The Chant of Savant

Tuesday 2 February 2021

Kituko cha Dk Godwin Mollel kwa Wezi wa Madawa Kitufumbue Macho


Pamoja na kuishi mbali na nyumbani, huwa napata habari na taarifa nyingi za nyumbani karibu kila siku. Hii ni kutokana na kuwepo mtandao ambapo watu hupashana habari ambazo zamani zingeweza kufichuliwa na waandishi wa habari tu. Ndiyo maana mtu kama mimi anayeishi kilometa maelfu na naweza kupata taarifa kama hizi na kuzifanyia kazi. Mojawapo ya taarifa nilizopata hivi karibuni ni zile zinazohusiana na mkutano wa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Molell alipokuwa akizungumza na watendaji mbali mbali hivi karibuni. Naibu Waziri aliwaambia watumishi husika kuwa anajua uoza wao mwingi kubwa ukiwa ni wiza wa madawa hospitalini. Pamoja na kadhia hii kuwa donda ndugu kwa taifa na watu wake, waziri husika alionekana kuwasaidia wahusika kwa kutoa onyo kuwa anajua mengi kuhusiana na kadhia hii bila kuchukua hatua ambazo kiongozi au mtu yeyote anayekerwa na kadhia hii angechukua. Mfano, Waziri alisikika kwenye clip yenye kiunganishi (https://www.youtube.com/watch? v=ZRV0SqMZxe4) iliyozagaa kwenye mitandao akisema “mfamasia, tunaibiana dawa. Hakya Mungu tunaibiana dawa. Hakya Mungu tunaibiana dawa. Tunaibiana? Dawa. Dawa Mount Meru kiwango kinachonunuliwa siyo kiwango kinachoingia. Sawa brother.” Mhusika alijibu “sawa” huku ukumbi mzima ukicheka kana kwamba jambo husika ni la kufurahisha wakati linawaathiri watu wetu wengi!
Katika kuonyesha kuwa anajua kila kitu ila––kwa makusudi mazima––hataki kuchukua hatua tokana na sababu anazojua mwenyewe, Naibu Waziri anakaririwa kwenye clip akisema “Hoya, jamaa yangu, nilete ushahidi nisilete?” Mmojawapo wa maofisa husika––huku akitabasamu––alijibu “leo usilete.” Hii maana yake nini? Sijui kama rais John Magufuli atapata clip hii atamuacha mhusika aendelee kucheza makidamakida na wizi huu ambao umegeuka donda ndugu. Kinachoumiza san ana kukera ni ile ya kuwa mhusika anawajua wezi wote na mitandao yao kama anavyosema kwenye clip husika. Kama kweli anawajua watuhumiwa na mchezo mzima bila kufaidika na kadhia hii au kuzembea, ni nini kilimfanya asiwachukulie hatua na badala yake awaonye au tuseme kuwastua? Je kiongozi wa namna hii anajua majukumu yake? Je ni mzalendo kweli anayefaa kuwa kwenye wadhifa husika?
Kwa mtanzania yeyote anayechukia uoza mbali na kuathiriwa nao, hakufurahishwa na alichofanya kiongozi huyu ambaye tena ni daktari kitaaluma. Kwa wanaojua kasi na spirit ya Dk Magufuli, alichofanya mtendaji huyu, licha ya kuweka wadhifa wake rehani, ni ushahidi tosha kuwa hajaelewa somo la rais wake. Pamoja na kwamba kusema ni dhahabu, wakati mwingine, kunyamaza ni almas. Hapakuwa na haja ya Naibu Waziri kujichafua na kuchafua sifa ya yule aliyemteua kwa kuchekelea wizi huu huku akitoa maonyo yasiyo na mashiko. Kimsingi, alipaswa kutumbua kama anavyofanya bosi wake ili wale wanaoendekeza uroho na upogo wapate onyo  mbali na kuwajibika kwa madhambi yao. 
Kwa wanaojua namna udokozi na wizi wa mali za umma ulivyolikwamisha taifa na kulirudisha umma, hawaoni faida ya kuwa na viongozi kama hawa wasiojua ni wakati gani kuchukua hatua hata pale wanapokuwa na ushahidi wa kutosha kama alivyobainisha mhusika. Molell aliwaonya watendaji kuwa mambo ya zamani sasa mwisho wakati kitendo alichofanya ni kile kile cha yale aliyotaka yafikie mwisho. Zama na kuonyana, kutishana au kuhamishana mtu anapoboronga ni mambo ya kizamani hasa wakati huu wa zama za serikali ya awamu ya tano ilijitofautisha na watangulizi wake kwa kuweka vitendo mbele na maneno nyuma. 
Naamini kuwa mhusika atakapopata salamu hizi toka makala hii, ama atatoa jibu ni kwanini hakuchukua hatua au kujitumbua pasina kungoja kutumbuliwa. Huu ndiyo uzuri wa kuwa na mawasiliano ya kisasa ambapo ni rahisi kufichua maovu.  Pia hili liwe onyo kwa watendaji wengine kuwa kufanya kazi kwa mazoea, kujuana, kulindana na kustuana umekwisha zamani. Nitashangaa kama mhusika ataendelea na wadhifa wake wakati, kwa kuwastua wahusika na kuacha kuwashughulikia wakati ana taarifa zote, naye amekuwa sehemu ya hujuma husika aliyotaka kuikemea akashindwa kwa kuwastua wahusika. Tufikie mahali tubadilike. Alichofanya mhusika kingefanyika nchi za magharibi, angetakiwa kujiuzulu siku hiyo hiyo akingoja kuwajibishwa kwa kuhusika na hujuma husika. Kwani alichofanya mhusika ni sawa na polisi kupewa taarifa ya uhalifu halafu akaenda kuwastua watuhumiwa badala ya kuwakamata.  Je hawa watoaji taarifa wetu (whistleblowers) waliomwezesha Naibu Waziri kupata taarifa nyeti kama hizi asizifanyie kazi watamwamini tena? Je watakuwa na motisha na mwamko wa kutoa taarifa nyeti na za hatari kwa kazi na maisha zao tena? Je kiongozi kama huyu–––licha ya kuhatarisha maisha  ya watoa taarifa na taarifa husika–––haoni kama analala kwenye usukani kiasi cha kuishiwa sifa na udhu wa kuwa na wadhifa husika? Maswali ni mengi kuliko majibu. Ila inasikitisha na kukatisha tamaa. Kwani wale wanaopaswa kuwa majemadari wa vita dhidi ya ubadhilifu wa mali za umma wanaishia kuwa washirika wa watuhumiwa ima kwa kujua au kutojua. Je mhusika alipotoa onyo hili hakujua kuwa alikuwa akirekodiwa au kukiuka kanuni za kiapo chake ambacho kinamtaka asifanye kazi kwa upendeleo wala huba au kushindwa kutumia uwezo wake wote kutenda haki? Kwa waziri ambaye amefikia ngazi ya udaktari tena wa binadamu, hili linampunguzia sifa na kuichafua ofisi na hadhi yake kitaaluma. 
Tumalize kwa kumuonya waziri na wengine wenye tabia kama zake kuwa alichofanya si haki kwake binafsi na wadhifa wake na wananchi ambao ni wahanga wa mchezo aliokuwa akikemea kwa kuwastua wahusika. Swali ambalo tungependa waziri alijibu ni kwanini waziri hakuchukua hatua ilhali alikuwa na ushahidi kama anavyokiri kwa kauli yake mwenyewe? Je ni wangapi wataumia kutokana na kauli na staili yake ya utendaji? Je mamlaka zinazohusika zitamwacha ilhali amedhihirisha wazi anavyopwaya? Daktari Molell, tafadhali, tusaidie kueleza umma ni kwanini ulichukua msimamo uliochukua badala yah atua wakati ulishapewa taarifa zote za uhali ilhali ukijua kuwa ni jukumu la mtanzania yeyote–––awe kiongozi au mwongozwa–––kuripoti kwa vyombo husika. Je kwanini hukutoa taarifa husika kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU)? Je unajua madhara ya msimamo wako? 
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: