The Chant of Savant

Wednesday 4 October 2017

Shambulizi la Lissu tulete wapelelezi wa kigeni

            Sina shaka ninapoandika makala hii kusema kuwa jaribio la kutaka kumuua mbunge wa Singida Mashariki na rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) mheshimiwa Tundu Lissu ni suala lililochafua sifa ya Tanzania ukiachia mbali kuondoa imani kwa baadhi ya vyombo vya usalama. Hii ni kutokana na kushindwa lau kuwakamata wahusika pamoja na kujitahidi kufanya hivyo. Shambulizi hili la kishenzi na kikatili linakatisha tamaa kiusalama hasa ikizingitiwa kuwa si la kwanza. Na kwa hali ilivyo, huenda si la mwisho.
            Watanzania wanataka usalama na si usalama tu bali usalama wa uhakika. Watanzania wanakata wahalifu waliotaka kukatisha maisha ya Lissu wakamatwe, kujulikana na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, hali ilivyo, uwezekano wa wahalifu hawa kukamatwa unazidi kufifia hasa ikizingatiwa kuwa muda unavyozidi kuyoyoma, ndivyo wahalifu wanavyozidi kuepuka kukamatwa. Wengi wanashangaa na kuhoji: je inakuwaje nchi yenye vyombo vyote vya usalama kushindwa na genge dogo la wahalifu? Je kweli tumeshindwa au tumeamua kushindwa?
             Asiyekubali kushindwa si mshindani. Nasi kama taifa tunalotaka kupambana na uovu na ukatili kama aliofanyiwa Lissu tukubali kushindwa. Tutakapofanya hivi –s kwa nia ya kuonyesha udhalili wala uhovyo bali kutaka kuwa na taifa salama –tutakuwa tayari kutafuta msaada kwa wenzetu. Hapa ndipo wazo la kutaka wapelelezi wa kigeni waitwe nao wajaribu. Hatutakuwa taifa la kwanza kufanya hivi. Alipouawa waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Kenya Robert Ouko mwaka 1990, baada ya jeshi la polisi na vyombo vya usalama vya Kenya kushindwa kuwakamata waliomuua, vilimkodisha mpelelezi toka Uingereza aitwaye John Troon kuchunguza kadhia hii. Hata hivyo, Troon alipokaribia kuwagusa wasioguswa, alifungashiwa virago na kuondoka Kenya ili kuwanusuru wahalifu wakubwa waliokuwa wamejificha nyuma ya madaraka.  Sitaki nifananishe tukio la kushambuliwa Lissu na la kuuawa Ouko. Hata hivyo, tokana na kuwa mwanasiasa wa upinzani, wapo wanaojenga dhana kama hii kuwa woga unaweza kuwa kikwazo cha kuleta wapelelezi wa kigeni.
            Kwanini napendekeza tulete wapelelezi wa kigeni? Kwanza, hadi sasa hatujajua waliomshambulia Lissu, na kwanini walitaka afe. Pili, tokana na mkanganyiko na ukimya vilivyotawala, kuna uwezekano ikajengeka dhana ovu kuwa mamlaka yako nyuma ya shambulizi hili jambo ambalo kwangu haliingii akilini. Tatu, tokana na unyeti wa hadhi ya Lissu kama mpingaji mkubwa wa serikali, upo uwezekano maadui wa serikali–hasa walisiopenda mambo makubwa yanayofanywa na serikali kwa sasa kama kupambana na ufisadi na maovu mengine kiasi cha kuwatibulia waliozoea vya dezo–wanaweza kukodisha wauaji ili serikali ionekane imefanya hivyo. Nne, pia inawezekana wakawapo wabaya wake nchini wenye nafasi ambao wanaweza kutumia nafasi zao kuamuru Lissu auawe kwa kujipendekeza tu kwa mamlaka.  Hapa lazima tuondoe dhana kuwa shambulizi la Lissu linaweza kuwa uhalifu wa kaiwaida hasa tukizingatiwa namna, mahali na wakati liliopofanyika. Dodoma ni mji mkuu wa Tanzania. Eneo alipopigiwa risasi Lissu linaishi watu wazito wenye ulinzi wa uhakika. Na pia wahalifu hawa hawakuchukua chochote zaidi ya kutaka kuchukua uhai wa Lissu. Ukiunganisha haya yote, unaona ukubwa, unyeti na utata wa shambulizi hili la kigaidi na kiuaji.
            Tano, wahusika, yaani wanaopaswa kualika wapelelezi wa kigeni wanapaswa kujiuliza maswali machache muhimu. Je ingekuwa mimi, mwanangu, mke wangu, baba au mama yangu, rafiki yangu, mkubwa mwenzagu na mengine kama haya, ningetaka nifanyiwe nini wakati huu? Mbali na hili, wahusika wanapaswa kujua kuwa kama wataalika wachunguzi na wapelelezi wa kigeni, watakuwa wanakata kidomodomo cha wanaojenga dhana potofu kuwa kuna mkono wa serikali kwenye shambulizi dhidi ya Lissu tokana na polisi kushindwa kuwakamata wahusika. Pili, kwa kuleta wapelelezi wa kigeni, serikali itakuwa inazidi kuwajengea imani watanzania kuwa inajali sana usalama wao na amani ya taifa. Maana, shambulizi hili, licha ya kupunguza imani kwa serikali na vyombo vya usalama, imechafua amani na sifa vya taifa letu linalosifika barani kwa kuwa kisiwa cha amani ambacho sasa ni kisiwa cha amani kwa imani lakini si matendo. Kama wahalifu waliojaribu kumuua mtu mkubwa kama Lissu wanashindikana kupatikana, watakapoelekeza mitutu yao kwa walalahoi hali itakuwaje?
            Tumalizie kwa kuitaka serikali iliangalie shambulio la Lissu kwa mapana na kina zaidi ili kuepuka kupoteza sifa yake na ya taifa. Shambulio la Lissu si kwake tu bali kwa Tanzania hasa ikizingatiwa namna maadui zetu wanavyoweza kulitumia kutuchafulia jina kama ukimya na kutokamatwa kwa wahusika vitaendelea. Tutaonekana kama taifa lisilo imara tena; lisilo salama na lisilojali hata uhai wa watu wake jambo ambalo ni aibu na machukizo. Tusiwape maadui yetu la kusema kwa kudhani kuwa wauaji wa Lissu hawakamatwi kwa vile yeye ni mpinzani wa serikali. Hivyo, kuruhusu kujengeka dhana potofu kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kumuondoa kwa vile anaonekana kuwa kikwazo. Tusifike huko. Mbali na hilo, tumuangalie Lissu kama mwanadamu yeyote mwenye haki ya kuishi hadi Mungu atakapotaka lakini si genge la magaidi uchwara.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: