The Chant of Savant

Wednesday 18 April 2018

Barua kwa rais Magufuli kutambua mchango wa mzee Ngoma

Naandika waraka huu wa wazi kwa furaha na shukrani mahsusi kumpongeza rais John Pombe Magufuli kwa maono na matendo yake ya mfano na somo kwa taifa. Hivi karibuni, kinyume na mazoea wala matarajio, alimtambua na kumtuza mvumbuzi wa madini ya Tanzanite mzee Jumanne Ngoma baada ya kusahauliwa, kudhulumiwa na kusota kwa zaidi ya miaka 50 huku watu wasiojua lolote wala chochote kuhusiana na madini haya aghali na pekee duniani wakifaidika wakati yeye akisota. Kitendo cha kishujaa na kizalendo cha Magufuli kinaanza kujenga mazoea mapya ambayo hapo awali hayakuwepo chini ya tawala za kibabaishaji na kifisadi. Kwani, kama taifa, tulifikia pabaya. Tulikuwa tukiwaheshimu na kutukuza wezi wakati wachapakazi tukiwakatisha tamaa na kuwaacha wafe kwa kinyongo na majuto. Binafsi, simjui mzee Ngoma; ila kwa hatua ya kimapinduzi aliyochukua rais Magufuli, itakuwa kichocheo na motisha kwa wengine kugundua au kujitokeza na kuonyesha taifa letu lilivyokuwa limegeuka la dhulumat, wasahaulifu na wezi wa fadhila.
Kuna kipindi taifa letu liliteuka la wajinga na wasioona mbali. Rejea mfano wenzetu waliogundua vitu kama bunduki, mabomu hata radio kuishia kusweka ndani badala ya kupelekwa kwenye maeneo husika wakapanue na kuendeleza ujuzi wao kama wanavyofanya kwenye nchi za magharibi. Kuvumbua kitu licha ya kuwa kipaji kwa mhusika, kunatoa mchango mkubwa kwa mhusika na jamii kusonga mbele. Mambo mengi tunayofaidi leo, yaligunduliwa na wahanga kama mzee Ngoma. Tofauti ni kwamba, wenzetu tunaodhani wameendelea, hawakuwapuuzia wavumbuzi wao. Waliwaenzi na kuwathamini ili kutoa motisha kwa wengine badala ya kuwafunga au kuwapuuzia kama ilivyokuwa kwa mzee Ngoma.
Hata hivyo, kama mhanga wa kadhia hii ya kushindwa kutambuliwa wala kuzawadiwa uvumbuzi wala kutambuliwa taaluma na kipaji chake, rais Magufuli alimuona mzee Ngoma na kuelewa hali yake hadi kutoa shilingi 100 kama kianzio cha kutambua mchango wake. Mwandishi wa makala hii ni msomi aliyekwishaandika vitabu vya kitaaluma zaidi ya kumi lakini hakuna anayetambua mchango wake wala kuvitumia kwenye shule na vyuo vyetu. Nadhani huu ni mwanzo mzuri kwa watu wanaotumia akili na vipaji vyao kuneemeka na kuneemesha taifa letu. Kwa vile waliomtangulia rais Magufuli, tokana na kutoona mbali au kutojali, hawakuwahi kuvumbua wala kupitia aliyopitia mzee Ngoma na Magufuli, ilikuwa vigumu kutambua mchango wake na kuuthamini na kuutuza. Pia nichukua fursa hii kumpongeza mwalimu Julius Nyerere aliyemtambua na kusaini nyaraka zilizomwezesha rais Magufuli kumkubali kama mvumbuzi wa kweli wa tanzanite.
Baada ya rais kuonyesha mfano, kama kawaida yake, ukiachia mbali usongo wa kutenda haki, tunapaswa, kama taifa na jamii kujiuliza. Utapata wapi uzalendo bila kuwatambua wanaolenga kuendeleza taifa badala ya kuacha wadandia ulaji wawe ndiyo wenye kuamua nani atambuliwe au kufaidika na jasho lake? Kwa uchungu na uzalendo mkubwa, rais Magufuli aliamua kumtambua, kumtambulisha na kumpa stahiki yake mzee Ngoma. Hili somo na suto kwa wezi wafadhila hasa waliopata madaraka wakayatumia vibaya kwa ubinafsi, uchoyo na upogo wakawasahau wenye haki na wenye shida. Mungu ampe maisha marefu rais Magufuli kwa kufuta machozi yam zee Ngoma. Je wapo akina Ngoma wangapi nchini?
“Leo sisi wote hapa tusingekuwepo kama si mzee huyu.” Kusikia maneno haya, nilitamani ningekuwa na simu ya mheshimiwa rais, ningempigia kumuomba asiishie kwa mzee Ngoma tu. Yeye ni mmojawapo wa wahanga wa kutotambuliwa alipogundua asidi fulani. Kwa vile ni rais, basi ajitambue na kuwatambua wengine kama yeye. Tuligeuzwa taifa la wanafiki, roho ya korosho na wezi wa fadhila kwa kuwatelekeza watu waliochangia pakubwa kwenye maendeleo ya taifa.
Nasema taifa letu liligeuzwa taifa dhulumat. Kwani waliodhulumiwa si Mzee Ngoma na wengine wasiojulikana wala kutambulika bali hata mkoa wa Manyara na Mererani yenyewe. Kwani, hadi rais Magufuli anamuibua na kumfariji mzee Ngoma, alisema kuwa Mererani haikuwa na gari la wagonjwa hadi alipolipeleka mwenyewe. Hapa rais hakusikiliza kilio cha wananchi wa Mererani bali pia ametambua umuhimu wao kama sehemu ya taifa la Tanzania. Wale waliozoea kumzodoa kuwa anatoa huduma kwao Chato sijui kama watakuwa na la kusema. Sijui kama hata barabara za Mererani ni za kisasa ikilinganishwa na maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro na mingine inayosifika kwa huduma safi bila kuwa na mchango mkubwa kwa taifa ikilinganishwa na Mererani.  Hili linanikumbusha mikoa ya Kusini na maeneo mengine muhimu kwa taifa kama vile Kigoma, Sumbawanga na kwingineko ambako watawala wetu waliyazira bila kutoa maelezo wala sababu za kufanya hivyo. Sijui kama Mererani wana maji na umeme wa uhakika kama sehemu nyingine. Sijui kama wana mawasiliano ya uhakika kwa ujumla.
Tumalizie kwa kumhimiza rais Magufuli kuendelea kufuatilia kwa karibu namna anavyotunzwa mzee Ngoma ili kumtendea haki na kutoa motisha kwa wazalendo,wavumbuzi hata wasomi wengine kuvumbua na kuchangia mambo mbali mbali wakijua kuwa kufanya hivyo, hakutakuwa chanzo cha kuteseka wala kusahauliwa. Yupo rais wa wanyonge kama alivyosema mzee Ngoma mwenyewe. Hongera rais Magufuli kumtendea haki yake mzee Ngoma.
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili, 2018.

No comments: