The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 29 October 2025

Fyatu anapomkumbuka Fyatu Mchonga kifyatu


 

Mpendwa Fyatu na mzee mwenzangu mwana wa Mzee Burito uliyelala kishujaa pale Mwitongo,
        Kwanza, nakusalimia kwa jina la Ujamaa na Kujitegemea uliotekwa, kupotezwa na kuuawa na baadhi ya mafisi na wahuni kama wabongo wako uliokufa ukiwalilia. Hebu tujuzane kifalsafa mafala wafulie. Kwa sasa, tuna uhujumaaa na kujimegeae. Wachache wanajimegeaa huku wengi wakifa njaa, kwani, hawana cha kujimegea baada ya uhujumaa kuwahujumuu. 
        Wahuni uliowakataa 1995–––baada ya miaka kumi ya jamaa yako, yule fyatu mwanafunzi wako Beni Nkapa–––walijipenyeza na kuwatesa mafyatu wakiwaibia walivyotaka. Sasa, wanatesa na kutanua wakikamua na kupiga kama hawana akili nzuri baada ya kujitoa ufahamu. Kule ikuu siyo patakatifuu patakatifuu bali patakachafuu pa patakachafuu. Acha nikusalimie halafu nikumegee stori nyinginezo.
        Una hali gani, ushaacha ufyatu? Je, huko ufyatu ni dili au mnalala tu? Vipi mzee Madiba na Kenneth Kaunda mshaonana? Basi, wape hi. Usiwasahau akina Sam Nujoma, Dawda Jawara, na mashujaa wengine walioko huko walioacha tuna na si uchafu kama mafisi wengine unaowaona huko kama vile Mobutu, Abacha, Bokassa, Bongo, Eyadema, Houphouet-Boigny, Kamuzu, Kenyatta,  na wengine.
        Pili, ujue sikukusahau kwa kuwasiliana nawe wiki moja nikiwa nimechelewa. Wajua? Siku hizi, mafyatu wenzako tunaisha mafichoni. Huko hakuna mtandao. Hata huu ujumbe unaoupokea leo ni kwa sababu nilikuwa mafichoni karibu na mpaka na kaya ya kufuata nyayo bila hata kufikiri wala kujua ni za nini. Sikwambii ni Lunga Lunga, Namanga, au Sirari. Hii ni chiri. Nikitaja, naweza kutekwa, kupotezwa, kuteswa, na kuteketezwa. Usijali. Nilimtwangia Madaraka na kumpa salamu amfikishie Mama Maria. Hayo tuyaache fyatu mwenzagu uliyesifika kwa ufyatu hasa kutetea haki na usawa na kupinga uhuni.
         Siku hizi, kuna mashetani wasiojulikana japo wanajulikana, wanaoteka, kutesa, kupoteza na kuua kana kwamba hakuna lisirkal. Mchezo huu mchafu ulianza baada ya kangosha kenye hasira kama nyoka kujipenyeza na kuufyatua unene. Ni pale wanamitandao uchwara ya jinai walipofyatuana. Kajamaa kaliwazidi kete hadi kuwavurugia kila kitu kabla ya kufyatuka roho ghafla kwenye mazingira yanayotatanisha.
        Juzi, kuna ‘mhuni’ mmoja aliyewageuka wenzake na kuanika uchafu wao hadharani. Si alijisahau akazoza bila kuchukua hatua! Walimnyaka. Mpaka sasa, hatujui kama bado yuko hai au mmeishaonana huko uliko. Huyu ‘mhuni’ mgeni kwenye kundi la wahuni aliibuliwa na kale kangosha. Kalimpandisha vyeo kama hakakuwa na akili nzuri. Ubaya ni kwamba jamaa mwenyewe alipewa usemaji wa chata lako na akajisahau na kusahau kuwa kutesa ni kwa zamu! Alizoza sana.
        Kale kajamaa kalipofyatuliwa, naye ulaji wake ukafyatuliwa akaamua kuwaumbua wenzake asijue wangemfyatua na kumpoteza. Huyu, pamoja na mchungaji, sorry, mchunaji kidhabu mwenye jina kama Jimmy walijisahau wakataka kufyatua huku na kule wasijue wahuni wenzao wasingevumilia uhuni na uchangudoa wa kisiasa. Mchunaji bado hawajamnyaka. Anapumlia mpira baada ya maduka yake ya roho kufyatuliwa.
            Ngoja nikupe inshu nyingine. Una habari kuwa kangosha kalihamishia makao makuu ya kaya Idodomya? Ila baada ya kufyatuliwa, naona kama waliokuwa wamefyatukia Idodomya sasa wanarejea Dar Si Salama. Je, wajua kwanini naiita Dar Si Salama? Misongamano baba. 
    Ukifika Dar utazimia kama siyo kujinyotoa roho kuepuka ngwalangwala na pikipiki kukunyotoa roho. Ukiwa Dar, siku hizi, unajiendeshea utakavyo kama huna ving’ora kama wale wanaong’ara kwenye vururu vururu na fujo usipime. Mijengo itokanayo na njuluku zenye kutia shaka imeota kama uyoga. Madereva wa sasa, hasa wa tukutuku, wana akili ndogo kuliko punda ambao wapitapo mitaani wako organised.
        Kaya imegeuka dampo la kila uchafuu toka Chaini, kaya yenye jina kama Bata mzinga, ugabacholiini, nk., usiseme. Viwanda ulivyoacha vikanusurika kufyatuliwa na mwanafunzi wako vilishapigwa mnada na kugeuzwa magala ya kupokelea uchafu sorry bidhaa toka nje. 
        Cha mno, siku hizi, ukiwa munene–––hopefully, unajua maana yake–––unaweza kumteua hata mkeo kuwa munene. Najua, uliwahi kuonya kuwa unene, hasa urahisi, haupaswi kutegemea ushauri wa mke, mume, au hawara. Siku hizi, ni ruksa kama alivyowahi kusema mzee ruxa ambaye nadhani mshaonana akakupa stori za huku. Kabla sijasahau, wahuni watatu waliokuwa viranja wa mtandao ulioupiga stopu, Ben, Ed, na Sam, nadhani mshaonana? Tuyaache.
        Kabla ya kumaliza, ngoja nikufyatulie inshu. Zamani, tukiitana ndugu bila kujali dini au kabila. Sasa, tuna matabaka ya mafyatu, wababe, na machawa wasifikao kwa kujikomba na kujigonga huku wale wanaojigonga kwao wasiwakemee kana kwamba wanafurahia na kuunga mkono jinai hii ya fyatu wazima kujigeuza wadudu tena wachafu na wanyonya damu. Tuyaache.
            Du! Ni usiku. Nasikia kama kuna watu nyuma ya maficho yangu. Acha nikuache nikitoe kabla hawajaninyaka na kunipoteza nikasahaulika. RIP Fyatu Mzee mwenzangu Nchonga.
Chanzo: Mwananchi Jtano iliyopita.

Kama unatafuta ‘malaika’ usioe au kuolewa

Kuna msemo wa Kiingereza wa Miss au Mr. Right” wakimaanisha mke au mume material au afaaye. Sisi, kama wanandoa, tumepitia kipindi hiki cha kusaka mchumba. Bahati nzuri si kupitia tu, bali tulihitimisha kwa mafanikio kiasi cha kuweza kutoa ushauri kwa wengine. Kama kichwa kionyeshavyo,bila kujali dini na kila kitu kikutofautishacho na wengine, kama unatafuta kuoa au kuolewa malaika, wala usipoteze muda wako. Hayupo, hakuwepo, na hatakuwepo. Kimsingi, kama ulivyo binadamu mwenye ubora na udhaifu, hata huyo unayemtafuta ni binadamu mwenye kila sifa uliyo nayo. Hivyo, katika kutafuta mchumba, epuka kutafuta malaika au mkamilifu. Hayupo.
            Kama ilivyo kwenye ukamilifu, pia ujue. Kama wewe, hakuna aliye shetani. Wote tuna ubora na mapungufu ambayo hatuwezi kuyavua bali kujifunza namna ya kuishi nayo tena kwa furaha. Hivyo, somo la leo litajikita katika kudurusu namna ya kupata anayefaa kwa viwango vya kawaida vya kibinadamu.
            Mosi, wakati ukitafuta mchumba, yakupasa ujichunguze na kujielewa kwanza ili uwe na taswira umtakaye. Mfano, kama wewe ni muovu, tegemea kupata muovu lakini si vinginevyo. Ingawa wakati mwingine hutokea watu wasiofanana kisifa kuoana japo hili nalo huwa na changamoto zake hasa wanapondua kuwa ni paka na panya ndani ya nyumba moja. Wapo wanaotambua udhaifu wao na kuufanyia kazi pia wasiokubali kubadilika.
            Pili, ujue kuwa kutafuta mchumba siyo mchezo wa kubahatisha bali kujitahidi uwezavyo kumtafuta na kumjua unayemtaka. Hapa, uhitaji kila aina ya ubunifu mfano, kumsikiliza mwenzio, kumsoma, kumdadisi, hata kumchunguza hata wakati mwingine bila ya yeye kujua. Hili ni muhimu sana kwa vile ukiishaingia, umeingia. Japo wapo wanaoingia na kutoka, ila huwa hawatoki salama. Hivyo, uwe makini wewe utafutaye mchumba. Washirikishe wazazi katika msako huu.
            Tatu, japo waweza kupata asiyelingana na vigezo na viwango vyako baada ya kujipima kama nawe unavyo, kuna fursa ya kubadilika kama mhusika akijua udhaifu wake na kuwa tayari kuufanyia kazi. Hapa, tuwe wazi. Kuna madhaifu yanayobadilishika na yasiyobadilishika. Mfano, mwenzio kama ana imani, tabia, na welewa tofauti, haya yanabadilishika. Ila kama siyo muaminifu na mwenye upendo, hapa kuna tatizo tena kubwa tu. Ni juu yako kuamua kama utakuwa tayari kuvumilia au kuachana naye kabisa kabla ya kuingia kwenye mkataba wa kudumu.
            Nne, ni vizuri kupima kama wote mnajua vilivyo mnachokusudia kufanya. Hapa, tuonye akina dada. Wapo wachumba wenye tamaa tena wasiojua wanachotaka wala kufanya. Hawa, wanaweza kumuingiza mtu mtegoni wakamharibia maisha halafu wakamuacha solemba. Tuna visa vingi tujuavyo ambapo mabinti hata wavulana waliacha wachumba wa maana wakaishia kuangukia kwenye mikono ya mashetani waliowaharibia maisha na kuwaacha.
            Tano, epuka na ogopa mtindo wa kuanza maisha ya ndoa kabla ya kufunga ndoa. Hapa, kuna aina mbili. Wapo wanaokubaliana kuanza kuishi kabla ya kufunga ndoa. Na wale wanaolazimika hasa wakishapeana ujauzito na kugundua kuwa hawafaani na hawawezi kuishi pamoja kama wanandoa. Wengine, hubambikiziana mimba ili kulazimisha wanaotaka wawaoe wawaoe wasijue mwisho wake waweza kuwa majuto yatokanayo ya kufanya makosa yasiyoweza kusahihishwa. Ukishakuwa mjamzito au kuanza kuishi kama wanandoa bila ndoa, ule ujana na mvuto wako vinaisha na haviwezi kurejeshwa tena. Kizungu wanaita spendforce au kukosa mantiki katika jambo ambalo ulikuwa na mantiki.
            Sita, epuka pupa na tamaa ya kuingia katika ndoa bila kujiridhisha kuwa umefanya homework yako vizuri. Maana, ukishaingia ni vigumu kutoka.
            Mwisho, tumalizie na ubinadamu wa mtarajiwa. Hili ni la kuzingatia sana. Binadamu wote tuna mapugufu sawa na ubora na huu ndiyo ubinadamu ingawa tunazidiana katika hili. Hakuna aliyekamilika japo yupo anayerekebishika. Hivyo, watarajiwe wajitahidi wawezavyo kupata wanaowafaa kwa vile hakuna malaika wala shetani bali binadamu. Kuna mapungufu kama vile elimu, kipato, na mazoea madogo madogo vinavyobadilika kulingana na utayari wa wahusika. Hivyo, katika kutafuta mtarajiwa, hakuna malaika wala shetani bali binadamu. Hivyo, wahusika waepuke kutafuta malaika. Kwani, hayupo na hawatampata. Wakimpata, wajue ni umalaika wa muda tu.
Chanzo: Mwananchi Jpili juzi.

Fyatu afyatuliwa kupenda ‘kupendwa’ na kusifiwa!

 



Mfyatuko wa leo si wangu. Hata kama ni wangu, si wangu. Hayo tuyaache. Msomaji na shabiki wangu mmoja aliniandikia yafuatayo, nami nikaona nishare nanyi. Sharing is caring. Fyatu huyu aliandika: Kuna mafyatu wana ugonjwa wa ukosefu wa ubunifu kiasi cha kugeuzwa wadudu. Mafyatu, sorry, wadudu hawa wana silaha moja tena ya hovyo. Nayo ni kujikomba, kusifia hata ujinga, kujigongagonga, kutabiri upuuzi, kuimba pambio na mashairi tena wamuimbiaye akiwa kipofu na taahira. Je, hapa tatizo ni nini? Ni wale wasifuo au wale wasifiwao au wote? Kwani, nani asiyejua? Kizuri huwa chajiuza na kibaya chajitembeza?

            Sijui sijui na kama najua sijui hali halisi! Sijui kwanini fyatu huyu aliniandika maneno ambayo naona kama hayanihusu au hanielewi, au niseme. Aliamua kunichafua na kunichafulia sifa nzuri ya kutopenda kufisiwa. Fyatu sitaki wala sihitaji kusifiwa tena wanafiki na wasaka tonge ambao wanaweza kukugeuka hata kukuuza wakati wowote wakiahidiwa na maadui zako tonge kubwa kuliko uwapalo hata kama ni uongo. Asiyejua hili ajue. Anayejua akupuuzia ajue. Anajipuuzia mwenyewe. Onyo, si kila wakusifuo wanakusifu. Wengi wanakuramba kichogo na kukugeuza bunga wakutumie na wakishafanikiwa, unatupwa kama diaper achia mbali ganda la muwa ambalo, lau, sisizimizi waweza kurirudufu. Wanakuponda wakikudanganya wanakupenda wakati ukweli mchungu ni kwamba wanakuchukia. Kahaba huwa hapendi wateja wake bali mifuko yao fedha. Zikiisha, nawe unaisha. Uliyedhani anakupenda, anaweza kukulinganisha hata na kaburi. Ukimpenda fyatu vilivyo na kimakwelini wamwamba ukweli hata kama wauma siyo kuuma na kupuliza.

Kitimoto ni kiti fire hata apakwe blusher. Juhaa ni juhaa hata aitwe mjuvi. Kiti fire ni mchafu tu hata apakwe mafuta na kufukizwa ubani na utuli. Fisi ni fisi hata avishwe ngozi ya kondoo. Cha hovyo ni cha hovyo hata kisifiwe vipi bado kibaki kuwa hovyo. Sijui kama kuna mashonde au ushuo(zi) mzuri. Sijui na sitaki hata kujua. Ubaya ni ubaya hata uitwe uzuri hauishi ubaya wake. Urongo ni urongo hata uitwe ukweli na kuaminika bado ni uongo. Hakuna uongo mbaya kama kuwadanganya wengine halafu nawe ukajidanganya. Isitoshe, hakuna uongo wa kudumu bali ukweli.

 Ni mpumbavu apangaye kupaka rangi upepo. Sikieni maneno haya ya mwenye akili lau yawaweke huru. Mtumwa awe wa kujituma au kulazimishwa ni mtumwa. Tofauti ni kwamba mtumwa wa kulazimishwa anaweza kujikomboa ilhali yule wa hiari anachukia na kuogopa ukombozi. Huyu, hana tofauti na kuku atagaye mayai na kulishwa nafaka kavu ilhali mayai yake yenye virutubisho yakiliwa na wengine. Mbwa hulinda mali lakini yu maskini daima. Sindano hushona nguo ila siku zote i uchi. Ngoja niachie hapa kupiga kelele kimya kimya na kuwaza kichini chini.

Hakuna mashindano mabaya na ya hovyo kama fyatu kushindana mwenyewe. Unajiuliza. Unapowaua au kuwazuia wapinzani wako kuingia uwanjani mshindane ukashindana na ombwe, kweli unashindana au unajidanganya? Huwezi kuniandikia haki halafu ukaziua na kunifanya nizipate zikawa haki. Hii si haki bali dhihaka. Woga ni ugonjwa mbaya ambaye humfanya mwoga kujifanya shujaa wakati ni mwoga. Kuna wakati mafyatu wasiofyatuka wakafyatua wanaogopa hata vivuli.

Asiyejua wala kuchelea kesho hana tofauti na maiti. Unawezaje Kutenda mabaya ukategemea mema? Unawezaje kuumiza wenzako nawe usiumizwe hata kama si leo wala kesho. Watenda maovu wanajua uovu wao. Hata hivyo, japo wanajua matokeo ya uovu huu, wengi hujifanya hamnazo na kujitoa akili wakidhani siku yao haitafika. Wenya akili sawa sawa huwapenda wanaowakosoa na kuchukia wanaowasifia ujinga na uongo. Heri akulaumuye kwa haki kuliko akusifuye kwa hila. Kwani, hawapo? Jana, jana walimsifu fulani. Leo wanambagaza. Walijifanya wanampenda. Leo, wanamchuuza tena kwa sababu ya sifa na udohoudoho. Hao ndiyo mafyatu wasiofyatuka. Wanaweza kukukweza nawe ukakwea usijue watakushusha kwa aibu!

Ndugu zanguni ogopeni sifa. Sifa za uongo ni mbaya kuliko hata upupu kwani, waweza kuoga ukakutoka. Sifa za wenye hila ni kaburi la wamsifiaye. Kwani, humpotosha na kumdanganya akapotoka, akadanganya na kujidanganya. Waweza kudhani mko pamoja kumbe kila mtu ana safari yake. Wapo wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa ili unogewe wakupige visu. Tumeyaona au tunajisahaulisha?

Ukiona mchugaji anamsifia ng’ombe unono, ujue ana mpango wa ima kumuua au kumuuza. Kuku hata alale kwenye kitanda, bado ni kuku. Atayarunda humo. Nani awezaye kumfuga swila asimng’ate. Heri swila swila kuliko swila mdudu. Kunyamaza si ujinga na kusema sana si busara. Kuna wakati fyatu anapaswa kukubali kujisuta kabla ya kusutwa. Heri ajisutaye kuliko asutwaye japo kote ni kusuta. Ni kiziwi pekee asiyesikia wala kufaidi muziki. Ni kipofu pekee asiyehitaji mwanga. Nondo ni mdudu wa ajabu. Huona moto na kujitupa mwenyewe akidhani anaota moto.

Hayo ndo yalinikuta mwenzenu toka kwa moja wa mafyatu wangu katika kaya yangu niitawalayo, Fyatuland. Onyo, usione wamenyamaa ukadhani hawajui chafu yako hata kukuzushia. Du! Hivi niko wapi?

Chanzo: Mwananchi J'tano leo.

Wednesday, 15 October 2025





Go Raila Amoro Odinga go
Though you were an enigma,
Go this is your karma
Go you have finished your work
We can cry, grieve, sing, and talk
Go Raila it is life
Life is like that
Go life and death are twins
Sometimes, one loses
The other time, some gains
Yours is a mixed story
Some cry will grief
Some with relief
Raila go never look back just go
Go it is time to go,
Go nary turn your head back
Go Raila Go
Go Raila though you've left a lot of controversy
To some, you're a hero
To others you're a mystery
Above all, you were a schemer
What a go-getter
A do-gooder
Go Raila Go.
It is your time to go
As you came just go
Heroically, go
Go, go, go never look back.

Wabongo walivyomfyatua Fyatu asifyatuke akawafyatua

Nikiwa nimelowea ughaibuni kwa miaka kadhaa na kujigeuza mtasha wakati ni Fyatu tena Njomba, si nikajifanya kurejea home japo kusalimia jamaa lau kukumbushia zama zetu kabla ya Gen Z kutegeuza zii japo si wote kwa vile tunao Gen Ziro wetu wasiojua wala kufanya kitu. Nilirejea kwa mbambamba na mbwebwe na Bi Nkubwa na vitoi tulivyovitengezea huku lau ndugu wavijue na vijuane visije, siku moja, kupelekeana mashambulizi na posa mabuda tukaonekana hamnazo au kujitoa ufahamu kama yule kiherehere wa Msonga. Hayo tuyaache.
            Baada ya kupoa kwa mwezi mmoja na ushei, niliamua kutia timu tena ughaibuni kuendelea na kubeba maboksi kama kawa. Unatokaje Bongolalaland bila lau kubebea vitu vya kibongo? Watoi watakwendaje kuwaringishia wenzao bila vitu vya bongo ili kuonyesha kweli stori zao si rongorongo za kitoi au kutafuta ujiko usipopanda kama mwanasiasa na wachunaji wauzao neno kwa roho na uroho mtakakitu?
            Bila kutonywa, si tukaingia zetu kule wanapokalia koo aka vururu vururu vurugu mechi ya bodaboda na ndinga na maduka yaliyojaa hadi mashimoni na joto. Si unajua tena. Mafyatu wa kibongo ukigoma kuchunwa, wanauchuna ili washenzi wa Kalia koo na kwengineko wakunyonyoe wahondomole. Bila kuchelea mtima nyongo huu, we! Si tukaingia kwenye duka la gabachoooli mmoja aliyetupokea kwa bashasha kana kwamba huwa hatubagazani, hatubanangana, na kubaguana!
             Kwa vile haya tushayazoea ughaibuni ambako watasha wabaguzi hutuita watu wa rangi aka people of colour kama signal ya kutubagua, tulimpuuzia na kuendelea kile kilichotupeleka, yaani kunua chocolate na kumuachia usanii wake ulioficha ubaguzi na unyama na kuishia kivyetu. Hata hivyo, tulijifunza kitu. Wabongo wengi hawajui biashara. Ukienda dukani kwake, badala ya kukuchangamkia, anakuona kama umeenda kubomu au huna duka kama yeye wakati wote mna shida, yeye njuluku yako, nawe bidhaa au huduma yake. Kiduka chake kipo mtaa wa kwanza au wa pili kutoka Shimoni Sokoni kuelekea Mnazi Mmoja. Ni mtaa uliojaa maduka yaliyosongamana. Kwa vile tulikuwa tumehamanika na kufurahia kupata hii kitu, si tukasahau kuangalia tarehe ya kuisha matumizi! We! Nani anaweza kuamini kuwa tuliuziwa chocolate zilizoexpire mwaka 2022? Ni roho mbaya na ulafi kiasi gani?!!
            Baada ya kufyatuliwa hapo kwenye chocolate, tulikwenda kununua dhahabu za Bi Mkubwa ili naye akawaringishie wenzake kazini. Tulipiga guu hadi maeneo ya mtaa wenye Jina la waziri mkubwa wa India aliyeuawa kwa kutwangwa shaba. Kuna huyu Msomali. Anatuchangamkia kwa basha na kutupunguzia bei. Tulifurahi sana. Tulinunua dhahabu ya madafu milioni kumi na ushei. Guess what? Kumbe alipotukaribisha kwa bashasha hakumaanisha kutupenda au kutushobokea zaidi ya kujenga mazingira ya kumsaidia kuminya kodi!
            Baada ya kupata bangili, hereni, mikufu na vikuku, si jamaa akatuambia bei. Tulilipa bila kuuliza hasa ikizingatiwa kuwa madafu siku zote yako chini mbele ya dolari. Baada ya kumkatia chake, tulitaka atupe risiti. We! Jamaa alitushangaa na kuuliza “nyie wageni hapa?” Nami nilimuuliza alikuwa akimaanisha nini? Alijibu bila aibu “kwanini mnataka risiti wakati tunaweza kuwaandikia certificate na kuwapunguzia mambo yakaisha?” Kwa ushamba wake wa ughaibuni, Bi Mkubwa alidakia “why should we do that!” Kusikia hivyo, jamaa alizidi kucheka kwa tunavyogtindiganya mambo! Mie nilishangaa nisielewe kwanini alikuwa akinicheka kwa swali la kizalendo kama hili? Nilidakia? Wewe iko Tanzania au somali? Kama iko Tanzania, sasa zalendo iko wapi? Yule muuza dhahabu alizidi kucheka na kusema “kaka wazalendo wako wapi nchi hii? Kweli wewe ni mgeni.”
            Nijifyatua na kujifanya sijamuelewa. Jamaa alisema “umeona misongamano na uvunjaji wa sheria wakati unakuja hapa? Kabla sijajibu, aliniuliza “unaishi wapi hapa mjini?” Nilimjibu “Mikocheni.” Alisema “alaa! Kumbe hujui ugumu wa maisha hapa mjini siyo?” Kukatisha hadithi ndefu, jamaa anifyatua shule ya bure nikajiona kama bongolala. Alisema kuwa ni kweli wanakwepa kodi. Je wanaotaka walipwe kodi zaidi ya kuzifyatua, wanazifanya nini huku kuacha mafyatu washi kana kwamba hawana lisrikal? Kuona hivyo, nilikubaliana naye, mambo yakaishia hapo japo, hadi leo, roho inaniuma nikishindwa kumlaumu au kujilaumu kwa sababu, kama kungekuwa na waongozaji wazalendo, nisingekubali kushiriki uhujumu huu.
            Baada ya kununua bling bling za Bi Mkubwa, tulikwenda zetu mitaa ya Msimbazi kununua zawadi za wakwe zangu na jamaa wengine. Kila tuliponunua vitu kama vile microwave, blenders, na madudu mengine ambayo ni top secret, hakuna aliyetupa risiti zaidi ya kutupunguzia bei na kumalizana hapo hapo. Je, kwa mchezo huu, kaya inapoteza kodi kiasi gani? Hata ingeipata, ingepigwa kiasi gani na wajanja walioko kwenye ulaji? Hivi tunamkomoa nani?
            Maswali ya waria yalinifikirisha. Je, kodi wakilipa wanapata mrejesho sawa wa faida na matumizi yake? Ughaibuni, hulazimishwi kulipa kodi. Utalazimishwaje wakati faida na matumizi yake unayoana na kuyahisi kila mahali? Inashangaza kuona mafyatu wanene wachache wanaishi peponi wakati wengi wakiishi motoni tena pa kutengenzwa na hao hao waishio kwenye pepo waliojitentgezea! Hivyo ndivyo wabongo walivyonifyatua. Roho inauma we acha tu.
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

Sunday, 12 October 2025

Ndoa yaweza kuficha hata umalaya


 Leo, tutadurusu visa vya umalaya au tuseme umalaya katika ndoa. Tafsiri rahisi ya umalaya ni ile tabia ya kuwa na mahusiano na watu tofauti kwa wakati mmoja. Hata hivyo, tutoe angalizo. Hili halihusishi ndoa za mitala zinazokubalika katika baadhi ya dini na makabila.

Hapa, lengo letu ni kuonyesha namna ambavyo ndoa zinaweza kuficha umalaya.

X ni mke wa mtu tena mama na heshima zake  ila wa hovyo afanyaye mambo yasiyo ya heshima. Pamoja na kubahatika kuolewa na mume mwenye kipato, ana mchepuko wake! Hatujui sababu za kuchepuka kwake japo ni umalaya tu. Tujuacho ni kwamba anachepuka. Hatujui busara na mantiki za kufanya hivyo ilhali akijua madhara yake. Kwa kumtazama juu juu, tunagundua kuwa, licha ya kuwa mfanyabiashara kama mumewe, anatumia fedha yake kuuridhisha mchepuko wake. Tusichojua ni kama huo mchepuko unachuna buzi ili kujiongezea kipato au ni mapenzi. Pamoja na kujua madhara ya anachofanya, X alishafikia mahali akapata mimba na mchepuko wake akainyofoa. Hatujui amezaa wangapi wa nje ndani ya ndoa yake.

 Kimsingi, X ni mama ‘mwingi’ au tuseme malaya anayehonga wanaume ili kuridhisha tamaa zake. Ukimuona wala huweza kumdhania. Ila kwa kuangalia migogoro isiyoisha katika ndoa yake, unaweza kubunia ni kwanini anafanya hivyo. Je, anafanya hivyo kumkomoa mumewe? Je, hili ni jibu? Je, anafanya hivyo kutokana na kutotoshelezwa nyumbani. Kusema ukweli, hatujui.

Yupo huyu Y. Kama X naye kaolewa kadhalika. Huyu ana pepo la uroda. Yeye anatoa au tuseme anagawa bure. Yeye habagui wala kuchagua. Kila ajaye, twende mradi lake litimie. Huyu hajui ndugu wala rafiki. Kila aingiaye 18 zake lazima aanguke naye. Wapo wanaodhani kuwa kuna kitu kamfanyia mumewe. Maana, anavyoaga na kurudi bila bughudha, si bure. Kuna kitu. Ama kweli, ndoa zina mengi!

Pia, yupo Z. Naye kaolewa. Japo kipato chao si kikubwa wala kidogo, yeye anajiuza ili aongeze. Hatujui kama anafanya hivo ili kuongeza kipato au kutokana na tabia ya uchangu tu.

Ajabu ya maajabu, Hawa wana ndoa wote siku zote wanaishi na waume zao. Je, hapa, tatizo ni nini? Hatuna jibu. Tuna dhana tatu. Mosi, wote ni wake za watu. Pili, wote ni malaya tu. Tatu, wanayofanya si sawa. Nne, ndoa yaweza kuwa chaka la umalaya.

Baada ya kusoma visa hivyo vitatu hapo juu, tujiulize. Kwanini wahusika wanafanya wanayofanya? Je, hili linatufunulia au kutufundisha nini? Japo si rahisi kutoa majibu sahihi, kwanza, tunadhani kuwa kuna tatizo kibinafsi na kijamii. Pili, ni ndoa ngapi zina malaya kama hawa ambao hawajajulikana?  Tatu, jamii ifanye nini kuondoa kadhia hii ambayo ni chanzo kikubwa cha kutengana, migogoro, talaka, ugomvi, hata vifo? Nne, hapa, tatizo ni malezi ya wahusika au tabia tu za hovyo?

Somo kubwa tulilopata katika visa hivi ni kwamba ndoa inaweza kuficha umalaya. Pia, kwa wanaoishi kwenye ndoa na kufanya uchafu huu, wanaweza kuwa wengi kuliko hata inavyojulikana. Wakati mwingine, tunajiuliza, kama unajijua ni malaya, unaolewa ili iweje?

Leo tumeongelea umalaya wa akina mama. Haina maana kuwa akina baba hawafanyi umalaya. Tofauti na wanawake, wanaume waufanyapo umalaya, madhara yake huonekana madogo tokana na kuishi katika mfumo dume. Hata hivyo, kwetu umalaya ni umalaya bila kujali jinsia na sababu za anayeufanya. Wawake wanapofanya umalaya kama kwenye visa hivyo hapo juu, huonekana wabaya zaidi. Licha ya mfumo dume, hatujui ni kwa sababu hawawalipii mahari waume wao au hawawezi kupewa ujauzito kama kisa cha X. Hatujui.

Tujuacho ni kwamba ndoa zinaweza kuwa kichaka cha umalaya japo si zote. Pia, tunajua kuna tatizo la kibinafsi na kijamii. Tunashauri wahusika waache mchezo huu mchafu. Hata ungepewa nyama za wanyama wote, unadhani utatosheka wakati binadamu hatosheki ila kukubali kutosheka? Jamii pia ikemee vitendo hivi pale vinapogundulika ingawa yanaweza kuchukuliwa kama mambo binafsi. Ijue kuwa madhara yake si kwa wahusika tu ila jamii nzima hasa watoto wasio na hatia au wanandoa wenye wenzi wa hovyo lakini wasiofanya kama wao.

Chanzo: Mwananchi Jpili leo.

Wednesday, 8 October 2025

Msituulize tulipopata njuluku tulowekeza uchaguzini


Siku hizi za uchafuzi, sorry, uchakachuaji, sorry, uchaguzi, tutaona mengi. Yote cha mtoto. Kinachomfyatua na kumtisha Fyatu na ujeuri na ushujaa wake akatetemeka ni makufuru yanayofanywa na vitegemezi vya makapuku wa kunuka, tena vilivyozaliwa jana. Kama hutapiga selfie na chopa au mindinga ya bei mbaya au wanene uchwara ambao wengi wanatia shaka kuhusiana na udhu wao mwaka huu, uje una matatizo kiakili. Hata hivyo, mambo mengine yanaudhi we acha tu.
         Juzi, katika pitapita zangu si nikakutana na vibaka wa kisiasa wa kisasa wenye visanga na visasi! Si niliahidiwa mshiko ili nikubali kupakizwa kwenye mindinga yao niende kuhudhuria na kushangilia ahadi za urongo urongo na uzwazwa. Kwanza, kuna kitu kiliniudhi kiasi cha kutaka kufyatuka peke yangu na kuwafyatua mafyatu vibao. Kwanini kubebwa na mindinga wakati wao wanatesa na chopa? Kwa utapeli na uzwazwa wao walidhani naweza kuhongwa viji-Tshirts, na bi Nkubwa wangu khanga tuwape kura zetu watufyatue kwa miaka mitano ijayo? Siye si chawa, funza, kunguni, wala ruba. Tuna akili tena zinazochemka kuweza kujua na kustuhikia huu ujambazi uliohalalishwa kwa kisingizio cha siasa.
           Pili, baada ya kushuhudia huo ukumbaff, niliamua kuwafyatua hawa majizi wa kisiasa. Hivyo, nawashauri mafyatu mazwazwa wanaoshabikia, kushobokea, na kupwakia rushwa hizi ambazo kimsingi, ni njuluku zao zilizopigwa na hawa majambizi wa kisiasa, kuacha kujitia vitanzi wenyewe. Kwanini msiwaulize hizo njuluku za kukodisha chopa na ndinga, kumwaga mabango mengine ya kujikomba wamezipata wapi kwenye kaya kapuku kama hii au ni za bwimbwi?
        Tatu, waulize. Wananunua nini ili kupata nini? Watazirudishaje kama siyo kuchuuza roho za mafyatu au kufyatua njuluku zao kwa kupewa rushwa na wawekezaji ambao nao si wawekezaji kitu bali wachukuaji?
            Nne, watakaopwakia jinai hii wasilie watakapofyatuliwa na kujikuta wakisota kwa maisha magumu. Hii ni shida ya kujitakia. Nachukia mafyatu yanayofikiri na kutenda kama mafisi. Wakati mwingine, najiuliza. Hivo vichwa visivyotumika walipewa vya nini? Fisi ukimtupia nyama ya fisi mwenzie, anaramba. Panya kadhalika. Kuku ndo usiseme. Ni aibu na hatari kwa mafyatu kulishwa nyama ya wenzao kwa mlango wa nyuma. Hiyo, njuluku mnayoshobokea ni jasho lenu. Ni yenu.
         Tano, hawa wanaohonga ni wahalifu mnaopaswa kuwafyatua wakaishia hata kuzikwa lupango. Hao wanaowahonga wengi ni vitegemezi vya wazazi makapuku tena wa kunuka. Ukiwaona hawa wanaokodisha chopa, wazazi wao hata wakiona picha ya chopa hawawezi kujua ni nini zaidi ya kuiamkia na kujua Sir God amewatokea tokana na kutowahi kuiona. Ajabu ya maajabu, wengi wanaotapanya njuluku kukodisha na kuchezea haya madude ni vitegemezi vya makapuku vilivyosoma kwa pesa ya ima gongo, au vitumbua na sasa vinatumbua visijue vinawatumbua wenzao. Sijui hii inasababishwa na ubinafsi, ufisi, ukatili, upofu, au uzwazwa?
            Sita, najisikia kupagawa kuona hata lisrikal–––we koma–––likiwafumbia macho majizi haya ya kisasa ya kisiasa. Je hii, kwa wenye akili tu, inawafundisha nini? Je jinai ndiyo sera za kisasa? Hawa wahongaji njuluku zetu, wakituuza, tutawalaumu au kujilaumu? Kura yako siyo njugu ugawa bure bila kujua atakayeliwa ni wewe kwa vile kura hailiwi bali kuwawezesha walaji kula tena dezo. Je, wale wanaoshabikia huu wizi nao si wezi wasio na cha kuiba au kutamani nao wangepata fursa wafyatue na kupiga? Namna hii, kaya itasonga mbele au kuendelea kuwa nyuma?
            Sabaacheni ufwala, ulimbukeni, na uzwazwa, na uvivu wa kufikiri. Fyatu fisadi linachezea fedha kwenye madude msiyoweza kuyagusa na kuwakoga, nanyi, kwa ufwala wenu, mnalishanglia badala ya kulizomea na kushinikiza liondolewe kwenye orodha ya wagombea. M mnashangilia mateso yenu. Wangapi wamewahi au watawahi kupanda chopa? Badala ya kumnyonyoa, mnajirahisisha anawanyonga. Mkiitwa wanyonge mkanyongea na kunyongwa, mtalalamika au kumlaumu nani? Kweli mafala ndiyo wafyatuliwao!
            Nane, hebu tujiulize kifyatufyatu. Hivi, hawa wanaotuaminisha kuwa wana sera na siyo sura (teana za kiwivi) za kutukomboa wana mpango wowote wa maana? Kama wanao, mbona hawaoni haya ambayo Fyatu nayaona ambapo mafyatu wanafyatuliwa kirahisi na kirejareja kana kwamba kaya haina mwenyewe au ni shamba la chizi? Usawa huu, kama tukitumia akili ya comonsense sawasawa, nani anaweza kupata njuluku ya kukodi chopa tena kwa kampeni na siyo kumuwahisha mgonjwa hospitali tena kijana mdogo ambaye hata muda wake wa kufanya kazi haufikii miaka ishirini? Jamani, tunawafyatua mafyatu kwa sababu waligoma kutufyatua hivyo, tunawaadhibu kwa kuwafyatua tusijue tuifyatua kesho yao na yetu.
            Kama mafyatu wangejitambua, nadhani swali la kwanza lingekuwa ni kutaka kujua hii njuluku imepatikana wapi, wananunua nini, na watairejeshaje. Pia, wangehanikiza wafujaji wa njuluku waondolewa. Na mwisho, wangependa kujua sera za wahusika badala ya kushabikia sura.
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.


Sunday, 5 October 2025

Wanandoa msibague Watoto wenu kijinsia

Kuna makabila yenye mazoea na mila za hovyo. Mila za makabila haya zimejengwa kwenye ubaguzi wa kijinsia ambao unaweza kuakisi namna jinsia inavyochukuliwa, kuthaminiwa hata kutothaminiwa katika jamii na mila za Kiafrika. Kwa makabila haya baguzi kijinsia, mama asipozaa Watoto wa kiume, kunakuwa na tatizo. Inapotokea hivyo, ndugu wa mume humuolea ndugu yao mke ili aweze kupata Watoto wa kiume. Katika kufanya hivi, haijarishi nani ni baba wa Watoto hawa isipokuwa uwepo wao.

Moja ya kisingizio yatumiacho makabila hay ani kkuwa mtoto amezaliwa kwenye mahari ya fulani wakimaanisha mahari yaliyotolewa kwa wazazi wa mke. Hivyo, hata ikibidi mama kutoka nje ya ndoa na kupata Watoto wa kiume wasio wa mumewe, hakuna shida. Tukijiuliza, mosi, hii ni nini kama siyo ubaguzi wa kijinsia? Pili, je, Watoto wapatikanao kupitia mila hii kweli ni wa baba anayewakubali ilmradi wanachangia kwenye ukoo wake? Je, hakuna njia nyingine ya kukabili ‘tatizo’ hili japo si tatizo?

            Kwa kuangalia kisa hicho hapo juu, kuna ubaguzi wa kijinsia wa wazi katika jamii husika. Isitoshe, ubaguzi huu umefichwa kwenye kisingizio cha mila za kizamani zisizo na nafasi katika jamii ya sasa. Je, nini kifanyike? Swali hili halina jibu rahisi wala moja. Kwanza, inakuwaje binadamu, pamoja na ubinafsi wake, kukubali watoto wasio wake kwa kisingizio cha mila? Ni wangapi wameathiriwa na mila hii? Wakati wahusika wakishabikia na kuridhika na mila hii, wajiulize. Kusingekuwako na watoto wa kike, dunia yetu ingekuwaje? Je, kuna mtu anayeandika barua ya maombi kwa Mungu azaliwe kama alivyo?

            Katika kudurusu na kujadili kadhia hii, kwanza, tunagundua kuwa sababu ya ubaguzi huu wa kijinsia ni welewa mdogo wa masuala ya uzazi. Kisayansi, anayesababisha jinsia ya mtoto si mama ilTa baba ingawa anayeadhibiwa na kuathiwa nayo ni mama na watoto wa kike. Kama ni adhabu, aliyepaswa kuadhibiwa si mama bali baba. Pili, tunadhani kuwa, licha ya ujinga, kuna kila dalili za wahusika kupenda mitala kwa kisingizio cha jinsia. Je, wakijua kuwa anayesababisha jinsia zote mbili ni baba, wataendelea na imani hii potofu na kuwaumiza akina mama na watoto? Kwetu sisi, mtoto ni mtoto bila kujali jinsia yake.

            Tutatoa kisa kimoja ambapo baba alimtelekeza mkewe na watoto wake wa kiume na kwenda kutafuta mke mwingine aliyemzalia watoto wa kiume naye akaridhika asijue Mungu ana mipango mingine. Huyu bwana, pamaoja na kuridhika, watoto walipokua, alijilaumu asijue la kufanya kwa sababu maji yalikuwa yameishamwagika. Maana, katika makuzi yao, watoto wa kike walibahatika kuwa na uwezo mkubwa darasani. Zaidi, waliolewa na waume wanaojiweza kinyume na kaka zao ambao wengi waliishia kuwa watu tegemezi tokana na kutojiweza kiakili.

            Miaka ilienda. Baadhi ya Watoto wa kiume walijiingiza kwenye jinai na wengine wao kuishia gerezani. Kwa upande wa Watoto wa kike, mambo yaliwanyokea. Akiwa amestaafu na nguvu zimemuishia, baba alijikuta akijipeleka kwa Watoto waliowatelekeza akiomba wamtunze. Yaliyofuata ni historia.

            Je, kisa hiki kinatufundisha nini? Funzo la kwanza ni kwamba watoto wote ni sawa. Pili, tusiwabague Watoto kijinsia. Tatu, umdhaniaye ndiye siye. Nne, majuto ni mjukuu. Wewe ni nani hadi umhukumu kiumbe wa Mwenye Mungu kwa jinsia yake wakati ya kesho hayajulikani? Je, ungekuwa wewe ungetaka utendeweje?

            Suluhisho ya tatizo hili ni kwa jamii na wana jamii kwa ujumla kujielimisha juu ya sayansi ya uzazi. Pili, ni kuacha mila chakavu, kongwe, potofu, na za hovyo. Tatu, wakati wakiwabugua watoto kijinsia, wawakumbuke ambao hawakujaliwa kupata mtoto hata mmoja. Nne, waathirika na wahanga wa tatizo hili walione na kulitumia kama nyenzo ya kujikomboa kijamii na kijinsia. Tano, wahusika wajue kuwa watoto waliozaliwa na baba wengine wakawalea wakijua ukweli, wanaweza kuwaadhibu wazazi bila hata ya wao kujua. Hivi, unajisikiaje kuwa baba yako ni yule baba jirani tajiri wakati baba yako feki ni maskini wa kutupwa? Sita, akina mama na baba wakatae mila hii kwa vile inawafanya walee au wasipate fursa ya kuwalea watoto wao.

Tumalizie. Kujua wazazi wa mtu ni haki yake ya msingi na amkoseshae au kumnyima haki hii mhusika, anamuumiza kulhali kisaikolojia, kijamii, hata kiuchumi.

Chanzo: Mwananchi Jpili leo.