The Chant of Savant

Wednesday 8 July 2009

Tunituni na Chekacheka wasameheni waishiwa


Nillinyaka juzi kuwa jamaa wa kupinda kawafunga walevi kamba eti mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwila utatwaliwa na kurejeshwa serikalini. Kwa juu, hii ni habari njema. Lakini ukiangalia tabia ya longolongo na sanaa za jamaa yangu Chekacheka, unhhh, unapata wasi wasi kama kweli wa kupinda anajua anachosema bila kupindisha.

Nao waishiwa, baada ya kulazimishwa kupitisha upuuzi, sorry, bageti ya Mstaafu Mkulu kwa kutumia katiba viraka, nao wamejitutumua! Wanataka kumjadili Tunituni kabla ya kunyang’anywa mgodi. Mlikuwa wapi muda wote huu?

Kusema ukweli, mimi na Chekacheka tusingetaka Tunituni ajadiliwe wala kuchunguzwa. Tunataka tuchukue mgodi ili kufunika kombe wanaharamu wapete. Waishiwa wakitaka tumjadili tutaumbuka wengi. Kwanza, Chekacheka alishasema atamkingia kifua hadi anang’atuka baada naye kunyakua atakochoridhia. Si unajua tena kaya ya ulaji na Bongolala.

Kwa vile waishiwa hata Chekacheka wanakabiliwa na kiminyo mwakani kwenye uchafuzi mwakani, kila mtu ajitutumue ili asikike. Sisi, tumeamua kurejesha mgodi kwanza, ili kumuepusha jamaa yetu Tunituni kwenda lupango kama jamaa yetu pale Zambia. Pili ni kutaka kupata kura za walevi. Maana ukifika wakati wa kampeni hili litageuka dili na sera. Si unajua tena mambo ya kuusaka ulaji wa dezo.

Hakuna haja ya kumchambua Tunituni kama karanga. Kwanza ni mtu safi anayemcha Mungu kweli kweli. Ila kumbukeni. Wacha Mungu tuko wengi. Mie namcha Mungu pesa; wengine Mungu madaraka na wengine Mungu sifa mradi kila mtu ni mcha Mungu. Hata yule jamaa yangu wa Richmonduli ni mcha Mungu kwelikweli. Amewahi kwenda hata Yerusalimu kuhiji baada ya kuona kuwa Mungu wake wa tamaa halipi. Hivyo aliamua kumrejea Mungu wa Israeli.

Kwa walevi wasiojua ulaji unavyolewesha, wanadhani Tunituni alikosea kukwapua alichokwapua. Hivi ulitegemea nini na angefanya nini wakati Bi. Mkubwa, kama alivyo wa Chekacheka, alikuwa akimweka majaribuni kila siku ukiachia mbali shemeji zake.
Kwanza angeogopa nini iwapo na geshi nalo alilipa ulaji tena unaomeremeta kama dhahabu na almasi? Kimsingi, Tunituni, kama Charles Ponzi na Bernard Madoff, ataacha legacy ya upatu. Wakati wachezesha upate wenzake walichukua pesa ya wateja wao, Tunituni alichukua mali za walevi wake.

Ingawa hayajawakuta, hali inavyokwenda, msishangae ya Tunituni mkaona ya Chekacheka. Heri ya Tunituni mvua tano za kwanza alifanya kweli kuliko Chekacheka aliyeshindwa kabla hata ya kuanza kuwatumikia walevi ambao aliamua kuwatumia badala ya kuwatumikia.

Nawaonea huruma waishiwa. Hivi wao wana udhu gani wa kumjadili Tunituni iwapo wamepitisha bageti ya makufuru na matusi? Kama kuna wa kumjadili Tunituni basi si wengine ni wale waheshimiwa wa upinzani lakini si waishiwa wa nambari ziro. Kwanza jamaa hawa ni wanafiki na woga. Juzi niliandika ukurusa mzima kuwasifia kwa kukamia kukwamisha bajeti ya Mkulu halafu wakaipitisha kwa kishindo cha Tsunami! Hawa hawafai na hawana hata maana.

Kwanza nawahurumia. Sijui kama wengi watarudi kutokana rekodi yao ya kupenda kukaa Bongo wakifanya umachinga badala ya kwenda kwenye majimbo kuwahudumia walevi. Wapo ambao wamepata nishani za ububu. Yaani jitu linalipwa mshahara na marupurupu mazito tena linatembelea shangingi halafu linakwenda bungeni kufanya ushangingi!
Nilishangaa kuona mmoja wa mabubu haya anajitutumua kuwataja nyangumi baada ya kumfichua kuwa yeye ni papa. Kwa maslahi ya waliompa kula hana muda wala maneno ya kusema. Ila kwa maslahi yake na Kagoda anachonga kama kasuku! Je huyu naye anapaswa kurudi jamani hata kama anawahonga wapenda nyama nyama?

Hakuna watu nina usongo nao kama wale mawaziri wanaojifanya uwaziri ni mali ya kurithi kiasi cha kuwadharau waishiwa. Hata kama ni waishiwa,si wameishiwa wenyewe lakini si wale waliowatuma. Hivyo, tutaona. Kama kuna watu wenye hati milki za uwaziri tutajua. Hata uwe shemeji yake bosi au mshirika wake, bado si dili kuwadharau waishiwa waliotumwa na walevi wawakilishe shida zao. Ajabu tena bila aibu, wengine walifikia hata kufuru ya kutetea mapapa wakijua kufanya hivyo ni kuwahujumu na kuwasaliti walevi. Hata kama ni walevi jamani watendeeni haki. Kwani hamjasikia? Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kuna kesho.

Turejee kwa Tunituni na Chekacheka na jamaa yetu wa kupinda. Tumeamua kurejesha huo mgodi ili kuepusha kuwasweka rumande jamaa zake hasa Bi Nkubwa na watoto. Baada ya kuona yaliyomfika first lady Regina Chiluba pale Zambia, washauri wetu wametwambia: tukiendelea kulaza damu Anna Tamaa Tunituni na vitegemezi, na vivyele vyake wanaweza kujikuta wakinoniho kwenye debe kule Ukonga alikowahi kusota mshikaji wake wa zamani Pesatatu.

Hivyo kuwaokoa hawa, ni kuchukua godi bila kutoa maelezo kibao ili kuepuka kuwapa wambea faida. Pia kufanya hivi ni kuepusha jamaa zetu kudaiwa fidia kwa muda waliolikamua godi.
Pia tunazuia waishiwa wa nambari ziro kujadili suala hili ambalo baadaye watalipitisha kama bajeti, ili kuepusha kuwapa nafasi wale waheshimiwa wa upingaji kuzidi kutuanika na kustukia madili yetu mengine.

Pamoja na yote, tumeona kuepusha lawama, tumpe wa kupinda alipue bomu. Maana yeye kwa cheo chake cha uwaziri mkubwa anateuliwa si kuchaguliwa kama sisi. Hivyo jamaa lazima afanye kazi ya kusafisha uoza wetu ili walevi watuamini na baadaye watupe kula tuwafungie mzigo kama Tunituni ngwe yetu ikiisha.

Kitu kingine, k ama waishiwa wangekuwa wanawawakilisha walevi kweli na si matumbo yao, wangekuwa na kila sababu ya kumjadili Tunituni. Wengekuwa safi wangefanya hivyo bila shaka. Pia kiama chetu hakiwezi kuruhusu mchezo huu kwa kujichoma kisu mwenyewe ikizingatiwa kuwa ukiruhusu mjadala watakaoumilki ni wapingaji wetu. Hata hivyo kwa mujibu wa sera zetu za chukua chako mapema, Tunituni ni shujaa wa kupigiwa mfano. Ndiyo maana wa kupinda aliamua kummwangia ujiko kibao. Ni muadilifu kuliko Tunituni na waishiwa waliopitisha libajeti lisilo na maana kwa walevi.
Naona simu ya Tunituni. Acha nikaijibu haraka.

No comments: