Thursday 9 May 2024

Mafyatu Wanataka Muungano si Mgongano

Juzi Tunda Lishe alilikoroga. Si alihoji mantiki ya Zenj kuua Tanganyika hata kutaka wadanganyika wawe na pasipoti kuingia Zenj. Baada ya kukinukisha, si kiliuma. Machawa na mazwazwa wajikombao wapate shibe si walilidhalilisha hata Bungo! 
        Alianza aliyetaka eti wadanganyika waingie Zenj kwa pasi ilhali wazenj waingie na kuishi bara kibwerere na watakavyo. Tunda alihoji mantiki ya wazenj kumilki ardhi Danganyika ilhali wadanganyika wasimilki ardhi, na uraia pacha japo hakuuita hivyo (wazenj wana uzenj lakini wadanganyika hawana udanganyika). Bila aibu, tunaambwa Tanzia hairuhusu uraia pacha. Iweje wazenj wana vitambulisho vya uraia tena wao na si wetu tunaodai unatokana na muungano huu mgongano? Nani anamtawala nani hapa?
            Lishe alipomwaga upupu, walizuka mazwazwa wanaojifanya kum’penda’ na kumtetea mama asiwakatishe kuramba asali kama alivyowahi kudai Mgoshi Makambaa. Walibwabwaja na kubwata wakitaka Tunda, CHAKUDEMA watengwe, wakaripiwe, hata kulaaniwa. Je kuna mantiki gani kuwachukia wanaosema ukweli? Najua sensitivity (unyeti) ya ninachoandika. Nitafyatua kama ifuatavyo kiuchache kifyatu:
            Mosi, kinachoitwa muungano si muungano bali mgongano hata mnyonyano tukizingatia ubaguzi katika kuuendesha. Iweje Zenj ambayo ni ndogo kuliko mikoa yote bara iwe na rahis badala ya mkuu wa nkoa, sirkal, na taasisi zake huru halafu tuzugane kuwa tumeungana? Muungano wa kweli ni kama ndoa. Wawili wauingiao lazima wawe na haki na stahiki sawa bila kunyonyana, kugongana, kutobozana, kutishana, na kuchukiana.  Hivi ni kosa kusema kuwa muungano wetu mgongano uliua Danganyika japo ulishindwa kuizika?
            Pili, mafyatu tunapaswa kufyatuka. Tuhoji tujue ukweli ili haki itendeke. Haiwezekani tujione tuko sawa ilhali wenzetu wana uraia pacha nasi tunao mmoja tu. Mbali uraia na urahis, tukiwa wakweli, unaweza kulinganisha uzalishaji kiuchumi na uchangiaji wa pande mbili za mgongano? 
        Zenj ina ukubwa wa eneo wa kilometa za mraba 2,462. Danganyika ina kilometa za mraba 944,841. Kwa hesabu za ngumbaru, Zenj inaingia kwa Danganyika mara 383.769694314. Hii maana yake nini? Kama tutatenda haki ikatendeka, kila fedha inayomilkiwa na Tanzia, Zenj ikipewa shilingi  moja, Danganyika ipewe 384. Kama ingekuwa kampuni, Zenj ikiwa na hisa moja, Danganyika inakuwa nazo 384. Haya ni mahesabu rahisi yaliyowapiga chenga walioasisi hiki kiini cha mgongano. Na huu ni ukweli hata kama mchungu.
            Tatu, tukubaliane kutokubaliana tuweze kukubaliana kwa busara kuwa muungano si muungano bali mgongano au chanzo cha migongano isiyoisha hadi tunaanza kutaka mafyatu wa bara wabebeshwe pasi za kusafiri kwenda Zenj. 
        Tukifanya hivyo, wadanganyika watakuwa na tofauti gani na wakenya, waganda, na wengine? Tofauti, hawa wengine hawatumii njuluku zao kuwagharimia na kuwastarehesha wengine wakati wao wakiumia kwa kujiumiza tokana na huu mgongano.                 Kwa wasiojua mantiki yake, wajue, tuliunganishwa na wamarekani kuepuka Zenj kuwa Kyuba ya Afrika. Liliandika Jarida la the New York Time (Machi 28, 1964, uk 18) “like Cuba, Zanzibar now turns steadily eastward for inspiration. Washington prays that President Karume, a stubborn if not impressively intelligent man, will emulate such nonaligned leaders as Tanganyika's Nyerere. But Karume is almost surely Zanzibar's Kerensky
        Tafsiri, Kama Kyuba, sasa Zanzibar, kwa kujiamini, imeelekea mashariki kwa ajili msukumo, Washington inasali au kuomba kuwa rais Karume, mtu msumbufu na mwenye akili ataigiza viongozi wasiofungamana wa Tanganyika ya Nyerere. Hata hivyo, Karume ana uhakika wa Zanzibar ya Kerensky.” 
        Alexander Fyodorovich Kerensky (22 Aprili 1881 hadi 11 Juni 1970) alikuwa mwanasheria na mwanamapinduzi wa kirusi aliyeongoza serikali ya mpito ya Urusi kuanzia Julai hadi Novemba mwaka 1917 kabla ya kujiunga na serikali ya kimapinduzi ya Urusi. Kuna mfanano baina ya Karume na Kerensky.  Wote waliunganisha serikali zao kuepa kupinduliwa na waliowapindua. Serikali zao zilidumu kwa miezi minne, Kerensky kuanzia 21 Julai 1917 hadi 7 Novemba, 1917 na Karume miezi mitano kuanzia 12 Januari 1964 hadi Aprili 26,1964. Wote walipoteza urais, Karume akawa makamu wa rais na Kerensky waziri wa vita. Tofauti na Karume, Kerensky na alioungana nao waliunda taifa lenye muungano wa kweli wakati Karume aliunda mgongano aka muungano unaoendelea kuzua minong’ono toka pande zote.
            Nne, nini kifanyike? Kama kiongozi wao, mafyatu wameniambia kuwa wanachotaka ni muungano wa kweli kama ndoa wenye sirkal moja kama Urusi na siyo huu mgongano. Wanataka Zenj iwe mkoa tena ambao utakuwa ndiyo wa pili kwa udogo ikizingatiwa kuwa mkoa mdogo Danganyika ambao ni Dar Es Salaam yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1, 393. Namba huwa hazidanganyi.
Leo sifyatui mengi. Muhimu nimetumia namba kuondoa mgongano na usanii wa kisiasa vilivyoleta ubaguzi wa kikatiba. Hivyo, wanaomzomea Tunda Lishe ndo wapaswao kuogopwa, kuzomewa, kukaripiwa, na kulaaniwa. Mafyatu wanataka muungano si mgongano. Hivi leo nimekunywa ngapi?
Chanzo: Mwananchi jana.

No comments: