The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 1 April 2026

Fyatu kutumia wese kufyatua mafyatu

Si kwamba najidai. Hasha. Kwa tunaomilki mikweche na mbavu za mbwa, imekula kwetu. Mwenzenu nimeweka kweche langu juu ya mawe. Naona yule anabeua midomo. Unadhani mchezo usawa huu wa kufyatuliwa na kufyatuana? Kama hujafyatuliwa, usinicheke wala kujihadaa. Utafyatuliwa tu. Tangu Tarampu na Niitenyau wakinukishe kule kulikoungua jembe ukabakia mpini, si mafyatu wachovu tutaipata. Tokana na vita hii ya kujitakia si wese limepaishwa. Leo, kila mwiz, sorry, fyatu anapanga kupandisha bei ya kila kitu. Ukiuliza kwai, waambwa vita. Unapata somo hapa? Hivi wese tutakalolanguliwa si liliingizwa miezi mingi iliyopita? Sasa itakuwaje kupandishia bei wakati wese tunalonunua ni kiporo kilicholetwa miezi mingi iliyopita?
            Juzi, niliwaita wapangaji wangu kuwaandaa kitakapoumana.Niliwaamsha usiku na kuwapa inshu! Walidhani kulikuwa na la maana la kuwapasha kumbe maumivu matupu! Si niliwafyatua kuwa kuanzia sasa kodi ya pango itapanda mara mbili! Walipouliza kwai, niliwajibu kuwa watazame runinga na siyo kushobokea shoo za kizwazwa. Niliwaliwashangaa wanaishi dunia gani wasijue wese limepanda. Si fyatu mmoja alidakia “kwani ubavu wa dogi, sorry, nyumba nayo inatumia wese kama gari?” Wee! Acha nifyatuke! Si alijifanya msomi tena wa sayansi ya wese. AlijibuNilimuuliza alichosomea na wapi kiasi cha kutojua bei ya wese ikipanda, kila kitu kinapaa.
            Nilibanja sana na kuwapa kavukavu kuwa atakayeona kupanda kwa kodi hakuwezi, atafute pa kwenda. Walipodadisi, niliwapa shule kuwa wese ndiyo roho ya biashara zote na wafanyabiashara wanaongeza cha juu watakavyo na hii ni fursa sawa kwa wote. Sijui nayo ilifia wapi? Kweli, kufa kufaana! Niliwapasha kuwa nilikuta bidhaa zote sokoni zimepaa. Hivyo, nimeamua kupaisha bei ya bidhaa yangu yaani pango. Tokana na mtanange huu, nimegundua kuwa hakuna fyatu salama vinginevyo awe sehemu ya lisirikali ambalo tukianza kupigwa na kufyatuliwa litaangalia na kutafuta namna ya kutufyatua zaidi. Usishangae hata ndata wakapandisha dau la kitu kidogo.
            Kuanzia sasa, nina mikakati ya kupambana na makali ya kufyatuliwa.
        Mosi, nitapunguza leshini home. Hakuna kula hovyo. Milo mitatu kwa siku mwisho. Huu ni uharibifu wa chakula na miili.
        Pili, ukiondoa vitegemezi vyetu vichanga, waliobaki kayani lazima waanze ‘mfungo wa wese.’
            Tatu, sitapokea wageni, vinginevyo wawe wemefunga. Sina bajeti ya wageni tena. Sifanyi hivi kwa roho mbaya, uchoyo, au ulafi. Wese limepanda jamani. Pia, wale waliozoea kuja kupiga soga wakati wa msosi, huu mwisho wao.
        Nne, nitaokoka. Sitakata kalaji kama nilivyozoea. Pia, nashauri ifuatavyo:
        a)     Wachunaji wanaotusumbua kwa fungu la kumi na sadaka wafunge hadi vita iishe.
        b)     Wanene wapunguze matumizi, safari, na vikao visivyo vya lazima. Najua watajifyatua ufahamu. Wakumbuke. Kama hawatapunguza kwa vile mali ya umma haiumi, Gen Ziro bado wapo. Watauma kama walivyofanya mwaka jana.
        c)     lisirikali lisijitoe ufahamu. Liingilie kati vinginevyo kinaweza kunuka. Si mnajua tena. Wakati tulio nacho kidogo tukilia, vipi hawa wasio na ajira wala kipato? Msitake kuongeza idadi ya majambazi na vibaka.
         Tano, kwa wenye viliba tumbo, huu ni wakati mzuri wa kupunguza uzito. Badala ya mafyatu wazima kukimbizana na barabara, punguza kubukanya na kupiga kanywaji mfurahie neema ya kupaa kwa wese.
        Sita, wauza vyakula na wenye vyombo vya usafiri, muogopeni Mungu. Siyo muanzishe vita yenu wenyewe kwa kupatupandishia bei mkisingizia wese.
        Saba, kwa vile nimeamua kuokoka na kuacha kupiga kanywaji, hata nyumba ndogo naachia. Nani atunze nyumba ndogo usawa huu wa kupaa wese? Na wale waliozoea kubomu, nao nawashauri wangoje vita iishe japo wese lishuke.
        Nane, kupunguza bili za umeme unaoliwa na miwaya, kuanzia sasa, kuangalia runinga ni saa moja tu. Baada ya hapo, wasiopenda lazima waanze kujifunza kulala mapema ili kupunguza matumizi ya umeme.
        Tisa, wale wote wanaonidai nawashauri wanifutie madeni au wangoje vita iishe pale bei na hadi pale bei ya wese itakaposhuka kama kweli itashuka. Maana, kwangu, hakuna kinachozalisha. Wajua kuwa hata bata na kuku wetu siku hizi hawatagi kutokana na kupanda kwa bei ya wese?
        Kumi, wale wa vikoba na kausha dau walie. Wasije kutusumbua na bi Mkubwa hadi vita iishe vingenevyo wanataka vita ya sisi kwa sisi.
        Kumi na moja, vitegemezi vyetu vilivyokuwa kwenye shule za upigaji na ufyatuaji za bei nawarejesha kwenye shule za Kayumba hadi wese lishuke. Kwa waliokuwa wanahudhuria tuisheni ndo mwisho hadi vita iishe. Maana, juzi kuna ticha kanipandishia bei ya tuisheni kwa sababu wese limepanda hadi kufikiri na kuandaa notice kunammalizia wese.
        Kumi na mbili, lisirikali lianze kumwaga njuluku. Yale ya maza anamwaga njuluku ambayo hajawahi kunimwagia, nayataka sasa kama ni ya kweli na si rongorongo za kisiasa za visasi. Wauza wese na lisirikali Mungu hata Sheitwani wanawaona.
Hivi leo nimekunywa chupa ngapi?
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

No comments: