Mwenyekiti Mao Zedong alilwahi kusema kuwa bila utafiti, hakuna haja ya kutoa madai. Pia, sheria inasema kuwa atoaye madai, atoe ushahidi. Hivyo, katika makala ya leo, tutatoa ushahidi kama ifuatavyo.
Mosi, kama tulivyosema hapo juu, ukitaka kujua ukweli wa dhehebu la dini au kanisa, waangalia wale wanaojiita viongozi wake. Angalia aina ya maisha wanayoishi na mahubiri wanayohubiri. Wengi wa wahubiri na viogozi wa kujipachika vyeo kama vile mchungaji, askofu, mtume, nabii na vingine, hawafanyi kazi zozote za kuwapatia kipato. Ni matapeli wanaowaibia na kuwanyonya waumini wao wavivu wa kung’amua vitu rahisi ima tokana na ujinga au kukata tamaa. Je huu utajiri wanaupata wapi kama siyo kuwaibia wafuasi wao ima waliokata tamaa au wajinga tu? Wapo wanaojihusisha na biashara nyingine hata bila kulipia kodi na hivyo kuiibia serikali na kujiingizia fedha nyingi kinyume cha sheria. Kwanini mamlaka hazijiulizi swali hili rahisi ambapo kinachofanyika hakina tofauti na ujambazi wa kawaida ambapo jambazi hulala maskini na kuamka tajiri bila kutoa maelezo? Kwanini mamlaka hazitaki kuuliza au kuna namna?
Pili, kujua mbivu na mbichi, angalia mhusika amepata uongozi au ukuu wa dhehebu husika namna gani. kama amejipachika kama wengi tunaowaona hata wakijiingiza kwenye siasa, anachofanya mhusika ni biashara ya kusaka tonge na fedha kwa mgongo wa neno la Mungu ambalo siku hizi limegeuka biashara kubwa duniani ambapo matapeli na waroho wengi wa utajiri hujipatia utajiri na ujiko.
Tatu, angalia namna kanisa au dhehebu husika linavyopitisha madaraka inapotokea kiongozi akafa. Utaratibu tuliozea kwa dini za kweli ni kwamba akifa kiongozi wake, hufanyika uchaguzi na kumpata mtu anayefaa ambaye mara nyingi huwa ameandaliwa hata kabla ya kiongozi kufa japo si kwa din izote. Mfano, makanisa maarufu kama vile la Kiroma, Kianglikana, Kilutheri na mengine yanayoheshimika, huwa na utaratibu wa kuteua au kufanya uchaguzi wa mrithi wa kiongozi anapostaafu au kufariki. Hata uislam una utaratibu huu. Mfano, anapokuwa shehe mkuu, hufanyika uchaguzi wa shehe mkuu mwingine ambaye mara nyingi hana uhusiano wa damu na anayemrithi. Hata papa anapokufa au askofu mkuu wa baadhi ya madhehebu yanayoheshimika, hali ni hii. Hakuna kurithishana madaraka kama ambavyo hivi karibuni tulishuhudia hapa nchini ambapo alifariki mmojawapo wa waliojipachika madaraka ambaye kanisa lake––––kwa vile lilikuwa duka lake lililopachikwa jina la kanisa––––lilirithishwa binti yake. Je kweli kanisa la Mungu laweza kurithishwa au kutafutiwa mtumishi? Je makanisa haya yanayorithishwa kwa kufuata damu ni makanisa au maduka tu? Utarithije kanisa la au msikiti wa Mungu?
Mfano mwingine wa hivi karibuni ni pale alipokufa tapeli mwingine nchini Nigeria aitwaye Temitope Bolugun Joshua almaarufu TB Joshua. Baada ya kifo cha ghafla cha tapeli huyu, ulizuka mgogoro katika urithi wa kanisa ambapo mkewe Evelyn alirithi duka la mme wake. Wakati matapeli wenzake wakimpa urithi mke wa Joshua, walitoa sababu hafifu na mbovu kuwa Joshua alizaliwa mtume na mkewe aligeuka mtume kupitia ndoa hasa ikizingatiwa kuwa mume na mke ni mwili mmoja! Je kwa huyu wa kwetu dhana hii chafu inasimama au tutaambiwa kuwa kwa vile binti yake ni damu ya mama basi nao ni kitu kimoja?
Nne, kujua kuwa dhehebu au kanisa husika ni duka la kuchuuza neno na roho, angalia namna wakubwa wake wanavyosaka umaarufu na matumizi makubwa ya vyombo vya habari au kujiingiza kwenye siasa. Nchini Uganda, Hayati Padre Simon Lokodo alifukuzwa upadre na Papa mstaafu Bendict XVI baada ya kujiunga kwenye mbio za kugombea jimbo la Dodoth ambalo alifanikiwa kushinda na kuliongoza hadi mauti yanamfika 29 Januari, 2022.
Tano, kujua kama dhehebu au kanisa husika ni la kitapeli au duka la kiroho ni kuangalia aina ya mahubiri ya viongozi au wenye duka husika wanayohubiri. Wengi wa matapeli hawa wakiroho uhubiri mambo makuu matatu, yaani utabiri, utajiri na kufanya miujiza ya urongo. Rejea mfano, yupo aliyeahidi kumfufua marehemu Amina Chifupa. Mbali na huyo, Joshua aliicha dunia hoi alipotabiri kuwa Hilary Clinton angeshinda urais wa Marekani akaishia kubwagwa na Donald Trump jambo ambalo lilifichua ujinga, utapeli na ubabaishaji wa tapeli huyu.
Leo sitaandika mengi zaidi ya kuwasihi wale wanaoibiwa kila uchao kutokana na imani zao, wawe makini. Wachunguze mambo matano tuliyodurusu hapo juu kujua kama wanachojiunga nacho ni duka la kiroho au dini. Wengi wanaibiwa na kuaminishwa kuwa kuna siku watabarikiwa na kuwa matajiri wakati hao wanaowaibia wanazidi kuwasikinisha, kuwadanganya, na kuwapotezea muda. Wakati wa serikali kuchunguza utajiri na taasisi za viongozi wa kujipachika madaraka umefika. Vinginevyo, serikali haiwasaidii wananchi wake. Pia, ifahamike. Imani katika miujiza ni chanzo cha uvivu na uuaji wa maarifa. Hivyo, licha ya kuathiri hali na uchumi wa wahanga, inaathiri uchumi wa taifa ukiachia mbali kuvunja sheria kwa kuhubiri uongo.
Chanzo: Mwananchi jana.
No comments:
Post a Comment