How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 4 July 2009

Pinda, unataka kumdanganya nani?


Nafahamu waziri mkuu Mizengo Pinda ni mwanasheria. Matamshi yake hivi karibuni kwa bunge kuwa atachukua mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira toka mikononi mwa rais mstaafu Benjamin Mkapa, familia yake na marafiki zake yana utata kisheria.

Yanaonekana kuwa ya kisiasa zaidi ya kisheria. Alikaririwa akisema, "Mimi nilichoamua... kama issue ya Kiwira ndio kitu kikubwa, nitahakikisha zile hisa zote zinarudi serikalini, zote,"

Aliendelea, "Nitachukua zote nitazirudisha serikalini tuanze upya ili tuone kuwa hiki tulichoanza nacho, pengine kitatupa tija tunayohitaji." Je hapa Pinda anaamua kama Pinda haoni kama anatoa mwanya kwa akina Mkapa kumshitaki na hatimaye kurejeshwa mgodi na kudai fidia? Anashindwa nini kusema serikali imeamua kama kweli ana nia nzuri ya kuurejesha mgodi huu? Je hajui kama ataamua kama waziri mkuu, kuna bosi wake juu yake ambaye alishasema hana mpango wa kumchunguza Mkapa?

Je kitendo cha Pinda kutaka jinai hii iishe kishikaji si njia ya kuwanusuru wengine wasio na kinga kama Mkapa? Je huu haujawa usanii na kutuhadaa na kutugeuza majuha? Kwanini uzuie bunge kujadili suala hili halafu mtu mmoja asiye na mamlaka yoyote kikatiba ajitwishe kadhia hii kama hakuna namna?

Kinachofanya nitilie shaka mikakati ya Pinda ni kauli zake. Hebu tazama nukuu hii. "Tunapomtaja Mkapa kuwa ni fisadi, tujiulize ufisadi wake upo wapi? Ameweka mabilioni ya fedha nje ya nchi… Naamini mtu huyu ni safi na namfahamu kuwa ni mcha Mungu,"

Ufisadi tafsiri yake si kuweka pesa nyingi nje ya nchi. Ufisadi ni ile hali ya mtu kutumia nafasi yake, ushawishi au vyovyote iwavyo kuuibia umma kama alivyofanya Mkap ana wenzake.

Eti Pinda hajui ufisadi wa Mkapa? Ajabu! Yaani anaona rais kutumia madaraka yake kutwaa mali ya umma ndiyo huo ucha Mungu anaotwambia Pinda? Huwezi kumuita Yuda Iskalioti mcha Mungu kwa kumsaliti Bwana. Kama Mkapa ni mcha Mungu ni kwa Pinda si kwa watanzania ambao hadi sasa wanaishi maisha magumu kutokana na ufisadi wake. Rejea kuiba nyumba za umma na kuzigawa miongoni mwake na mwaziri wake akiwamo Pinda na bosi wake. Reja kuingia mikataba ya kijambazi ya uwekezaji kama ule wa kuleta Net Solution Group kulikofanywa na shemeji zake. Rejea kuiua na kuiuza iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Rejea kulihujumu shirika la umeme Tanesco kwa kuingia mikataba kama IPTL. Rejea kuruhusu familia yake hasa mkewe kutumia NGO kujineemesha kwa mgongo wa ofisi ya rais bila kusahau kupata mikopo nafuu na kujitwalia mali za umma kama Kiwira.

Pinda anajikaanga mwenyewe kwa kutoa madai yaliyopinda. Anakiri kuwa Mkapa alishiriki ujambazi wa Kiwira lakini bado anamuita mcha Mungu! Inaelekea ndugu yetu hajui maana ya neno mcha Mungu.

Alikaririwa akikiri. "Tuangalie, inawezekana aliburuzwa kutokana na matatizo ya wakati ule," Kwanini mtu mwenye akili timamu na kila nyenzo ya usalama aburuzwe kama kweli hakuwa na nia ya kujineemesha kwa kutumia madaraka? Mbona Mkapa alishauriwa akawachukia waliofanya hivyo hadi kufikia hata kuwafutia uraia baadhi yao ? Huyu si mtu wa kuburuzwa bali kuburuza kama anavyotaka kutuburuza mtetezi wake Pinda.

Kuna haja ya kustukia na kupinga mbinu za Pinda, Mkapa na wenzake. Inadaiwa kuwa mgodi wa Kiwira unamilikiwa na Nick Mkapa, Foster Mkapa na B. Mahembe ambao wanamiliki kampuni ya Fosnlid wakati kampuni ya Devconsult LTD wamiliki wake ni D.Yona na Danny Yona J.R.

Makampuni mengine ambayo yaliungana na kununua mgodi huo ni Choice Industries, ya Joe Mbuna ambaye ni kivyele cha Mkapa na Goodyeer Francis na kampuni ya Universal Technologies, ambayo inamilikiwa na Willfred Malekia na Evance Mapundi. Wabia hawa ndio waliounda kampuni ya Tanpower Resources Ltd inayomiliki mgodi huo.

Je haoni kwa kunyang’anya mgodi kienyeji ni kuwaepusha wamilki wengine kufikishwa mbele ya sheria na kuwajibika? Je hasara iliyokwisababishwa na kuendelea kumilkiwa kwa mgodi huu kinyume cha sheria anaiweka upande gani? Ni vizuri Pinda akaelezwa ukweli kuwa anachofanya ni usanii na kushirikiana na wahalifu kutaka kuendelea kulihujumu taifa.

Ni vizuri Pinda na wenzake wakajua kuwa watanzania wamekomaa. Hivyo kuwafanyia usanii wa kitoto ni kuwatukana matusi ya nguoni.

Kwanini Pinda asiseme wazi kuwa ametumwa amtetee Mkapa? Ingawa anajitahidi kufanya hivyo hata kwa kuweka kiapo chake rehani, hawezi kumsafisha Mkapa. Kwanini asimwache Mkapa akajitetea hata mawakili wake? Hivi Pinda hajui kuwa analipwa na umma huo huo anaotaka kuudanganya na kuuhujumu na si Mkapa anayemtetea? Kama wanajuana na Mkapa, hili ni suala binafsi. Lisiingizwe kwenye mambo ya taifa. Mkapa si kichanga cha kutetewa na kila anayejihisi kufanya hivyo. Kuendelea kwa watawala walioko madarakani kumtetea Mkapa kunaweza kutoa ishara kuwa ima walishirikiana naye au nao wana mpango wa kufanya kama yeye watakapostaafu kisheria. Namna hii amani uchwara tunayojivunia itatoweka. Maana wananchi wamechoka kugeuzwa nepi na ngazi na kila fisi na fisadi ajae na kujihomolea.

Leo Pinda kaja na Kiwira kwa usanii ule ule. Kesho atakuja na Richmond ambayo nayo inawahusisha wakubwa wenzake bila kusahau Kagoda na EPA ambavyo vimegeuka serikali ndani ya serikali.

Hivyo basi wabunge wana haki ya kujadili jinsi ya kurejesha Kiwira na hatua za kuwachukulia wahusika. Sheria za nchi ziko wazi hasa zile za uhujumu uchumi. Hapa kinachopaswa kuangaliwa sana sana ni kinga uchwara ya rais ambayo matumizi na tafsiri yake inaanza kutumia kifisadi. Pinda, tell it to the birds. Unachofanya ni uhujumu na kulindana.
Chanzo: Tanzania Daima, Julai 1, 2009.

No comments: