How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 21 April 2010

Kijiwe chajipanga kugoma, kuandamana

BAADA ya lisirikali la kifisidunia kuchezea masilahi ya wanuka jasho wafa na ngwamba, kijiwe kimeandaa mkakati wa kweli kugoma ili kuona nani ni nani katika kaya hii.

Baada ya walevi kugundua kuwa kumbe wenye maulaji wanaishi kutegemea jasho lao, wanataka sasa dunia ijue nani bonzo na nyundo.

Kutokana na walevi kukaa kimya huku mafisidunia wenye mamlaka wakijihomoloea wakidhani walevi ni majuha wasioweza kujua kuwa kupe anamhitaji ng’ombe kuliko ng’ombe asiyemhitaji kwa lolote.

Tukiwa na nyuso zilizojaa ndita, tunakutana haraka chini ya mwenyekiti Mgosi Machungi na kutoa tamko rasmi la kupinga wizi ndani ya wizi unaofanywa na wadharauliwa tunaowaita waheshimiwa. Kwanini wajipandishie mishahara wakati wanatukopa miaka nenda rudi?

Huku tukiapa kwa kila miungu kwa usongo, tunaazimia kuwa lazima lisirikali na mafisadi wake watupe chetu. Kipindi hiki hatutalamba mtu miguu. Badala yake tutalambwa sisi.

Hamjaona Chekacheka anavyoanza kutulamba miguu japo tuna shaka kutokana na kuwa bingwa wa sanaa. Ila ajue. Asije na longo longo za amani. Nani atakuwa na amani wakati mfukoni kuna moto?

Kwa vile watawala wetu hawana masikio, tunaamua kugoma na hatimaye kuandamana ili umma wa walevi ujue kuna vijogoo kwenye kaya hii ya mazumbukuku waibiwao mchana wakiaminishwa wanapelekwa Kanani.

Kwanini pesa ya kutulipa hakuna lakini ya kutanulia na kulipia ujambazi wa Tunituni Kiwila inapatakiana? Kwanini pesa yetu isipatikane yapatikane mabilioni ya uchafuzi? Mnadhani hatuna akili? Kusururu wote.

Mkiti Machungi anaanza. “Wagosi, najua. Tina taaifa. Chekacheka ana mpango wa kutifunga kamba ili tisigome. Huu ni usanii kwa kia hai tikubaliane.”

Mara mzee Kidevu anatukana: “Hana sera wala sura kusum kibaki mkubwa.”

Mpemba hangoji. Anakatua mic. “Yakhe kumbe twakosea kudhani biashara ya mihadarati ndo yalipa haraka. Hebu fikirieni. Yaani Chekacheka watumia siasa kutudhulumu. Hivi hii kaya yapelekwaapi jamani? Kwanini pesa ya Kagoda na Richmond ipatikane haki zetu zisipatikane?”

Mipawa hajivungi. Anachomekea. “Ami unashangaa nini iwapo uchafuzi umekaribia na EPA na Richmonduli mpya zinatengenezwa? Taarifa nilizo nazo toka jikoni ni kwamba wanuka jasho tutalainishwa na kitita kitakwenda kwenye uchaguzi mwakani amini ndugu zangu.

Juzi nilisikia mpambavu mmoja akisema eti tukigoma tutahatarisha masilahi ya taifa! Nani anahatarisha masilahi kati yetu tunaochapa kazi na wanaowalinda mafisadi?” Anatukazia macho kuona tunavyopokea ufunuo huu.

Tukiwa tunatafakari bomu la Mipawa, Mbwa Mwitu anakwanyua mic. “Tukubaliane. Kaya yetu sasa inaongozwa na mafisi. Heri ingeongozwa na Mbwa Mwitu kama mimi angalau wangekula na kubakiza kuliko fisi wasiobakiza kitu.”

Kabla ya kuendelea, Mchunguliaji anakwapua mic. “Je, mmepata skandali ya ujambazi kuwa mtandao wa EPA umevamia mabenki na kuiba zaidi ya trilioni moja kwa ajili ya uchafuzi? Jamaa wanaiba kana kwamba kaya haina watu wenye macho wala akili za kawaida au pipo wiz just common sense.”

Hatuna mbavu kwa jinsi Mchunguliaji alivyobukanya kiswanglish kuonyesha amepiga vitabu kama jamaa zetu wa Idodomya wafanyavyo kuficha jinsi walivyoghushi shahada zao. Mchovu ukighushi wanakufunga maisha wakati wao wanapeana ulaji maisha! Rafiki yangu Chitahira anajua nimaanishacho.

Tukiwa tumezama kwenye kicheko, Mgosi Machungi ambaye hacheki hata kidogo anakuja na mpya. Anadabua mic. “Tikubaliane jamani. Kupiga piga keee haitisaidii kitu; muhimu tihakikishe tinagoma na baadaye tiandamane hadi huko ikuu angau titupe jiwe moja kumtaifu kuwa tinajiandaa kumtia adabu.”

Kapende anandandia. “Mtalii haishi huko siku hizi. Yuko kwenye matanuzi na shotii wake kila uchao. Mkitaka kumpata mngojeeni uwanja wa ndege.”

Mzee Maneno hajivungi kuonyesha usongo wake. “Mie nitaongoza maadamano yetu. Maana nina hasira na pimbi hawa sina mfano.”

Anakatua kashata yake na kunywa kahawa kidogo ili kupandisha mdadi na kuendelea. “Nikikumbuka ngurumbili hawa walivyo vichwa maji na waongo natamani nile nyama yao. Ukisema hawana akili wakajitia kujua.

Mnakumbuka walivyokuwa akisema eti uwekezaji ndiyo njia pekee ya kutukomboa tusijue kumbe walimaanisha uchukuaji kama RITEZ uliosababisha wasitulipe haki zetu. Hapa lazima tufe na watu, yaani hawa wanaohomola na kutanulia wakati sisi tunatanuliwa na dhiki.”

Kabla hajaendelea huku akitweta, Mbwa Mwitu anachomekea. “Mnatanuliwa wapi na dhiki? Tufafanulie.”

Mzee Maneno anakatua mic tena. “Nyie hamjui! Tunatanuliwa pande zote iwe nje au ndani.”

“Du! Chunga lugha mzee mwenzangu. Mambo ya kutanuliwa yametoka wapi tena?”

Mgosi Machungi anaingilia. “Jamani nasi wabongolala timezidi. Kia neno tinaligeuza maana na kufanya utani. Hapa tinaongeea masilahi ya taifa. Hapa hakuna mambo ya kutaniana. Hawa wadudu wananajisi kaya yetu. Hivyo tiazimie kwenda kuwatia adabu sasa hivi.

Tipange mikakati ya kugoma na kuandamana si kubadii maneno jamani.”

Tom aliyekuwa akisikiliza muda wote kwa makini anaamua kutia guu. “Mgosi usemayo ni ya kweli. Mnashangaa wanuka jasho kukosa mishahara wakati kuna pesa ya uchafuzi!”

"Loo!" Mpemba anadakia. “Yakhe waona sote twatanuliwa tena kwa njia mbaya! Sie Pemba hatutanui mtu au Popobawa kama nyie Bara. Sana sana huyu anayetanua ndiye atatanuliwa siku moja.”

Baada ya Mgosi kuona tunaleta gozi gozi anaamua kutuchochea tena. “Wagosi, siungi mkono msimamo wa kunung’unika. Nataka tiandamane sasa hivi kueekea huko ikuu kutoa taiifa kuwa timechoka na ujambazi wa mchana unaofanywa na watawaa wetu ambao wamegeuka watu waa watu. Tianze kuandamana sasa hivi.”

Bila ajizi tunakubaliana na Mgosi na kuanza kutimkia nonihino tukiimba wimbo wetu mpya uliotungwa na Mfiliseni usemao:

“Mkuu wa kaya na wenzako mpo? X2
Mashujaa tumekuja, tumekuja.

Tumekuja mashujaa tumekuja.

Tumekuja kukujulisha, tumekuja,
Kuwa tunajua janja yako, tunajua.

Usichezee haki zetu, haki zetu.

Pambana na mafisadi, mafisadi
Hata kama wewe ni fisadi, fisadi.

Mara tunaingia mitaa ya Uhuru na kuelekea Posta tayari kulianzisha pale Upanga na Ikuu.

Tukiwa hatuna hili wala lile, mara vihere here wenye magwanda si walijitokeza maeneo ya ubalozi wa Ujep.

Hatukujivunga. Tuliendelea na sheshe hadi tulipofanikiwa kuwanyuka na kufikisha ujumbe kwa mkuu ambaye alikuwa kagwaya kama kuku mbele ya kicheche.
Chanzo: Tanzania Daima April 21, 2010.

No comments: