Tuesday, 25 August 2009

Ukapa + Ukwete = Ufisi na Ufisidunia


HAYAWI hayawi; yamekuwa! Tulisema na kulonga bila kukoma kuwa kuna siku nyoka atajivua ngozi. Hata ajivue ngozi mara elfu bado nyoka ni nyoka na dawa yake ni kumpondaponda bichwa lake na kumteketeza.

Siku nyingi walevi walikuwa wakiniuliza sera ya lisirikali letu ni ipi. Niliwahi kujibu; ubangaizaji, usanii, ujambazi mbuzi, ufisi na ufisadi. Wazushi waliita mzushi huku wasanii wakiniita msaliti wasijue wao ndiyo.

Hakika Mungu si Mpayukaji. Wale wale waliokuwa wakikana hata kwa kutishia kulamba pua zao hata kutishia kuonyesha makaburi ya Adam na Eva, sasa Wamejiumbua kwa kubariki na kutia ubani maneno yangu kuwa sera yetu kijiweni hakika ni ujambazi, ufisi na ufisadi.

Hakuna dhambi isiyostahili msamaha kama kuulaani ujambazi na ufisi huu. Ukitaka kujua nimaanishacho, muulize kipaza sauti Sam Six au Joni Machela. Juzi nasikia walilazimika kulamba viatu vya kaisari kwa kosa la kusema yu uchi. Nasikia walidhalilishwa kiasi cha kutamani ardhi ipasuke. Lakini adui yako muombee njaa.

Matumbo yaliwazuia kutema ulaji wa masimango na masharti utadhani kiama ndiyo mtoa riziki pekee. Huku nako ni kujidhalilisha na ubabaishaji hata usanii ukiachia mbali kuwa uchumia tumbo.

Nasikia majambazi kama Luwasha, Makorongo, Roast Tamu na wengine waliangusha bonge ya pate huku Joni Chilyagt akizidi kujivua nguo na kuonyesha alivyo mtupu kama Tambo Hizo (Mrundi ajiitaye Mgosi), kihiyo na changudoa wa kisiasa aliyeridhia kutumiwa.

Tambo Hizo, Chilyagt, Kimdunge Mwehu na Makorongo wamepayuka. Bado namsubiri shangingi wa kihaya. Naye lazima ataropoka kumfurahisha Bwana.

Kuna ngedere mmoja toka Idodomya aitwaye Kuzila. Huyu ndiye hana maana kabisa. Eti anasema kina Sam Six na Machela wafunguliwe mashtaka ya uhaini. Hivi ngedere huyu anaujua uhaini au anaota?

Zamani nabii Mpayukaji nilihubiri na kutabiri kuwa muandae maziko ya Genge la Gwagu na Majambazi (GGM). Nilionekana naota mchana. Juzi shehe Njaa Ubwabwa, Haya naye alitia guu kwenye unabii wangu ingawa alitumwa na njaa baada ya kuona ngedere wenzake wamemzunguka.

Turejee kwenye gwena la juzi. Ingawa GGM sasa inaanza kuonja joto ya jiwe kiasi cha kuanza kulamba matapishi yake-kukanusha, ukweli ni kwamba ni genge la mafisadi. Hebu jiulize; kwa nini wanamchukia Sam Six wa kijiwe cha Idodomya? Ni simpo. Aliruhusu Eddie Ewassa kusulubiwa kwa niaba ya Njaa Kaya.

Hawa wawili kama alivyotahadharisha nabii Mchonga ni hatari kwa usalama wa kaya. Wana tamaa kama fisi kiasi cha kulala kitanda kimoja na mafisadi wakila kwa miguu na mikono bila kunawa. Ushahidi? Tazama wanavyokufuru kusema eti tumuenzi Denjaman Makapu bin Tunituni kwa kutuibia!

Kama kuna wa kumuenzi si mwingine bali Anna Tamaa, Njaa Kaya, Joe Makombo, Dani son of Jonah, wachukuaji waitwao wawekezaji kina Richmonduli na ndegere wenzake walioiba mahindi ya watoto huku wakiwaacha wafe njaa.

Kama tutamuenzi Tunituni na Mchonga tutamfanya nini? Acheni matusi ya rejereja. Jamaa mmoja alinitonya kuwa Sam Six anachukiwa kutokana na kuanza kuandaa mazishi ya Njaa Kaya na Salama Kikwekwe wa MAWA watakapokuwa wamekitoa.

Maana kama Regina Chiluwa anapaswa kunyea debe Keko au Ukonga huku Anna Tamaa akihukumiwa kunyongwa maana ndiye aliwaletea kina Salama pepo la kupenda pesa utadhani wanatokea karibu na mlima Nonihino. Pesa babangu. Pesa lasima ujenge nyumba ati. Kimaro umekataa kuiba utakula mafi yako. Niliwahi kumsikia jamaa mmoja akitania jamaa hawa.

Kimsingi, kilichofanyika ni GGM kuwaonyesha Wabongo inavyowachukulia kama mataahira ambao hata ikiamrisha wale viungo vyao wanaweza kama wawafanyiavyo mazeruzeru huku wakidai amani na ustawi. Huu ni uchokozi usio na kifani kama walevi wetu watatia akilini.

Njaa Kaya na genge lake wamedhihirisha walivyo wa kuogopwa kuliko hata ukoma au ukimwi. Kimsingi, vikao vilivyokwisha vimezika matumaini na Tanzia. Kilichobaki ni tulie na kusaga meno ndugu zanguni.

Kwa ufupi kilichofanywa na vikao vya GGM licha ya kumvua nguo Mchonga, ni msiba kwa kaya. Tunyoe nywele, kujipaka majivu na kuvaa magunia. Tuomboleze kifo cha mkabala wetu na kaya yetu.

Ajabu genge hili bado linawadanganya walevi kuwa linaheshimu uhuru wao. Thubutu. Utamheshimuje mtu wakati unamfunga mdomo hata asikwambie ukweli baada ya kugwaya kukuzaba vibao? Hawa ni wa kuchomwa moto kama vibaka, kama walevi wasingekuwa woga. Lakini yana mwisho na mwisho wenyewe unakaribia. Maana wahenga walisema: ujanja ujanja mwishowe huzua janga.

Kwa wenye akili baada ya kuondoka, Mchonga tulijua msiba mkubwa unaandaliwa. Hakuna siku tulianza kuvaa magunia kama siku alipopitishwa Njaa Kaya eti kugombea ukuu. Tulijua. Ewassa atamtumia kabla ya wengine kumtumia. Maana jamaa ni mtupu hakuna mfano.

Laiti angekuwa kinara wa miziki na mipira si haba. Ajabu na msiba mkubwa, baada ya wendawazimu kama Kimdunge Ngumbaru Mwehu kuwa wazee wa gwena tulijua mambo kwisha. Ukitaka kujua nimaanishacho, jiulize Kimdunge na nkewe wamefanya nini pale mabung’o.

Babu linafanya mambo ya kitoto kuogopa lisiumbuliwe kwa ufisadi wake. Mwl. Mchonga alisema: ogopeni wehu wanaotumiwa na wake zao na wakatumia ushauri wa kitandani kufanya mambo ya umma. Yuko wapi Tunituni? Ameponzwa na Delila sawa na Njaa Kaya atakavyoumbuliwa naye siku si nyingi.

Hivi ulitegemea nini kama wachenza mdumange kama Joe Makambo kuwa kinara wa gwena? Hivi unategemea nini kutoka kwa vihiyo kama Mkukuchikaji? Unategemea nini kutoka kwa walu walu kama Joe Masahauni au kibaka kama Makorongo?

Kama kuna jinsi ya kulinganisha gwena la juzi, basi kwa kukopa maneno ya rafiki yangu wa kichina aitwaye Xian Cham, kilikuwa ni cha manyani na ngedere.

Kwa ufupi huu ndiyo ukapa kujumlisha ukwete uliozaa ufisi uliojukuu ufisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 26,2009.

No comments: