Sunday, 7 February 2016

Magufuli atumbue na majipu mikoani na wilayani pia


            Ama kweli rais John Pombe Magufuli hana mchezo. Utumbuaji wake wa majibu unazidi kuwafurahisha wengi ingawa si wote. Wapo wanaoridhika na kasi yake. Pia wapo ambao hawaridhishwi kabisa na kasi yake huku wakingoja kuona atakavyotumbua mabusha kama vile kashfa ya wizi wa mabilioni ya shilingi ya escrow ambayo hivi karibuni imelitishia bunge utadhani nayo ni serikali ndani ya serikali. Sijui hawa IPTL wanaotishia bunge letu tukufu wanapata wapi hii jeuri au kuna namna wameishahakikishiwa ulinzi? Maana tujuavyo, serikali ya Magufuli si ya ubia wala ya kuchezea chezea. Je inakuwaje hawa IPTL wanakuja na vitisho kana kwamba hawamuoni Magufuli?
            Ukiachana na mabusha kama escrow, pia yapo majipu mengi yanayongojea kutumbuliwa mojawapo likiwa la wakuu wa mikoa na wilaya ambao hata ndege wanajua hawana sifa za kuteuliwa zaidi kujuana, kufadhiliana, kupeana ulaji na kulindana ukiachia mbali wale waliopewa vyeo hivyo tokana na kufanya kazi chafu ya kuwachafua, kuwadhalilisha au kuwatisha wengine kwenye mchakato wa katiba mpya na uchaguzi wa mwaka 2005 ulioingia kwa mtaji wa kashfa ya EPA.
                        Juzi Magufuli alipotumbua majipu ya ughaibuni kwa kuwarejesha nyumbani baadhi ya mabalozi, wengi walishangilia hatua hii ambayo inapaswa kuwa mwanzo wala si mwisho. Kwani kuna majipu mengi ughaibuni sawa na nyumbani. Nchi ilikuwa imeoza.  Tunaamini huu utakuwa ni mwanzo tu. Maana bado kuna mabusha kibao yanayopaswa kutumbuliwa haswa. Itakuwa ajabu mabalozi wa Tanzania waliopo Kanada, Washington, Urusi, Msumbuji, Kinshasa na kwingineko wanaokabiliwa na kashfa lukuki wasipotumbuliwa. Hilo moja.
            Pili, itakuwa ajabu ya maajabu iwapo baadhi ya wakuu wa wilaya kama vile Paul Makonda anayekabiliwa na  kashfa ya kumshambuliwa waziri mkuu, mwanasheria mkuu wa zamani na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Ukusanyaji Maoni ya Katiba mpya Jaji Joseph Warioba,  Mihingo Rweyemamu  aliyelipwa fadhila baada ya kuwachafua wagombea tishio kwa aliyemteua, wakuu wa mikoa  ambao ni watupu kabisa wasio na sifa waliopandishwa ghafla toka ukuu wa wilaya ambao nao hawakuwa na sifa nao ukiachia mbali wale waliopewa ulaji baada ya kubwagwa kwenye kura za maoni za ubunge. Kwetu hawa wakuu wa mikoa, wilaya na baadhi ya mabalozi ni zaidi ya majipu, ni mabusha yanayopaswa kutumbuliwa haraka sana.
            Pia Magufuli aende mbali zaidi akiwatumbua watoto wa vigogo waliojazana kwenye balozi zetu ukiachia mbali maofisa wastaafu wanaoendelea kulipwa na kulipiwa pango ughaibuni wakati waliishastaafu. Akimaliza kutumbua haya mabusha, aelekee kwenye mahakama ambako wamejaa majaji vihiyo na wenye kashfa kama alivyowahi kuwatuhumu mbunge wa Singida Kaskazini, Tundu Lissu akapuuziwa na rais aliyepita kutokana na ubovu wake katika uteuzi. Lissu alidai kuwa kuna majaji ambao hawawezi kuandika hata hukumu ukiachia mbali ambao walishiriki vitendo vya rushwa wakiwa mawakili binafsi.
            Pia angalie wenyeviti wa bodi za ulaji mmojawapo akiwamo mama mmoja aliyewahi kuteuliwa kuwa balozi kama fadhila ya kampuni yake ya uwakili kufanikisha madili ya wakubwa ikiwemo EPA. Pia wale wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na kashfa kama Buzwagi (ambayo iliuawa kinamna), EPA, Richmond na Escrow hawakupaswa kuwa kwenye serikali ya Magufuli.  Pamoja na kuwa mmoja wa watuhumiwa wa escrow na wa kughushi wako tayari ndani ya serikali –kama rais alivyoweza kumrejesha mtuhumiwa mwingine mikoani baada ya kuonja utamu wa kuwa TRA –hata hawa watuhumiwa wa escrow na kughushi afikirie kuwafanyia hivyo mara moja ili kuondoa doa kwenye serikali iliyojizolea umaarufu kwa uchapakazi  na utumbuaji wake majipu ingawa mabusha bado.
            Hivi majuzi aliyekuwa mkurugenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (DRT) aliwekwa kando. Ajabu, wakati mkuu huyu akiwekwa kando, tunashangaa kwanini washirika wa DRT wasio rasmi UDA ambayo kutwaliwa kwake ni utata hawajatumbuliwa? Maana, kwa wanaojua kilichotokea UDA watakubaliana nasi kuwa UDA si jipu tena bali busha linalopaswa kutumbuliwa haraka.
            Magufuli –kama daktari wa kutumbua majipu –bada ana kazi kubwa tu. Unaweza kusema kazi ndiyo inaanza. Bado anangojewa a mabusha kama vile kurekebisha mikataba ya madini ambao iliingiwa na maafisa mafisi na mafisadi kiasi cha kuendelea kuigharimu nchi bila sababu. Hata hii sheria ya kutoa miaka mitano kwa wawekezaji wakaishia kubadili majina kila baada ya miaka mitano ni busha kubwa tu.
Kwa ufupi ni kwamba umma wa watanzania unangojea kuona Magufuli akiwatumbua majipu wakuu wa mabalozi na maafisi wengine ubalozini, wakuu wa mikoa, wilaya na yote katika yote UDA, Escrow, mikataba mibovu ya madini bila kusahau wauza unga.
            Tunataka nchi isiyo na majipu wala mabusha. Tunahitaji nchi isiyo na upendeleo, kulindana, kulipana fadhila. Badala yake tunataka nchi ya watu wazima wachapa kazi na wasafi badala ya huu uchafu uliotamalaki ambapo watu wasio na sifa yoyote zaidi ya wanayemjua kupewa madaraka mazito na makubwa wasiyo nayo uwezo.
Chanzo: Dira, Feb., 8, 2016.

No comments: