The Curse for Salvation
Wednesday, 23 July 2025
Fyatu kufyatua na kujinoma na king’ora!
Tuesday, 22 July 2025
Wanandoa msijidhalilishe hata uwe na shida vipi
Wednesday, 16 July 2025
Kwanini tusiite kaya Chaitan au Tanghasia?
Baada ya kusota muda mrefu na muda wa kupaa kuwadia, nilienda tena kwenye geti la kupandia. Kwa mara nyingine, nilikuta wachaina kibao. Hivyo, ilibidi nimuulize mfanyakazi mmojawapo kama njiwa iliyokuwa inaondoka ilikuwa inaelekea Chaina au Ufyatuni. Akiwa ameshangaa kidogo, alijibu kuwa ilikuwa inaelekea Ufyatuni na si Chaina. Du! Nilianza kuskuti lau nipate jibu nisipate. Basi, Fyatu nilifyata nikingoja pipa litue nione yaliyokuwa yakinisibu kuhusiana na hawa wachaina. Kutua, tu, nikasikia wengine wakitema uswa japo wakichainachaina.
Kusema ukweli, sikuamini kuwa fyatu mwenye akili timamu ana anayetaka kuishi angeweza kupanda haya majeneza yasiyofunikwa yaitwayo toyo. Sikuamini kuwa kidude kinachopaswa kubeba mafyatu wawili tena wakiwa, kisheria, wanapaswa kuvaa helmet kwa usalama wao, kingeweza kupakizwa mafyatu watatu na wakati mwingine wanne. Funga kazi ni pale niliposhuhudia abiria wakipanda haya madude ya kifo bila kuvaa helmets. Je, hapa tatizo ni wahusika au mfumo mzima usiofuata maadili wala sheria bali madili na shari? Kwa mujibu wa hali na jinai, kwanini Ufyatuni isiitwe Tanghasia?
Nilitaka kushambuliwa na presha pale nilipolipia tikiti ya kuingilia na kuishia kulipishwa tena kuwaona waanimo? Je huu siyo uanimo kunipiga kuwaona waanimo wakati nshalipia kuingia kuenjoy kila kitu? Kumbe nina jet lag inayochizisha akili?
Jengeni kwako siyo kwenu
Utawasikia wazazi wakimuulizwa binti wao kazi au vyeo vya mtarajiwa wake. Wengine hujisifu kuwa mabinti zao wameolewa na watu matajiri au wakubwa kana kwamba wao nao ni wakubwa au matajiri. Hii ni aina fulani ua umaskini wa kijamii na kiuchumi ambapo utu wa mja huzidiwa thamani na vitu fedha na mali. Wengine huwambia kabisa kuwa wanataka binti awaletee mchumba wa aina fulani kana kwamba wao ndiyo wanaoolewa. Japo ni haki ya wazazi kutunzwa na watoto wao, wazazi wa aina hii ni vibaka au wezi wa kawaida wanaotumia mabinti zao kwa kuwageuza watumwa wa vitu bila kujali madhara yake.
Kama wanandoa mna uwezo iwe wa kifedha au utashi, si jambo baya kuwajengea wazazi wa pande zote mbili kama hawakubahatika kujijengea. Pia, si vibaya kusomesha wadogo zenu na mengine kama hayo kama yatafanyika kwa faida ya pande zote. Hata hivyo, mfanye tokana na mapenzi na uwezo wenu na si mashinikizo toka kwa wazazi au wenzi wenu.
Muhimu, mnapofanya haya mambo ambayo yaweza kuwa majukumu yenu, msibague au kupendelea au kuutenga upande mmoja. Ajabu, hao wanaotaka wafanyiwe yote hayo, hawakuwafanyia wakwe zao! Hapo ndipo dhana ya jinai ya unyonyaji, uvivu, na wizi inapojengeka. Hata hivyo, hiki kinapaswa kuwa kipaumbele namba moja, yaani kuwajengea wao kabla ya kujijengea au kuwasomeshea watoto wao?
Tuanzie hapa. Kwanza, tunajua. Wapo wazazi, hasa wenye uwezo, wanaowajengea watoto wao nyumba na kuwapa mali mbali mbali. Pia, wapo wanaowapa vyeo tokana na nafasi walizoshika. Hapa, tunaongelea wale ambao wana uwezo wa kawaida, yaani wanaoanza maisha. Je ni haki kuwajengea wazazi wenu hasa wa mke kabla ya kuwa na nyumba yenu wenyewe? Je, ni halali na sahihi kwa mmoja wenu kuweka kipaumbele upande mmoja huku akiuacha upande mwingine?
Pili, kabla ya kutoa jibu au majibu, tuulize maswali tena. Kabla ya kuwajengea wazazi wenu, jiulizeni. Je wao waliwajengea mababu zenu? Kama jibu ni hapana, kwanini? Kama jibu ni ndiyo, je, walifanya hivyo kibaguzi na kwa shinikizo tena la upande mmoja? Kama kipaumbele cha mmoja wenu ni kuwajengea wazazi wake, jiulize. Kwako utajenga lini? Kwanini uanze na kwenu badala ya kwako? Je na mumeo akiamua kujenga kwao, nawe kwa wazazi wako, kwenu mtajenga lini? Je, kwako, ndoa ni kitega Uchumi au mfumo wa maisha tena ya kudumu baina ya watu wawili na jamii zao? Je hakuna namna ya kuwasaidia wazazi wenu bila ya kubaguana, kujiumiza, kuhujumiana, na kutumiana? Hivi, hali kama hii inapotokea, nani waathirika nan ani wanafaa kuwa wanufaika? Wakati mama ukimshinikiza mumeo awajengee nyumba wazazi wako au kuwasomesha wadogo zako, jiulize, hayo yangefanywa na wifi yako kwa wazazi wako ua mkamwana wako kwako, ungejisikiaje na kufanya nini? Hili ni suala na swali muhimu. Kulijibu uzuri, epuka dhana na imani ya mkuki kwa nguruwe. Wahanga wa jinai hii waweza kuonekana kama nguruwe wanaopaswa kupata mkuki bila kujua hawa wanaowachoma hii mikuki wanaweza kuwa nguruwe wa kesho.
Hivi, inawezekana kuishi sehemu mbili au kutumia mabwana wawili kwa wakati mmoja? Je wanapoamua kuanzisha hujuma hii, huwa wahusika wanajiuliza kama wanaotaka kuwahujumu nao wana akili timamu hata kubwa kuliko zao? Jengeni kwenu kwanza kabla ya kwa wengine. Huu ni usia wa leo.
Wednesday, 9 July 2025
Tumechanganywa, tumechanganyikana, na kuchanganyikiwa
Namshukuru huyu fyatu chawa maana, sikuwa na mpango wa kutumia wiki nzima nikifuatilia tulivyochanganywa, tukachanganyikiwa, kuchanganyana hadi kuchanganyika, kukachanganya uongo na ukweli vikachanganyikana kifyatufyatu. Hivi kuchanganya dini na siasa ni nini? Katiba wala sheria havisemi lolote! Je dini na siasa ni tofauti au watoto mapacha? Nitajibu swali hili mwenyewe, nawe uongezee. Kimsingi, taasisi hizi zina sifa zifuatazo:
Mosi, Zote chimbuko lake ni ughaibuni kabla na wakati wa ukoloni. Umewahi kujiuliza kama kuna mchango wa wahanga kwenye kuanzishwa na kuingizwa vitu hivi ambayo hutumia maguvu yawe ya mitutu au imani? Sasa, jiulize, na ujijibu mwenyewe.
Pili, vyote ni kolonishi, yaani, vinatawawala mafyatu na kuwatumia vitakavyo hata kuwachanganya kiasi cha kuchanganyikiwa na kuanza kuchukiana mbali na kunyonyana hata kunyotoana roho.
Tatu, vyote hutegemea mafyatu kama mashamba yao na kuvuna visipopanda. Vikipanda, hupanda maneno na kuvuna njuluku. Mfano, siasa hutumia ushawishi hata ahadi za uongo kuwaingiza mkenge mafyatu ilhali dini hutumia vitisho vya moto na ahadi za vinono kuwatwisha mkenge mafyatu. Hamjaona pale Ubunguo? Fyatu mwenye duka lake la kuuza roho kasepa. Mafyatu wanafanya nini? Si wanakutana kila j’pili na kupigwa na ndata wakitetea fyatu asiyeweza kujitetea? Kwanini wasimuachie god wake amtetee? Si aliwahi kujidai kuwa hatishwi na yeyote wala chochote? Atokee na kufyanya fyoko akione cha moto.
Nne vyote hutumia njuluku za mafyatu zwazwa bila kukaguliwa na yeyote kiasi cha kuwatajirisha matapeli wa kiroho na kuwasikinisha mafyatu zwazwa.
Tano, vyote hudai vimetoka kwa God. Utawasikia hata matapeli wa kujipachika wakisema wao ni mashushu au wawakilishi wa god. Wanasiasa wakiukwaa ukuu, watakwambia maulaji yote hutoka kwa god. Hivi maulaji ya nduli au M7 yametoka kwa God? Mbona hamjui kitu rahisi hivi!
Sita, vyote uahidi unono hata kama mwishowe ni uchungu. Kila siku, utasikia wanasiasa wakiahidi kuleta maendeleo yasiyofika! Ukichunguza ni maendeleo ya nani? Hili sijibu. Jibu mwenyewe.
Sita, vyote hufanya matanuzi na kukemea wafuasi wake kuyachukia. Utamsikia mwanasiasa fisadi akilaani ufisadi majukwaani wakati ni ufisadi huo huo mtaji wake. Tapeli wa kiroho atakwambia mbinguni wataingia maskini ilhali yeye ni mkwasi!
Saba, vyote hupenda madaraka na ujiko. Kila palipo na kamera au waandishi wa umbea, lazima wawili hawa wawepo. Japo wanene wa dini hawakutangaza dini zao kama biashara, siku hizi, hata runinga na radio vinatumika kuwaingiza mkenge mafyatu.
Nane, vyote vilichanganyika tangu kuanza kwake kule Uropa ambapo popu alikuwa kiongozi wa lisrikal mbali na ntume naye kuwa mkuu wa dola. Kwani, hamjui au hamsomi historia?
Ngoja nichimbe zaidi. Dini na siasa vinachanganyikana na ni mapacha ila inategemea unavichanganyaje na kwa maslahi ya nani. Mfano, muimbaji wa nyimbo za injili akiimba nyimbo za kusifia wanene siyo kuchanganya dini na siasa. Akiimba za kukosoa, hapa, anachanganya dini na siasa kiasi cha kutishia amani na utulivu vya walaji na wanene.
Siasa inachanganyikana na kila kitu.
Mosi, mfano, mjeshi akiteuliwa kwenye nafasi ya kisiasa hachanganyi ugeshi na siasa?
Pili, ndata akisimamia uchakachuaji au kupendelea chama twawala, hachanganyi undata na siasa? Nani anahoji au kukataza?
Tatu, mchungaji wa bandia akijiunga na watawala, hachanganyi dini na siasa. Ila akikengeuka kutaka kuendelea kuwatumia, anaambiwa achanganya dini na siasa!
Nne, waumini wakintetea bosi kwa sababu ni dini moja, wanachanganya siasa. Na lazima waonywe hata kufungiwa kwa kuleta udini na kuchanganya dini na siasa.
Sita, waumini au viongozi wakilipa kodi wakahoji matumizi yake, wanachanganya dini na siasa!
Saba, dini zikiwahimiza waumini kushiriki uchaguzi na kuchagua chama twawala, hawachanganyi dini na siasa.
Mwisho, tunaposema dini na siasa havichanganyiki wakati tunavichanganya, huku si kufyatuka kuchanganyana na kuchanganyikiwa? Basi, tuchanganyeni tuchanganyikiwe tuchanganye na kuchanganyikiwa kama lengo ni kutenda haki na kuleta maendeleo vya kweli. Kifyatu, dini na siasa ni mapacha au nimechanganya kujichanganya, kuwachanganywa, kuchanganyana na kuchanganyikiwa?
Mafanikio yasikuvunjie ndoa
Pili, alianza kwenda ughaibuni akiandamana na waheshimiwa wenzake wa kiume na maafisa wakubwa wakubwa wa serikali. Huko, walikaa kwenye mahoteli ya bei mbaya wakila na kunywa na kulala pamoja. Ghafla, uzalendo ulimshinda. Alianza mahusiano yasiyo na heshima na waheshimiwa wenzake. Walipika na kupakua kiasi cha kunogewa. Jambo hili, lilimpelekea kutokuwa na hamu na mumewe kiasi cha kuanza kuanzisha kasheshe hadi ndoa ikavunjika.
Tatu, badala ya mafanikio kufanikisha ndoa, yalifanikisha kitu kimoja tu ambacho ni kuivunja ndoa na kuacha majuto na mateso si kwake tu bali mume na watoto na hata ndugu na jamaa.
Japo si wengi wala wote wanaojitokeza kueleza ukweli huu wa aibu na uchungu, je hawapo? Je ni akina mama wangapi wenye madaraka wamevunja ndoa zao? Je kwanini ni wanawake ambao ni wahanga wa madaraka au kuna na wanaume? Jibu laweza kuwa sababu ni kwamba jamii yetu inatawaliwa na mfumo dume ambapo wanaume wana uwezo wa kufanya watakalo na wasifanywe kitu na wenzi wao wa kike.
Katika kudurusu kisa hiki, je nani wa kulaumiwa. Je ni mfumo au mhusika mwenyewe? Je hii inatoa somo gani kwa wale ambao hawajaingia na yakawakuta haya yaliyomkuta dada huyu ambaye wakati anaupata uheshimiwa alikuwa mdogo miaka 30 na ushei? Je hiki hakiwezi kuwa kikwazo kwa wanawake wengi ambao wangetaka kuingia siasa? Je wahusika wachague kipi kati ya madaraka na ndoa? Wakati mkitafakari kujibu maswali hayo hapo juu, tunaweza kuwapa mwangaza au ujanja wa kufanya uamuzi bora. Tutatoa angalizo kuwa madaraka ni ya muda na ndoa ni ya kudumu. Kwa mwenye akili safi na busara, atachagua cha kudumu na kuachana na cha muda. Je ni wangapi wanaweza kuchagua ndoa na kuachana na madaraka? Je hatuhitaji kubadili mfumo wetu wa kisiasa ili kulinda ndoa za waheshimiwa wetu na kuwahakikishia usalama akina mama ili wawe na mazingara salama na sawa kushiriki katika siasa? Je hili ni tatizo la watu binafsi au la jamii kwa ujumla pamoja na mfumo wake? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Pamoja na kwamba makala hii inahusika na ndoa za waheshimiwa na madhara wapatayo, inawakilisha dhana nzima ya madaraka kijinsia. Kwanini wanaume wanapopata madaraka hayavunji ndoa zao? Kwanini madaraka ni tishio kwa ndoa za akina mama wengi japo si wote? Je nini kifanyike?
Je katika kudurusu kisa husika, wewe kama mwanandoa, unamsikitikia, kumlaumu, kumhukumu, au kutojali kwa vile hayakuhusu? Je ungekuwa wewe, ungechagua nini na kwanini? Tunauliza maswali hii kutaka kuwaelimisha wasomaji wetu kuwa madaraka si uheshimiwa tu bali ni dhana mtambuka. Kuna haja ya wanandoa kushirikiana katika jambo hata kama ni madaraka au mafanikio vinginevyo, yanaweza kugeuka maanguko si kwa mmoja bali wao, watoto wao, na hata wazazi, mafarafiki na familia zao.
Tumalizie kwa kuwataka wahusika na jamii kwa ujumla kukomesha na kuepusha balaa hili kwa ndoa litokanalo na mfumo dume na fisasdi. Kwenye nchi za magharibi, waheshimiwa huchunguzwa sana na kupewa adhabu kali wanapopatikana kuvunja kanuni za maadili wanazopaswa kuzifuata. Hata hivyo, wana mazingira mazuri ya kuwezesha waheshimiwa kulinda. Nasi, baada ya kugundua tatizo hili, kama jamii yenye akili timamu, tuchukue hatua kulikomesha ili kuepusha mateso kwa familia nyingi na wanandoa mbali na kuwepo mazingira magumu kwa wanawake kufanya siasa kwa uhuru bila kuchelewa yaliyompata mhusika kwenye kisa husika.
Thursday, 3 July 2025
Fyatu Kutoa Gari kwa kila Mpika Kura ya Kula
Kama mjuavyo, uchakachuaji, sorry, uchaguzi mkubwa umekaribia, na ninagombea urahis na lazima nitashinda hata kama ni kwa goli la mkono kama lile na Mapepe Tunaye. Hivyo, kwa vile mie ni muwazi, naweka wazi mikakati na ukarabati wa kushinda hii kitu mapema asubuhi kama ifuatavyo:
Mosi, kuanzia sasa, nitamwaga ndinga kali na za bei mbaya za kisasa kuhakikisha kila mpika kura anapata moja ili anipe kura ya kula. Mie, siyo wa kumwaga vikwata wala tukutuku visivyo na utukufu zaidi ya utukutu. Si wa baiskili kama Sikiri maskini. Hivyo, kaeni mkao wa kula usawa huu wa kuvuna ambapo hamkupanda na kupanda ambapo hamtavuna.
Pili, nimeamua kukopa njulu nje na ndani kuhakikisha mradi wangu wa ushindi unafanikiwa. Japo nimesikia baadhi ya mafyatu wakizoza na kupayuka kuwa nakopa sana, wanataka nifanye nini? Nani kawaamba kuwa kukopa ni kosa wakati ni harusi ingojeayo matanga ya kulipa kwa walipaji? Najali nini wakati sitalipa? Acheni kuuliza mambo haya nisiwapoteze bure.
Tatu, kuanzia sasa, nitatembelea kaya nzima kuanzisha na kukagua au kufungua ‘miradi’ ya kipwagu na pwaguzi ili kuwavutia wapika kura. Katika safari na ziara zangu, lazima nimwage njuluku kama sina akili nzuri.
Nne, nitakuwa mkarimu na mpole huku nikichanganyikana na mafyatu bila ulinzi kama ilivyokuwa kabla ya kuanza kampeni za kampani hadi waniamini na kuingia laini. Nitaingia kwenye majumba yote ya ibada na kuwamwagia mamilioni. Natoa angalizo. Mnene wa dini yeyote, orijino au feki na ya kujipachika, atakayenipinga, nampiga stopu kwa kuchanganya dini na siasa. Wajue, nitafunga maduku yao ya kuuza roho na neno. Atakayeniunga mkono na kunipigia ndogo ndogo, ruksa. Maana, huku si kuchanganya dini na siasa bali kudumisha amani na mshikamano japo kwa imani ya amani.
Tano, kila nitapozuru, lazima kutoa ahadi milioni kidogo bila kusahau kumwanga njuluku kwa wapika kura ya kula na kuwaahidi kwa kuwafyatua kuwa huo ni mwanzo tu ili wangie bila kujua kuwa, nikishaukwaa, nitawafyatua mkenge. Najua, mafyatu walivyofyatuka, watanipa. Na wakinipa, sitawapa baada ya kupewa. Watajua kuwa hawajui na wakijua hawatajua kuwa hawakujua.
Sita, nitaanza ‘kukemea na kukoromea uoza’ ili kuwafanya mafyatu waote kuwa kaya yenye haki na tajiri kuliko zote duniani. Mfano, kila niendapo, nitatoa takwimu za kupikwa kuwaweka sawa. Nitawambia kuwa mimi ni muaminifu kuliko hata malaika na kwa Joji Kichaka na Trumpet, ndiyo maana nakopesheka.
Saba, kwa vile sina wapinzani wa maana, nitawakandia wapingaji, ambao wengi wao wako mfukoni mwangu, kuwa hawaaminiki kama mimi japo wote, kiukweli, hatuaminiki sorry, tunaaminika. Nitawasilibia na kuwakandia kinomi. Nitasema kuwa wao wakipata ulaji, wataanza kuwatumia badala ya kuwatumikia. Watadanganya badala ya kuwaambia ukweli, kuwadhalilisha badala ya kuwaheshimu, kuwaibia badala ya kuwa waangalizi wa njuluku na mali zao.
Nitasiliba zaidi na kusema kuwa wao wanawaita funza badala ya mafyatu kiasi cha kuwaburuza badala ya kuwashawishi, kuwatesa badala ya kuwadekeza, kuwatenga badala ya kuwaunganisha.
Nane, nitaamuru magazeti yangu ya umbea kunipamba kuwa hajawahi kutokea kiongozi kama mimi tangu dunia kuumbwa. Hivyo, mafyatu wakinyima kura, wajue, wanajitia kitanzi wenyewe. Pamoja na kuwa njuluku nitakayotumia ni ya mafyatu, nitawaambia wapambe na waimba mapambio yangu waseme kuwa hii ni njuluku ya Fyatu kila ninapotoa njuluku.
Tisa, nitahubiri amani na mshikamano katika kupeana ulaji lakini si katika kula. Hivyo, yeyote anayenipinga, anapinga amani, maendeleo, na mshikamano wa mafyatu.
Kumi, nitapiga marufuku mikutano ya wapingaji na wapinzani wangu iwe ni wa wazi au kwa kificho. Nitaamuru wakubwa wa ndata za mafyatu kuvuruga mikutano ya wapingaji iwe ni kwa kuwakataza, kuwachelewesha, au kuwapa maeneo yasiyovutia ili niwapige chini kirahisi japo nao si wapingaji bali wasanii wanaotafuta ubwabwa na kutaka kuuma umma wa mafyatu. Hamjawasikia wala mafyatu wa chata la CHAKUUMA? Je wanawauma nani kama siyo mafyatu waliogeuzwa ubwabwa? Mtawaona wakidemadema na kusepasepa msijue kuwa kinachoitwa pilau si kingine bali nyinyi muhongwao udohoudoho na kuishi kwenye uchochole tokana na kughairi kufyatuka, kuendekeza tamaa, na uzwazwa hadi mkafyatuliwa kizwazwa. Nani awezaye kumvua samaki bila chambo au kwa chambo kitupu? Thubutu yako? Nioanavyo na nijuavyo, japo samaki ni hayawani, ni wajanja kuliko mafyatu wanaofyatuliwa kizwazwazwa hivi. Japo mafyatu nitakaowafyatua wanadhani wananifyatua, ukweli tutauona nikiisha ukwaa na kuanza kuwafyatua bila huruma. Nadhani hawa hawanijui uzuri.
Mwisho, nitachapisha mabango makuuuubwa tena ya mabilioni na kuyaweka kila mahali ili mafyatu wanione na kunipa. Najua. Wap viherehere wakataotaka kuhoji namna nilivyotengeza huu ukwasi na ninanunua nini. Hawa wasiwape taabu. Nitawazushia kesi kibao na kuwasweka lupango hadi mtiti uishe na kupita ndo niwaachie waendelee kupayuka huku mie nikikamua. Du! Kumbe naota!
Chanzo: Mwananchi Jana.
Faida za Kutofichana Siri na Vipato
Hakuna kitu kizuri na chenye faida na furaha kwa wanandoa kama kutofichana mambo au siri. Hapa tutaongelea athari na madhara ya kufichana kipato au kila mwanandoa kuwa na chake badala ya chetu. Wanandoa wanapokuwa wawazi kwa wenzi wao, licha ya kuwapa kuaminika na kujiamini, huwasaidia pale wanapokumbwa na misukosuko ya kifedha au kiuchumi kama vile kufilisika, kuachishwa kazi, kuugua, na mengine kama hayo. Faida nyingine ya kutoficha kipato ni kutosumbuliwa kwa kudaiwa matumizi ambayo mhusika hana uwezo nayo. Mbali na hilo, pia, hujenga kuaminiana na kushirikiana katika dhiki na raha.
Faida nyingine ya kutokuwa na siri ni ule uhuru katika maisha ukiachia mbali kutojiruhusu kuujengea moyo wako shinikizo litokanalo na kutunza siri au uwezekano wa kufichuliwa siri. Kimsingi, siri ni kama mgando kwenye moyo (clot) wa mwenye kuiweka. Au tuseme ni moto unaounguza taratibu wenye kusababisha maumivu makali na makubwa yasiyotabirika wala kuisha. Siri ni mateso kwa mwenye kuitunza hasa siri yenyewe inapokuwa haina ulazima. Mwenye kuficha siri hana uhuru wala amani moyoni. Mwenye kutunza siri inayoweza kuivunja ndoa yake hana tofauti na mgonjwa wa kansa. Haiponi na mwisho wake ni maangamizi na misiba kwa wanandoa na familia zao. Kimsingi, mwenye kuwa na siri ana mzigo mkubwa tena unaoumiza moyo wake kila siku mbali na kumgharimu fedha, furaha, hata uhai wakati mwingine.
Kitu kingine kinachoweza kutoa funzo na mwanga juu ya siri ni ule ukweli kuwa duniani hakuna siri tena siri ya watu wawili au zaidi. Ipo siku, kama harufu, inzi mmoja ataifichua na kuwaumbua na kuwaumiza wenye siri husika. Hii ni kutokana na ukweli kuwa binadamu hatutabiriki. Wewe unaweza kutunza siri yako. Je mwenzako au wenzako wanaweza? Kawaida, siri huvuja pale mmoja wa watunza siri anapofurahi au kuchaganyikiwa akaitoboa kwa mwingine adhaniye naye ataitunza kama yeye asijue bindamu hatutabiriki na tunabadilika. Kama serikali yenye maguvu na vyombo vyote vya usalama inatunza siri za uhai na utendaji wake, wanandoa ni nani wasifanye hivyo? Kama Mungu ametunza siri kama vile ya uumbaji na kifo, sisi ni nani tuanike siri zetu hadharani. Kwa faida gani na ya nani wakati tunajua hatari na madhara ya kufanya hivyo. Tia maanani. Dawa ya siri ni kutokuwa na siri.
Turejee kwenye kipato. Mfano, utakuta baba au mama anajali kazi yake kuliko hata ndoa! Tunakwenda wapi huko kusiko na maana wala mwelekeo? Busara haachi kuhoji hata akiitwa mkale na aliyepitwa na wakati. Ajabu, huyu ajalie kazi na kuvunja ndoa yake, akimaliza, hujikuta kazi haimtoshelezi kiasi cha kuanza kutafuta ndoa hata kwa watu wazima kuwaandama hata kuwatumia vijana wa umri wa watoto wao. Je huku si kudhalilika au kujidhalilisha?
Nani alijua kuwa ndoa inahitaji karatasi badala ya mapenzi na uaminifu? Tumeona makasisi wakizini hadi kufikishwa mahakamani. Wengine wamenajisi hadi kuuawa kwenye uchafu wao. Wengine wanaongozwa na mashoga. Je hawa na wauaji wana tofauti? Lakini bado wanatunza siri hii ambayo baadaye hufichuka na kuwaumbua na kuwaumiza. Maana, muuaji siyo auwaye mwili bali hata auawaye roho. Auwaye roho ni muuaji mbaya kuliko auawaye mwili. Mwili huoza. Nani anajua majaliwa ya roho iliyouawa na wale iliowaamini wakati hawaaminiki? Nani anajali wala kujiuliza swali kama hili? Kisu na mnafiki heri kisu maana waweza kukitahadhari. Heri mlevi umuonaye mtaani kila siku kuliko mnafiki aliyejificha kwenye utauawa au madaraka akidhani ni siri. Tusemayo siyo mapya, jipya ni kuyasema na kuyaandika.
Tumalizie kwa kushauri na kusisitiza kuwa hakuna faida ya kuwa na siri kwa wanandoa ingawa ni vizuri kutunza siri za ndoa yao huku wakiepuka kuwa na siri nje ya ndoa yao. Siri ni mbaya na nzuri kutegemea na hiyo siri ni juu ya nini, inawahusisha nani na kwa faida gani na ya nani. Kama siri inalenga kujenga na kuimarisha ndoa, inafaa na kuswihi. Kama siri husika ni ya kubomoa ndoa, basi iepukwe mara moja.
Mwisho, katika ndoa hakuna kazi wala mali yangu au yake bali yetu hata kama mna kazi, mali, na majukumu tofauti.
Chanzo: Mwananchi J'pili iliyopita.