleza ushiriki wa kila kinara ingawa mbunge wa Igunga Rostam Aziz anafahamika alivyo swahiba wa Lowassa na Kikwete hasa baada ya kutuhumiwa kuwa nyuma ya sakata la Richmond. Alianza kujulikana pale alipotajwa na waziri wa zamani wa nishati na madini aliyetimuliwa na kashfa ya Richmond Dk Ibrahim Msabaha pale aliposema kuwa yeye alikuwa Bangusilo kwa kikwao akimaanisha kuwa mbuzi wa kafara-kwa vile mradi mzima wa Richmond ulikwa wa serikali ukishinikizwa na Lowassa kwa niaba ya bosi wake Kikwete huku akishinikizwa na aliyetajwa kama mwarabu wake yaani Rostam. Historia ya genge hili ni ndefu.
Tuje kwa mhusika mkuu wa makala hii, Edward Lowassa mbunge wa Monduli. Huyu baada ya kujeruhiwa na marehemu baba wa taifa kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 1995-akishutumiwa kuwa amejilimbikiza mali nyingi zisizo na maelezo, hakukata tamaa. Kwa kujua hatari iliyokuwa ikimkabili baadaye, alijiunga na Jakaya Kikwete aliyeonekana kushinda kinyang’anyiro cha kubeba bendera ya CCM lakini akakataliwa na Nyerere akidai hakuwa amekomaa kisiasa- hivyo kutostahili kuongoza taifa wakati ule.
Wazungu husema a good politician is a schemer yaani mwanasiasa mzuri lazima awe mwenye mbinu. Hivyo Lowassa baada ya kugundua hili, aliamua kuweka dau lake kwenye farasi aliyeonyesha kushinda yaani Kikwete.
Wapo wanaosema kuwa Lowassa licha ya kujua kuwa Kikwete alikuwa turufu pia alijua udhaifu wake-ulegelege. Hivyo alijua ushindi wa Kikwete ungemuwezesha kuwa kingmaker au mtengenezaji wa wafalme ambaye baada ya Kikwete angejitengeneza. Hivyo kuwa rais.
Wanasiasa mara nyingi hawakati tamaa. Wana subira ya fisi. Baada ya Lowassa kuteuliwa kuwa waziri mkuu na akaanza kuonyesha cheche zake akitenda karibu kila jambo huku Kikwete akiwa kama kaenda likizo, wengi wenye kutaka urais walianza kustuka na kufikiria la kufanya.
Bahati mzuri kwa kundi hili, mtu aliyeonekana kuwa tishio lake alianza kujimaliza kwa kuanza kuingia deal zilizommaliza hatimaye kubwa ikiwa Richmond. Hapa inabidi ieleweke kuwa Richmond haukuwa mradi wa Lowassa pekee bali Kikwete na Rostam na serikali nzima.
Je ni kwanini msalaba ulimuangukia Lowassa? Kwanza alikuwa waziri mkuu ambaye kimsingi ni mtendaji mkuu wa rais. Hapa ndipo dhana nzima kuwa kupatikana na hatia kwa Lowassa kulitosha kuiangusha serikali nzima ya Kikwete kama si watanzania kuwa na muono mfupi na ushabiki wa kijinga. Ila kama Lowassa, kutokana na jina baya alilokwishapewa na marehemu Nyerere, alikuwa ni mtu muafaka kubebeshwa zigo ili amuokoe rafiki yake na serikali yake.
Sababu nyingine ya kubebeshwa msalaba kwa Lowassa ni ukweli kuwa aliingia mkenge wa Richmond kwa pupa kutokana na chumo binafsi ambalo lingepatikana. Naye hakuwa wa kwanza kuwekeza kwenye jinai hii. Rejea rais mstaafu alivyoingia kwenye kashfa ya kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira na kuilazimisha Tanesco kununua nishati toka kwake kwa mwendo wa kuruka. Hivyo huu ni utamaduni mchafu ulionza kuota mizigo kiasi cha kuacha nchi yenye raslimali ikiomba omba. Anayebishia hili arejee tukio dogo la hivi karibuni ambapo afisa tawala mkoa wa Kilimanjaro Hilda Gondwe alijiuzia gari aina ya Toyota Land Cruiser VX (shangingi) lenye thamani ya shilingi 155,000,000 kwa bei ya kijambazi ya shilingi 6,000,000.
Kwenye nchi iliyotawaliwa na upanya na ufisi, hili ni jambo la kawaida na kila mbuzi anakula kwa urefu wa kamba yake.
Sasa si siri wala fununu. Lowassa ni majeruhi kisiasa. Yupo chumba cha wagonjwa mahututi. Wale madaktari mzungusho au spinning doctors-wenzake na mbwa wao yaani walamba viatu na makanjanja wako mbioni kutaka kumsafisha ili hapo baadaye awe rais. Je hili litafanikiwa bila muujiza? Tuazime maneno ya spika wa bunge akimpiga kijembe alipouliza: je yawezekana maji taka yakamsafisha mtu akatakata? Anayetilia shaka hili ajiulize ni vyombo vingapi vya habari vimeishaingia kazini kwa ujira wa pipi kumjenga huku vikiwabomoa wapinzani wake.
Ila wale wanaoota mchana kumsafishia njia Lowassa inabidi wajiulize maswali makuu muhimu.
Je anasafishika Je madhambi yake watayaficha wapi? Je watanzania watakuwa wasahaulifu na majuha kiasi hiki? Je anafaa baada ya kuonyesha uroho na uhovyo usio kifani? Je hatalipiza visasi tena kwa watu wasio na hatia bali kuwa wakweli? Je hatuna watu wengine wenye udhu kutuongoza? Je tuko tayari kurudia madudu tuliyo nayo? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Chanzo: Dira Juni 2010.
No comments:
Post a Comment