Thursday, 2 June 2011

Kikwete aende ughaibuni, mawaziri vijijini

Kikwete akibembea na mkewe alipokuwa Jamaica


KATIKA semina elekezi ya hivi karibuni iliyofanyika mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete alikaririwa akiwafokea na kuwaagiza mawaziri waende mikoani kufafanua ‘mafanikio’ ya serikali yake!

Hii si mara ya kwanza kwa Kikwete kufanya semina elekezi isiyoelekeza kitu bali kula pesa ya wananchi. Alianzia kule Ngurdoto 23 – 27 Agosti, 2006. Semina hii ilihusisha wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya.

Kama kawaida yake, Kikwete alitaka aonekane anajua uongozi na kuwajali wananchi. Alitoa maelekezo yafuatayo kwa walengwa wa semina husika:
Alikaririwa na vyombo vya habari akisema: “Nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa kuzingatia kuwa tabia nzuri na mwenendo mwema ni sifa ya msingi ya kiongozi. Ukipungukiwa sifa hiyo unapunguza hadhi yako mbele ya jamii unayoiongoza.”

Wakati akisema haya yeye alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kufanya ziara nyingi hadi baadahi ya wabaya wake kumwita ‘Vasco da Gama wa Afrika.’
Aliendelea: “Tumieni madaraka yenu vizuri, msiyatumie kuonea, kudhulumu, kuomba au kutoa rushwa au kulipiza kisasi.”

Wakati akisema hayo alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuwakingia kifua mafisadi akiwamo mtangulizi wake kutokana na kadhia ya kujimilikisha machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira. Hakupata kukanusha tuhuma hizi.

Kikwete aliendelea: “Zingatieni na kuheshimu sheria za nchi na kanuni zinazotawala utendaji wa serikali. Kama Viongozi tuwe mfano wa kuzingatia hayo. Watumieni sana makatibu tawala wa mikoa na maofisa tawala wawajulishe sheria, kanuni na taratibu.”

Katika hili, bahati mbaya hakujiangalia. Kwani ni wakati huu alikuwa akishutumiwa kumruhusu mkewe kutumia ofisi ya rais kujizolea mabilioni ya fedha kwa kuanzisha NGO yenye kutia shaka kama alivyofanya mke wa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.

Tuko na Kikwete bado. Aliendelea kupiga siasa: “Muwe na mahusiano mazuri na viongozi wenzenu na wananchi mnaowaongoza.”
Wakati akitoa nasaha hizi alisahau kuwa alikuwa akishutumiwa kwa kulea mitandao ya kimasilahi ndani ya chama chake iliyokuwa ikifanya nchi isitawalike kutokana na vita ya ndani kwa ndani ya kugombea ulaji.

Nukta ya tano ya Kikwete alisema, “Muwe wepesi katika kushughulikia matatizo ya wananchi. Muwe kimbilio la wananchi kwa jua na mvua. Muwape nafasi ya kuwasikiliza na kushughulikia matatizo yao.” Maskini Kikwete alisahau kuwa wakati akiwaambia watendaji wake wawe kimbilio la wananchi, yeye alikuwa kimbilio la wawekezaji huku akiwakimbia wananchi kwa kufanya ziara ambazo Profesa Lipumba aliwahi kusema hazikuwa na maslahi kwa taifa.

Katika nukta ya sita, Kikwete alikaririwa akisema: “Jengeni moyo wa kujituma, kufanya kazi bila kuchoka, na kushirikiana na wananchi.

Tufufue moyo wa kujitolea miongoni mwa mwananchi. Yapo mengi yanayoweza kufanywa na wananchi wenyewe bila kusubiri serikali. Kinachotakiwa ni uongozi ambao ni kazi yetu.”

Hapa alisahau pia alisahau kuwa alionywa kutounda serikali kubwa akadharau.

Nukta ya saba Kikwete alisema: “Simamieni halmashauri zenu vizuri.” Hivi wangepata wapi mshipa wa kusimamia halmashauri zao wakati yapo malalamiko kuwa rais hasimamii nchi vizuri?

Nukta ya nane Kikwete alisema: “Kasimamieni vizuri kilimo na hasa Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP)”

Kwanini wao wasimamie kilimo programu za kuendeleza kilimo wakati yeye alikuwa akisimamia programu za kuendekeza uwekezaji kama wa madini ambao leo hauna tija hadi kuibua migogoro kama ile ya Nyamongo?

Nukta ya tisa Kikwete alihimiza: “Hakikisheni kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anakwenda sambamba na kuwa na sekondari kila kata. Aidha maandalizi ya ujenzi wa shule za sekondari yaanze sasa ili kuweza kukabiliana na idadi ya wanafunzi watakaofuzu kuingia kidato cha kwanza mwaka 2008.”
Hapa, rais alisahahu kwamba shule alizozipigia chapuo ziliishia kuwa si shule za kata tu, bali pia shule za kata elimu na kuongeza ujinga!

Kumi Kikwete alisema: “Simamieni kikamilifu utoaji wa huduma za afya na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukimwi.” Hapa sina chakuongeza.

Kumi na moja Kikwete alilonga: “Simamieni kikamilifu ujenzi na utoaji wa huduma za kiuchumi katika mikoa yenu.” Wakati akisema haya, alikuwa akipuuzia malalamiko ya wananchi kutoka mikoa ya Mara, Mwanza na Shinyanga ambako wawekezaji wake walikuwa wakiwabughudhi hata kuwaua wananchi.

Kumi na mbili Kikwete alisema: “Simamieni na hakikisheni suala la hifadhi ya mazingira. Hili jambo ni la kufa na kupona.”
Binafsi najiuliza, mazingira yangehifadhiwa vipi wakati serikali ilikuwa ndiyo imezidisha mgawo na ulanguzi wa umeme, vitu vinavyowalazimisha wananchi kukata miti ili kupata mkaa kufidia pengo la umeme.

Kikwete hakungoja watendaji waende na kutekeleza aliyowatuma. Badala yake aliwamwagia matarajio yake likiwemo hili.

“Tuwe na uhusiano mzuri na vyombo vya habari. Tufanye kazi na vyombo vya habari vitusaidie kufikisha ujumbe wetu kwa watu wengi kwa urahisi na kwa wakati mmoja”. Kazi kwako msomaji kutathmini hayo.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 1, 2011.

3 comments:

Mcharia said...

Hii kweli KALI na inafikirisha. Na na na na DAH!!!.

Jaribu said...

Kikwete huyu ni mpiga domo tu. Hayo yote aliyotamka ameandikiwa, sidhani kama anaelewa anachoongea.

Mzee wa Changamoto said...

Nimeongea na MCHAMBUZI huko Tanzania na kinachoonekana sasa ni KILIO.
Jamaa (ambaye ametoka Canada) anasema kuwa NCHI IMEMSHINDA.
Nami nabaki kusikitika kwa kuwa waumiaji "wameshiba njaa"