Baada ya kushuhudia kilichotokea kaya jirani kwa fyatu mwenzangu hayati Ken Aliyeunda kaya, nimestuka na kuogopa japo najiamini sana. Kwa wasionyaka inshu ni kwamba, kule Dhambia, kitegemezi cha munene wa zamani kilijikuta pakanga. Katika kufanya uchunguzi na unoko, lisrikal la kule kwa ‘roho’ mbaya yake si liliinyaka kuwa kitegemezi cha munene wa zamani aliyenyotoka roho kule kwa Fyatu Madiba kilikuwa na ukwasi wa kutisha. Kila mwanakaya alishangaa namna kitegemezi ambacho hakijawahi kupiga mzigo wowote hata kufagia chumba chake zaidi ya kubukanya mali za mafyatu kilivyokuwa na ukwasi wa kunuka. Je, viko vingapi kama hivi kwenye bara hili lililopotea kwa uzwazwa wakati lina uchumi lakini linaukalia?
Inshu iko hivi. Mtoi wa mdosi wa kule wa zamani alikuwa anamilki mahekalu, madude ya bei mbaya usipime ambavyo hakuna maelezo ya miujiza iliyotumika kwa fyatu kula kulala alivyoipata. Je, aliupataje huu ukwasi ambao unawahangaisha na kuwashinda Mafyatu wachakalikaji? Simpo. Dingi wake alikuwa dingi wa kaya. Hivyo, kwa kutumia mamlaka na ubini aka surname wa dingi, jamaa alipiga njuluku ndefu pakubwa. Wakati wanakaya wakisota hadi kunyotolewa roho na ukapuku, mtoi alikuwa akijienjoi tu na kuwacheka na kuwashangaa. Je, wapo wangapi kama huyu chawa, au tuseme funza, barani kwetu? Kweli, usiposhangaa ya Abudili aka mtoi wa madili, utashangaa ya Dalie mwana wa rungu. Jamaa alikuwa na ndinga kama mia hivi na mihekalu kama hamsini. Hapa, hatujagusia njuluku alizosweka ughaibuni na zile anazotapanya akijichotea ujiko kumbe jizi tu. Anyways, hayo ndo maajabu ya bara letu linaloitwa kapuku wakati ni tajiri wa kunuka.
Juzi, tulifanya kikao cha ghafla na Bi Mkubwa na kudurusu kadhia hii nyemelezi ya mafyatu nyemelezi watumiao unene wa madingi au ndugu zao. Tulikuja na mkakati wa kuokoa mali za Mafyatu na kulinda hesima yetu. Baada ya hapo, tuliwaita vitegemezi wetu wote na kuwapasha inshu na uamuzi wetu kuntu.
Kwanza, hawakuamini. Walidhani tulikuwa tunawatania wakati huwa hatuna utani nao. Ilibidi waumie tu na kukubali haya mabadiliko adimu duniani japo kwa shingo upande.
Pili, walijaribu kupinga. Niliwapa wazi kuwa unene wangu si wao. Nao, wakatafute wao kama ni rahisi kama walivyokuwa wakifyatua njuluku za mafyatu kwa kunitumia. Mie ni faya na nomi kinomi. Siyo kama akina Mobutu na M7.
Tatu, walistuka na kuchukia. Baada ya kuwapasha inshu, tuliazimia kuwa, kuanzia sasa, maulaji yangu kama prezo wa Mafyatu utakuwa wangu na Bi Mkubwa tu. Hivyo, wajiju,
Nne, tumepiga marufuku kutumia ubini wetu kuwapiga Mafyatu. Tumewapa wazi kuwa tunachelea mafyatu wanaweza kufyatuka wakatufyatua kwa kuwafyatua kizwazwa. Wewe uliona wapi mtoto mchanga kunyonyesha? Uliona wapi?
Zamani, nilidhani wachunwao na vyaungudoa ni warume wakwere. Kumbe na wanene wanachunwa tena na vitegemezi vyao, jamaa, mashosti, na marafiki zao! Fyatu zima linaacha kuchapa kazi. Linanyonya na kuwafyatua mafyatu kwa vile ni rafiki, toi, au shosti la munene. Acheni uvivu. Tafuteni ngori mheshimike.
Kwa vile mie naona mbali, nimeamua rasmi kukomesha upigaji wa kutumia mamlaka yangu. Hata Bi Mkubwa tumekubaliana afute ile asasi yake ya ulaji Ulaji iitwayo BiMkubwa Opportunity and Maulaji ya Unene (BOMU). Hata ile bajeti iliyokuwa ikipangiwa ofisi yake nimeipiga panga. Lazima kieleweke. Kuanzia sasa, nakinukisha kwa wale wote wapenda dezo kwa kutumia migongo ya madingi wao wanene. Nimewaamuru vitegemezi vyetu kutafuta kazi halali. Kwa vile vimeishatimiza umri wa mafyatu wazima, havitaruhusiwa hata kupewa ndinga za mafyatu. Kwani, alivichagua nani na vinamtumikia nani zaidi ya matumbo na tamaa zao? Lazima tubadilike kabla hatujabadilishwa. Isitoshe, ulaji wa dezo na unene vina mwisho.
Vitegemezi nilivyovipa uteuzi sasa naubatilisha vikahangaike nyenyewe nymbaff kabisa.
Katika kutenda haki, kuanzia sasa, nimetoa amri ya watoi wote wa wanene na wanene wenyewe kusoma alama za nyakati. Itawabidi wajiandae kusomea kwenye shule za Kayumba kama mafyatu wengine. Kwa wanene, hakuna kupeleka watoi ughaibuni au kwenye intaneshno skuli wakati shule na vyuo tunavyo hapa tena vya kumwaga. Hii, itasaidia kuwazuia wanene kupiga njuluku za mafyatu. Pia, natoa amri wanene wote kwenye Fyatuland kuacha kwenda ughaibuni kujichunguza afya zao wakati hapa tunayo mahospitali lukuki.
Kuongoza kwa mfano, nimeamuru vitegemezi vyetu viwili vilivyogoma kwenda chuo, vitafute vyuo na kuchukua nkopo kama mafyatu wengine. Hakuna cha kutegemea jina langu tena kuishi dezo kana kwamba havina mikono na vichwa. Nimechukua hatua hizi adimu duniani kwa kuogopa kuendelea kuwafyatua mafyatu hadi wafyatuke wanifyatue. Mwenye macho asikie uzuri. Mwenye masikio ajionee.
Lazima ningoze kifyatu tena kwa mfano. Kuanzia sasa, hakuna ndugu yangu awe wa kweli au wa kuokoteza atapewa upendeleo. Hata kule kijijini kwetu ambako tulikuwa tumeanza miradi ya upendeleo, nimepiga kalamu. Nimesemaje? Kwani, niko wapi?
Chanzo: Mwananchi Jtano jana.
No comments:
Post a Comment