Kwa mfano, takwimu za mwaka 2019 za jeshi la polisi nchini zilitaarifu kuwa wanaume 750 waliua wake zao na 74 kati yao wamejiua huku wanawake 158 wakiua waume zao na 39 kati yao kujiua. Mwaka 2020 waume walioua wake zao ni 226 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 30, huku wanawake walioua waume zao ni 71 na kati yao 12 walijiua baada ya kuua waume zao. Wimbi la mauaji ya wanandoa liliendelea. Mwaka 2021 (hadi Septemba 30) waume walioua wake zao ni 156 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 16, ilhali wanawake walioua waume zao ni 29 na kati yao 9 walijiua baada ya kuua waume zao. Duniani kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, 40% ya vifo vya wanawake duniani 6% hutokana na vifo visababishwavyo na wenzi wa wanandoa.
Wapo wanaoua wanaoua watoto kwa sababu za kubambikiwa na wenzi wao kadhia ambayo imeshamiri na kuweza kubainika baada ya kugundulika kipimo cha DNA kinachoshughulika na urathi. Pia, wapo wanaoua akina mama na kuwaacha watoto wakati pia wapo wanaoua wote ukiachia mbali wanaoua wote nao wakijimaliza. Akina mama acheni jinai na mchezo huu ambavyo, licha ya kuweza kuwaumiza, pia huumiza watoto wenu wasio na hatia. Japo si rahisi kuvaa viatu vya watenda na watendewa, hatujui kama kuna binadamu mwenye haki ya kuutoa uhai wa mwingine hata angekosewa vipi hasa ikizingatiwa kuwa sifa mojawapo ya binadamu ni kukosa na kukosea.
Je, ni nini kifanyike?
Kuna masuala na maswali ya lazima na muhimu tunayopaswa kuhangaishwa nayo ili tuweze kushinda na kuondoa kadhia hii inayoelekea kuwa janga kwa binadamu wengi wasio na hatia ambao ni tegemeo la kesho kwa kila jamii. Hivi Mungu angeamua kutumia kutuhukumu, wangapi wangeendelea kuishi na kufaidi mema yake? Unauaje kiumbe au viumbe ambao huwezi kuumba? Je, wanapowaza kuwaua watoto huwa wanajiuliza kuwa kama wangekuwa wahanga, wangefanya au kutaka kufanyiwa nini?
Tuzidi kujiuliza zaidi. Hivi watoto huwa na makosa gani au mchango katika jinai hii zaidi ya kuwa wahanga na matokeo ya visababishi tajwa hapo juu? Je, wauaji au wale wanaopanga kufanya hivyo waliwahi kujiuliza wangekuwa wapi kama wazazi wao wangekuwa katili na hovyo kama wao? Hii inatoa picha gani kwa watoto kwa ujumla? Kwani hakuna namna nyingine ya kutatua matatizo yenu hata kuadhibiana ikibidi zaidi ya ukatili na mauaji dhidi ya watu wasio na hatia? Je, wanapowaua au kuwatesa wahanga, wanapata nini zaidi ya kuongeza uzito na ugumu wa tatizo?
Japo wahusika wanaweza kujitetea, kuhadaa wengine au kujiridhisha hata kujidanganya na kujipa imani bandia kuwa wanafanya mauaji na ukatili dhidi ya akina mama na watoto kutokana na kuudhiwa, hawana sababu zozote za msingi kufanya hivyo.
Tuhitimishe kwa kushauri akina baba wanaogundua jinai kama hii, watulize akili zao na kuvaa viatu vya wahanga. Kama wakifanya hivi, hamna haja ya kuwaua watoto wasio na hatia hata hao waliowabambikizia. Cha msingi ni kuachana nao salama na kuanza maisha upya pamoja na kuumizwa sana. Pia, ni vizuri kukumbuka kuwa wakati mkipendana hao watoto hawakuwapo wala hawakushiriki zaidi ya kuwa matokeo ya kazi yenu.
Chanzo: Mwananchi leo.
No comments:
Post a Comment