The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Wednesday, 30 September 2026

Mambo mengi ni mipango ya Mungu


Hakuna changamoto kubwa kwa wanandoa wengi kama vile Ugumba. Pamoja na hivyo, usishangae mgumba anaolewa na mwenye uwezo wa kuzaa––– walati mwingine akizaa mapcha–––ni single mother. Ukiona hivyo, usimcheke kwa vile umeolewa.
     Mwingine ana uwezo wa kifedha lakini hana watoto wa kuitumia. Usimcheke kwa vile umeoa. Shukuru Mungu kuwa kilichomfikisha hapo hakikufikisha wewe.
Usishangae yatima asiye wa kumkanya na kumuongoza akawa na tabia nzuri hadi kufanikiwa na kuheshimia ilhali mwenye wazazi akaharibikiwa na kutia aibu. Usishangae yatima kuolewa ilhali mwenye wazazi–––tena wenye heshima na uwezo––– anatafuta mume asimpate! Usishangae anayejipaka mkorogo au asiye na sura nzuri anaolewa wakati cheupe tena mrembo wa haja akidoda!
            Vipi ukikuta mwenye mapengo anaolewa ilhali mwenye meno–––tena meupe na yaliyopangika vizuri na kuvutia–––akidoda? Usishange kuona mfupi tena mnene tu akiolewa wakati portable figure au mrefu akidoda. Si ajabu mtoto wa single mother kuaoa au kuolewa wakati mwenye wazazi akidoda. Usishangae mtoto wa mshika dini akawa ‘shetani’ wakati mtoto wa mwenye dhambi akimwa mcha Mungu.
            Hebu fikria hili. Usishangae kuona binti ambaye umri umeishakwenda akiolewa wakati kigoli mbichi akitafuta wa kuoa au kumuoa asimpate! Usishangae kukuta maskini asiye na chakula cha kuwalisha watoto akiwa na watoto wakati tajiri mwenye kila kitu akitamani hata apate mtoto mmoja ale na kurithi kila kitu.
            Je, ni wangapi wana magari lakini hawawezi kuyatumia wakati wasio nayo wakihaha na kudhalilishwa kwenye daladala? Ni wangapi huyaacha magari yao wakaenda kutembea au kukimbia kujipa mazoezi ilhali wapo wasio na magari ambao maisha yao ni mazoezi tosha? Ulishajiuliza ni kwanini mtu mbovu akawa na mume au mke bora wakati mwema akiwa na muovu? Usishangae mpangaji akalala usingizi mnono kuliko mwenye nyumba au dereva kuwa na furaha kuliko bosi wake.
            Ulishajiuliza ni kwanini chui pamoja na mabio yake hupata mawindo kidogo kuliko kinyonga ambaye akilenga lazima akamate? Je, kinyonga angekuwa na mabio kama chui, dunia ingekuwaje? Hapa ndipo yalipo majaliwa. Nyuki ana hasira lakini hana mwili na nguvu. Je, nyuki na hasira zake angekuwa na mwili kama wa tembo dunia ingekuwaje au tembo angekuwa na hasira na ukali kama wa nyuki?
            Ajabu tembo ana mwili na nguvu ila hana hasira. Hivi tembo angekuwa nyuki au nyuki angekuwa tembo, dunia yetu ingekuwaje? Wakati mwingine, tushukuru Mungu kwa alivyotujalia. Hiyo mifano ina mafunzo mengi kuhusiana na wanandoa. Unapomuona mwenzio hafai, wenzio wanasema tutampataje? Kila kiumbe Mungu kakipa nyenzo na uwezo katika kuendesha maisha yake bila kkujali ukubwa, udogo, ujanja au ujinga.
            Njiwa hawafungi ndoa, hawatoi mahari, hawapeani ahadi wala zawadi. Ila ndoa yao huwavutia hata binadamu. Kama walivyo mchwa ambao hujenga maghorofa bila nyenzo, wanandoa wanapaswa kutumia vipawa vyao kuijenga ndoa yao.
            Je, ni wapi pa kuanzia? Kwanza, ni kujikubali na kuwakubali wenzio kama walivyo. Pili, ni kukubali kuwa watu wote hawafanani wala kulingana. Huyu kapewa hili na mwingine kapewa lile. Vyote vinahitajika katika maisha. Mke anamuhitaji mume sawa na mume anavyomuhitaji mke. Hivi, wanaume wangekuwa wanabebea mimba, dunia ingekuwaje? Je, wanawake wangekuwa na hisia na tabia za kimaumbile kama za wanaume, watoto wangekuwa wapi? Ni mwanaume gani anaweza kuhimili kelele, mahitaji, maudhi, na usumbufu wa kichanga?
            Hapa, hatujaongelea misukosuko ya mimba na uchungu wa kujifungua. Asikwambie mtu. Tofauti ya kifo na kujifungua ni kwamba mzazi hupitia na kuhimili mengi tena makubwa ambayo, kimaumbile, wanaume wasingeweza hata robo.
            Tumalizie. Kwenye ndoa, sawa na kwenye maisha, tuheshimu na kuthamini majaliwa yetu. Tupo tulivyo si kwa sababu ya ujanja, ujinga, ushawishi, au utashi vyetu. Tupo tulivyo kwa majaliwa na mipango ya Mungu. Hivyo, baadhi yetu wasijifanye miungu kuwaona wenzao wana thamani pungufu kuliko wao.
            Inakuwaje baba azae nje ya ndoa na kuomba msamaha lakini mama akifanya hivyo, anaishia talaka? Kwa ufupi, hakuna tabia mbaya iliyo nzuri. Tabia mbaya ni mbaya bila kujali anayeifanya.  Kabla ya kumtenda, kumtenza au kumuumiza mwenzio jiulize. Ningekuwa yeye ningependa nitende na kutendewa vipi? Kama yalivyo maisha, wakati mwingine mambo mengine ni majaliwa ikiwamo ndoa.
Chanzo: Mwananchi J'pili iliyopita.

No comments: