The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 29 October 2025

Kama unatafuta ‘malaika’ usioe au kuolewa

Kuna msemo wa Kiingereza wa Miss au Mr. Right” wakimaanisha mke au mume material au afaaye. Sisi, kama wanandoa, tumepitia kipindi hiki cha kusaka mchumba. Bahati nzuri si kupitia tu, bali tulihitimisha kwa mafanikio kiasi cha kuweza kutoa ushauri kwa wengine. Kama kichwa kionyeshavyo,bila kujali dini na kila kitu kikutofautishacho na wengine, kama unatafuta kuoa au kuolewa malaika, wala usipoteze muda wako. Hayupo, hakuwepo, na hatakuwepo. Kimsingi, kama ulivyo binadamu mwenye ubora na udhaifu, hata huyo unayemtafuta ni binadamu mwenye kila sifa uliyo nayo. Hivyo, katika kutafuta mchumba, epuka kutafuta malaika au mkamilifu. Hayupo.
            Kama ilivyo kwenye ukamilifu, pia ujue. Kama wewe, hakuna aliye shetani. Wote tuna ubora na mapungufu ambayo hatuwezi kuyavua bali kujifunza namna ya kuishi nayo tena kwa furaha. Hivyo, somo la leo litajikita katika kudurusu namna ya kupata anayefaa kwa viwango vya kawaida vya kibinadamu.
            Mosi, wakati ukitafuta mchumba, yakupasa ujichunguze na kujielewa kwanza ili uwe na taswira umtakaye. Mfano, kama wewe ni muovu, tegemea kupata muovu lakini si vinginevyo. Ingawa wakati mwingine hutokea watu wasiofanana kisifa kuoana japo hili nalo huwa na changamoto zake hasa wanapondua kuwa ni paka na panya ndani ya nyumba moja. Wapo wanaotambua udhaifu wao na kuufanyia kazi pia wasiokubali kubadilika.
            Pili, ujue kuwa kutafuta mchumba siyo mchezo wa kubahatisha bali kujitahidi uwezavyo kumtafuta na kumjua unayemtaka. Hapa, uhitaji kila aina ya ubunifu mfano, kumsikiliza mwenzio, kumsoma, kumdadisi, hata kumchunguza hata wakati mwingine bila ya yeye kujua. Hili ni muhimu sana kwa vile ukiishaingia, umeingia. Japo wapo wanaoingia na kutoka, ila huwa hawatoki salama. Hivyo, uwe makini wewe utafutaye mchumba. Washirikishe wazazi katika msako huu.
            Tatu, japo waweza kupata asiyelingana na vigezo na viwango vyako baada ya kujipima kama nawe unavyo, kuna fursa ya kubadilika kama mhusika akijua udhaifu wake na kuwa tayari kuufanyia kazi. Hapa, tuwe wazi. Kuna madhaifu yanayobadilishika na yasiyobadilishika. Mfano, mwenzio kama ana imani, tabia, na welewa tofauti, haya yanabadilishika. Ila kama siyo muaminifu na mwenye upendo, hapa kuna tatizo tena kubwa tu. Ni juu yako kuamua kama utakuwa tayari kuvumilia au kuachana naye kabisa kabla ya kuingia kwenye mkataba wa kudumu.
            Nne, ni vizuri kupima kama wote mnajua vilivyo mnachokusudia kufanya. Hapa, tuonye akina dada. Wapo wachumba wenye tamaa tena wasiojua wanachotaka wala kufanya. Hawa, wanaweza kumuingiza mtu mtegoni wakamharibia maisha halafu wakamuacha solemba. Tuna visa vingi tujuavyo ambapo mabinti hata wavulana waliacha wachumba wa maana wakaishia kuangukia kwenye mikono ya mashetani waliowaharibia maisha na kuwaacha.
            Tano, epuka na ogopa mtindo wa kuanza maisha ya ndoa kabla ya kufunga ndoa. Hapa, kuna aina mbili. Wapo wanaokubaliana kuanza kuishi kabla ya kufunga ndoa. Na wale wanaolazimika hasa wakishapeana ujauzito na kugundua kuwa hawafaani na hawawezi kuishi pamoja kama wanandoa. Wengine, hubambikiziana mimba ili kulazimisha wanaotaka wawaoe wawaoe wasijue mwisho wake waweza kuwa majuto yatokanayo ya kufanya makosa yasiyoweza kusahihishwa. Ukishakuwa mjamzito au kuanza kuishi kama wanandoa bila ndoa, ule ujana na mvuto wako vinaisha na haviwezi kurejeshwa tena. Kizungu wanaita spendforce au kukosa mantiki katika jambo ambalo ulikuwa na mantiki.
            Sita, epuka pupa na tamaa ya kuingia katika ndoa bila kujiridhisha kuwa umefanya homework yako vizuri. Maana, ukishaingia ni vigumu kutoka.
            Mwisho, tumalizie na ubinadamu wa mtarajiwa. Hili ni la kuzingatia sana. Binadamu wote tuna mapugufu sawa na ubora na huu ndiyo ubinadamu ingawa tunazidiana katika hili. Hakuna aliyekamilika japo yupo anayerekebishika. Hivyo, watarajiwe wajitahidi wawezavyo kupata wanaowafaa kwa vile hakuna malaika wala shetani bali binadamu. Kuna mapungufu kama vile elimu, kipato, na mazoea madogo madogo vinavyobadilika kulingana na utayari wa wahusika. Hivyo, katika kutafuta mtarajiwa, hakuna malaika wala shetani bali binadamu. Hivyo, wahusika waepuke kutafuta malaika. Kwani, hayupo na hawatampata. Wakimpata, wajue ni umalaika wa muda tu.
Chanzo: Mwananchi Jpili juzi.

No comments: