The Chant of Savant

Tuesday 7 June 2011

RENATA BENEDICTO ANATAFUTWA



Yaweza kuwa binafsi lakini ni kwa kuwa nahitaji msaada.
Desemba mwaka 1999 nilikuwa miongoni mwa wasafiri waliokuwa kwenye hilo basi la Tawfiq ambalo kwa bahati mbaya lilipata ajali na kuua watu wengi alfajiri ya tarehe 23. Wengi tulijeruhiwa japo wengine tulihitaji huduma zaidi kulingana na majeraha yetu. Katika safari hiyo nilikuwa nimekaa na binti mdogo ambaye baadae alijitambulisha kwangu kama Renatha Benedicto. Alikuwa kidato cha pili shule ya sekondari Kibasila, Dar. Kuwa mdogo ama mwanafunzi, si sababu ya kumsaka leo. Namsaka kwa kuwa alikuwa shujaa katika siku hiyo na ninasikitika kuwa juhudi zangu nyingi za kusaka mawasiliano naye (zikiwa ni pamoja na kutumia redio) zimeshindwa kunirejeshea mawasiliano naye.
Katika ajali hiyo, nilijeruhiwa vibaya. Nilichubuka sehemu kubwa ya uso upande wa kulia. Nilipasuka juu ya jicho, ndani ya mdomo, sehemu mbili za kidevu, michubuko ya magoti. Pia nilikatika ulimi na kunifanya nishindwe kuongea kwa siku nilipokuwa hospitali. Pia ilinitibua mgongo ambao kwa miaka 9 iliyofuata nimekuwa nikipita kwa wataalamu mbalimbali kupata matibabu. RENATHA alikuwa zaidi ya mhudumu kwangu. Alitafuta dawa, kuhakikisha natibiwa, pia alihangaika kusaka mawasiliano ya kuwajulisha walio nyumbani kuwa tukingali hai (bahati mbaya mawasiliano hayakupatikana). Alihangaika wakati wote ambao nilikuwa siwezi kusema lolote kutokana kushonwa ulimi. Alitengeneza "chakula" kilichoweza "kushuka" kunipa nguvu na kuwa msemaji wangu akitumia taarifa nilizomuandikia kwenye karatasi na passport (kwa kuwa hatukuwa tukifahamiana kwa majina). KWA HAKIKA ALIKUWA MSAADA MKUBWA KWANGU.
Baada ya likizo tuliendelea kuwasiliana na mpaka alipomaliza shule mwaka 2001 na mara ya mwisho kuonana naye alikuja kuniaga (2002) akisema anakwenda Songea kusomea ualimu. Aliahidi kuwasiliana nami baada ya kufika huko na kwa bahati mbaya nami nikahama. Baada ya hapo nikaanza pilika za maisha zilizonifikisha huku nilipo, lakini kila nikifikiria "njia" ya maisha nauona mchango mkubwa alioweka maishani mwangu na najaribu kumtafuta bila mafanikio..
Nimeona leo niweke hapa ili kama kuna anayemtambua anisaidie kurejesha mawasiliano naye.
Ni Renatha Benedicto. Alisoma Kibasila Sekondari kati ya 1998- 2001 kisha akasema anakwenda Songea TTC.
Njia rahisi ya kuwasiliana nami ni barua pepe ambayo ni
changamoto@gmail.com

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Mungu ni mkubwa dada Renatha atapatikana tu...

Anonymous said...

he! ni marehemu kwa sasa ni dada yangu mpendwa jamani umenikumbusha machungu R.I.P dada