The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Sunday, 5 October 2025

Wanandoa msibague Watoto wenu kijinsia

Kuna makabila yenye mazoea na mila za hovyo. Mila za makabila haya zimejengwa kwenye ubaguzi wa kijinsia ambao unaweza kuakisi namna jinsia inavyochukuliwa, kuthaminiwa hata kutothaminiwa katika jamii na mila za Kiafrika. Kwa makabila haya baguzi kijinsia, mama asipozaa Watoto wa kiume, kunakuwa na tatizo. Inapotokea hivyo, ndugu wa mume humuolea ndugu yao mke ili aweze kupata Watoto wa kiume. Katika kufanya hivi, haijarishi nani ni baba wa Watoto hawa isipokuwa uwepo wao.

Moja ya kisingizio yatumiacho makabila hay ani kkuwa mtoto amezaliwa kwenye mahari ya fulani wakimaanisha mahari yaliyotolewa kwa wazazi wa mke. Hivyo, hata ikibidi mama kutoka nje ya ndoa na kupata Watoto wa kiume wasio wa mumewe, hakuna shida. Tukijiuliza, mosi, hii ni nini kama siyo ubaguzi wa kijinsia? Pili, je, Watoto wapatikanao kupitia mila hii kweli ni wa baba anayewakubali ilmradi wanachangia kwenye ukoo wake? Je, hakuna njia nyingine ya kukabili ‘tatizo’ hili japo si tatizo?

            Kwa kuangalia kisa hicho hapo juu, kuna ubaguzi wa kijinsia wa wazi katika jamii husika. Isitoshe, ubaguzi huu umefichwa kwenye kisingizio cha mila za kizamani zisizo na nafasi katika jamii ya sasa. Je, nini kifanyike? Swali hili halina jibu rahisi wala moja. Kwanza, inakuwaje binadamu, pamoja na ubinafsi wake, kukubali watoto wasio wake kwa kisingizio cha mila? Ni wangapi wameathiriwa na mila hii? Wakati wahusika wakishabikia na kuridhika na mila hii, wajiulize. Kusingekuwako na watoto wa kike, dunia yetu ingekuwaje? Je, kuna mtu anayeandika barua ya maombi kwa Mungu azaliwe kama alivyo?

            Katika kudurusu na kujadili kadhia hii, kwanza, tunagundua kuwa sababu ya ubaguzi huu wa kijinsia ni welewa mdogo wa masuala ya uzazi. Kisayansi, anayesababisha jinsia ya mtoto si mama ilTa baba ingawa anayeadhibiwa na kuathiwa nayo ni mama na watoto wa kike. Kama ni adhabu, aliyepaswa kuadhibiwa si mama bali baba. Pili, tunadhani kuwa, licha ya ujinga, kuna kila dalili za wahusika kupenda mitala kwa kisingizio cha jinsia. Je, wakijua kuwa anayesababisha jinsia zote mbili ni baba, wataendelea na imani hii potofu na kuwaumiza akina mama na watoto? Kwetu sisi, mtoto ni mtoto bila kujali jinsia yake.

            Tutatoa kisa kimoja ambapo baba alimtelekeza mkewe na watoto wake wa kiume na kwenda kutafuta mke mwingine aliyemzalia watoto wa kiume naye akaridhika asijue Mungu ana mipango mingine. Huyu bwana, pamaoja na kuridhika, watoto walipokua, alijilaumu asijue la kufanya kwa sababu maji yalikuwa yameishamwagika. Maana, katika makuzi yao, watoto wa kike walibahatika kuwa na uwezo mkubwa darasani. Zaidi, waliolewa na waume wanaojiweza kinyume na kaka zao ambao wengi waliishia kuwa watu tegemezi tokana na kutojiweza kiakili.

            Miaka ilienda. Baadhi ya Watoto wa kiume walijiingiza kwenye jinai na wengine wao kuishia gerezani. Kwa upande wa Watoto wa kike, mambo yaliwanyokea. Akiwa amestaafu na nguvu zimemuishia, baba alijikuta akijipeleka kwa Watoto waliowatelekeza akiomba wamtunze. Yaliyofuata ni historia.

            Je, kisa hiki kinatufundisha nini? Funzo la kwanza ni kwamba watoto wote ni sawa. Pili, tusiwabague Watoto kijinsia. Tatu, umdhaniaye ndiye siye. Nne, majuto ni mjukuu. Wewe ni nani hadi umhukumu kiumbe wa Mwenye Mungu kwa jinsia yake wakati ya kesho hayajulikani? Je, ungekuwa wewe ungetaka utendeweje?

            Suluhisho ya tatizo hili ni kwa jamii na wana jamii kwa ujumla kujielimisha juu ya sayansi ya uzazi. Pili, ni kuacha mila chakavu, kongwe, potofu, na za hovyo. Tatu, wakati wakiwabugua watoto kijinsia, wawakumbuke ambao hawakujaliwa kupata mtoto hata mmoja. Nne, waathirika na wahanga wa tatizo hili walione na kulitumia kama nyenzo ya kujikomboa kijamii na kijinsia. Tano, wahusika wajue kuwa watoto waliozaliwa na baba wengine wakawalea wakijua ukweli, wanaweza kuwaadhibu wazazi bila hata ya wao kujua. Hivi, unajisikiaje kuwa baba yako ni yule baba jirani tajiri wakati baba yako feki ni maskini wa kutupwa? Sita, akina mama na baba wakatae mila hii kwa vile inawafanya walee au wasipate fursa ya kuwalea watoto wao.

Tumalizie. Kujua wazazi wa mtu ni haki yake ya msingi na amkoseshae au kumnyima haki hii mhusika, anamuumiza kulhali kisaikolojia, kijamii, hata kiuchumi.

Chanzo: Mwananchi Jpili leo.

No comments: