WAZIRI wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa, amelitangazia taifa kuwa serikali itachukua asilimia 51 ya hisa za kampuni ya Reli ya India (RITES) zilizokuwa zinaunda kampuni ya Reli ya TRL.
Alisema, “Lazima tufahamu kuwa TRL si ya RITES peke yake. Tunamiliki asilimia 49 ya hisa za kampuni hiyo. Kwa hiyo matatizo yanayotokea na sisi tunahusika. Ndiyo maana tunatoa fedha kuweka mambo sawa.”
Tunakubaliana na hoja za Kawambwa. Mwekezaji aliyekabidhiwa jukumu la kuendesha TRL amethibitika kushindwa kazi.
Serikali iliingia mkataba na kampuni isiyokuwa makini, isiyokuwa na uwezo, hadhi wala sifa ya kuendesha shirika muhimu kwa uchumi wa taifa.
Ikiwa serikali imekiri kuleta kampuni ya aina hiyo kuendesha Shirika la Reli la Taifa (TRC), basi inakiri kufanya maamuzi mabovu. Maana yake ni kwamba serikali iliyopo sasa imepoteza sifa ya uadilifu na umakini.
Watawala wamebeba mwekezaji badala ya kumfukuza; na sasa wana mkakati wa kujadiliana naye jinsi ya kununua hisa zake.
Hii ni hujuma. Katika kupamba hili, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo amekaririwa akisema, “Serikali itafanya matayarisho ya msingi; kurekebisha kasoro na kuangalia mustakabali wa TRL kabla ya kutafutiwa mbia mwingine wa kuiendesha.”
Kurekebisha kasoro ni muhimu. Lakini muhimu zaidi ni kujiuliza: Unarekebisha kasoro zipi na katika eneo gani? Hili ndilo swali ambalo mkutano wa baraza la mawaziri ulipaswa kuhoji waziri Kawambwa na katibu Luhanjo.
Kimsingi, bila kuondoa ulafi wa kimfumo, hata wawekezaji wangetoka mbinguni hatutafanikiwa kuwaendeleza watu wetu kwa kutumia raslimali zilizopo.
Kwenye uwekezaji mwingi uliofanyika na ambao umeonyesha wazi kuwa kuna harufu ya ujambazi ndani yake, serikali imekuwa ikitoa mitaji kwa makampuni ya kigeni, tena chini ya shinikizo la sheria.
Kinachokera ni ukweli kuwa mikataba hii iliingiwa baina ya serikali na wawekezaji kwa kuwakilishwa na watu waliodhaniwa kuwa wenye uelewa na ufahamu wa kulinda maslahi ya nchi yao. Kumbe sivyo ilivyo.
Lakini kibaya zaidi, hata pale ilipothibitika kwamba tumeingizwa mkenge, serikali haijawahi hata mara moja kuwajibisha wahusika. Imeendelea kuwakumbatia kana kwamba nchi hii ina uhaba wa wafanyakazi.
Kigine ambacho kinasikitisha ni kuwa hii si mara ya kwanza kwa serikali kutangaza kuwa imenunua au inajirejeshea hisa katika kampuni ilimokuwa na ubia.
Haya yalitokea katika Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) lililokuwa limekodishwa kwa kampuni ya ndege ya Afrika Kusini, tena kwa bei ya kutupa.
Tulisikia serikali ikibeba zigo la mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira uliokuwa unadaiwa kumilikiwa na baadhi ya wanafamilia na marafiki wa rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Pamoja na lundo la wataalamu iliyonao, serikali haikujua kuwa RITES haikuwa na uwezo wala mtaji wa kuendesha shirika ililolikabidhi?
Mbona wafanyakazi wa shirika hili walionya, hata kabla ya shirika lenyewe kubinafsishwa, kwamba mwekezaji aliyetafutwa hakuwa na sifa?
Je, si kweli kwamba wafanyakazi ambao kimsingi ndio walikuwa waendeshaji wakuu wa TRC, walitoa hata mbinu za kuliokoa shirika, lakini wakapuuzwa kwa madai kuwa mbinu zao zinaingiliana maslahi ya wakubwa?
Ni wafanyakazi hawa wa kizalendo waliofufua baadhi ya injini zilizotelekezwa na mwekezaji, jambo ambalo limeokoa mamilioni ya shilingi.
Lakini wakubwa serikalini hawakuona umuhimu wa uamuzi huo kwa kuwa kwao kuna faida kupeleka injini India kuliko kazi hiyo kufanywa na wazalendo kwa malipo kiduchu.
Ya RITES ndiyo yaleyale ya Net Group Solution iliyotelekeza Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO). Ni yaleyale ya ATCL.
Ni wazi sasa kuwa serikali imeruhusu uhuru kwa kila mtu kujichomolea atakavyo kana kwamba taifa hili linaelekea kifo.
Chanzo: MwanaHALISI Machi 31, 2010.
No comments:
Post a Comment