LEO niseme wazi. Sitapayuka bali kueleza kilio changu. Nalia na kuomboleza kiasi cha kupanga kwenda The Hague nimshitaki refa-mchezaji, audhubillahi minaa shaitwan rajiim, Joni Tenda, ambaye amenitenda mambo mabaya baada ya kupewa tenda ya kutuhujumu ili adui yangu mkuu apete asipopaswa.
Taarifa kwa umma ni kwamba siridhiki na jinsi mchezo (mchafu) navyochezeshwa na refa mchezaji niliyemtaja hapo juu. Naamini nawe unamjua na kujua mchezo mchafu na rafu anaotuchezea tena kwa kulipwa kodi zetu.
Unajua kuwa anatumwa na bwana wake, kiasi cha kujidhalilisha kila uchao kumridhisha huyu mshitiri wake kibaka mkuu.
Tuache kuzungusha. Juzi nilijifaragua kwenda kusajili Chama changu Cha Jeuri (CCJ).
Kwanza nilifanya kosa kubwa kuamini kuwa refa mchezaji na rafiki mkubwa wa jamaa yangu, audhubillahi mina shaitwan rajiim, Njaa Kaya ambaye simfichi. Ni Tenda. Sikujua kuwa nilikuwa napeleka kesi ya ngedere kwa nyani anifanyie unyani nyani na ungedere mchana kweupe bila hata chembe ya aibu! Niliamini kuwa katiba viraka ya kaya inazuia makocha, majaji, mapolisi na watumishi wengine wa kaya kuwa wanachama wa timu yoyote.
Hii imewekwa makusudi kuzuia ushikaji, hujuma, upendeleo, kujipendekeza na mambo mengine kama haya.
Hii ililenga kuzuia vurugu zinazoweza kusababishwa na waamuzi baada ya kulishwa takrima na kuonjeshwa kitochi.
Inatia aibu na kinyaa kukuta watumishi wa umma nao wana kadi fichi za vyama tena wakizitumia kuonea timu nyingine bila wasiwasi wowote kana kwamba wanachofanya ni kwa mujibu wa sheria!
Kwani hamuwajui majaji, wakuu wa majeshi hata mahakimu wenye kadi za chama kinachowala? Kama huwajui basi nakutajia mmojawapo yaani Tenda ambaye tenda yake ni kuhakikisha vyama vingine vinakufa ili chama chake cha maulaji kipete milele.
Anayebishia hili ajiulize wale majaji na wakuu wa majeshi wastaafu waliotaka kuwania urais na ubunge chini ya chama fulani chenye kutia mashaka walikuwa wamepata wapi kadi kama si kuwa wanachama hata walipokuwa kwenye ofisi za umma!
Nani zaidi ya mimi anayeshinikiza wafikishwe mbele ya haki ingawa na haki yenyewe siku hizi ni bidhaa sokoni? Je, hawa si wahalifu wa kawaida hata kama ni waheshimika?
Je hawa si matapeli wanaoweza hata kughushi vyeti vya taaluma hata vya kuzaliwa?
Ni juzi tu jamaa yangu alianzisha sera yake haramu ya kitochi ili kuweza kupeta bila kustahiki. Hayawi hayawi sasa yamekuwa!
Nilipoanzisha Chama changu Cha Jeuri, mafisadi wa Chama Cha Maulaji walianza kuchachawa na kuchanganyikiwa wakijua kiama chao kilikuwa hatimaye kimefika nisijue watatembeza takrima na kunijeruhi!
Ni juzi tu wamechangisha pesa chafu na haramu ili kuwahonga wapiga kula hatukusema. Sasa wametafsiri kimya chetu kama woga kiasi cha kumtumia huyu gendaeka Tenda kuendelea kujeruhi vyama vingine! Kaya hii ya walevi inapelekeshwa wapi na kwa spidi hii?
Niseme wazi. Ni upuuzi kwa refa kuwa mchezaji. Ni jinai sina mfano kuona jitu linalopaswa kuheshimika na kufanya mambo ya heshima kufanya upuuzi. Kama unapenda kucheza si uunde timu yako au ujiunge rasmi na timu nayoipenda na kuipendelea kwa kutuumiza wengine. Kinachonikera nusu ya kujinyotoa roho ni ile hali kuwa hili jamaa linalipwa mamilioni ya pesa ya madafu toka kwenye kodi yangu na walevi wengine.
Kwanini Tenda asiachane na kujidhalilisha akaunda chama chake na kujaribu kukisajili akajua machungu tupatayo hata akajiwajibisha na kutangaza kushiriki siasa kihalali badala ya kufua nepi za chama cha maulaji? Kujificha nyuma ya vyeo vya kupewa ni mojawapo ya woga na ujuha ukiachia mbali upakacha.
Pakacha huwa halina ubongo wala halichagui cha kubebeshwa. Huku ni kujigeuza mtu mzima hovyo kwa makusudi mazima kiasi cha kuishi kutegemea uchangudoa wa kisiasa ambalo si jambo jema kwa mja.
Niliamini refa huyu angekuwa huru na mstaarabu na si mleta fujo na mambo mengine ya hatari kwa kijiwe kama ambavyo siku zote amejinadi. Kumbe refa mwenyewe fisadi na fisi!
Kwa umri na cheo chake ni aibu isiyo kifani kufanya mambo ya kitoto.
Tutakuja kuchenjiana kama jamaa hataacha upuuzi wake au hata kuweka kando ili wenye udhu watuhudumie kwa mujibu wa katiba.
Nani angeamini kuwa mtu mwenye akili tena na cheo kikubwa kama cha refa huyu angeweza kutoa kadi nyekundu hata kabla ya kabumbu lenyewe kuanza? Wote mu mashahidi. Mmeona alivyoifanyia mtimanyongo timu yangu, tena changa.
Zamani nilikuwa nikishangaa wachezaji wanaoanzisha zilzali baada ya kuonewa na waamuzi vicheche kama Tenda mtenda mabaya.
Ingawa sina mpango wa kuanzisha vurugu, siwalaumu tena wanaofanya vurugu baada ya kuhujumiwa kama nilivyofanyiwa. Hata hivyo nitaanzisha vurugu gani iwapo Tenda keshaianzisha kwa sababu anazojua yeye ambazo bila shaka hata wewe unazijua-rushwa, takrima, ufisadi na ufisi.
Tufikie mahali tuachane na mambo ya kizamani, yaani kudhani kila mtu ni juha kama wewe kwa vile unaweza kufanya uhalifu na wahalifu wenzio wakakulinda kwa vile uliwafanyia kazi yao chafu.
Ni fikra mgando kudhani kuwa umma utaendelea kunyamazia matendo haya machafu ambayo ni uchokozi na hatari kwao na kaya yao.
Ajabu ya maajabu zee zima halioni hata aibu. Utaliona kwenye runinga likijidai kutenda haki wakati linaihujumu. Hili linafaa kuchapwa bakora.
Hata wale linaowabeba utawaona wakicheka cheka na kujisifu eti wameleta mema wakati wameleta zahama. kusuru wote.
Nyie ni majizi hata kama mtajificha nyuma ya utukufu usio mbele wala nyuma. Siku zenu zinazidi kuhesabika. Kuna siku tutawapeleka Segerea mkanyee mitondoo. Siku hiyo ikifika hakutakuwa na cha msalie mtume wala nini bali kufanya kweli.
Nimalizie kwa kumshauri Tenda aende milimani kwao akauze nyanya kama urefa na kutumia akili vimemshinda. Usidhani namshambulia. Thatha nifanyeje kama jitu lenyewe linatia kinyaa na aibu kiasi hiki tena kwa umri huu?
Acha nianze kuchapa mguu. Maana hata magari nayo siku hizi yananichukia kiasi cha kunigomea nisiyapande.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 16, 2010.
No comments:
Post a Comment