Delonising Education

Delonising Education

Tuesday, 10 October 2017

Kijiwe chaadhimisha miaka 18 ya kifo cha mzee Mchonga

            Image result for the cartoons of julius nyerere    Mgoshi Machungi anaingia akiwa ameshikilia kitabu cha Ujamaa na Kujitegemea kilichoandikwa na mzee Mchonga mwenyewe. Kila mtu anashangaa. Kwani, licha ya kutoonyesha usomi, Mgoshi, hajawahi kuja na hata kipande cha gazeti kijiweni. Kila mtu anashangaa kugundua kuwa kumbe Mgoshi ni bonge la mbukuzi tena mwenye maktaba yake iliyosheheni vitabu bab kubwa!
            Kama vile amesoma mawazo yetu, Mgoshi anajisifia. “najua wengi minashangaa kuona Mgoshi nimebeba tabu kubwa tena la msomi mkubwa kama mzee Mchongameno mwana wa Musa. Msikonde. Siyo azima tiseme kia tinachofanya. Cha mno nataka tikae kama kamati ya kijiwe na kumduusu huyu ngui japo tionyeshe, heshima, kumbukumbu na mapenzi yetu kwake. Au shiyo?”
            Msomi anayeoonyesha kufurahia kitendo cha Mgoshi anaamua kula mic “Mgoshi leo umenifurahisha kweli kweli. Huyu nguli na msomi mwenzetu namkubali. Nimesoma karibu maandishi yake yote. Huyu bwana hakuwa kiumbe wa ulimwengu huu; na alikuja kabla ya wakati wake. Umenikumbusha mbali sana. Umenirudisha kwenye zama ambapo usomi ulikuwa mali na si ufisadi, wizi, na uuzaji bwibwi kama ilivyokuja kuwa baada ya mzee Mchonga kutundika daruga. Zama zile uongozi hakukuwa utawala bali uongozi. Kiongozi alifanana wale aliowaongoza bila kujali kama wanakubaliana na mawazo yake au la.”
            Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic “hata mimi iko penda na hesimu sana hii giji hata kama nataifisa mali nyingi ya hindi. Hii zee iko tofauti. Iko sawa na Gandhi. Iko nafanya mambo kubakuba sana kwa taifani hii.”
            Kabla ya kuendelea, Mijjinga anamkwapua Kanji mic na kuzoza “Kanji, huwezi kumlinganisha mzee Mchonga na Gandhi aliyesifika kwa ubaguzi. Mlinganishe na Nelson Lolihlahla Madiba Mandela Dalibunga, Osegafyo Kwame Nwia Kofi Nkrumah, Seretse Goitsebeng Maphiri Khama, Ernesto che Guevara na magwiji wengine lakini siyo na mbaguzi aliyewabuga waafrika tena nchini mwao kule Afrika Kusini akidai kupewa haki ya kuwa tofauti na waafrika aliwaita makafiri.”
            Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anachomekea “Du Mijjinga kumbe wewe ni tabu la historia! Unawataja majina utadhani wadogo zako! Ama kweli kusoma ukaelimika raha!”
            Kapende naye anaamua kutia guu “nakubaliana nawe Mijjinga. Mzee Mchonga hawezi kulinganishwa na Gandhi. Kufanya hivyo, ni kumdhalilisha hasa ikizingatiwa kuwa hakuwa mbaguzi wala msanii. Anyway, hayo tuyaache. Mie ningependa kumkumbuka na kumdurusu mzee Mchonga kama kiongozi ambaye hakuwa mwoga wala mbabaishaji. Alipenda sana kukosolewa ilmradi anayefanya hivyo awe na hoja nzito na zenye mashiko. Akitokea mtu wa namna hii mzee Mchonga alizoea kumjibu kwa hoja nzito na zenye mashiko. Nadhani watu kama totoTundu Lissu wangekuwapo wakati wa mzee Mchonga wala wasingechukiwa wala kumiminiwa shaba.  Kitu muhimu kilichofanya nimgwaye mzee Mchonga ni kupenda haki na usawa. Yeye hakuwa na rafiki zaidi ya wabongo. Hakuwa tayari kumkingia kifua mhalifu yoyote kama ilivyokuja kutokea baada ya kuachia madaraka. Unadhani huu ungekuwa wakati wa mzee Mchongo mizigo kama Bashit na wababaishaji kama yule mchunaji Gwajimmy wangepata muda wa kutanua na kutanuliana wakati wote wana madoa? Thubutu!”
            “usinikumbushe huyu baba ambaye aliheshimu kila mtu. Bila yeye wala mimi nisingepata hii elimu, hata  kama ni haba, niliyo nayo. Bila yeye baba na mama yangu wasingejua kusoma na kuandika. Nani mara hii kasahau elimu ya watu wazima aka ngumbaru? Mungu iweke peponi roho ya baba yetu mzee Musa Mchonga Nyerere.” Anasema Sofia Lion aka Kanungaembe. Hata hivyo anashindwa kuendelea kuongea tokana na uchungu kiasi cha kumwaga chozi huku Mbwamwitu akimfariji kwa kumkumbatia.
            Msomi anamchomekea Sofia “dada usinikumbushe nguli huyu. Maana bila yeye hata mimi nisingeweza kupata PhD zote hizi nilizo nazo. Ni nani mtoto wa kapuku kama mimi angeweza kuitwa daktari kama mimi? Ni bahati mbaya. Wengi wa walionufaika na sera na upendo wa nguli huyu wamesahau kila kitu kiasi cha wao kugeuka mafisadi papa kama akina mzee wa Vijisenti, Anae Kajuamlo, Ben Tunituni Makapa na wengine wengi. Inauma na kusikitisha sina mfano.”
            Mpemba anamchomekea Msomi “ami usemacho cha kweli ati. Kwani bila huyu nguli nani angeongelea muungano wa Bara na Visiwani? Wallahi wengine tungekuwa twaendelea kuonekana wageni kwenye nchi yetu kama si huyu maalim Nyerere.”
            Mipawa aliyechelewa kufika, hivyo, akaamua kuisoma mada kwanza anaamua kutoa mchango wake “kusema ukweli, Daganyika haitakaa ipata gwiji kama huyu tena. Maana madini kama haya hutokea mara moja maishani. Hata hivyo, napenda nitofautiane nanyi kidogo kuhusiana na gwiji huyu. Alifanya mambo mengi isipokuwa baya moja; yaani kuwaamini na kuwapigia hata kampeni mafisi walioiuza kaya yetu kiasi cha dokta Kanywaji sasa kuhangaika kuinyosha. Maana kama siyo huruma yake, huenda kaya yetu ingepata kiongozi mahiri na kusonga mbele badala ya kurudishwa nyuma.”
            Kabla ya kuendelea mzee Maneno anakula mic “ni kweli aliwaamini mafisi. Je alifanya hivyo kwa nia mbaya au kutoelewa? Tumuache mzee wetu apumzike huku tukisamehe lolote alilotenda ambalo hatukulipenda. Hata hivyo, yeye alikuwa binadamu si malaika. Muhimu tuenzi mema yake yote kama vile kutominya wale aliotofautiana nao mawazo.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si tukaamua twende Butiama kwenda kumpa tafu mama yetu Maria!
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.

No comments: