Sunday, 14 February 2016

Vita ya ufisadi: CCM wanamdanganya nani?

  • SHEREHE YA KUMBUKUMBU YA MIAKA 14 YA HAYATI BALOZI WILSON TIBAIJUKA
            Hivi karibuni katika maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mjini Singida, Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete alisikika akiwazodoa wapinzani akisema waache kudai kuwa chama chake kimeiba sera zao.
            Kwa kujigamba na kujiamini, Kikwete aliwataka wapinzani kusoma ilani ya CCM ili wajue kuwa CCM haikuiba sera zao. Alikwenda mbali na kukiri kuwa kama wameibiwa sera zao basi waiunge mkono CCM kwa inapotezitekeleza. Nani anaweza kumuunga mkono mwizi anayejidai kwa shati alilomuibia?
            Wanaojua sera kuu ya upinzani ya kupambana na ufisadi–kabla kuisusa baada ya kumkumbatia waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa alipojiunga nao na kupitishwa kuwa mgombea wao–wapinzani waliibua ufisadi karibia wote nchini kiasi cha watanzania kujua kuwa sera kuu ya upinzani ilikuwa kuibua na kupambana na ufisadi uliokithiri chini ya utawala dhaifu uliopita kiasi cha kuilazimisha awamu ya tano kusimamisha mambo mengine na kupambana na ufisadi uliolelewa na serikali hiyo.
            Bahati nzuri, aliyejitapa kuwa sera ya chama chake ni kupambana na ufisadi ni mwenyekiti wake aliyekuwa rais wa awamu ya nne. Swali la kujiuliza–na kumuuliza–ni je kama kweli sera ya kupambana na uovu na ufisadi ni ya CCM ilikuwaje akashindwa kuitekeleza akiwa na kofia mbili, urais na uenyekiti wa CCM? Je Kikwete anataka kumdanganya nani anapodandia mgongoni mwa rais John Pombe Magufuli ambaye–kwa kiasi kikubwa–amejitofautisha na chama chake kiasi cha kukitia kiwewe hasa vigogo wake wengi wanaojulikana kuwa nyuma ya ufisadi kama EPA, Richmond waliyomtwisha Lowassa, Dowans, SUKITA, Escrow, UDA na nyingine nyingi ambazo hazijafichuka.
            Tukirejea kwenye nani mwenye sera ya kupambana na ufisadi kati ya CCM na wapinzani, nadhani watanzania si wasahaulifu kiasi hiki. Wanakumbuka kuwa ni upinzani huu huu unaobezwa ulioibua kashfa mama ya zote kwa kutaja orodha ya mafisadi papa akiwamo Kikwete mwenyewe huko Mwembe Yanga Temeke mwaka 2007.
            Kama haitoshi, ni wapinzani hawa hawa walioibua kashfa ya Escrow ambayo Kikwete alishindwa kuishughulikia akaishia kujifanya msemaji wa watuhumiwa kwa kudai kuwa fedha zinazodaiwa kuibiwa zilikuwa zao bila kueleza kwa vipi wakati vyombo vingine vya dola vilishatamka wazi kuwa fedha ya Escrow ni ya umma. Nani hakumbuki kuwa kashfa ya Escrow iliishia mlangoni pa Kikwete baada ya mtendaji wake mkuu Gurumo kuhusishwa moja kwa moja?
            Kikwete anaonekana ima ni mwepesi wa kusahau au kuwafanya wenzake ni wasahaulifu kiasi cha kutaka kujidanganya na kuwadanganya akafikiri atafanikiwa. Nani hajui kuwa sera ya CCM chini ya Kikwete ilikuwa ni kulinda ufisadi? Nani hajui kuwa ni Kikwete huyu huyu aliyewahi kudai kuwa vyombo vya upelelezi vilimpa orodha za mafisadi, majambazi, wauza unga hata wezi bandarini akazikalia hadi anaondoka? Je kupambana na ufisadi ingekuwa ya CCM–ikizingatiwa kuwa rais alisharahisishiwa kazi kwa kuletewa orodha–angeshindwa nini kushughulikia orodha husika ambazo amestaafu nazo? Ni Kikwete huyu huyu aliyewasihi wananchi kumuacha mzee Mkapa apumzike na kashfa ya kujitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa umma wa Kiwila yeye na familia yake na marafiki zake? Hapa hujataka kashfa ya juzi ya kusafirisha wanyama hai ambapo ikulu ya Kikwete imeguswa na isikanushe.
            Tumkumbushe Kikwete na CCM kuwa vyombo vya usalama vilipoibua majambazi papa na kukuta kuwa wengi walikuwa wafadhili wa CCM hiyo hiyo alifanya nini zaidi ya kusitisha zoezi husika huku akiwakatisha tamaa walioshughulikia kadhia hii? Hivi kweli kupambana na ufisadi ingekuwa sera ya CCM wangeua rasimu ya Katiba mpya iliyolenga kupambana na ufisadi kwa vitendo badala ya maneno? Inashangaza hata Magufuli aliyeingia na gea ya kutumbua majipu amepata kigugumizi kufufua mchakato ili angalau apate katiba ambayo ingemsaidia kupambana na ufisadi vilivyo. Hapa ndipo wenye kufikiri wanapata wasi wasi kama kweli Magufuli anaungwa mkono na chama chake kwenye vita yake na kama atafanikiwa au kuishia kuwa nguvu ya soda kama fagio la chuma la mzee Mwinyi lililoishia kufagia uchafu na kuufichia uvunguni mwa kitanda cha CCM.
            Kuna haya kuwaambia CCM wazi kuwa waache kuhadaa watu ili kuwakatisha tamaa wapinzani au kuwahadaa wananchi wadhani upinzani hauna kazi baada ya Magufuli kuanza kupambana na ufisadi nusu. Nadhani bila upinzani kuwapo hata kutajwa tajwa kwa kashfa ya Escrow kungekuwa hakuna. Na nijuavyo–kwa maudhi aliyoonyesha Kikwete–amewapa wapinzani mishale ya kuzidi kuishupalia kashfa husika.
            Kama kuna sera ya CCM ya kupambana na ufisadi chini ya Kikwete haikuwa nyingine bali kula na mafisadi. Rejea Kikwete alivyowataka wezi wa mabilioni ya EPA kurejesha fedha huku akikamata vidagaa na kuwaacha mapapa kama kada wa CCM mwenye kampuni ya Kagoda aliyetajwa kuwa ni Rostam Aziz. Tumkumbushe Kikwete na CCM. Kama sera yao ilikuwa ni kupambana na ufisadi, anaweza kueleza alishindwa nini kuwashughulikia wezi wa fedha za rada ambao wenzao wa Uingereza walishafikishwa mahakamani na kutozwa faini? Je Kikwete anakumbuka swahiba yake na mwanasheria wake mkuu Fredrick Werema alivyomtishia balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave baada ya kudai kuwa serikali ya Kikwete ilikuwa ikiwanyima ushirikiano kuhusiana na urejeshwaji wa mabilioni yaliyofichwa na vigogo huko Uswisi ambayo mpaka sasa hakuna anayoengelea akiwamo Magufuli mwenyewe. Tuwaongezee dozi nyingine. Nani anaongelea nyumba za umma zilizoibiwa chini ya utawala wa awamu ya tatu ambapo hata Magufuli mwenyewe aliguswa? Nadhani kwa nyodo za CCM wanazidi kujipalia mkaa.
            Tumalizie kwa kuwataka CCM waache kuwadanganya wengine nao wakajidanganya.
Chanzo: Mwanahalisi, 14, Feb.2016. 

No comments: