Kudos to President Magufuli

Saturday, 20 February 2016

Mlevi agoma kusimamia uchakachuaji kwa M7


            Baada ya wajinga fulani kutaka kunigeuza juha kama wao wakitaka eti niende kwa M7 kuangalia uchakachuaji wakati nikijua kura zitaibiwa na imla atachukua na kuweka waa, niliwatolea nje kuwa siwezi kugeuzwa juha na majuha. Hata hivyo, wapo waliokubali kuwa majuha kwenda kubariki wizi wa mchana ambapo M7 alishashinda hata kabla ya kuchakachua. Sijui kama kunaweza kuwapo uchaguzi huru na wa haki zaidi ya uchakachuaji.
            Baada ya maswahiba wengi kunisihi niende, niliwazodoa kuwa wao wa Zenj umewapiga chenga, watakuwaje na uchungu wala udhu wa uchakachuaji wakati uchaguzi umewashinda kiasi cha kuendelea kuishi kwa kitatange kiasi cha kukwamisha juhudi adhimu za my friend Dk Kanywaji? Shame on them! Walidhani mimi ni mtu mzima hovyo kama jamaa yangu wa Loliyondo alivyokubali kugeuzwa bunga kwenye kubariki wizi na kuhalalisha haramu kule kwa M7.
            Kama kusimamia uchaguzi dili basi nitasimamia ule wa kwa Joji Kichaka baada ya bwana mdogo Obamiza kuachia ngazi. Kwa vile huyu dogo alikuwa mwanafunzi wangu wakati nikifundisha kwenye chuo kikubwa cha Havard, nitaenda kumpa tafu na kumpongeza kwa kumaliza ngwe bila shobo wala uchafu kama jamaa zangu wa kayani ambao sasa wamegeuka vyangu wa kudandia kila mnuso baada ya mwalimu JPM Nyerere kuwatilia ngumu kwenda ughaibuni kuzurura na kuteketeza njuluku za walevi.
            Kwa tathmini yangu ya kilevi ni kwamba hakuna uchaguzi unaoweza kufanyika kwenye eneo la maziwa makubwa kutokana na kujikita kwa udikteta na udhalilishaji wa katiba ambapo miungu watu wanataka watawale na kufia madarakani kama Jimmy Kinyatta na Kamuzi Banda ukiachia mbali M7 na mdogo wake ka-Game. Nikiangalia kilichotokea Urundi kwa Nkurumbwiza na wenzake wakamgwaya, sina imani tena na domoghasia. Hivi unategemea nini toka kwa gendaeka ambaye amezoea kuchakachua kula kwa zaidi ya miaka thelathini sasa. Muulize M7 aliingia madarakani lini. Watoto waliozaliwa akiwa maulajini nao sasa wanasimama kumpinga lakini haoni hata aibu. Ama kweli wakati mwingine mtu mzima hovyo ukiachia mbali wengine kuzeeka vibaya. Kwa mijitu iliyokosa aibu ikatawaliwa na tamaa na njaa ustaarabu ni msamiati mgumu na adimu kwao.
            Kwa mtu mzima mwenye akili sawa sawa hata kama sina soksi nisingekubali kujiingiza kwenye wizi na kejeli kama hii eti kwenda kubariki udikteta unaoitwa demokrasia. Kiakili, huwezi kwenda kusimamia jizi lililokubuhu ndani ya kaya yake ukajidanganya kuwa utalikamata.  Lazima litakuzidi akili kwa kutumia mbinu ile ile ambayo limetumia miaka nenda rudi kuendelea kuwa kwenye ulaji. Kuna dawa mbili kukomesha jizi kama hili. Mosi, ni kuliambia tena kwa shinikizo liache wizi kwa kufuata kanuni za uchaguzi badala ya viini macho. Ukiona huna mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya jizi hili unaamua kulisusa na kulisusia jinai yake ili usiwe sehemu yake. Huu ndio uoni wa watu wenye bongo zinazochemka na si haya manungaembe ya kifikira yanayoendekeza tumbo na kutafuta sehemu ya kugangia njaa na kupoteza muda kama  jamaa yangu aliyedanganywa juzi kuwa atakuwa dingi wa kusuluhisha waathirika wa Kadhafi wakati waliomteua waliambiwa wazi kuwa walikuwa wakimuunga mkono habithi Kadhafi hivyo hawana maana wala uwezo wa kuhusishwa kwenye zali na Ulibyani. Kama watasha wenzao wameshindwa hawa wamakonde ndiyo watakaowapatanisha wakati watasha wenyewe wanawabagua watasha na kuwaona kama kenge wa kawaida? Huu ndiyo ukweli hata kama unauma au kuwa wa kilevi. Again, who cares if somebody has gotten another opportunity of globetrotting after Dr Kanywaji put a pin on it? My friend Njaa Kaya, upo hapo hapa kaka?
            Tukiachana na hili la kwenda UG, ngoja turejee nyumbani. Mlevi hadi sasa anajiuliza nini kitafanyika baada ya kugundua kuwa kumbe magabacholi wanawaita waswahili kalu na abisiii yani nyani au sokwe. Baada ya kulalamikia hili na kutishia kuingia Bombey kufanya kitu mbaya, naona kama wachovu wamesahau na kurejea kwenye maisha yao ya kijungu jiko. Mtaliwa sana kama tabia yenu ni hii.
            Leo nataka niwape ushauri wa bure.  Ili kuondokana na hawa nguchiro wanaotubagua huku wakija kwetu na kutanua, tuanze kuacha roho ya kwanini ambapo mlevi akianzisha biashara zake wenzake wanamkwepa kwenda kununua kwa hao hao wanawaita kalu na absiii. Kwa tabia hii ya kutojitambua kweli nyinyi si absiii hata kalu? Kuna mambo mengine hata hayataki elimu kubwa au msokoto wa bangi. Ni suala la kutumia kichwa kufikiri badala ya kutumia masaburi. Sasa mmeishaambiwa mnavyodharauliwa, kunyonywa na kubaguliwa. Kama jamii mmeamua kufanya nini kama jibu ya kadhia hii ya kishenzi na kinyama.
Chanzo: Nipashe, DWb 20, 2016.

No comments: