Tuesday, 22 July 2008

Rostam asitutoe kwenye mjadala wa EPAIngawa suala la kutaka kulitumia kanisa kama nyenzo ya kusafisha mafisadi linakera, halikeri sana kama kashfa ya EPA.

Hivi karibuni kulitokea mvutano baina ya mbunge wa Igunga-CCM, Rostam Aziz na kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Ni baada ya mbunge huyu kutoa pesa zipatazo milioni 7,5 kwa kanisa hili. Hili lilichukuliwa kama kanisa kukubali pesa chafu toka kwa watu wachafu wanaolenga kujisafisha. Inakera kweli kweli. Pia kadhia hii ilifichua ulafu na unafiki wa baadhi ya watu wanaojifanya watu wa Mungu ilhali ni wachumia tumbo sawa na wengine. Ni wabovu na hovyo sawa na wale wanaowatumia. Hata mfumo unaowakumbatia ni wa hovyo na mchovu sina mfano. Bahati mbaya serikali haijakemea jinai hii.

Kuzidi kulinogesha suala mambo, zilitolewa shutuma na ushahidi wa mchungaji mmoja machachari aliyekuwa amelivalia njuga suala hili hadi kutishia kwenda mahakamani. Mengi yaliandikwa na kusema. Inakera sana. Hawa watu waroho na wachafu watatusababishia presha kiasi cha kutishia kuuondoa uhai wetu kwa hasira na hasara wanayotusababishia. Nina hasira nao.

Ila pamoja na hasira zangu dhidi ya wanaojiita wachungaji kumbe chui kwenye ngozi ya kondoo na waheshimiwa wachafu, bado kashfa ya EPA hata Kiwira na Richmond zinakera zaidi. Hawa nawaacha na roho wao mtakakitu aliyempindua roho mtakatifu tuliyemzoea.

Kuepuka kufanya mambo kipare (samahani ndugu zangu wapare nami nimeyakutia hivyo), siko tayari kuuza ng’ombe kwa kesi ya kuku. Pesa aliyotoa mheshimiwa ni milioni saba na ushei. Zimezua mjadala kiasi cha kutawala vyombo vya habari na jamii kwa ujumla huku kashfa mama lao ya EPA ikianza kuwekwa pembeni. Je huu siyo mtego wa wahusika wanaojuana kwa vilemba kututoa kwenye mjadala wa maana na kuanza kujadili vijisenti ilhali mabilioni yakizidi kuteketea? Je nasi ni wa hovyo kama wao kuuingia mtego huu uchwara?

Kwa msingi huu basi, nashauri vyombo vya habari visivyo nyumba ndogo ya wakubwa na wadau wote tusipoteze nguvu na wakati kwenye kushupalia uchafu wa kanisa, mchungaji na mbunge. Badala yake tusimame kidete kuibana serikali itupe maelezo kuhusiana na wezi wa EPA. Hii haina maana kuwaunga mkono mafisadi waliojiingiza kwenye altare. Hasha. Tuwajadili. Lakini nguvu kubwa ielekezwe kwenye EPA na kashfa nyingine zinazotugharimu mabilioni lukuki.

Maana serikali imezidi kujikanganya na kusua sua kutoa maelezo na hatua mujarabu zitakazochukuliwa dhidi ya wezi hawa.

Nani sasa anawajadilia akina Lukaza na Maregesi? Nani anauliza mantiki ya waziri mkuu mfukuzwa Edward Lowassa kulipwa mafao ya ustaafu wakati hakustaafu bali kufukuzwa? Nani anaulizia mmilki halisi wa machimbo ya mkaa wa mawe ya Kiwira ambaye jina lake lilipaswa kuwekwa wazi na waziri wa nishati na madini William Ngeleja ambaye anazidi kulipiga kalenda?

Nani anaulizia kurejeshwa kwa nyumba za umma zilizoibiwa na utawala uliopita na kuanza kuridhiwa na wa sasa? Nani anaulizia kurekebishwa kwa mikataba ya kiwizi ya uwekezaji hasa kwenye sekta za madini na nishati? Nani anaulizia matumizi mabaya ya pesa ya umma yanayofanywa na serikali? Nani anaulizia utatuzi wa mtafaruko wa Zanzibar ambao umeanza kufunikwa na upuuzi wa serikali tatu na kama Zanzibar ni nchi au la?

Tusiingie mtego wa mafisadi kijinga kwa kupwakia mjadala wa shilingi milioni saba na ushei tukasahau kushinikiza wezi wa mabilioni ya EPA na Richmond wayarudishe kisheria badala ya kurejesha kwa mlango wa nyuma kama ilivyo sasa.
Tusikubali usanii wa kuihamisha hadhira toka kwenye jambo la msingi na kuhamia kwenye upuuzi mdogo kama huu.

Bahati mbaya huu umekuwa ndiyo mchezo wa mafisadi wetu. Wakati yalipoibuka madai ya kuwepo ufisadi kwenye ngazi za juu serikalini, hadhira iliamka na kudai haki itendeke. Ikiwa haina hili wala lile, liliingizwa suala la kuawa kwa mbunge wa CCM aliyekuwa akisimama kidete kupambana na wauza unga, marehemu Amina Chifupa. Baada ya hapa mara tuliletewa timu ya taifa kupelekwa bungeni kupongezwa. Upuuzi wote huu ulifanyika ili kuepusha hadhira kuliona hili la ufisadi.


Kama siyo wapinzani kusimama kidete huenda kashfa hizi zingezimwa kinamna namna kama hii ya EPA na Richmond vinavyoelekea kuzimwa na kuondolewa mbele ya hadhira.

Tukatae uchafu huu. Tusikubali kuchezewa mahepe mchana kweupe. Maana, kama tutachezewa nasi tukaridhia, tutabaki kuathirika huku wezi wachache wakiendelea kututumia kama mashamba yao ya kujitajirishia.

Wala tusiridhike na mafanikio kidogo yaliyokwishapatikana kama kufukuzwa kwa Lowassa na wenzake. Tusimame kidete kuhakikisha haki inatendeka na pesa yetu inarejeshwa haraka sana iwezekanavyo. Au na hili litangoja uchaguzi ujao? Kama itakuwa hivyo basi aminini sisi ni mataahira sina mfano!

Tusifanye hivyo kwa kuangalia aina ya watu waliotimuliwa. Bado tuna mafisadi wengi serikalini wanaopaswa kufukuzwa. Na kazi hii ni ya wananchi. Maana rais ameishaonyesha wazi asivyo na mpango wa kuwashughulikia mafisadi. Na hakuna malaika atakayekuja kufanya kazi hii muhimu na adhimu isipokuwa sisi wenyewe wananchi.

Nje kidogo ya mada, hivi karibuni kulifichuka jinai ya mke wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa mama Anna kuwaibia walimu kwa kuwatoza riba zaidi ya aslimia 60. Najua wengi wanakumbuka jinsi tulivyompayukia Kikwete amchunguze Mkapa na familia yake na akatutolea nje.
Hawezi kufanya hivyo. Kwa sababu naye mke wake ana tabia na sura sawa na mama Mkapa. Rejea kuunda NGO ya WAMA pindi alipoingia madarakani mumewe kama alivyofanya Anna.

Kimsingi tunachofanya ni kuendelea kufanya uzembe kumwamini mtu asiye na mpango nasi. Ni upuuzi. Ni sawa na kumpa jini damu au mbwa nyama akutunzie. Utalia baadaye sawa ana ambavyo watanzania watalia.

Wengi tumeanza kujenga imani kuwa Mkapa bado anatawala kwa mlango wa nyuma ingawa Kikwete alituaminisha hana ubia na mtu kwenye serikali yake wakati anao wabia yaani Mkapa na familia yake, watuhumiwa mbali mbali wa ufisadi ambao hawashughulikii. Na kubwa zaidi ya yote, Chama Cha Mapinduzi na makampuni yake yanayotumika kuliibia taifa.

Ila Kikwete ajue. Kuna uwezekano huu urahimu na kutojali kwake vikakimaliza chama cha mapinduzi na kuishia kuwa KANU kule Kenya. Ama kweli madaraka hulevya kweli kweli!

Haya ndiyo masuala mazito ya kujadili badala ya kupoteza nguvu nyingi kwenye vipande thelathini vya Rostam kwa wachungaji walafu na mbwa mwitu wawararuao wajoli wa Mungu.

Umefika wakati kwa watanzania kuamka na kuidai nchi yao iliyobinafsishwa kwa wawekezaji na mafisadi wajifichao nyuma ya pazia la madaraka. Suala hili nitalijadili sana kwenye kitabu changu kiitwacho Nyuma ya Pazia ambamo mhusika mkuu ni waziri mkubwa, Edmond Mpendamali Mwaluwasha anayetumia ofisi yake kama kijiko cha kulia maini ya watu wake.
Source: Dira ya Tanzania Julai 22, 2008.

No comments: