Thursday, 13 August 2009

Kikwete, lini utatangaza mali zako?


HII ni mara ya tano namkumbusha Rais Jakaya Kikwete kutangaza mali zake, mkewe na familia kwa ujumla kama alivyoahidi kwenye kampeni za uchaguzi mwaka 2005.

Mara ya mwisho nilifanya hivyo pale mwenzake wa Urusi, Dimitry Medvedev, alipotangaza azma yake ya kuweka wazi utajiri na mapato ya familia yake, ikiwa ni kuthibitisha dhamira yake safi ya kupambana na ufisadi.

Moja ya sababu kwa Watanzania kumchagua Kikwete, ni ahadi zake za kupambana na ufisadi, ambao kimsingi kwa sasa nadhani umemshinda.

Rejea kuibuka kwa wizi wa kutisha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) pale Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na ule mkataba wa kampuni hewa ya Richmond, ambao amejitahidi kujitenga nao bila mafanikio.

Rejea serikali yake kushirikiana na watuhumiwa wa ufisadi kama ilivyotokea hivi karibuni ilipompa onyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea badala ya kumwajibisha, kumchunguza na kumfikisha mbele ya sheria.

Rejea kuendelea kumkingia kifua Rais mstaafu, Benjamin Mkapa mkewe, marafiki na washirika wake, ukiachilia mbali kutaka kuwazawadia sh bilioni 50 baada ya kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, kinyume cha sheria.

Rejea watendaji na watumishi wa karibu na rais wanaonuka na kutia kila aina ya shaka kama washauri na wasaidizi wake, mfano Kingunge Ngombale Mwiru anayetuhumiwa kwa ufisadi na uhujumu kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo.

Hakuna ubishi. Kikwete alichaguliwa kutokana na ahadi alizotoa wakati wa kampeni ambazo sasa zimegeuka kuwa sanaa kama wasemavyo watani wake.

Ni wazi Kikwete kashindwa kuwakamata mafisadi kutokana na ukweli kwamba, wengi wao ni watu wake wa karibu. Hata kutangaza mali zake nako ameshindwa! Hivi mwakani wakati wa uchaguzi atawaambia nini Watanzania wamwelewe? Je, Kikwete anaogopa nini kutangaza mali zake?

Pamoja na tuhuma zinazomwandama Mkapa, angalau alitangaza mali zake ingawa nayo ilikuwa kama danganya toto. Kwani baada ya kuchuma, hakufanya hivyo alipokuwa akiondoka madarakani.

Naamini kwamba, mtu anayeshindwa au kuogopa kutangaza mali zake na familia yake, hawezi kuwa safi. Hivyo hafai katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Kitu kingine ambacho kinanipa wasiwasi, kwamba rais anaelekea kushindwa kupambana na ufisadi, ni ile hali ya mke wake kuwa kile Wazungu waitacho 'typical replica' ya Anna Mkapa, mke wa rais anayetuhumiwa kwa ufisadi na upindishaji wa sheria.

Hakuna ubishi. Mzee Mkapa sasa yumo msambweni kutokana na tamaa za mkewe na nduguze. Nahisi hili litajirudi kwa Rais Kikwete. Mkewe, anaendesha NGO iitwayo WAMA. Nimewahi kumwandikia kuonyesha kutoridhika na biashara hii ambayo kwangu ni ufisadi wa kutumia vibaya ofisi ya rais. Bahati mbaya hadi naandika makala haya, hajanijibu.

Kwa nini Salma Kikwete hana tofauti na Anna Mkapa? Kwanza, ameonyesha wazi anavyopenda kutumia madaraka ya mumewe. Soma logo ya WAMA kwenye wavuti yake ya wamafoundation.or.tz. Kuna maneno yasemayo WAMA Foundation the office of the First Lady of the United Republic of Tanzania.

Kisheria, hakuna ofisi ya First Lady of the United Republic of Tanzania. Ukifungua katiba yetu, pamoja na udhaifu wake haina mamlaka haya. Je, yanatoka wapi na kwa nini rais anaridhia yawepo kama hana faida nayo?

Nimeona kwenye sakata la kashfa zinazomkabili Mkapa. Naamini kwamba nyingi zimeasisiwa na kutekelezwa na mkewe. Ninashangaa kwa nini Kikwete hataki achukuliwe hatua. Je, anaogopa na mkewe baadaye yasimkute ambayo yanapaswa kumkuta Anna Mkapa? Je, mtu wa namna hii anaweza kupambana na rushwa?

Hata ukisoma 'pre-amble' ya WAMA hukuti popote iliponukuliwa sheria iliyoanzisha WAMA! Hata ukiangalia wavuti ya EOTF ya Anna Mkapa, ambayo ni eotfz.org hakuna kitu kama hiki. Huu ni ushahidi kuwa NGO hizi zilizoanzishwa baada ya waume zao kupata madaraka, hazipo kisheria na zipo kama ofisi za kujineemesha. Anayepinga hili anipe ushahidi kisheria. Je, madaraka ya rais hapa hayajatumika vibaya tena dhidi ya wale waliomchagua?

Huu ndiyo utawala wa kienyeji aliosema Hassy Kitine, ingawa hakufafanua. Mie huuita utawala wa kilevi, yaani ulevi wa madaraka na njaa ya utajiri. Huu ndiyo upogo na kile Wazungu huita myopia kama si mania. Kuna haja ya kuliangalia suala hili kwa makini.

Muasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kumkaripia aliyemfuatia zilipoibuka shutuma kuwa mkewe, alikuwa anatoa vimemo kwa watu kwenda kuchukua mikopo benki.

Hii ilimkera sana Mwalimu kiasi cha kuonya; 'msipende kusikiliza ushauri wa wake zenu. Mambo ya chumbani yasitumike kuamua au kuendesha mambo ya taifa'. Kweli, Mwalimu kwa kipindi chote cha urais wake, hakuruhusu madaraka yake yatumiwe vibaya na familia yake.

Leo, tuna watu wamewajaza watoto na wake zao kwenye 'ulaji' ndani ya chama tawala, BoT na NGO halafu watu hawa watuhadae wanaweza kupambana na ufisadi. Huu ndiyo usanii wanaosema watoto wa mjini.

Kisaikolojia, taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani. Je, kama Kikwete ameshindwa kutaja mali zake kwa miaka mitano akitegemea kugombea tena, atafanya hivyo kwenye ng'we ya mwisho ambayo mara nyingi hutumiwa kwa watawala kusimama tena kwenye uchaguzi?

Rejea Mkapa alivyochapa kazi vizuri kipindi cha kwanza, akaivuruga nchi kwenye lala salama ambapo ujambazi kama EPA, Tanpower, ANBEN, Fosnik na mwingineo uliasisiwa. Je, Watanzania bado tunakubali tena kumpa Kikwete ng'we ya pili atufanyie aliyotufanyia mtangulizi wake?

Mpumbavu ni yule awekaye mayai kwenye kapu moja. Je, tu wapuuzi kiasi hiki? Kuna kashfa zinazohusisha chama tawala, yaani CCM, kutajwa kwenye kashfa karibu zote zinazohusisha wizi wa mabilioni ya pesa.

Hakijatoa utetezi kwa vile ushahidi ni kile wanasheria wanachokiita 'water tight'. Hii ikiongezewa na ukimya wa Rais Kikwete na hali ya familia yake. Je, kuna haja ya kuirejesha CCM iliyoshiriki kwenye Kagoda, EPA, Meremeta, Deep Green Finance na hata Richmond?

Leo sitasema mengi. Natoa changamoto kwa Rais Kikwete kutangaza mali zake kabla ya kumaliza muhula huu ili hata atakapogombea angalau tujue kama ni safi ama la! Hili la mke wa rais kuwa na NGO halimsaidii zaidi ya kuwa kishawishi. Ni kipofu kiasi gani kuanguka alipojikwaa jana Mkapa? Kwa wananchi, uchaguzi wa mwakani agenda kuu iwe ni nani anafaa kupambana na ufisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 12, 2009.

No comments: