Thursday, 20 August 2009

Nina usongo na damu ya mtu

BAADA ya munene wa nguvu na raismali kuhalalisha ujambazi kwa kutangaza kuwa Beni Njaa Makapu, nkewe, vitegemezi na washirika zake wangezawadiwa bilioni mia tano, nilijisikia kupandisha mwenembago kiasi cha kutamani kunywa damu ya mtu, nikishushia nyama yake.

Bill Ngurumbili Ngereza, bosi wake na sirikali kwa ujumla waliamua kumzawadia mjasirimali ulaji kwa kuonyesha mfano katika kujasrimali akiwa ikulu.

Si siri. Baada ya kusikia upuuzi huu nilitamani nikutane na jamaa hawa kwenye mitaa ya giza nikiwa nimejihami na zana za maangamizi kama vile sime na mikuki, nondo, bisbisi na panga ili lau niwafanyie kweli.

Hivi ulijisikiaje uliposikia kufuru hii ambapo majembuzi badala ya kupelekwa lupango yanazawadiwa njuluku za apache alolo kama wewe nami?

Mie sikuamini kama viumbe hawa hayawani watu wana akili timamu. Pendekezo langu ni wapelekwe Mirembe wakachunguzwe bongo zao kabla hawajaleta madhara zaidi.

Pili sikuamini kama jamaa hawa mafisi wa mafisidi walisoma na kuelewa somo la uzalendo wakati wa Mchonga. Sijui kama walielewa hata dhana nzima ya kujitegemea na kujenga taifa.

Kama wangeielewa vilivyo wasingejitegemea kwa kuibia makapuku wa kaya hii huku wakilijenga kwa kulibomoa. Hakika upuuzi na ujambazi unaoendelea unanikumbusha wimbo maarufu wa zamani wa bomoa tutajenga kesho.

Tatu, sikuamini gendaeka hawa waliumbwa na chembe ya aibu. Watakuwa nayo vipi iwapo wanayofanya hata mbwa na kunguru wanawazomea na kuwacheka? Maskini hawasikii wala hawaoni. Wakisikia neno utajiri au pesa, basi utu huwatoka na kuvaa ufisi kiasi cha kuendekeza ufisadi.

Hayawani watu hawa bila shaka. Hivi ni akili gani hata kama ni mbovu kwa jizi hata kama heshimiwa kuiba mali ya walevi likazawadiwa mara mia badala ya kulambwa bakora na kuozea lupango? Au ni kwa vile walio na madaraka leo hawana tofauti na majizi wayalindayo ukiachia mbali kuwa nao ni matokeo ya majizi haya haya?

Natamani ninywe damu mtu hasa hawa mafisi fisidi. Hawa waibakao kaya wanapaswa kubakwa pia. Ndiyo. Sikio kwa sikio, jino kwa jino. Mwenye masikio na asikie ipo siku itakuja.

Hivi akili gani kwa jizi hata kama jiheshimiwa kuiba mali ya walevi halafu likazawadiwa mabilioni badala ya kula mboko na kuozea lupango? Bado nina usongo na kiu na damu ya fisadi heshimiwa. Laiti Musa angerejea leo na torati si haba tungewatia adabu fisi watu hawa fisidi.

Eti, jitu linatumia vibaya patakatifu pa patakatifu na makahaba zake halafu linazawadiwa njuluku za makapuku hata kama walevi! Kwanini kondoo wafe njaa ilhali chui na fisi wakinenepeana kwa nyama ya kondoo?

Ajabu fisadi jingine bado linajichekesha chekesha kama changu likiwahadaa walevi litawaletea maziwa na samli nao wanaliamini!

Hali ni mbaya hadi Shehe Ubwabwa anatabiri maangamizi na misiba kwa mafisadi. Ingawa Shehe Ukoko huyu haaminiki kwa sanaa zake za utabiri, kuna jambo. Hapa pamoja la laghba zake amelenga. Lazima tuchenjiane kieleweke tena na mapema.

Siamini pamoja na ulevi wao, kama walevi wataendelea kukubali kunajisiwa mchana hivi. Sikutegemea miaka mitano ingeyoyoma kabla ya nyumba za kaya zilizoibwa na Tunituni na mbweha wenzake hazijarejeshwa.

Ajabu, pale Tanisico tunasikia wezi wakikarabati majumba kwa mabilioni na kujiuzia kwa malaki! Uwiii! Najisikia kunywa damu ya fisadi na kushushia na nyama yake.

Sikutegemea kama hata lile jambazi la CPB eti lingeonywa badala ya kukatwa shingo na mali lilizojilimbikizia kurejeshwa kwa walevi. Kwanini tusilivue nguo hadharani na kulifanyia ufilauni ili liwe somo kwa wengine?

Hakika sikutegemea kama Mwana wa nyika naye angeendelea kupeta ilhali yu kibaka wa kutupwa. Jamani hamkusikia ya bwana microfoni Sam Six na kujaza vinyakuzi kwenye ofisi za pale Idodomya?

Kuna ajabu la maajabu. Yaani omba omba wanazawadiana bilioni 50 kama njugu na walevi wasisituke na kufanya kweli lau kwa siku moja! Je huu mchezo ni kutafuta pesa ya kuchangiana kwenye uchafuzi wa uchaguzi baada ya EPA na Richamondu mpya kustukiwa au namna gain?

Yaani hadi hapa walevi hawajaambua hadi mzee nipasue koo!

Jana nilijisikia vibaya nusu kujinyotoa roho. Si ndege walinicheka na kunizomea nilipopita jirani ya mti walipokuwa wametua wakitanua na kuvuta sigara na bangi zao.

Niliwasikia kwa masikio yangu wakitujadili na kudai tumo kwenye fungate na pepo ya mabwege ambapo mabwege wakubwa wanawageuza mabwege wadogo na mabwege wadogo wanakubali ubwege wa mabwege wakubwa.

Katika ndege wote, hakuna aliyenikera kama Kunguru au Indian crow ambaye alilinganisha kaya yetu na kundi la maizi yakipiga kelele huku mafisi yakiufaidi mzoga.

Hakuna kilichiniudhi hadi nizidi kutamani kula nyama ya nyang’au hawa fisidi. Nilitamani niwadonye na kutoa macho lau wasione hizi bilioni hamsini.

Ajabu hadi niandikapo majambazi watukufu wanazidi kuombana ulinzi huku vibaka wakiendelea kuteketezwa na walevi hawa hawa woga wa kuwapa dispilini majambawazi-heshimiwa. Hivi tumeingiliwa na nini? Mbona hapo nyuma hatukuwa hivi?

Nirejee kisa cha kuzomewa na kunguru. Walinizomea sana huku mafisi yakicheka na kuzidi kunitishia niache kuingilia mzoga wao. Mafisi yaliniamba nikapimwe akili nisiyeona neema iliyonizunguka badala yake nikashikilia kulaani. Yaliongeza kuwa wa kupimwa akili si mimi peke bali ukoo mzima wa walevi!

Mafisi walishangaa kuona nagombea ubinadamu ugeuzwe sera badala ya ufisi huku siku zikizidi kuyoyoma. Je hizi sera za ufisi zitatumika wakati wa kutupa vijiti? Kama zitaendelea kutumika, je walevi watafanya ufyongo waendelee kuridhia ufisi badala ya utu na maendeleo? Mie simo kusema ukweli.

Baada ya kuvuka kunako ule mti wa kunguru nilianza kutafakari. Ya kweli. Kweli eti! Hawa gendaeka wanatuona mazezeta wa mazumbukuku kiasi cha kututembezea ufisi na ufisadi tena hadharani kwa namna ya dharau na wazi wazi.

Kama si hivyo wangechelea lau kiama siku si nyingi. Lakini ajabu hawachelei chochote zaidi ya kuzidi kukwapua! Wangehofu wangesema siku ile inakuja ambapo kila fisadi atapewa adhabu yake. Wangechelea wangeandaa mapito badala ya kufanya madudu. Wasagaliwa hawa wanazidi kuiba mchana tena bila aibu!

Kila siku litajwapo jina la jamaa mwenye Njaa kwenye Kaya na Beni Njaa natamani nikutane nao kwenye sehemu za kiza totoro nikiwa na zana zangu za kazi kama vile panga, nyundo hata bunduki nitoe taarifa kwa kufanya kweli.

Natamani nikutane na gendaeka hawa wakiwa wawili bila walinzi tena wamelewa ili nitoe fundisho kwa dunia.

Nikiwapata umma utajua nilivyo na damu ya morani na laigwanani haki ya nani. Natamani nitenganishe viwili wili vya watu hawa mchana kweupe na mizoga yao niwape fisi na mbwa wale bila hata ya chembe ya huruma.

Nina usongo wa damu na nyama vya watu.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 19, 2009.

No comments: