The Chant of Savant

Wednesday 6 March 2024

Mgao wa Umeme ni Uhujumu Uchumi, Haki

Doktari Okot, sorry, N’Dotto Meshaka Bitek’o salama fyatu wangu? Kwanza, nikushukuru kupenda kusoma vitu vyangu. Nilifurahi nilipojua kuwa nawe ni fyatu wangu. Tuyaache. Juzi nilikusikia ukitoa kali. Uliahidi kuwa mgao donda ndugu wa umeme utaisha baada ya siku 18 kuanzia Jumamosi 24 Februari. Hivyo, kama unamaanisha na si kuwafyatua mafyatu, ifikapo tarehe 13 Machi uitangazie dunia miujiza ambayo liiyotenda kaya tena bila kuombewa na wachunaji.
    Tokana na uzoefu wa siasa za ahadi, utapeli, rongorongo, na kupeana matumaini yasiyokuwepo, kwanza, ngoja nikufyatue maswali. Je ulimaanisha kweli au ni ngonjera za kibashiti, kisanii, na kisiasa za kuwafyatua na kuwapumbaza mafyatu mkiwemo nyinyi? Je ifikapo tarehe hiyo na mgao ukaendelea kung’ata kama kawa, mafyatu wakufanyeje wewe hata lisrikal lenu? Je unajua maana ya jambo kuwa historia? Au ulimaanisha kuwa ukweli utakuwa historia lakini si migao kama ilivyozoeleka kayani? Ngoja nichomekee, mbona umeshindwa upigaji wa akina Riz One kule Mirirani? Utatenda miujiza gani kutatua dude kubwa lenye wapigaji wengi na akina Riz One wengi au ni yale kama ya Kawe na Gwaijimmy na kuigeuza majuu wasijue walifyatuliwa?
       Nakupa ushauri bure. Ukitaka kuondoa mgao uwe historia, kwanza, mwajibishe waziri anayehusika hata kama ni kujiwajibisha mwenyewe maana amechemsha. Waziri wa nishati anapaswa kuwajibishwa hata mgao ukiisha, maana ulipaswa uishe wakati wa Adamu na Eva. Mgao ni uhujumu wa uchumi na haki za binadamu kwa mafyatu. Ni shughuli ngapi zinakwama na kwa muda gani na kusababisha hasara, mateso, na usumbufu? Japo hamkubali ukweli, hatupaswi kuwa na migao na kuzidiwa na vijikaya visivyo na vyanzo wala raslimali. Yote ni matokeo na ushahidi kuwa tuna uhaba wa wanene wabunifu, wenye common sense, wazalendo, na wanaofaa. Tatizo si vyanzo vya umeme. Nakumbuka. Mwaka 2012, Njaa Kaya yule ambaye lisrikal lake lilitupiga kutumia Richmonduli alitufunga kamba kuwa mgao ungekuwa historia wakati wa ubazazi wake. Hadi anatokomee, ndiyo ulikuwa unauma zaidi.
        Njaakaya alitufyatua kwa kudaganya kuwa tungejitosheleza kwa kutumia umeme wa gesi asilia utadhani gesi hiyo yetu. Hamjui kuwa gesi, sawa na madini, viko kwetu lakini siyo vyetu bali vya wachukuaji waitwao wawekezaji wanaokula na wanene? Kama siyo hivyo, gesi yetu inakwenda wapi na inamnufaisha nani?
        Pili, muweni wakweli au realistic kwa kinyasa mtoapo ahadi. Mnapochemsha, mjifyatue siyo kungoja mafyatu wawafyatue au maza ambaye sijui kama ana udhu wa kumfyatua yeyote katika hili. Wako wapi akina Janu’wali Makambale waliopiga wakazawadiwa ulaji zaidi wapige zaidi?
        Tatu, mgao utaondoka kama mafyatu watagoma kulipa kodi, kuandamana, na kuhakikisha wanene mizigo na magamba wanapigwa chini ili kuwaamsha nyinyi mliolala mchape kazi badala ya kuchapa siasa kama akina Bashite. Lazima mafyatu washike usukani na kuonyesha hii kaya ni mali yao na si mali ya wanene uchwara/wachukuaji wanaowafyatua tena kitoto.
        Nne, piga marufuku biashara ya majenereta. Yanasababisha mafyatu waridhike badili ya makali ya migao kuwatafuna na kuwafyatua nao wakafyatuka na kuwafyatua nyinyi mnaowafyatua kwa maigizo, ngojera, na ahadi za urongo. Pia, majenereta yanasababisha uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele na moshi ukiachia mbali usumbufu magonjwa ya akili na moyo yatokanayo na mikelele. Mmefanya kaya iwe ya machizi kwa mikelele kila sehemu. Ajabu hamstuki. Mnaendelea kusifiana na kupongezana!
         Tano, tafuteni chanzo cha matatizo ya umeme. Je nyinyi kama sirkal, huwa mnalipa ankara zenu kila mwezi au mnatumia bure na kuendelea kuinyonga Tanesko inayobebeshwa lawama mnapofyatua? Kama Tanesko inafanya biashara isiyo kichaa, kwanini ishindwe kujipanua na kupanua huduma na shughuli zake? Hamlijui hili hata madoktari kama kweli ni madoktari wa kweli? Hamjui kaya yetu inawalangua mafyatu umeme na litanesko linazidi kufa?
         Sita, tunzeni mazingira hasa vyanzo vya maji, panda miti, punguza/ondoa matumizi ya mkaa, kuweni wabunifu muendeleze nishati mbadala mfano umeme wa upepo, themo, gesi, na madude mengine.
          Saba, pambana na ufisi na ufisadi vinavyosababisha kuingiza wapigaji mnaowaita wawekezaji. Ukiangalia historia ya miradi ya uwekezaji kwenye nishati na madini, ni upigaji mtupu. Tunaonekana kama vile mataahira tusiojua faida wala thamani ya mali tunazochezea kwa ukumbaff wa wanene wachache waroho. Hivi yule singasinga Habinger Singa Setii wa IpTiL aliishia wapi au mmeishamtema na kumrudisha kwao atanue au yumo mitaani kama Shavda aliyetupiga akishirikiana na wanene waliomrudisha na kumficha Masaki kwa miaka?
          Nane, kwa vile wewe hupenda kujionyesha kama fyatu serious, nashauri bila kupepesa macho. Kama umeme hautageuka historia, jiandae wewe na lisrikal lako kufyatuliwa na kugeuka historia. Kama mafyatu wataufyata wakashindwa kuwafyatua, namuomba Mungu awafyatue lau mtieni akili na mjue kusema uongo ni dhambi na kosa.
          Mwisho, nawashauri mafyatu wasikubali kuwa wasikilizaji na wapumbazwaji. Kwa vile mnene kajiingiza mwenyewe kwa kutoa ahadi ya kugeuza mgao historia, hakikisha mnamfyatua ageuke historia hata lisrikal lake kama watashindwa kugeuza mgao historia kama walivyozoea. Ifikie mahali mafyatu tuwe serious ili watuchukulie seriously.
        Amini nawambieni mgao ukigeuka historia lazima tutafute maana halisi ya neno historia.
Hivi umeme utarudishwa saa ngapi leo?
Chanzo: Mwananchi wiki jana.

No comments: