The Chant of Savant

Wednesday 24 February 2021

Pongezi Takukuru Kuchunguza Taasisi za Kidini


Tangu wakoloni waingize dini za kigeni kama nyenzo fichi za kuchunguza, kupumbaza watu wetu na kurahisisha ukoloni barani Afrika,  walizipa upendeleo katika uendeshaji wake kutokana na ukweli kuwa zilikuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha ukoloni kwa kuwapeleleza watu wetu na kuwaripoti kwenye mamlaka za kikoloni.  Dini husika, kwa mfano, ziliruhusiwa kutukana na kuharibu mila za kiafrika kwa kuziita za kishetani hata kama zenyewe zina ushetani ambao waswahili, pamoja na kusingiziwa ushetni, hawakuwahi kuufanya. Rejea, kwa mfano, kisa cha Sodoma na Gomora. Waswahili, hata wanyama wao, hawakuwahi kutenda unyama na uhayawani huu ambao kwa sasa baadhi ya mashetani wanauita haki za binadamu. Hivi kama miaka zaidi ya 5,000 iliyopita kuna jamii za watu ziliweza kuharibikiwa hadi kugeuzana, kuna la kujifunza toka kwa imani, jamii na tamaduni kama hizi? Mbali na kurahisha ukoloni, dini zilitumika kuwanyonya, kuwadanganya na kuwagawanya watu wetu kuwa wapiganie ufalme wa mbinguni na kuacha mambo ya dunia kana kwamba walikuwa wanaishi mbinguni. Hii yote ililenga kuwapumbaza wapuuzie ukoloni kwa imani kuwa maisha yao hayako hapa duniani bali mbinguni jambo ambalo ni ndoto ya mchana.
            Kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), hivi karibuni, kuanza kupanua wigo wake wa kuchunguza kadhia ya rushwa na wizi wa aina nyingine kwa visingizio mbali mbali ni cha kupigiwa mfano na kupewa shime. Hivi karibuni TAKUKURU ilikubali kufanyia kazi malalamiko ya baadhi ya waumini wa dhehebu fulani walioamini wakubwa wao walikuwa wakifuja mali yao. Kwa mara ya kwanza, Watanzania wameamka na kuwa wamilki wa taasisi za kidini badala ya kuwaachia wezi wachache, ima waliozianzisha au kuziongoza, kuzitumia kuwaibia na kufuja fedha zitokanazo nao kama ilivyozoeleka. Kabla ya hili, wiki zilizopita tulishauri serikali kuchunguza wafanyakazi wa sehemu zenye fedha kubwa. Tulisahau kuongeza na taasisi za dini ambazo–––licha ya kusamehewa kulipa kodi–––huwa zinaingiza fedha nyingi bila kufanya lolote isipokuwa kutoa ahadi za pepo na mambo mengine.
        Wasichunguzwe kwa rushwa tu bali hata kipato, lifestyle audit, watangaza mapato na matumizi ya taasisi zao na wao binafsi. Kwani, si ajabu tena kuona viongozi wa baadhi ya madhehebu–––waliogeuza madhehebu yao biashara binafsi–––wakitajirika bila kujulikana chanzo au vyanzo vingine zaidi ya taasisi zao. Wanaishi kwenye majumba makubwa na kuendesha magari makubwa kuliko hata wakurugenzi wa baadhi ya biashara. Je hiyo fedha wanaipata wapi? Tumeona kwenye nchi nyingine zinazosifika kwa ubadhilifu watu kama hawa wakimilki hata ndege bila kuulizwa wamezipata kwa biashara gani.
        Kimsingi, wenye kumiliki mali nyingi zisizo na maelezo huku nyingi ya mali hizo ikidhaniwa kutokana na kuwakamua watu wetu wengi wanaodhani wanamtolea Mungu, si wachungaji bali wachunaji wa kondoo. Hata Yesu au Mohamad wanaowahubiri hawakuwa matajiri. Wangekuwaje matajiri wakati walikuwa na kazi moja, yaani kuwasaidia maskini waliowazunguka? Wangekuwaje maatajiri, tena wa kunyonya maskini, wakati walihubiri na kuishi walichohubiri na kuhubiri walichoishi tofauti na wakubwa wetu wengi wa dini siku hizi? Lazima tuwachunguze, kuwatoza kodi na kuwahakiki kila mara. Mali bila daftari huharibika bila kujua. Tunapaswa tujue wanapata kiasi gani. Na kama watanzania wengine, kila kipato kitozwe kodi. Haiwezekani tukatoza kodi kipato cha watu wenye mishahara kidogo lakini muhimu katika jamii lakini tukaacha taasisi za dini–––pamoja na ukwasi wote–––zikaendelea kutolipa kodi wakati zinawanufaisha watu binafsi kwa jina la Mungu. Mungu si maskini kiasi hicho. Hali wala hanywi na hatumii hizo fedha zinazopatikana. Ni sheria za kikoloni zilizoanzisha uchochoro huu wa kufanya taifa maskini huku wachache wakitumia kutajirika. Wakoloni walikuwa na kila sababu ya kuziacha taasisi za dini bila kulipa kodi kwa vile zilikuwa mawakala wao waliofanikisha ukoloni kuenea kirahisi katika Afrika. Siku zote fisi na simba huwinda na kula pamoja. Katika mchezo huu, kondoo na mbuzi hawana lao.
        Tokana na dini kuwa kichocheo na kichochoro cha utajiri wa haraka tena usiolipiwa kodi wala kuhitaji kuusotea baada ya kusota darasani, kumekuwa na ongezeko la dini mpya. Kila anayetaka kutajirika haraka, hana haja ya kufungua duka au biashara nyingine zaidi ya taasisi ya kidini. Nani apoteze muda kufungua duka au biashara nyingine wakati zinabanwa kulipa kodi wakati kuna biashara ambayo mhusika huchuma bila kulipa kodi? Kwa wale wanaoshangaa kuona kuongezeka kwa utitiri wa taasisi za kidini sasa wana jibu.
        Kimsingi, taasisi za kidini, zaidi ya kuwa nyingi kuliko hata vyama vya kisiasa, nyingi, kama vyama vya kisiasa zinafanya shughuli ile ile. Kama serikali za kiafrika zitaamua kuzika sheria na tabia za kikoloni zinazoruhusu taasisi za kidini kufanya biashara bila kulipa kodi na kuamua kuzitoza kodi, zitatoweka siku moja.
Mwisho, mbali na TAKUKURU na mamlaka nyingine za kiserikali kutupia jicho taasisi za kidini, kuna haja ya bunge kutunga sheria inayoruhusu raia yoyote kufungua kesi au kuomba taasisi yeyote ya kidini kuchunguzwa anapohisi kuna ubadhilifu. Na kubwa katika yote, ni kuhakikisha tuna sheria zinazowataka watanzania, bila kujali vyeo au taasisi watokazo, kutaja mali na kujaza taarifa za mali zao kila mwaka ili kuepuka kuendelea kutumika kama shamba la bibi ambapo wachunaji wachache na mapatapeli hutumia udhaifu wa sheria zetu kuhujumu taifa na kuwaibia watu wetu wengi wakiwa wajinga maskini waliokata tamaa wanaoweza kuamini kwenye kila upuuzi kutatua matatizo yao.
Chanzo: Raia Mwema.

No comments: