How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 10 June 2010

Mgomo wa wafanyakazi ungelikomboa taifa

KWA mara ya kwanza kwenye historia ya taifa letu, serikali na chama tawala hawakukaribishwa kwenye kilele cha sherehe za wafanyakazi maarufu kama Mei Mosi. Tunaambiwa. Wafanyakazi walikataa kumwalika rais kutokana na waziri wake kuwadharau na kuwahadaa.

Walikaririwa wakisema kuwa hata hivyo hawana ugomvi na rais bali waziri wake! “Hatuna ugomvi wala chuki na Rais Kikwete, tumeshindwa kumwalika katika maadhimisho ya kesho (leo) kwa sababu TUCTA haikutaka baadhi ya viongozi wa serikali wahudhurie katika sherehe zetu. Wao ndio kikwazo cha sisi kutotimiziwa mahitaji yetu.” Alikaririwa Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholaus Mgaya akisema.

Tamko la namna hii ama linalenga kuzidi kumpa kichwa rais ili wafanyakazi wamuumize au ni kupigwa siasa kirahisi ukiachia mbali kujidhalilisha na kujikomba kwa serikali.

Kama tamko hili ni mawazo binafsi ya msemaji aonywe na kuanza kuangaliwa kwa makini kama ni msimamo wa wafanyakazi, basi ni tatizo kubwa tu.

Hii ni ajabu kidogo! Huwezi kumchukia waziri anayeshughulikia wafanyakazi ukampenda aliyemteua na kumbakiza madarakani hata baada ya kuvurunda. Kufanya hivyo ni kujidanganya, danganya, kujenga mazingira kwa rais kukudanganya. Ni kumpa rais sifa asiyostahili.

Kimsingi, serikali ambayo kwa muda mrefu imekandamiza wafanyakazi na kuwanyonya ni ya rais si ya waziri. Wafanyakazi walipaswa kulielewa hili na kulizingatia.

Maana hata huyo waziri hana mamlaka yoyote kufanya lolote bila kuidhinishwa na kikao cha baraza la mawaziri. Hii ni sawa na kupenda boga ukachukia ua lake au kumpenda mama ukamchukia mtoto wakati wote ni wamoja.

Kadhalika kuna dhana nzima ya uwajibikaji wa pamoja kwa serikali katika kila jambo, liwe baya au zuri.

Rais na serikali yake wanaweza kukwepa na kumtumia waziri mhusika katika sehemu nyingine lakini si katika uwajibikaji wa pamoja.

Je, ni kwanini serikali imefikia kushikwa pabaya wakati huu mbaya wa kuelekea uchaguzi? Jibu ni rahisi. Watawala wamezoea kutawala watakavyo wakidhani Watanzania wa sasa ni sawa na wale wa mwaka 47, ambapo hakukuwa na utandawazi na kupanuka kwa haki za kiraia na upinzani.

Ingawa tuko kwenye mfumo wa vyama vingi, serikali imo kwenye usingizi wa chama kimoja! Ni bahati mbaya sana kuwa na utawala wa namna hii.

Mgomo ungefanikiwa ungeweza, kwa mara ya kwanza, kuiwajibisha serikali baada ya upinzani kupoteza nafasi wakati wa kashfa ya Richmond ambapo serikali ilimtoa kafara waziri mkuu ili isianguke.

Kama mgomo huu ungefanikiwa, licha ya kuwa hatua muhimu kuelekea ukombozi kamili wa taifa, ungeweza kuwa ukurasa mpya wa kufikia ukombozi mapema na kwa njia ya kistaarabu na si umwagaji damu.

Sababu nyingine inayoipa kiburi serikali kuwahadaa na kuwadharau wafanyakazi ni ile hali ya kuua upinzani. Hivyo, serikali bado ina mazoea kuwa hakuna awezaye kuitia kashi kashi.

Wafanyakazi walipoteza nafasi adhimu na muhimu. Tunasahau kuwa mapinduzi ya Ufaransa yaliletwa na wafanyakazi. Tunasahau hata historia ya juzi nchini Poland ambako Chama cha wafanyakazi cha Solidarity kikiongozwa na Lech Walesa kilivyoporomosha tawala zandiki kule.

Ni rahisi kuuminya hata kuua upinzani lakini si sauti na mshikamano wa wafanyakazi. Ingawa serikali inaangalia tishio la mgomo kama suala la wafanyakazi na serikali kwa upande mmoja, ukweli ni kwamba ni mtafaruku wa kitaifa.

Kama wafanyakazi wangeacha woga na ujinga wakatimiza azima yao ya kugoma, na wakulima ambao nao ni wafanyakazi tukiondoa majina ya kisiasa, wangejiunga na mgomo ule.

Walaji kadhalika wangekuwa sehemu ya mgomo. Watu kama wanafunzi wasingebaki nyuma. Mgomo ungesimamisha shughuli zote kiasi cha kuathiri maisha ya kila mmoja-wanaopinga na wanaounga mkono mgomo.

Tunajua kuwa waajiri wengi ambao wengi ni wageni hawakuunga mkono mgomo huu kutokana na wao kuwa wanufaika wa unyonyaji wa wafanyakazi. Rejea taarifa kuwa uchumi wa Tanzania unamilikiwa na wageni kwa asilimia 90.

Je, ni kwanini serikali ilifanikiwa kutumia vitisho kuepuka kutofanyika mgomo kwa kutumia ujanja ujanja kama ambayo imekuwa ikifanya?

Wafanyakazi sawa na Watanzania wengine wamedanganywa sana na serikali ya sasa ambayo inasifika kwa matumizi mabaya na kulea ufisadi kutokana na kuwa tunda lake.

Je, tumejifunza nini au kujiandaa kuchukua hatua gani? Hili ndilo swali kuu tunalopaswa kulijibu ili tuweze kujikomboa.

Serikali haiwezi kuendelea kuwaambia wafanyakazi kuwa haina pesa wakati kila siku unaripotiwa ufisadi wa mabilioni ambayo yangeweza kuendesha nchi kwa mwaka mzima bila kuomba au kukopa.

Serikali haiwezi kuendelea kuwaambia wafanyakazi haina pesa wakati ikipandisha mishahara ya wazito kila uchao ukiachia mbali matumizi ya hovyo kama ununuzi wa magari ya bei mbaya, kulipana posho kubwa bila kufanya kitu, ziara za mara kwa mara za watawala ndani na nje na matumizi mengi ya kutia shaka ukiachia mbali kusamehe kodi.

Serikali ya sasa imekuwa ikiwahadaa Watanzania kila mwaka. Yako wapi matunda ya kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya? Iko wapi safari ya Kanaani au ni kwa vile wakubwa walishafika na kuishi huko huku umma wa ukiishi motoni?

Iko wapi mipango na sera zinazoingia akilini ukiachia mbali hizi zinazotumika za kujinufaisha baada ya zile tulizoambiwa ambazo rais mstaafu Benjamin Mkapa alisema hazitekelezeki?

Ajabu CCM bado inategemea sera hizo hizo zisizotekelezeka kuwashawishi wapiga kura waichague! Wakifanya hivyo watakuwa wamejivika kitanzi wenyewe.

Tuwahimize wafanyakazi kuanza kufikiri upya juu ya kugoma wakijua wazi kuwa kufanikiwa kwa mgomo wao ni ukombozi si kwao tu bali taifa zima. Na wajue.

Ndiyo njia ya kistaarabu na kisasa ya kuondosha mfumo fisadi na ovu uliopo ambao unawabinafsisha waajiri yaani serikali na wawekezaji kwa gharama ya wafanyakazi na wakulima wa taifa hili.

Wafanyakazi wakiweka zana chini hata hao wanaojiona wakubwa watamomonyoka kama kipande cha theruji kwa siku moja. Maana hakuna aishie bila kupanda mgongoni mwa wafanyakazi ajue au asijue.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 9, 2010.

No comments: