The Chant of Savant

Saturday 7 June 2014

Mwanunua rada au radada ya wizi wa rada?

Miaka kama 10 na ushee iliyopita kaya ilitikiswa na kufumuliwa ukweli kuwa kaya kapuku iliweza kununua mkangafu wa rada kwa dola milioni 40. 
Licha ya kushangaa, wenye akili tunaowabomu kila siku, walituona kama hamnazo kiasi cha kuamua kuturejeshea chenji yetu ambayo nayo sijui imeishia wapi?
Kuna haja ya kujipa muda kuchunguza isijeishia kuwa kama hii ya ‘escrow’ ambayo majizi yameiba na kujifanya hamnazo yalipobanwa.Nitakuja kuroga mtu wallahi kama majizi haya hayataacha kuiba njuluku zetu.
Tumeingia kwenye historia kama kaya kapuku iliyojiibia na kulanguliwa mkangafu tokana na mawazo mkangafu ya kutumia matumbo badala ya vichwa. Sitaki kusema wahusika wanatumia massaburi kufikiri japo ni hivyo.
Kama haitoshi, mkangafu wenyewe ulikufa hata kabla ya kuzaliwa bi maana kuwa si kwamba ulikuwa mkangafu bali mfu wa rada.Tushukuru.
Hata ujambazi huu uliowahusisha wazito hadi wa mwisho ulipofumuliwa walevi waliendelea na ulevi wao kana kwamba hakuna kilichokuwa kimetokea!
Siku wakistuka kutachimbika bila jembe na patakuwa hapatoshi. Ukisikia ulevi wa kunywa na kulewa hadi kuangusha bodi na kufanyiwa kitu mbaya mtaani ndiyo huu.
Amkeni. Mtaliwa mkijiona hadi lini? Mshikwe wapi ndipo mstuke wana hizaya nyie walevi.Nani aliyewaroga kudhani kuwa shetani anaweza kuwaingiza peponi wakati kwake ni motoni?
Juzi katika pita pita vijiweni, nilisoma habari kuwa kumbe siri kali ina siri nyingine kali ya kununua mkangafu mwingine baada ya ule mfu kuendelea kuoza na kunuka huku walioutumia kutuibia wakiendelea kutesa na kupiga njuluku kama kawa.
Je! mara hii tutanusurika kuibiwa tena? Je! waliotuingiza mkenge ambao, kimsingi, walipaswa kunyongwa hawako nyuma ya biashara hii tena?

Au ni yale yale tunayoshuhudia kwenye sanaa za UdA ambapo kila mtu anajifanya hamnazo kiasi cha mali ya walevi kuendelea kuteketea?
Nafurahi. Tokana na mishemishe zangu, nimeinyaka siri ya kugawiwa UdA. Mwaweza kuamini kuwa nyuma ya ujambazi wa UdA kuna mtoto mmoja wa kigogo mmoja mkubwa kayani ambaye anatajwa kuwa na umaarufu wa tamaa kuliko hata fisi?
Anayebisha ajiulize ni kwanini sirikali ilimsamehe yule kiherehere anayejifanya mmiliki UdA kodi ya mabilioni kwa kuingiza mikangafu 300.  Bila shaka rafiki yangu RizOne atakuwa anachekelea nyuma ya pazia. Tuyaache haya leo humu si mwake.
Pamoja na mibangi na gongo vyangu, nina hakika nina akili kuliko hawa mataahira wanaoruhusu mali na njuluku za walevi vichezewe.Haiingii akilini kila siku kila mwezi kila mwaka kaya inapata hasara halafu hawa wanaojifanya kuisimamia wawe na akili?
Leo tunaletewa habari za msiba wa kununua mkangafu kesho utasikia machungu mengine. Kaya hii ya Bongolalaland yenye bongo zilizolala haiishiwi vituko.Kila siku wanakuja majambazi wa nje wakishirikiana na wa ndani na kutuingiza mkenge huku nasi tukiangalia kana kwamba tu hamnazo au ni kwa sababu ya kanywaji kupita kiasi? Hadi sasa nashangaa kilichowaroga walevi. Una habari ule ujambazi aliofichua David
Kafulia ambapo vigogo sita wameiba zaidi ya bilioni 200 ni kama unafifia kiasi cha wahusika kuanza kuleta sanaa na ngonjera tena za kuwapaka wenzao matope?
Sioni walevi wakiingia mtaani angalau kutaka shingo za akina  Sossie Muongo, Eliar Maswie, Bennie Ndururu na majizi mengine makubwa tu.
Ajabu ya maajabu hata walevi wanaonekana kujifanya hamnazo kwa kujifanya hayawahusu!
Mnadhani msipowashupalia hawa kuna mtu wa kuwapeleka mahakamani wakati wote ni mibaka mijambazi na mikwapuzi? Jiulize. Wale waliotorosha wanyama wamechukuliwa hatua gani zaidi ya kumtorosha gabacholi aliyetumiwa kuwasafirisha?
Jamani mliwe mara ngapi hadi mstuke? Hii ya kutorosha wanyama haina tofauti na ile ya Chavda ambapo baadhi ya madingi walisuka misheni wakampa atekeleze ili wao wasiumbuke.
Ujambazi wao ulipofichuka wakamfukuza Chavda ili asiwataje. Kama mnadhani ninazusha shaurienu.Nyie kalieni ukondoo huku mkiliwa mtajikuta mmeisha kama siyo kuuzwa utumwani.
Na bahati yenu ni kwamba utumwa wa kusafirisha watu ulibadilishwa kuwa wa kuwatumia walipo vinginevyo mngepigwa mnada kama kuku.
Kaya yetu ni ya ajabu sana. Pamoja na kuwa kibarua cha kuwafurusha Ali Shabaaabi wenzetu wa Kenya hawanunui rada kila mwaka.
Uganda pamoja na kukabiliwa na kitisho cha LRA hawanunui rada kila mwaka kama sisi.
Hata DRC yenye migogoro na vita kila mahali hainunui rada mara kwa mara kama sisi.Je! tatizo ni rada au hao wanaopenda kununua rada ili wapige njuluku?
Huwa nikiwaona watuhumiwa waliotuibia kwa kununua huu mfu rada natamani niwakamate na kuwachinja na kuwafanya kitoweo cha mbwa wangu lau nijiridhishe kuwa nimewatendea haki wanayostahili.
Sioni sababu ya kuendelea kuchekea mijizi kama Andru Chengee, Iddiliisha Rashid na yule ponjoro Visirani ambaye bila shaka ameishachonga mchongo mwingine tayari kutuingiza mjini.
Kama kungekuwa na rada za kuchunguza wezi wanaotumia rada kutuibia basi ningeshauri zinunuliwe hizo.
Nadhani kuna haja ya kununua matunguli ili kuwazindika walevi wasiendelee kuibiwa kibwegebwege na hawa majambazi bwege.
Pia napendekeza kununuliwa  pilipili na bangi ili vikitumiwa na walevi viwafanye wakali kupambana na majambazi na majizi yanayowaibia kila uchao kupitia schemes mbali mbali kama EpA, Escrew, NiC, Meremeta, Mwananchi Gold, SUkiTA, UdA, Richmonduli, DoWans, IpTL, RITES, Ticts, mkangafu wa Rada na Dege lenye mafua la mkuu.
Tumalizie kama tulivyoanza. Je! ni kweli mwanunua rada au mwaradidi wizi wa rada?
 
CHANZO: NIPASHE Juni 7, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

CCM makes me sick

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

CCM makes me mad and sick so to speak.