The Chant of Savant

Thursday 29 April 2010

HEPA mpya ya uchaguzi wa mahepe

Makala hii imemchukiza rais kiasi cha kuamuru gazeti liitwe kutoa maelezo. Hii ni kweli.


Hebu piga picha. Mpayukaji anachaguliwa kuwa rais wa nchi yako. Jiulize. Itakuwaje kumuona mzee mzima akila kiapo na kuanza kuitwa mheshimiwa rais. Je utamtungia kitabu cha sifa na kuuambia umma kuwa sasa tumaini limerejea au nabii yule hatimaye kafika? Piga picha bi mkubwa amejitona migold akiwa amenizunguka na vitegemezi vyetu wakipiga mahesabu jinsi ya kuanza kupunyua kodi yako na kutanua. Hayo tuyaache.

Help for Election Parsimonious Associates (Msaada kwa washirika wezi wa kura) au HEPA, ni mpango nilioubuni kuweza kushinda ukuu wa kijiwe kwenye uchaguzi ujao. Nimeamua kuchangisha pesa toka kwa washirika zangu baada ya wanakijiwe kunistukia nilipotaka kukwanyua pesa ya kahawa. Tunatarajia kuchangishana shilingi 50,000 ambazo ni sawa na bilioni 50 kama ingekuwa nchi.

Kwanza, ili kupata pesa rahisi ya kupunyua, nilikihadaa kijiwe kitoe pesa ya kusisimua uchumi wa kijiwe yaani stimulus tuliyowapa washirika wetu na nyingine kuificha kwa ajili ya uchaguzi.

Pili, nilitunga sheria ya kuwazuia wenzangu halafu nikaivunja kutokana na kuisani bila kuisoma. Unajua? Huwa sina muda wa kusoma. Nitaupata wapi wakati kuna matanuzi na makamuzi mengi yakiningoja? Soma taratibu na usimwambie mtu. Huwa muda wangu mwingi nafikiria jinsi ya kuwatoroka wanakijiwe na kujivinjari na totoz. Usimwambie mtu bi mkubwa shortie asije kustuka na kuninyotoa roho. Hayo tuyaache kama ya Babu Seya na kesi yake ya kutatanisha.

Baada ya kuona walevi wamestukia kamba na sanaa zangu kuwa sikuwatendea chochote hasa kutimiza ahadi zangu, niliamua kuanza kupiga kampeni mapemaaa. Hamkusikia mgosi Machungi wa Makambale alivyokuwa akinipiga ndogo ndogo ingawa mlisema anajikomba nisimtimue ukuu? Hata kama hana kisomo, anajua kupayuka hasa kuwapanga walevi.

Hata kama hana kisomo, mwanae Februari anacho na ananisaidia sana ofisini kwangu. Kwanza ni rafiki yake mwanangu Riz ukiachia mbali kuwa mtoto wa kigogo mwenzangu.

Kuhakikisha sikosi ushindi wa mtikisiko kama mibomu ya Mbagala, bi mkubwa hakosi sehemu sehemu kuwahonga akina mama wanipe. Riz mwenyewe anawafunga kamba vijana ili nao wanipe. Bado wale waramba viatu wanaojipendekeza ili nikishaukwaa niwape vyeo kama nilivyomfanya Silvia Rweyependekeza almaaruf shangingi wa kihaya. Wote wakinipa bila shaka nitashinda. Hapa bado polisi wangu akina Mchunguliaji hawajayapigia chenchi kota masanduku ya kula.

Sasa turejee kwenye dili na HEPA. Mshirika si siri. Baada ya kuona walevi wamewakomalia washirika zangu akina Kanji almaaruf Roasttamu, nimeona nichangishe kwa njia ya simu kwa vile hakuna awezaye kujua namba za watu wote hakuna atakayenistukia.

Nilidhani walevi wangestuka tulipowatangazia kuwa kijiwe kinatumia pesa mara mbili ya kipato chake. Maskini hawakujua. Wangejua yote hii inasababishwa na gharama fichi za uchafuzi wasingenipa kula hata ya dawa! Acha wakome. Majuha ndiyo waliwao. Kama hawakujifunza nilivyowaingiza mjini kwenye uchafuzi uliopita niwafanyeje? Hata hivyo hakuna haja ya kuwalaumu. Wanasumbuliwa na ugonjwa uitwao UKIKI au Ufisadi wa Kimfumo na Kiakili unaosababishwa na UUMI yaani Ukosefu wa Uadilifu Mioyoni. Haya magonjwa kwa mstakabali wa kijiwe nitayaongelea siku nyingine na kuwataja waathirika wakubwa yaani wafanyabiashara na wanasiasa. Ukikumbwa na ugonjwa huu hatari utauza nchi watu wako hata wewe mwenyewe. Kwani unakuwa huna uwezo wa kujitambua bali kutumbua tu usijue baadaye utatumbuliwa. Wakati ukitumbuliwa washirika zako toka ughaibuni wanakutosa na kubakia kukucheka.

Mna habari kaya yetu imeendelea sana? Inayo sifa kubwa tu ambayo imeleta heshima kubwa. Nayo ni kuongoza katika kanda kuruhusu wanyabihasara wa kigeni kutorosha mabilioni ya dolari nje huku wanakaya wakisota kwa ukapa ile mbaya!

Juzi nilipata taarifa toka kwa washirika zangu wa Marekani nilipokuwa kule wakinitonya: nisijivunge kugombea hata ukuu wa kaya. Mshiko wa dezo upo. Walihoji: inakuwaje vibaka wengine wapunyue na kuukwaa ukuu wakati hawana akili, sera wala uzalendo ilhali mimi nimejaa uzalendo busara elimu na sera? Wamenichochea kuanza kufikiria kuachana siasa za kijiwe na kujikita kwenye za kaya. Sipati picha bi mkubwa wangu atajinoma vipi siku nikiwa presida wa kaya ya Tanzia!

Tuache utani. Nikiwa rahisi Riz wangu nitamteua kuwa waziri huku mama yake nikimteua kuwa makamu wa rais na waziri wa fedha ili aachane na mambo ya kuunda NGO za uongo na ukweli kufanya biashara ya kimachinga. Hata kama zinalipa biashara chafu kama hizi zinatia aibu ingawa wanaozifanya hawakujaliwa kuona aibu kutokana na kutokuwa na roho bali uroho.

Kama nitafanikiwa kuchota pesa kama zile za EPAA, nitahakikisha nabadili jina la chama changu cha UNM yaani Ugali Myama na Maharagwe. Nitakiita CCM yaani Chama Cha Maulaji. Sera yangu itakuwa Ukwasi mpya, Hali mpya na Uwezo mpya. Nikishawabamiza mkenge naikimbia sera na kuanza majisifu kuwa nimefanya hili na lile hata kama ni kamba tupu. Kwa vile walevi ni majuha hawatanistukia. Lakini nani atanistukia iwapo kila mlevi ni mwizi kwa nafasi yake? Na jueni. Hii ndiyo siri ya mafanikio ya maulaji wetu. Tunakula kwa sana na kuwadondoshea makombo. Walatini husema: Noli prohicere maccaritas ad porcos yaani usiwatupie nguruwe vito. Nami nawatupieni mabaki si kile nilacho hata kama chaweza kuwa mabaki ya wakubwa matajiri.

Msishangae. Kwani wagiriki husema alloi kamon, alloi onanto yaani wengine hutoa jasho na wengine hufaidi.

Rais wenu Mpayukaji atawaruhusu mjihomolee mtakavyo ili kaya iwe na amani. Kila raia ataruhusiwa kwenda benki na EPA yake huku kila mfanyabiashara mzalendo akisaidiwa kutengeneza Richmonduli yake. Mpo hapo? Bila shaka hapa mtanipa zote.Tuachane na hayo.

Juzi nilikuwa zangu kwenye matanuzi kwenye jiji la Nyuyoko. Nilishangaa maghorofa si kawaida. Nilitanua na kutanua na kutanua hadi nikajisikia kama nazimika. Kama siyo bi mkubwa kuingilia kati, huenda ningenyotoka roho. Maana nilipoona yale mabarabara makubwa na majumba kama miche ya sabuni kusema ukweli roho ilinisuta. Hivyo nimerudi nimepania kujenga ma-flyovers kwenye miji yote ya Tanzia. Na hii ndiyo sera yangu mpya kuelekea uchaguzi. Nitazunguka miji mikuu yote ya ulaya kujifunza ili nikija kujenga huku nisikosee wala kuruhusu majizi kujichotea njuluku. Akina Roastamu son of Kagoda na Ewassa son of Richmonduli mlie tu.

Naona yale yanatoa mimacho na kukodoa kuwa kiama chao kisiasa kimefika. Msiogope. Mie nagombea kwenye kijiwe si kwenye kaya. Sina shida hiyo ati. Nani agombee upuuzi wa kutawala mijitu isiyo na akili? Heri ya walevi wangu. Kuna siku ulevi utawaisha na wataamka na kunipa changamoto.

Msisahau. Kama kawa sikuwataja niliondamana nao kwenye makamuzi yangu yaliyoongezewa muda na mavumbi ya volcano toka Iselandi. Mngejua idadi ya nilioandamana nao na njuluku tulizotumiwa toka kwenye kodi yenu mngenyonga bure. Mungu anipe nini?

Ha! Naota niko New York natanua! Kumbe niko Bongo! Ngoja nijikate kabla ya ndata hawajanidaka.
Chanzo: Tanzania Daima April 28, 2010.

No comments: