Yoo-hoo, Africa Is Yowling

Yoo-hoo, Africa Is Yowling

Sunday 9 June 2024

Misingi na nguzo kuu za ndoa

Katika makala iliyopita tuligusia misingi na miiko baadhi ya ndoa. Leo tunaendeleza tulipoishia.
Uhuru
Ndoa inapaswa kuwa huru na isiyotegemea au kuingiliwa na watu wengine katika uendeshaji wenu. Mliapishwa wawili tu na si mia mbili. Hivyo, jukumu na wajibu wa kutunza kiapo chenu ni lenu. Si la watoto wenu, marafiki, wazazi, mashoga, na wengine hata muwapende, kuwathamini, na kuwaamini vipi. Ndoa ni kama sehemu zenu za siri. Hakuna apaswaye kuziona au kuzihudumia isipokuwa wanandoa wenyewe. Nani mpambavu huanika chupi zake hadharani?  Hivyo, ndoa inapaswa kuwa taasisi huru ambapo uhuru huu ulindwa kwa wivu na tahadhari kubwa. Tutoe mfano. Jamaa mmoja alizoea kuwapa marafiki zake siri za mwenzie. Moja ya siri alizotoa ilikuwa ni ukubwa wa maumbile yake na namna alivyojua shughuli.
    Katika hao marafiki, walikuwamo wakware waliokuwa wakimmezea mate mwenzie. Hivyo, kutotunza na kulinda siri za ndoa yake kuligeuka angamizi la ndoa yenyewe hasa wahusika walipokula njama kumuandamana mhusika. Binadamu tumeumbwa na kujipenda kuliko wengine. Mafanikio yako ni yako siyo ya kuwasimulia wenzako. Kitanda usicholalia, hupaswi kujua kunguni wake.
        Japo kuna kipindi mambo huzidi kiasi cha waliotanzwa kutafuta msaada. Katika ndoa, linapotokea tatizo, ni muhimu likashughulikiwa na wahusika peke yao tena kwa usiri. Ndiyo mana tunasema siri za ndani ziishie chumbani. Zisivushwe hata kuchungulia sebuleni. Hao mnaowafuata nao wana changamoto, kasoro, na matatizo yao. Kama ikizidi sana, wahusisheni wazazi wa pande mbili japo nalo hili linataka utafiti na umakini vya hali ya juu. Mnapozoea kuwapelekea watu matatizo yenu, mnayazidisha na kuyafanya yawe magumu zaidi kuliko mkiyashughulikia wenyewe. Mlipoamua kufunga ndoa mlifanya hivyo peke yenu japo baada ya hapo, mlitoa taarifa kwao kama sehemu ya hitajio la kijamii na kisheria. Kwenye changamoto, matatizo, na migogoro ya ndoa, msiwahusishe hata wapambe au mashahidi wenu. Hakimu wa kwanza wa kushgulikia changamoto na matatizo ya ndoa ni wanandoa wenyewe na mahakama yao ni chumba cha kulala.
Ithibati
Pamoja na miiko na misingi mingine, ithibati katika ndoa ni muhimu. Ithibati huonyesha kuwa mhusika anaaminika na anajiamini. Hivyo, zinapotokea changamoto katika ndoa yako, jambo kubwa la kwanza muhimu ni kujiamini. Hii hukupa fursa ya kufikiri na hata kufanya utatifi na kulidurusu tatizo ili ulipatie ufumbuzi. Mfano, unaweza kuchunguza au kutafiti chanzo au vyanzo vya tatizo. Mara nyingi, kama tulivyosema hapo juu, adui mkubwa wa ndoa ni wanandoa. Kadhalika, chanzo au vyanzo vya changamoto ni wao pia iwe kwa bahati mbaya, kutojua, kutokusudia, au kukusudia. Hivyo, sehemu ya kwanza kutafutia changamoto ni wanandoa wenyewe.
        Pili mwitikio na namna wanandoa wanavyopokea na kushughulikia changamoto zan doa yao ni muhimu. Hapa, unaepusha kumtafuta mchafu, wa kumtwisha lawama au kuepuka lawama kwa kufanya hivyo. Changamoto za ndoa ni sawa na maladhi mwilini. Ni mwenye mwili anayeyabaini hata kabla ya daktari. Hivyo, silaha imara ya kwanza kuelekea matatizo ni kujichunguza kwa wanandoa wanaokabiliwa nazo. Hapa, kunahitajika ukweli na uwazi ili kuepuka kufukuza tatizo au kutafuta suluhu mahali ambapo si sahihi au lilipo. Mfano, ukiwa unaumwa kichwa, huwezi kutafuta tatizo kwenye mguu. Lazima ukisikilizie kichwa hata kutafuta ushauri wa daktari juu ya kichwa siyo mguu.
Kanuni
Kama zilivyo taasisi nyingine, ndoa ina kanuni zake. Nyingi za kanuni hizi hazikuandikwa popote. Zinatengenezwa na wanandoa. Mfano, ni jambo gani hupenda kufanya bila kukosa wakati wa kuamka au kulala? Ni jambo gani wanandoa wanakubaliana au kutofautiana katika ndoa? Hata hivyo, methali moja ya kimombo inasema kuwa wanandoa wanaoimba pamoja huishi pamoja.
        Tutoe mfano wetu wenyewe. Siku moja tulinunua gari jipya aina ya Chevy Equinox. Baada ya kulinua, mmoja wetu aliamua atumie gari la zamani Kia Soul. Hata hivyo, kuna wakati tulikuwa tukibadilishana magari kulingana na tulipokuwa tukienda. Nkwazi alikuwa akiendesha Chevy zaidi na Nesaa akitumia Kia Soul. Kuna kitu tulitofautiana. Baada ya kununua Chevy Equinox, Nkwazi alinunua cover ya usukani nyeusi yenye manyoya. Nesaa hakuipenda hata kidogo akisema inaweza kutunza uchafu na ni vigumu kuisafisha. Mwishowe, tulikubaliana kuweka cover ya ngozi na changamoto ikaishia hapa. Kwa kanuni zetu, hatukujiruhusu kitu kitufarakanishe zaidi ya kukubali yaishe kwa msingi wa give and take kama tuutumiavyo kwenye taaluma ya utatuzi wa migogoro na kupata win-win solution au suluhu ambamo wote mnafaidika.
Mwisho, ukiangalia ukubwa wa changamoto, unaweza kuona ni kama jambo dogo. Si dogo. Kumbuka hata mbuni alianza na yai dogo mbali na mbegu za kiume na mayai ya kike visivyoonekana kwa macho. Mbali na hili, kanuni yetu kubwa ni kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani na mshindwa wa leo anaweza kuwa mshindi wa kesho.
    Hivyo, ni vizuri kuzingatia msingi na nguzo za ndoa sawa na unavyofanya kwa taasisi nyinginezo. 
Chanzo: Mwananchi leo.


No comments: