Kuna visa vingi ambapo ndoa nyingi zimeharibika na kuvunjika kutokana na michepuko. Je, inakuwaje watu wawili waliopendana huamua kusalitiana wakijua wazi kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwa na mwisho mbaya licha ya kuwaumiza wenzao? Jibu si rahisi na wala moja. Kuna sababu nyingi sababishi mfano, kuingia kwenye ndoa bila kufanya utafiti, maandalizi, uaminifu, na kukurupuka kwa wahusika. Sababu nyingine ni ukosefu wa maadili kijamii ambapo, zamani, mambo haya yalionekana kama machukizo tofauti na sasa yanapoanza kukubalika kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kijamii na kiuchumi.
Inakuwaje wanandoa wanakosa uaminifu ilhali wawalikutana, kupendana, na kuamua kufunga ndoa? Kama ilivyo kwenye swali kuu, majibu ni mengi na si rahisi japo zipo sababu nyingi.
Mosi, licha ya watu wengine kutokuwa na uaminifu, kuna uwezekano walipooana, walifanya pupa na matarajio makubwa kuliko uwezo wao wa kuyakidhi. Kujua hili, tujiulize. Kwanini watu huoa na kuolewa? Mtaalamu na mwandishi wa masuala ya ndoa Jennifer Pace anatoa sababu kadhaa.
Mosi, kupata uhalali wa kisheria wa wawili kuishi pamoja bila kubughudhiwa ambapo huanza maisha ya pamoja kupata kibali/uhalali kuishi pamoja toka kwa familia na jamii kwa ujumla, kutambulika, kuheshimika na kuwa na haki zote pamoja.
Pili, kuonyesha kujitoa kwa kila mmoja kwa mwenzake na kupendana, kulindana, kuhifadhiana kwa wawili walio katika ndoa kuishi na kujenga familia pamoja.
Tatu, ni hatua ya juu ya kuonyesha mapenzi kwa mwenzi kiasi cha kutegemeana na kusaidiana katika maisha ya wawili, na kujenga mtandao thabiti na wa kuaminika wa huduma kwa wawili. Mfano, unyumba ambao ni mojawapo ya hitajio na msingi mkuu wa ndoa, japo yeyote anaweza kuupata atakapo, si kila autakapo ataupata nje ya ndoa kutokana na vikwazo vilivyopo katika mahusiano ya binadamu. Mbali na unyumba, kuna kuzaa na kulea watoto, kuwalea, na kuwatunza . Hili uhitaji ukaribu na utayari kulitekeleza. Hii pia, hutoa fursa kwa watoto kujifunza mahusiano na upendo mbali na kuwahakikishia usalama wanandoa na watoto wao.
Mbali na sababu tajwa hapo juu, kuna sababu nyingine kama vile mazoea ya binadamu kuwa lazima wahusika wafunge ndoa ili kujenga familia na kuzaa watoto mbali na kuishi pamoja kisheria na bia kuingiliwa wala kubughudhiwa.
Pili, wapo wanaofunga ndoa kutokana na msukumo wa jamii hasa familia. Wazazi wanataka kuona wajukuu wao na kuendeleza ukoo. Pia, wapo wanaolazimika si sababu wamependa au kupanga kufanya hivo. Hapa, ndipo linapokuja suala la ndoa za mkeka, ndoa za kutafuta vitu kama vile wazazi kutka mahali kubwa iwe fedha ua wanyama, kufuata kipato au utajiri wa mhusika mmojawapo na mengine kama mengi.
Wakati tukiyadurusu haya, tukumbuke. Binadamu ni mwenye tamaa anayejijali kuliko wengine. Je anaachaje tabia hii? Hakuna jibu moja kukubaliana na ukweli kuwa ndoa ni tiba ya tatizo hili lisababishalo kutafuta michepuko wasijue si jibu bali tatizo. Hawa, sawa na wengine wanaofanya hivi, huwa wana tatizo ambalo wanashindwa kulitatua. Hamjasikia kuwa utamaliza mabucha lakini nyama ni ile ile? Kama nyama ni ile ile, sasa inakuwaje mtu anakimbia “nyama ile ile” kwenda kutafuta nyama ile ile? Hapa ndipo mzizi wa tatizo, yaani kukataa kukubali kuwa nyama ni ile ile. Hivyo, chanzo kikubwa cha tamaa na uwepo wa michepuko, licha ya tamaa, ni ujinga na kukataa halisia wa kimaumbile na ukweli.
Tunashauri wanandoa waangalie faida na hasara za michepuko kwa afya na maisha yao na wenzao. Michepuko, licha ya kusababisha msongo wa mawazo wa kutunza siri, inasababisha watu wengi wapunguze umri wao wa kuishi tokana na msongo wa mawazo na shinikizo la kutumikia mabwana wawili. Hapa jibu ni kuacha tamaa. Kwani, nyama ni ile ile.
Chanzo: Mwananchi, Jpili leo.
No comments:
Post a Comment