ZA mwizi huwa arobaini. Na malipo ya uovu huwa ni hapa duniani, walinena wahenga. Pamoja na kulipa wapambe na walamba viatu wake wamtetee, jamaa yangu Njaa Kaya, kama Ben Njaa Makapu, anaanza kuadhirika.
Na kweli ataumbuka, aminini nawambieni. Arobaini yake inazidi kukaribia huku akizidi kuchanganyikiwa na kujichanganya. Leo, walamba matapishi yake wanakuja na hili; kesho na lile, ili mradi sanaa tupu.
Wengi wanajiuliza: Je, yule mbuzi wa kafara wa Richamundi, Eddie wa Ewassa, ameamua kumwaga mtama ili kila mtu abebe furushi lake? Je, huu ni mwanzo wa mitandao uchwara kuraruana na kulipuana? Japo sipo nyuma ya pazia, ni kwamba hakukaliki na mambo si mambo.
Je, walevi wataendelea kubugia sanaa na longo longo, ghiliba na utetezi uchwara au wataamua kumtia Yuda msalabani kweupe? Liwalo na liwe. Lazima asulubiwe mtu hapa.
Zile saa za kuwika majogoo alizosema mwana wa Adamu Nabii Mpayukaji kwenye unabii wa Tanzia punde yatatimia na ang'aaye atachafuka na kufichuka uchafu wake uliofichwa nyuma ya utukufu na utukutu.
Saa ya Yuda kupandishwa majili kupata malipo yake ya usaliti karibu itawadia na wenye macho wataona huku wenye masikio wakisikia, wasiamini kuwa kumbe walimfuga nyoka kwenye unga! Itakuwa aibu, kilio na kusaga meno kwa Yuda na salata wenzake wajilishao upepo.
Hakuna siri chini ya jua. Kila jiwe litafunuliwa na msaliti atawekwa wazi mbele za walevi na kuumbuliwa bila huruma. Je, walevi watamtia adabu gendaeka huyu mkuu wa machukizo na maangamizi katika uso wa nchi?
Mpayukaji alipotabiri alionekana mbaya. Je, mbaya hapa nani? Asemaye Kaisari yu uchi au walamba viatu na wala makombo wajipendekezao ili waambulie makombo kama malipo ya aibu, uchafu na usaliti wao?
Jamani, wakati wa kumfichua mwovu, salata, fisadi aliye tunda la ujambazi na jinai ya ufisadi umewadia, jiandeeni kumdhihaki na kumnnywesha siki huku akivikwa taji la miba.
Walevi wana hamu ya kuwaona kina Kagoda, Richmond, EPA na wengine wakiumbuka na kutiwa adabu kwenye majili ya umma. Wamehanikiza na kusema patakatifu pa patakatifu pamechafuka na si patakatifu tena.
Pamevamiwa na majambazi, vinyama vya mwitu na makahaba wa matumbo yao. Panahitaji kufukizwa ubani na kutoharishwa huku Yuda wa Nabkadnezzar, akiwambwa msalabani, nyumba yake na washikaji wake.
Japo Yuda kajitahidi kuwatoa kafara wahalifu wenzake, hajafanikiwa. Tazama. Naona kina Pesatatu Nusurupia, Dan na Mgonjwa wakitolewa kafara kumwepusha Yuda bila mafanikio. Kitafutwacho ni matumaini na imani vilivyopotea.
Hakika, walevi wanataka baba wa jinai ya ufisadi na ujambazi ajitiaye utukufu apatilizwe ili liwe somo kwa wengine. Imeandikwa. Aishie kwa upanga, atakufa kwa upanga. Achumaye asipopanda ni mwizi astahikiye kunyongwa.
Yote katika yote, akweaye kwa uchafu na jinai atashushwa navyo. Je, hayakutimia aliyotabiri nabii Musa? Hakika walevi wanataka ule ushirika mchafu uliojivisha utukufu uangamizwe na wana wa Aliye juu, wakombolewe kutoka kwenye makucha na ukahaba wa Kaisari Nero.
Wakati wa kuita kulego kwa jina lake halisi umewadia na kila mtu ajifunge mshipi tayari kuukabili ukweli na mapigo yake. Hakika amini nawambieni. Wana wa Musa watauvua ukondoo na kuuvaa usimba huku wakifanya ambacho hakikutarajiwa kwa namna ambayo haikutarajiwa.
Yashikeni maneno haya ya unabii wa Mwovu Yuda kuumbuka na kusulubiwa mchana. Tazama. Wana wa Musa watauvua umbwa, ukuku na ulamba viatu wakipania kujikomboa na kuitangazia dunia iwatambue na kuwaheshimu. Watamkabili kidhabu na genge lake kama vile chungu chungu wamkabilivyo nune.
Hakika kidhabu huyu aliyetabiriwa na manabii kuwa atageuka shubiri badala ya sukari, akakwezwa na walevi kutokana na ulevi wao wasijue ni mauti yao, atatiwa adhabu na kuondolewa kwenye uso wa dunia ya ulaji.
Mwana wa yule mwovu lazima apatilizwe na mapema. Lazima magenge yote na vinyamkera na vitimbamkwiji waliomzunguka nao wateketee naye kwenye bahari ya moto uchomao fisidi na hasidi.
Pakuu pa pakuu patatayarishwa na kurejeshewa kilicho chake huku somo la milele juu ya adili na idili likifundishwa kwa dunia ya wapenda haki na maendeleo.
Tunahitaji kuvaa silaha zetu za kivita ambazo ni kujiamini, ushirikiano, uwazi, uthubutu na ukweli, tayari kumkabili mwovu salata na watu wake. Kwa silaha hizi, hatutamwogopa mtu wala magenge yake ya makenge watu. Tutamkabili yeyote kwa mustakabali wetu na vizazi vyetu.
Karibu minara, vinara na mihuri ya wizi, ufisadi, ujambazi na kila jinai itadondoshwa na uovu utaporomoka huku walevi wakijitambua na kufanya mapinduzi ya kifikra ili kutorudia kosa.
Alianza yule aitwaye Asi wa Ewassa na sasa atafuatia yule aitwaye Njaa Kaya, mwenye makeke kama Kitwitwi hadi akaitwa Kitwitwi. Atafuata yule mwanzilishi wa salata aitwaye Makapu na mama watoto wake. Huyu zake zazidi kwisha asijue maskini.
Baada ya hapo kishindo kikubwa kitasikika huku baragumu ikipigwa na mwovu mkuu atawekwa ugani akiwa uchi wa mnyama tayari kuipokea hukumu ya umma. Natamani siku hii kila mmoja asilale na awepo kushuhudia kushindwa kwa fisidi na hasidi mkuu.
Siku hiyo ikitimia vigogo vingi vitaporomoka kama unyoya kwenye mgongo wa ng'ombe ambaye huwa hauhisi unyofolewapo. Tuandae mapito ya kaya mpya yenye kila kitu kipya na walevi waliojitambua walioitwa Danganyika wakadanganyika kwa uongo wa kila jizi.
Tumaini jipya na mwelekeo mpya vitaonekana siku hiyo kuchukua mahali pa kiza, ulafu, salata, ukahaba na ujambazi. Hakika imeandikwa. Heri kijana maskini mwenye busara kuliko mfalme tajiri mpumbavu ajilishaye pepo asijue ni kuni za maangamizi yake. Aaminiye wamlao akidhani wanamhami asijue wanahami matumbo yao. Atumiwaye akadhani atumia asijue anapaa mkaa kama pweza mpumbavu.
Sikizeni enyi Tanzia. Yule habithi aliyetiwa muhuri wa uovu atatiwa hatiani siku si nyingi huku wapambe wake wakiasiwa na kunyofolewa ndimi ziwapazo kiburi na majisifu.
Hakika wote watatupwa gerezani aminini nawambieni ili yatimie yaliyotabiriwa na kuandikwa kwenye kasri la nabii Mpayukaji mwana wa Msemakweli aitwaye Msemahovyo.
Hakika imeandikwa. Kila jambo lina mwisho wake, ingawa uongo huaminika kuliko ukweli. Lakini ukweli hauuawi na ukweli huweka huru.
Tuufie ukweli kwani utatuweka huru. Umefika wakati wa kuwazika majambazi wa Richamundi, ambapo wataumbuka ambao hatukutegemea.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 12, 2009.
No comments:
Post a Comment