The Chant of Savant

Thursday 15 October 2009

Kikwete ameshindwa, ameangusha umma


NIMEVUTIWA na mjadala unaoendelea juu ya utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete. Niseme kuwa Tanzania haijawahi kupata rais mwenye kutatanisha na aliyekatisha tamaa kama huyu wa sasa.

Kazi na wajibu wa serikali yoyote duniani ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Serikali isiyoweza kusimamia hayo basi haiwezi kuitwa serikali, bali kitakuwa kikundi cha watu kinachojipachika jina la serikali.

Kikundi hicho kinaweza kikawa na sura ya serikali kwa maana ya kuwa sehemu ya mihimili mitatu ya dola. Lakini bila kutimiza wajibu wa kuhakikisha usalama wa mali na raia wa nchi inayoongozwa, hakifai kujiona au kuitwa serikali.

Ukiangalia tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani, haraka utagundua kwamba haijatimiza matarajio ya wananchi. Na ukiangalia wakati unavyoyoyoma kuelekea uchaguzi mwingine, haraka utajua kuwa kile ambacho watoto wa mjini hupenda kuita “changa la macho” kimetimia.

Rais Kikwete na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliahidi Watanzania mambo mengi. Kikubwa waliahidi maisha bora kwa kila mwananchi.

Kabla na baada ya kuingia madarakani, Kikwete aliahidi kwamba serikali yake itapitia upya mikataba ya madini, itaboresha hali za wafanyakazi na itatokomeza rushwa katika serikali na ndani ya chama chake. Yote hayo sasa yamebaki kuwa tamthilia.

Hadi sasa akiwa anatimiza miaka minne madarakani, Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi hata moja wala hakuna dalili kwamba atatekeleza hata nusu ya ahadi zake.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wengi wameanza kukata tamaa. Wanamuona rais wao kuwa ni mtu anayetoa ahadi, lakini anayeshindwa kuzitekeleza.

Wengi wanamuona Kikwete aliyeitwa “chaguo la Mungu” siyo huyu wa leo. Huyu wa sasa ni dhaifu asiye na ubavu wa kuchukua hatua.

Kikwete huyu anabeba makundi mawili: Kulia ana wananchi, kushoto amebeba kundi dogo la mafisadi. Matokeo yake ahadi zote alizoeleza wakati anaingia madarakani zimepoteza matumaini kwa wananchi.

Hakika, chanzo cha kuanguka kwa uongozi wa Kikwete kinajulikana. Uongozi na ushindi wake vilipatikana kwa hila, kuchafuana na rushwa ndani na nje ya chama chake.

Amejitahidi kukaa kimya kila zinaporushwa tuhuma kwamba chama chake kilichota mabilioni ya shilingi za umma ili kumuwezesha yeye kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Ameshindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na ushindi wake kuhusishwa na hongo iliyokusanywa kwa njia ya kuuibia umma.

Kashfa mbili kubwa kati ya nyingi zilizogeuka jinamizi la utawala wake ni ile ya EPA, Deep Green Financial kwa upande mmoja na Meremeta na Tangold kwa upande wa pili.

Ni Kikwete aliyetuhumiwa na wenzake katika chama kwamba alitumia vyombo vya habari kubomoa wenzake huku vikimjenga yeye. Mbinu hizo sasa zimeanza kupwaya, ingawa amejitahidi kupenyeza watu wake kwenye baadhi ya vyombo hivyo ili kusaidia kumjenga.

Chanzo kingine cha kushindwa na maanguko ya Kikwete ni aina ya watu aliojizungushia. Licha ya kurithi makapi ya watu fisadi wa utawala uliopita, Kikwete aliongeza watu wake chini ya dhana ya mtandao.

Hawa ni wawezeshaji imara kwenye wizi wa kura au wa fedha. Na hii ndiyo imekuwa sababu kuu ya Kikwete kushindwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani waliowezesha wizi wa mabilioni ya shilingi za umma.

Minong’ono imeanza kuzagaa kwamba Kikwete anahofu ya kushughulikia wenzake hawa kwa vile watamwanika.

Kukwepa hili Kikwete anaonekana kufurahia ufunguzi wa kesi zisizo na mashiko. Wengi wanaona kesi hizi kama “danganya toto” na njia ya kupoteza muda.

Serikali ya Kikwete, licha ya kutotimiza ahadi, imebainika kuwa na matumizi mabaya na makubwa ya fedha za umma. Rejea ugunduzi wa upotevu wa Sh. 1 trilioni uliogundulika kuwa umefanyika katika wizara kadhaa katika serikali yake.

Kinacholipa nguvu hili ni ile hali ya Kikwete, serikali yake na chama chake kushindwa kutoa angalau maelezo zaidi ya vitisho na visingizio.

Kitu kingine kinachoonyesha kushindwa vibaya kwa Kikwete ni ile hali ya kutokuwa na falsafa wala sera za kutawalia. Ukimuuliza Kikwete, hata baadhi ya Watanzania wengine, nchi yao inatawaliwa kwa sera zipi, utaambulia upigaji domo tu.

Kikwete aliwapa ahadi Watanzania kuwa angewaletea “maisha bora” kwa kile alichoita safari ya Kanani ambayo imegeuka kuwa safari ya kuishia Misri au jehanamu.

Leo maisha ni magumu kuliko hata yalivyokuwa wakati akiingia madarakani ukilinganisha na hali ya mambo ya Misri.

Wakati haya yakiendelea, Kikwete anajikuta akikabiliana na matishio makubwa manne.

Kwanza, kushindwa kutimiza ahadi zake. Pili, kutoonyesha ushawishi kwa kubadili maisha kiasi cha kuhofia kupoteza kwenye uchaguzi ulioko mlangoni sasa.

Tatu, kukata tamaa kwa wananchi na migawanyiko kwenye chama tawala. Rejea migomo na migongano ya mara kwa mara baina ya serikali na wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wanaodai malimbikizo na kuongezwa maslahi mengine.

Nne, kuanza kuandamwa na waliokuwa maswahiba zake kwenye mtandao alioshindwa kuwalinda au kutimiza matarajio yao.

Hali hizi zimefanya baadhi ya Watanzania kukosa imani na serikali ya Kikwete na hata Kikwete mwenyewe. Vitu hivi vinamchanganya Kikwete ambaye watani zake kisiasa wamempa jina la “Msanii” huku kila asemacho wakikiita ngonjera. Na kweli ni hivyo.

Kwa mfano alimwaga pesa isiyo na maelezo ya jinsi ilivyopatikana, maarufu kama mabilioni ya Kikwete. Haikufua dafu. Hadi leo ukiuliza imeleta mabadiliko gani, hakuna jibu la maana utakalopewa.

Kipindi kuelekea kwenye uchaguzi baadhi ya wachumia tumbo walitunga vitabu kumuonyesha Kikwete kama tumaini lililokuwa limerejea. Waulize sasa wanasemaje? Ni aibu tupu! Wengi wao hawataki hata kumuongelea.

Sina hakika kama mwandishi wa kitabu hicho leo anaweza kutoka hadharani na kujitangaza kuwa yeye ndiyo mtunzi wa kitabu hicho. Kwani licha ya kutokuwa na maana ni uongo na kujikomba vikilenga kumhadaa Kikwete na wananchi.

Jingine kubwa linalotia doa utawala wa Kikwete ni kushindwa kuchukulia hatua mtuhumiwa mkuu wa ukwapuaji wa EPA ndani ya BoT – kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Huyu Bwana Kagoda ndiye kinara wa ukwapuaji. Anajulikana kwa wengi. Kuna wanaodai kuwa ni mmoja wa maswahiba wa rais. Mwenyewe anatamba ameweka serikali mfukoni.

Katika mazingira hayo, wananchi hawana tena matumaini na serikali. Hawana tena imani na Kikwete. Ni jukumu la Kikwete kuamua, ama kufanya kazi na kurudisha matumaini hayo au kuendelea kukatisha tamaa wananchi.
Chanzo: Gazeti la Mwanahalisi Oktoba 15, 2009.

2 comments:

Anonymous said...

Nkwazi huwa napenda makala zako. Huzungushi wala kuogopa. Kikwete ni let down ya aina yake. He is a failure by all standards. Nimesoma makala zako nyingi. Wewe ni king'ang'anizi wa hoja. A good thing.
This is among the best of your pieces I have ever read. Big up boy.

Sirili Akko said...

akipewa tena ataangusha na kijiko!