Leo, tutadurusu visa vya umalaya au tuseme umalaya katika ndoa. Tafsiri rahisi ya umalaya ni ile tabia ya kuwa na mahusiano na watu tofauti kwa wakati mmoja. Hata hivyo, tutoe angalizo. Hili halihusishi ndoa za mitala zinazokubalika katika baadhi ya dini na makabila.
Hapa, lengo letu ni kuonyesha namna ambavyo ndoa zinaweza kuficha umalaya.
X ni mke wa mtu tena mama na heshima zake ila wa hovyo afanyaye mambo yasiyo ya heshima. Pamoja na kubahatika kuolewa na mume mwenye kipato, ana mchepuko wake! Hatujui sababu za kuchepuka kwake japo ni umalaya tu. Tujuacho ni kwamba anachepuka. Hatujui busara na mantiki za kufanya hivyo ilhali akijua madhara yake. Kwa kumtazama juu juu, tunagundua kuwa, licha ya kuwa mfanyabiashara kama mumewe, anatumia fedha yake kuuridhisha mchepuko wake. Tusichojua ni kama huo mchepuko unachuna buzi ili kujiongezea kipato au ni mapenzi. Pamoja na kujua madhara ya anachofanya, X alishafikia mahali akapata mimba na mchepuko wake akainyofoa. Hatujui amezaa wangapi wa nje ndani ya ndoa yake.
Kimsingi, X ni mama ‘mwingi’ au tuseme malaya anayehonga wanaume ili kuridhisha tamaa zake. Ukimuona wala huweza kumdhania. Ila kwa kuangalia migogoro isiyoisha katika ndoa yake, unaweza kubunia ni kwanini anafanya hivyo. Je, anafanya hivyo kumkomoa mumewe? Je, hili ni jibu? Je, anafanya hivyo kutokana na kutotoshelezwa nyumbani. Kusema ukweli, hatujui.
Yupo huyu Y. Kama X naye kaolewa kadhalika. Huyu ana pepo la uroda. Yeye anatoa au tuseme anagawa bure. Yeye habagui wala kuchagua. Kila ajaye, twende mradi lake litimie. Huyu hajui ndugu wala rafiki. Kila aingiaye 18 zake lazima aanguke naye. Wapo wanaodhani kuwa kuna kitu kamfanyia mumewe. Maana, anavyoaga na kurudi bila bughudha, si bure. Kuna kitu. Ama kweli, ndoa zina mengi!
Pia, yupo Z. Naye kaolewa. Japo kipato chao si kikubwa wala kidogo, yeye anajiuza ili aongeze. Hatujui kama anafanya hivo ili kuongeza kipato au kutokana na tabia ya uchangu tu.
Ajabu ya maajabu, Hawa wana ndoa wote siku zote wanaishi na waume zao. Je, hapa, tatizo ni nini? Hatuna jibu. Tuna dhana tatu. Mosi, wote ni wake za watu. Pili, wote ni malaya tu. Tatu, wanayofanya si sawa. Nne, ndoa yaweza kuwa chaka la umalaya.
Baada ya kusoma visa hivyo vitatu hapo juu, tujiulize. Kwanini wahusika wanafanya wanayofanya? Je, hili linatufunulia au kutufundisha nini? Japo si rahisi kutoa majibu sahihi, kwanza, tunadhani kuwa kuna tatizo kibinafsi na kijamii. Pili, ni ndoa ngapi zina malaya kama hawa ambao hawajajulikana? Tatu, jamii ifanye nini kuondoa kadhia hii ambayo ni chanzo kikubwa cha kutengana, migogoro, talaka, ugomvi, hata vifo? Nne, hapa, tatizo ni malezi ya wahusika au tabia tu za hovyo?
Somo kubwa tulilopata katika visa hivi ni kwamba ndoa inaweza kuficha umalaya. Pia, kwa wanaoishi kwenye ndoa na kufanya uchafu huu, wanaweza kuwa wengi kuliko hata inavyojulikana. Wakati mwingine, tunajiuliza, kama unajijua ni malaya, unaolewa ili iweje?
Leo tumeongelea umalaya wa akina mama. Haina maana kuwa akina baba hawafanyi umalaya. Tofauti na wanawake, wanaume waufanyapo umalaya, madhara yake huonekana madogo tokana na kuishi katika mfumo dume. Hata hivyo, kwetu umalaya ni umalaya bila kujali jinsia na sababu za anayeufanya. Wawake wanapofanya umalaya kama kwenye visa hivyo hapo juu, huonekana wabaya zaidi. Licha ya mfumo dume, hatujui ni kwa sababu hawawalipii mahari waume wao au hawawezi kupewa ujauzito kama kisa cha X. Hatujui.
Tujuacho ni kwamba ndoa zinaweza kuwa kichaka cha umalaya japo si zote. Pia, tunajua kuna tatizo la kibinafsi na kijamii. Tunashauri wahusika waache mchezo huu mchafu. Hata ungepewa nyama za wanyama wote, unadhani utatosheka wakati binadamu hatosheki ila kukubali kutosheka? Jamii pia ikemee vitendo hivi pale vinapogundulika ingawa yanaweza kuchukuliwa kama mambo binafsi. Ijue kuwa madhara yake si kwa wahusika tu ila jamii nzima hasa watoto wasio na hatia au wanandoa wenye wenzi wa hovyo lakini wasiofanya kama wao.
Chanzo: Mwananchi Jpili leo.
No comments:
Post a Comment