The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Monday, 24 March 2025

Tunashangaa, Tunashangazwa, na Kushangaza

 

Huwa nashangaa. Sijui kama nawe hushangaa kushangaza? Kama hushangai, unashangaza. Kama unashangaa, pia, unashangaza. Hata nami nashangaza kwa kushangaashangaa bila kufyatua. Huwa nashangaa kwa ninayosikia bila kuona ukiachia mbali ninayoona bila kuyasikia. Katika kaya yetu ya kushangaza, kuna vitu vinashangaza. Kila siku nasikia mafyatu wakilalamikia ukapuku wa kutengenezwa wakati kuna wanene waliofyatua njuluku hadi wanakufuru. Hawa hunishangaa kama nishangaavyo. Tunashangaana, kushangazwa, na kushangaza. Hapa, sijaongelea upigaji wa kutisha kila siku. Unashangaza. Unashangaa kwanini tunapigwa tukaendelea kushangaa hadi tunashangaza. Kwa kushangaa kwetu, tunashangaza na kushangazana. Ukinishangaa, nakushangaa. Usiponishangaa kwa kushangaa, nakushangaa kiasi cha kushangaza kwa kushangaana na kushangazana.

            Siachi kushangaa. Hushangaa kusikia mapambio, mashairi, ngonjera, na sifa tena vya kushangaza. Waimbaji ni mafyatu, wanyama, hata wadudu tena wanaoshangaza. Mfano, wapo waishio kwenye ukwasi wanaoshangaza wanaowashangaa waishio kwenye uchochole wa kushangaza. Licha ya kushangaana, wote wanashangaza. Wapo wanaoshangaa. Wanashaangana na kushangazana. Inakuwaje fyatu awe kapuku kwenye kaya inayosifika kutenda miujiza karibu katika kila jambo? Inashangaza. Wakati wenye njuluku wakiwashangaa wasio nazo, nao wanawashangaa namna walivyozipata wakati wao wakikosa. Inashangaza. Wanashangaa na kushangaza.

Hakuna kitu hunishangaza kama taarifa ya Mkaguzi mkuu wa njuluku za kaya (KAGO). Je huwa kweli anazikagua au zinamkagua? Inashangaza. Kwanza, hizo njuluku ziko wapi na ni kiasi gani? Inashangaza. Pili, kwa zinavyopigwa, sijui kama kweli zipo za kukagua. Inashangaza.  Kwanini asikague hata njuluku za wenye nazo waliozipiga toka kwa mafyatu wnaoashangaa na kushangaza? Nashangaa. Kago anashangaza kiasi cha kumshangaa. Sijui kama naye anajishangaa kwa taarifa atoazo za kushangaza. Je huwa anatushangaa? Kila mwaka, huwa anaripoti upigaji na madudu kibao udhani kazi yake ni kufyatua habari mbaya kwa mafyatu. Inashangaza. Kingine kinachoshangaza ni ile hali ya waliofyatua tena njuluku ndefu kuhamishwa vituo kwenda vingine badala ya kupelekwa lupango. Inashangaza.

 Wakati nikishangaa hili, huwa nashangaa namna Mwendesha Makesi wa Kaya (Dipipii) anavyoweza kukukamatisha, ukapozwa hata kusahaulika lupango halafu anajitoa welewa na kusema eti amekufutia mashtaka. Inanishangaza. Huwa namshangaa na vitu kama hivi vya kushangaza. Je huu muda fyatu wapotezao lupango unalipwa na nani? Inashangaza. Huwa nashangaa kama hii nayo ni haki, sheria, na utawala bora. Juzi, nilimuona mzee Silaha, akiwa amechakaa. Nilishangaa. Alikaa lupango kwa mwezi na ushei. Inashangaza. Ukiuliza nini mbaya alifanya? Unashangaa. Unashangaa ni kwanini ndata walimnyaka na kumsweka lupango bila kupeleka kwa pilato! Unamshangaa yeye kuswekwa lupango bila kosa. Unawashangaa ndata hawashangai hili. Pia, unawashangaa wanene wanaoshangaza kwa kudai kuwa wameleta maendeleo na ustawi. Inashangaza. Hivi vinaweza kupatikanaje bila haki? Inashangaza!

Wakati nikiwashangaa Kago, Dipipii, na ndata wa kushangaza pia, humshangaa munene anayeshughulikia njuluku asifikaye kwa kutoa misamaha ya kodi kwa wenye nazo huku akizidi kuwakamua wasio nazo kwa njia mbali mbali kama vile maokoto, tozos, na madude mengine ya ajabu ajabu na kushangaza. Inashangaza. Kabla ya kumaliza kumshangaa jamaa wa njuluku, huwa nashangaa kusikia kuwa kaya imefunguliwa. Inashangaza. Kwani, nani alikuwa ameifunga na kwanini na ili iweje? Inashangaza.

Hakuna kitu nashangaa kama kukatikakatika kwa umeme. Inshangaza sana kwa namna tunavyoahidiwa kuwa migao ingegeuka historia wakati wowote. Inashangaza namna ambavyo mambo ya kushangaza hutokea na ahadi za kumaliza migao kugeuka donda ndugu. Inashangaza ni kwanini hawa wanaotoa ahadi za kushangaza hawajishangai pamoja na kushangaza! Inashangaza na waathirika wasivyowafyatua. Inashangaza sana kwanini wanaofeli katika kutoa huduma nyeti kama hii kutoachia ngazi ili wenye uwezo waingie na kurejesha heshima ya kaya. Huwa nashangaa. Nashangaa sana kuona kuwa wale wale wanaotudanganya, wanafanya hivyo si mara moja wala mbili. Inashangaza.

Ngoja nifyatue mfano japo mmoja wa kushangaza mjue kwanini nashangaa na kushangazwa.Waziri mkubwa alikaririwa mwaka jana akisema “kwanini Muentertain wizi? Watu wanaiba mara ya kwanza, mara ya pili mmeshindwa kuchukua hatua za kuwadhibiti wasirudie tena?” Inashangaza. Nasikia mafyatu wanafyatua hata pesa ya wagonjwa. Je nini kimefanyika badala ya kulalamika? Inashangaza. Waziri mkubwa, pamoja na mamlaka yake, anashangaa. Inashangaza kweli kweli.

Naendelea kushangaa haya mambo ya kushangaza. Mfano, rahis, akihutubia buge, mwaka 2021 alisema “naomba kutumia jukwaa hili la Bunge lako Tukufu kuwaonya wale wote wanaodhani kuwa usimamizi wa mali ya umma kwa maslahi ya wananchi, kukataa ukwepaji wa kodi, wizi, na kukemea uzembe vitasimama kwa sababu tu Rais Magufuli hayupo.” Inashangaza.

Kwa ufupi ninashangaa, inashangaza, nawashangaa japo mnanishangaa kiasi cha kushangaza na kushangazana kama siyo kushangazwa. Wakati mwingine natamani tuitwe washangaaji kama siyo washangazaji. It’s too much. I wonder.

Ninashangaa kwanini nashangaa! Je wewe unashangaa au unashangaza? Hakika. Tunashangaa, kushangaana, na kushangaza. Mafyatu itikieni ‘kweli inashangaza na mseme amina.

Chanzo: Mwananchi, Machi 12, 2025.

No comments: