The Chant of Savant

Wednesday 4 April 2018

Waraka wa Profesa Emeritus Mpayukaji kwa masadukayo


Baada ya kuona kila masadukayo wanakuja na nyaraka kwa wachovu kila wakijisikia na wakidhani mambo yanakwenda ndivyo sivyo, nami profesa emeritus mtumishi wa Mungu aliye juu ya miungu yote ya kigeni nakuja na waraka wangu kwa masadukayo. Kama ilivyo haki kwa masadukayo kuja na nyaraka zao kwa umma, naona ni haki kwangu pia kufanya hivyo. Tofauti na nyaraka za masadukayo, huu waraka ni tofauti na nyaraka nyingine ambazo wachovu wamezoea. Kwani, waraka huyu si wangu bali ni maneno ya mwenye dunia mwenyewe ambaye wengi humtumia kujipatia ulaji na ujiko kirahisi tofauti na mimi ambaye ndiye kinywa chake pekee kilichobakia. Hivyo, wewe unayeusoma, ujue unaongea na Mungu moja kwa moja. Hii ni bahati yako na utapata baraka tele kwa kusoma na kutafakari waraka huu mtakatifu usio na uroho mtakakitu bali roho mtakatifu na mtukufu. Kama utaupuuzia waraka huu, laana zake mwenyewe mwenye kutisha zitakuandama hadi utakapokuja kwangu kutubu kabla mengine mengi na zahama havijakukuta. Mimi si askopo wala mtume wa kujipachika. Wala si mchunaji wala mchungaji bali msemahovyo lakini kweli tupu unabii niliorithi toka kwa mzee Waambie mwana wa Wapasha bila woga wala kutafuna maneno.
Kwanza, nitamke wazi wazi. Kaya hii si mali ya mja yoyote isipokuwa wachovu wote kwa umoja wao. Hivyo, hakuna mwenye stahiki ya kumburuza wala kumTunduLissu mwenzake.
Kabla ya kumwaga ujumbe wa mwenyewe, naanza kwa maswali: Je wao wanafanya yale wanayotaka lisirikali lifanye kama vile kuwa na demokrasia kwa kondoo wao wanaoburuza na kuwachuna kila uchao huku wao wakiishi maisha ya kutanua wakati wanayedai kumhuribiri alikuwa kapuku wa kunuka hadi akashindwa hata ndururu ya kumpa Kaisari hadi samaki alipompa taafu?
Je wako tayari lisirikali kuingilia anga zao na kuwataka wafanye kama lionavyo? Je muda wote walikuwa wapi hasa wakati ule kaya yetu ilipogeuzwa shamba la bibi na akina Mzee Ruxa, Njaa Kaya na Denjamani Makapi?
Aliyejuu anaonya kuwa, ukimuelekezea mwenzako kidole jua vitatu vinakuelekea wewe. Kwa kulijua hili, nachelea kuhukumu wala kushinikiza ili nisijegeuziwa kibao siku moja.  Kwanini inakuwa rahisi kuona maovu ya wenzao wakati yao wakiyalimbika kana kwamba wachovu hawaoni wala kujua wanavyotanua kwa zaka na mapato ya makapuku?  Je kwanini leo si zama zile za utwahuti wa wazi kimfumo na kitaasisi hadi kaya inapata jembe la kuikomboa hata kama ni kwa kuminya baadhi ya haki jambo ambalo halikubaliki? Wakati wachovu wakiuzwa na kubinafsishwa kishenzi mbona hawakutoa waraka? Je ni kwanini hawakutoa waraka baada ya kuibuka tuhuma dhidi ya wenzao wanaotuhumiwa kubaka na kulawiti ukiachia mbali waliojipatia ukwasi kwa kuwahadaa na kuwaibia wajinga wetu maskini kwa kuwaahidi miuya wakati miuya yenyewe ni kuwaibia? Nangoja majibu si majipu tena yanayoingia kichwani.
Tokana na wengi kukwazwa na kuudhiwa na mambo ambavyo yanakwenda ndiyo siyo, nawashauri, ili waeleke wako upande gani, basi waanzishe chama cha siasa lau tuwajue kuwa ni wanasiasa. Usawa huu ni wa uwazi wa kweli na ukweli wa ukweli unaomtaka kila mmoja wetu asimame hadharani na kuonyesha upande anaolalia. Kwani, haiwezekani kutumikia mabwana wawili yaani aliyeko juu na hawa walioko chini. Lazima mhusika aamue kufanya maamuzi magumu. Kwani si vizuri kutumia majukwaa ya kiroho kufanya mambo ya kisiasa wala kutumia majukwaa ya kisiasa kufanya mambo ya kiroho. Huu ni uroho tena uliopindukia. Kwani Bwana mkubwa mwana wa Maria alisema kuwa kabla hujatoa boriti jichoni mwangu, ni vizuri kutoa kibanzi kilichoko jichoni mwako au siyo?
Nilimsikia mmoja akisema kuwa wao kufanya siasa kumekuwapo tangu yapata miaka 2,000. Je siasa hazikuwapo pia? Kama anataka kujua ni namna gani zilikuwepo siasa kabla ya hata roho mtakakitu, ajiulize akina Farao kule Masri walikuwa wakifanya nini? Si walikuwapo kabla ya hao wanaojifanya wana kila sababu ya kupiga kelele?
Nikigeuka upande wa pili, jamani, tufike mahali tuache kuburuzana, kutishana wala kunyotoana roho ukiachia mbali kusakiziana kesi feki.  Huku nako ni kughshi haki sawa na wale wanaoghushi sifa za kitaaluma na kiroho kama masadukayo wa kujipachika hadi wengine wanapayuka kuwa wana mchele kuliko lisirikali. Anayedhani amesimama achunge asianguke. Mamlaka na ulaji ni kama maua kwenye shamba. Huwa na msimu wake na ukiisha hunyauka. Nani mara hii kamsahau Tunituni Makapi aliyefanya kila makufuru na kuwaita wachovu kuwa wana uvivu wa kufikiri wakati yeye alikuwa ndiye mwalimu na kiongozi wao katika uvivu huu uliogeuza kaya shamba la bibi huku bibi mkubwa akimtumia bwana mkubwa kupiga njuluku. Wako wapi kwa sasa zaidi ya kutegemea hisani tena ya vijana wadogo?

Ndugu zanguni, nimalizie kwa kuwaasa muwe na busara katika mapito yenu. Kwani kila lenye mwanzo huwa na mwisho. Na wote tuliopo chini ya jua si chochote wala lolote bali wasafiri waendako wasikokujua. Mamlaka, nguvu na utajiri vina thamani gani iwapo tufapo kila mtu huondoka na shuka moja? Mwenye akili na azingatie unabii huu kwa wote.
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano, April4, 2018.

No comments: