The Chant of Savant

Wednesday 11 April 2018

Kuna haja ya kutoa elimu ya matumizi ya barabara nchini

            Ajali za hivi karibuni nchini na nyingine kabla ya hapo baada ya Tanzania kuondokana na barabara za matope, zinasikitisha japo zina somo kubwa kwa taifa. Tokana na kujirudia kwa ajali zenye kugharimu maisha ya watu wetu wasio na hatia, kuna dalili kuwa, kama taifa, ima tumeshindwa au kukataa kujifunza au hatuna la kufanya. Je inawezekana kuendelea kushuhudia mamia ya watu wakipoteza maisha wakati kuna namna ya kuweza kujenga mfumo na utaratibu wa kukabiliana na janga hili linaloonekana kutokana na maendeleo?
 Kwanza, tunatoa rambirambi zetu kwa wahanga wa ajali za barabarani ambazo hivi karibunizimegharimu maisha ya watu wengi. Pamoja na kwamba kuna msemo wa wahenga kuwa ajali haina kinga, ni wakati ule. Japo hatuwezi, kama taifa, kuondoa ajali kwa ujumla wake, tunao uwezo wa kuzipunguza na kuzizuia baadhi. Leo katika makala hii nitajikita katika nini kifanyike kupunguza au kuondokana na ajali zinazoua watu wetu.
Kabla ya kuzama kwenye nini kifanyike, ni vizuri kukiri na kupongeza juhudi za serikali ya awamu ya tano za kuhakikisha taifa linakuwa na miundombinu bora kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa. Hakuna ubishi. Dhana nzima ya maendeleo inalenga na kujikita kwenye ustawi wa jamii na watu wake. Ndiyo maana serikali ya rais John Magufuli imejikita kwenye ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine nchini. Hata hivyo, pamoja na nia nzuri ya serikali, kuna mapungufu mengi tokana na mfumo na mazoea mabovu ya zamani kabla ya kuwa na barabara za kisasi ambazo tunapaswa kuchunga sikigeuke barabara za kisasi. Mfano mzuri ni wimbi la ajali zilizopoteza maisha ya mamia ya watu wetu kwa sababu tu hawajui kutumia barabara vizuri. Kuna haja ya kubadili mfumo wetu wa utoaji wa leseni za udereva na matumizi mengine ya barabara.  Utashangaa, kwa mfano, kuona mtu anavuka barabara tena kubwa kwenye eneo lisiloruhusiwa. Kimsingi, kufanya hivi ni kujihukumu adhabu ya kifo kirahisi. Je hakuna namna ya kuwaelimisha watanzania namna ya kutumia barabara kisheria na vizuri? Je sheria zetu zinasemaje kuhusu watu wanaovunja sheria za barabarani wawe ni madereva au waenda kwa miguu?  Kwa vile wimbi la ajali limezidi na kwa vile tunajua vyanzo vyake vikuu, kuna haja kuhakikisha wote wanaozivunja wanatungiwa sheria zenye kutoa adhabu kali hasa ya vifungo ili kuwa onyo na somo kwa wengine.
Ngoja nitoe mfano wa nchi ya Kanada niliyo nayo uzoefu juu ya matumizi ya barabara na vyombo vya moto. Ni jambo lisiloingia akilini achia mbali kulitenda chombo cha moto bila kupitia mafunzo ya udereva yanayohusisha sheria na kanuni za utumiaji barabara na vyombo vya moto.
Mbali na mafunzo ya namna ya kutumia barabara na vyombo vya moto yanayochukua si chini ya miezi tisa, kuna eneo jingine ambalo taifa hili lilolendelea na lenye barabara nyingi kuliko idadi ya wakati wake. Sheria za Kanada zinatoa adhabu kali kwa makosa yanayohusiana na matumizi mabaya ya barabara na vyombo vya moto. Kwa mfano, mtu akipatikana na hatia ya kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa, hata kama hajasababisha ajali, hufungiwa leseni yake kwa muda kulingana na kosa na historia yake ya matumizi ya barabara na vyombo vya moto. Pia mamlaka za bima hupandisha bima ya mhusika ukiachia mbali wengine kulazimika kulipia leseni zao za udereva kwa bei mbaya sana. Mfano, kwenye jimbo ninamoishi, bei ya leseni ya udereva ni dola 40 kuanzia. Bei hushuka kila mwaka au kupanda kulingana na namna dereva anavyoendesha. Wale waliohusika kwenye ajali nyingi bila kufungiwam, hujikuta wakilipia leseni hii hii hata kwa dola 1,000 kwa mwaka. Mbali na hili, wakanada wana utamaduni wa kuripotiana wanapogundua kuwa mtu anaendesha vibaya gari. Wanafanya hivyo kwa kujua kuwa kuendesha gari kwa namna isiyokubalika ni kuweka maisha ya madereva hata waenda kwa miguu na wanyama hatarini.
Hatua nyingine iliyoweka kuhakikisha inapambana matumizi mabaya ya barabara ni kuweka kamera kwenye maeneo mbali mbali. Kanada ni moja ya mataifa yanayotumia kamera kwa ulinzi wa aina mbali kuanzia wa barabarani, madukani hata kwenye maeneo ya umma.
Sambamba na hatua tajwa hapo juu, Kanada hutoa elimu ya matumizi ya barabarani kila mara kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, matangazo ya barabarani.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Kanada ni kuhakikisha barabara zinawekewa alama za barabarani na zinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili kuepuka kuharibika na kutengeneza maeneo korofi.
Eneo jingine lililoshughulikiwa ni kufanya upakiaji mizigo au watu kwenye magari kosa la jinai lenye adhabu kali. Hata kama ni gari binafsi, huruhusiwi kupakia gari zaidi ya uwezo ulioelekezwa kwenye manua ya gari.
Mwisho, adhabu zitokanazo na makosa ya barabarani ni kubwa kweli. Mfano, hapa ninapoishi, ukikatiza kwenye taa za barabarani, unatumia tiketi ya si chini dola 200.
Hivyo, nashauri mamlaka zetu zianze kuangalia namna ya kutumia elimu, sheria, teknolojia na tabia za jamii kupambana na ajali za barabarani.
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 11, 2018.

No comments: