The Chant of Savant

Thursday 23 July 2009

Kilango, Selelii na wengine someni ya Wilfred Kajeke

IF "I have this mandate to stop this reckless and irresponsible mortgaging of our country and I cannot do it, then there is no reason for me to continue being in this House. That is why I am leaving, not for a UN job, rather, to liberate my conscience.”

Tafsiri: “Kama mamlaka haya niliyo nayo (ya kuwa mbunge) hayawezi kuzuia uchuuzi huu wa nchi yetu, na siwezi, basi sina sababu ya kuendelea kuwa kwenye bunge hili. Na hii ndiyo sababu naondoka, si kwa kupata kazi Umoja wa Mataifa bali kujikomboa.”

Haya ni maneno mazito ya Mbunge Wilfred Kajeke wa Jimbo la Mbale, Uganda baada ya kuchoshwa na tabia ya bunge kugeuzwa muhuri wa kubariki ufisadi wa kimfumo kama ilivyo hapa kwetu.

Alijiuzulu kwa hiari baada ya kukaa bungeni kwa miaka minane na kugundua kuwa anazidi kujiumiza roho kwa kushiriki ujambazi wa kimfumo kama ilivyo hapa kwetu.

Baada ya kusoma tukio hili la kusisimua na somo kuu katika uwajibikaji na uwazi, haraka haraka majina ya mashujaa wetu wa maneno lakini woga wa vitendo kama Anne Kilango Malecela, Lucas Selelii, Fred Mpendazoe na wengine yalinijia haraka.

Nilitumia muda mrefu kufikiria kuandika makala hii kuwakumbusha wahusika kuwa, wanachofanya ni kujidhalilisha hata kama kuna watu wachache wanaoona kama ni ushujaa au ujasiri. Ujasiri si kusema bali kutenda. Wako wapi kina Kajeke wetu?

Mbunge aligundua kuwa anabeba dhambi kubwa kushiriki uharibifu na uchuuzi wa nchi yake, tena akiwa amekalia kiti cha uwakilishi wa umma. Ameona ni heri akose maulaji na ujiko kuliko kuendelea kuwa mnafiki na mtumwa wa tumbo. Ameaamua kutumia kichwa baada ya kuchoka kutumia utumbo.

Je, wabunge wetu waliotuaminisha wangekwamisha, kwa mfano, bajeti ya Mstaafa Mkulo na baadaye wakalamba matapishi yao kwa kuipitisha, wanaposoma au kusikia habari kama hizi wanajiona wa hovyo kiasi gani?

Je, wabunge wa namna hii si watumwa wa hiari? Je, hawa wanaopinga ufisadi kwa midomo na kuubariki kwa kura zao katika kupitisha miswaada si mafisadi kuliko mafisadi wenyewe ambao kimsingi hujikalia kimya ili umma uwajue wao ni nani kuliko hawa mafisadi wanaojifanya wanapinga ufisadi kwa midomo na kuubariki kwa mikono yao?

Lazima uwe moto au baridi lakini si vyote kwa wakati mmoja. Lazima uwe na mimba (fisadi) au usiwe nayo.

Hakika msimamo wa Kejeke ni somo na suto kwa wachumia tumbo wetu wanaojigeuza mbogo dhidi ya ufisadi kila uchaguzi ukaribiapo ili kuwaaminisha wananchi kuwa wanawawakilisha ili baadaye wawachague waendelee kuwabamiza mkenge.

Wamekuwa mabingwa wa kulipua mabomu yasiyoweza kuua hata nzi! Kila siku viapo na chokochoko visivyozaa matunda. Mafisadi wanaendelea kupeta huku wao wakikauka makoo kumbe lao moja.

Kama si moja basi achieni ngazi kama Kajeke. Fanyeni kweli. Tumechoka na longolongo zenu. Kama hamuwezi mnyamaze kuliko kutupigia mikelele wakati nanyi ni mafisadi.

Katika hili, Kajeke ana ushauri: “Either to join the system and fully participate in the looting or say enough is enough. I have chosen the latter and I am leaving.”

Tafsiri: “Ama kujiunga na mfumo (serikali) na kushiriki ujambazi au kusema imetosha. Nimechagua la pili na naondoka.”

Kama mamlaka uliyo nayo hayakusaidii kuepusha nchi yetu kutaifishwa na kina EPA, Richmond, ANBEN, TICTS, Dowans, IPTL na wengine, basi wewe ni mtumwa na roho yako inakusutu. Kuendelea kukaa bungeni ni utumwa wa hiari kwa ajili ya kutumikia tumbo lako. Unahitaji ukombozi kwa kuacha kuchaguliwa ili kina Kajeke waje wawakomboe wananchi baada ya kujikomboa wao.

Je, tunao kina Kajeke wangapi Tanzania? Huwa nashangaa mantiki hata ya wabunge wa upinzani kuondoa shilingi ili bajeti ikwame na rais avunje Bunge kama kisemavyo kifungu cha Katiba cha 90 (2) (b), ambacho Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alikitumia hivi karibuni kuwanyamazisha na kupitisha bajeti ambayo kimsingi ni ya maangamizi kwa wale wanaodai kuwawakilisha.

Hapa ndipo ukweli kuwa unaweza kumuamini yeyote lakini si mwanasiasa unajidhihiri. Ingawa tumekuwa tukiwasifu wabunge tunaowaita machachari, ukweli ni kwamba umachachari wao kama hauwezi kuiadabisha serikali ikaacha kutuibia ni sawa na umachachari wa kibonzo au katuni. Hawa wabunge ni sawa na simba wa karatasi asiyeweza hata kumpoka nzi.

Tumalizie kwa maneno ya Kajeke. “Don't let the people of Uganda down. If you do, one day you will encounter them at your gate or on the streets of Kampala, demanding for their share.”

Tafsiri: “Msiwaangushe wananchi wa Uganda. Mkifanya hivyo, siku moja mtapambana nao kwenye geti au mitaani Kampala wakitaka shea yao.”

Nanyi wabunge wetu wapenda sifa na kulipua mabomu, msiwaangushe wananchi wa Tanzania. Kuna siku usaliti huu utawatokea puani. Kwani wamevumilia vya kutosha na sasa wamechoka.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 22, 2009.

No comments: