How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 23 July 2009

Kijiwe chaandaa nishani ya ufisadi kumtuza Njaa Kaya


KWANZA Kijiwe kinaomba msamaha. Ilipita miezi mingi bila kuwasikia akina Mgosi Machungi, Mzee Kidevu, Mbwa Mwitu, Mpemba, Kapende na Mzee Maneno pamoja na wengine bila kumsahau Makengeza au Kenge kwa ufupi.

Tunaye mwanakijiwe mpya Mipawa wa Pawa. Tulikuwa na udhuru mkubwa hasa kushiriki chaguzi kule Biharamulo na Busanda ambapo lafu ilichezwa sina mfano.

Baada ya kuachana na mambo ya siasa, sasa Kijiwe kimerejea kwenye shughuli za kawaida. Kumbuka hiki si kama kile cha Idodomya ambapo kutishana na kuapizana kukwamishiana bajeti ni maigizo ya kawaida.

Sisi tunafanya shughuli za kijiwe vilivyo. Hatupayuki ili wanakijiwe watuchague tuwabamize tena mkenge kama jamaa zetu wa Idodomya ambao, kama vyura, kila mmoja anahanikiza utadhani anawapenda walevi wakati anawaponda! Sisi tunawakilisha wanakijiwe na si matumbo yetu.

Nikiwa nimejiinamia nikimsaka mtu wa kubomu lau nyumbani watoto waende nonihino, mara Mpemba anatuamkua “Assalaam alaykum jamia.”

Muuza kahawa anakuwa wa kwanza kuitikia “Walikuwa waislamu.”

Inaonekana Mpemba ana jambo linamhini. Kwani hata utani wa muuza kahawa hausikii. Anaanza hata bila kungoja kuulizwa ni yaje.

“Mmesikia hawa walafu na mafisadi eti wasema mafuta si saala la muungano? Sie Pemba twaangalia tu. Mbona wao walitumia karafuu yetu kujenga Unguja hatusemi? Sasa washikilia mafuta hata yasovumbuliwa."

Kabla hata ya Mpemba kujibiwa, mara Mgosi Machungi anaingia na gazeti la “Waambie”. Anatusomea habari. “ rofesa Ibueim Ipumba amuipua Njaa Kaya Kikwekwe na kusema ndiye baba wa ufisadi wa EPA na Richmond.”

Kapende anadandia mic. Anasema, “Hii si habari mpya. Sema kwa vile aliyemtaja msanii ni mzito wa chama. Je, walevi watastuka na kumshikisha adabu? Hata kunguru wanajua Njaa Kaya, nkewe na genge lake walivyo EPA na Richmonduli.”

Anakohoa na kubwia kahawa yake kidogo na kuendelea. “Mna habari Njaa Kaya alidhani anaweza kuukimbia ukweli kwa kumtoa kafara Mzee wa Richmonduli Ewassa.”

Mzee Maneno anakwanyua mic. “Ushuzi siku zote huwezi kuuficha kwa kujitia marashi. Inzi lazima watakufuata kama ambavyo Njaa Kaya hataukimbia ukweli. Kila mtu anajua alivyotumia pesa ya EPA na Richmond kutoa takrima na kuibuka kwa ushindi wa Tsunami unaogeuka kuwa Tsunami kweli.”

Mgosi Machungi anadakia. “Ajabu bado anatiaminisha timchague aibe tena. Kama kipindi cha kwanza ametiibia hivi hiyo lala saama itakuwaje; si atatiibia hata wake zetu jamani.”

Mipawa hajivungi; anajibu haraka. “Awaibe mara ngapi? Hamuoni, kama Tunituni na Anna Tamaa, anavyowatumia wake zetu chini ya NGO, lake wizi mtupu? Wake zetu wameishaibiwa taka usitake.”

Mbwa Mwitu anachomekea haraka haraka. “Kuiba au kutowaiba wake zetu mimi haliniangaishi. Kinachonihangaisha ni kuiba mstakabali wa taifa.” Wakati akisema haya Mgosi Machungi anamkata jicho na kusema. “Ina maana wewe huna uchungu na mkeo!”

Mbwa anajibu kwa utani. “Nina uchungu hasa na mkeo.”

Machungi anatahadhalisha. “Mbwa angaia maneno yako. Tinaweza kutoana macho wenyewe kwa wenyewe. Kama una uchungu wa kuipiza kisasa si uende unchukue mke wa Njaa Kaya anayetumia wake zetu ili nae aone uchungu?”

“Loo! Mbwa Mwitu ndiyo unazidi kulikoroga kabisa, eti anawatumia wake zetu!” Anachomekea Makengeza.

“Anatutumia wote. Huko nyuma haikuwa hivyo. Je tumelogwa kiasi cha kujirahisi na kuendelea kuchezewa kuliko huko nyuma.” Alidakia Mchunguliaji aliyekuwa akichungulia vichwa vya habari.

Mara Kapende anadaka mic. "Jamani wabongo kwa matusi sina hamu. Huko nyuma na kuchezewa maana yake nini?" Wakati huo Mzee Maneno ndiyo alikuwa anamalizia kipisi chake cha sigara kali.

Abusu mic. "Njaa Kaya kweli anatuchezea na kujichezea mwenyewe. Maana anafanya mambo kana kwamba hakuna kesho. Nasikia anaumwa ugonjwa wa moyo kutokana na kutaa taa akitafuta jinsi ya kulizima jinamizi la EPA na Richmond. Kwani hata alipomtoa kafara rafiki yake Ewassa bado zimwi linamuandama vilivyo."

Kabla ya kuendelea, Mzee Kidevu anamwingilia na kusema. "Nasikia kweli jamaa anaumwa. Maana akina Kagoda wametishia kumfichua kama atawafichua au kuwafikisha mahakamani. Hivyo anaomba Mungu uchaguzi ufike mwakani apete na ahomole na kukitoa akingojea majaliwa yake kutokana na atakayemrithi."

Machungi anatia timu tena. "Kuna kipindi tinapaswa tijilaumu wenyewe kwa kuendeea kugeuzwa mazuzu. Kwanini tisiandamane hadi ikuu kumwambia akitoe wenye akili wationgoze?"

Mpemba hajivungi. Anakwanyua mic. "Yakhe Ngosi, mie naunga nkono mawazo yako. Kutonkabili Njaa Kaya kwamfanya aone wote wakeze ati. Jamaa ana roho ya paka yule. Hata useme vipi yeye anyamaa na kuendelea vuruga mambo. Umeona alivonywea kwenye sakata la mahakama ya kadhi na chochoko choko cha kujiunga na OIC?"

Anatwaa kombe na kulibusu kidogo na kuendelea. "Sasa kila kitu afanya huyu wa Kupinda ambaye naye apindisha mambo ati. Wajua huyu bwana njinga sana? Wakumbuka alivontetea Nkapa eti si fisadi, ni ncha Mungu wakati jizi na familia yake?"

"Yakhe mwache huyu jamaa. Nilikuwa namheshimu sana. Lakini baada ya kujigeuza dodoki la fisadi Tunituni nimemponda kuliko hata kuku na Njaa Kaya. Sikujua jamaa angetumiwa kufanya uchafu kama huu. Tusilaumu sana. Tunatawaliwa na mafisi na mafisadi." Anachomekea Mbwa Mwitu.

Mzee Mzima naona kama mada itaisha bila kukamua. Naamua kuvamia uga ili nisije nikafulia. "Wazee tuambizane ukweli. Njaa Kaya anapoteza muda. Hata Tunituni alipoonywa kuhusu ufisadi hasa wa mkewe alijigeuza mbogo. Njaa Kaya ameamua kutumia njia ya kunyamaza akidhani atapona. Kila lililo na mwanzo sharti liwe na mwisho."

Nakatua kashata na kuendelea. "Jamaa kaishiwa hakuna mfano. Siku hizi gazeti lake la umbea la Daily Wizi linaonyesha video ya safari yake kwa Obama. Ajabu wanaandika upuuzi eti Obama alimsifia kuwa kiongozi wa kuigwa barani wakati yu habithi!

Kama alimsifia kwanini aliamua kumpiga kibuti na kufanya ziara nchini Ghana badala ya Bongolala? Alijua jamaa lilivyo sanii na fisadi. Wataendelea kuwadanganya wajinga wenzao lakini si kijiwe chetu. Mie naona tungeandaa nishani ya usaliti na ufisadi tumpe Njaa Kaya ajue sisi si wa kuchezea. Nishani ya pili tumpe nkewe na ya tatu tumpe Tunituni na Anatamaa. Mnasemaje wazee?"

Wanakijiwe wanalipuka kwa vicheko na vigelegele huku makelele yakihanikiza kiasi cha kuwavuta wapita njia ambao wanasimama kwa mshangao na mshawawasha. Si mnawajua wadanganyika kwa kupenda kushangaa.

Mie sijali naendelea. "Aibu kuwa na sanii kwenye patakatifu pa patakatifu. Mnaona aibu aliyotuletea kwa kumuunga mkono habithi Humer Shari wa Sudan? Jitu limenyonga watu wake nasi tunaliunga mkono lisikamatwe na mahakama ya kimataifa ya jinai. Mnafahamu yule mwendesha mashitaka wa ICC, Luis Moreno Ocampo tulisoma naye ughaibuni?"

Wanakijiwe wanaonyesha mshangao. Wanajua hizi ni kamba za mzee mzima. Ila ukweli ni kwamba Ocampo ni rafiki yangu na kuna siku nitamkaribisha kuwakamata wauaji wa kwenye migodi kule Musoma wanaoua watu kwa kuchafua mazingira.

Mara Mgosi Machungi anachomekea. "Hata Njaa Kaya na kundi lake wanapaswa kufikishwa Uhoanzi kujibu tuhuma za kuua wadanganyika kutokana na ufisadi wake. Nao wanafanya mauaji ya haaiki kwa kutumia umaskini badala ya bunduki."

Tom anaingilia kati. "You are right Mgosi. Una habari kama kosa la kuuibia umma litatafakariwa vizuri akina Njaa Kaya ni wauaji sawa na wale wanaofanya genocide nchini Sudan? Normally ufisadi huzaa upendeleo na chuki miongoni mwa wanajamii kiasi cha kusababisha umwagaji damu. Tunaelekea huko ingawa wezi wetu hawataki kukubali.

Hebu nieleze. Bunge letu lina maana gani iwapo bajeti za kipumbavu kama ile ya Mstaafu Mkulu inapita huku pesa nyingi ikiibiwa kwenye bajeti iliyopita? Actually, we need to.."

Kabla ya kuendelea mzee Kidevu anaamua kuvamia uga kumtahadharisha Tom apunguze umombo.

Anasema. "Msomi taratibu. Unatuaacha nyuma. Angalia lugha msomi."

Kabla ya Tom kuendelea, naona vimbelembele wawili wakiwa kwenye magwanda yao wakijongelea kijiwe kutokana na zile shamra shamra za kutaka kutoa nishani. Kila mmoja anajikata kisilesi na kumwacha muuza kahawa akitaataa na vyombo vyake tayari naye kutimka.

Tuonane wiki ijayo inshallah.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 22, 2009.

No comments: